SHEREHE KUZIMU (34)
Zephiline F Ezekiel
---

Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA THELATHINI NA NNE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Alijua kuwa mpenzi wake atakuwa ameteketea ndani ya moto ule. Hakuona sababu ya kuendelea kuishi bila kuwa na Benedict maishani.
Alichukua uwamuzi wa kukimbilia ndani ya nyumba ili na yeye aweze kuteketea na mpenzi wake.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Malengo yake hayakufanikiwa kwasababu alikamatwa na askari wa zima moto. Adela alizidi kulia kwa uchungu hadi mashuhuda wa tukio lile wakamuonea huruma. Baada ya kulia kwa muda mrefu alipoteza fahamu hadi saa mbili asubuhi alipojikuta yupo hospitali.
Mshumaa uliokuwa unaangaza nuru maishani mwake tayari ulikuwa umeshazimika. Aliyachukia maisha kiujumla. Alihisi moyo wake umepata jeraha ambalo hakujua litapona mwaka gani. Hakuona sababu ya kuendelea kukaa jijini Mwanza, ili hali kilichokuwa kimempeleka kilikuwa kimefikia tamati japo kwa maumivu makubwa.
Aliondoka hospitalini pale na kuelekea katika kituo cha mabasi, kusudi aweze kurudi kijijini kwao. Alipanda daladala ya kumtoa pale hospitali kumfikisha kituo cha mabasi. Daladala ilipowasili mjini aliteremka na kuanza kutembea kuelekea kwenye vibanda vya kukatia tiketi. Wakati alipokuwa akitembea alishangaa ghafla amevamiwa na chizi na kuanza kupewa kipigo kisichokuwa na mfano.
“Wee achaaa achaaa.” Watu walijaribu kumkemea mwendawazimu yule lakini hakuonekana kujali kelele zao. Dhamira ya chizi yule ilikuwa ni kumbaka, kwahiyo alizungushana naye huku na kule ili aweze kumuangusha chini. Alikuwa akipiga kelele kuomba msaada huku akijaribu kujinasua mikononi mwake. Nguo zake zilichanika kiasi kwamba, alikuwa akidhalilika kwa jinsi ambavyo walikuwa wakizidi kuparangana kufa kuona. Hata hivyo mwanaume ni mwanaume tu, alizidiwa nguvu na kuangushwa chini, puuuu!
Wakati kichaa yule alipokuwa anapambana naye pale chini ili aweze kumbaka, wanaume wenye nguvu waliokuwa pale stendi walifanikiwa kumkamata chizi yule hatimaye Adela akasalimika. Wanawake walivua kanga zao viunoni na kisha kumsitiri Adela ambaye alikuwa amechaniwa nguo zake na kichaa yule. Alilia sana kutokana na kitendo kile cha udhalilishaji alichofanyiwa. Macho yake yalijawa na aibu kutokana na kwamba alidhalilika kwa kiasi kikubwa. Achilia mbali hayo yote lakini pia mwili wake ulijaa majeraha ya kung’atwa na kukatwa na wembe uliokuwa mkononi mwa chizi.
Kwa hasira wananchi walimvamia chizi yule na kuanza kumuangushia mkong’oto mkali, lakini baada ya muda polisi waliweza kuingilia kati kumuokoa. Adela alihisi kuchanganyikiwa kwasababu maisha yake yalikuwa hatarini kutokana na kwamba, alikatwa katwa na wembe ambao hakujua ulikuwa unatumikaje awali. Zaidi ya hilo, chizi yule alikuwa na kidonda kibichi katika mdomo wake wa chini. Hivyo basi kama chizi yule ameathirika na virusi vya UKIMWI basi moja kwa moja atakua amemuambukiza na yeye kwa njia ya yale majeraha ya kung’atwa.
Adela alijawa na wasiwasi mwingi sana. Machozi yahayakukauka katika macho yake. Kilichofanyika ni kwamba maaskari walimchukua kichaa yule pamoja na Adela na kuongozana nao hadi hospitali. Lengo ni kwenda kumpima yule kichaa ili kufahamu kama ana maambukizi ya VVU. Majibu ya vipimo vya daktari vilithibitisha kuwa yule kichaa ni muathirika wa virusi vya UKIMWI. Kwahiyo moja kwa moja Adela atakuwa ameambukizwa virusi hivyo.
Adela aliposikia hivyo alidondoka chini na kupoteza fahamu kwa muda wa masaa manne.
Presha ilipanda ghafla baada ya kusikia kwamba yule chizi ni muathirika wa virusi vya UKIMWI. Alilia sana na kumlaumu Mungu kwanini ameruhusu yale yote yatokee katika maisha yake. Alitafakari jinsi ambavyo familia yake inajitahidi kumsomesha kwa shida ili mwisho wa siku aje kuwa msaada kwao katika maisha ya mbeleni, lakini tayari maisha yake yalikuwa yameshadondokewa na doa lisilobanduka hata kwa jiki. Alivuta picha jinsi ambavyo mama yake atamlilia siku ambayo atakuwa amelazwa ndani ya jeneza, kwasababu ya gonjwa ambalo limemdondokea kama zali. Fikra zake zilienda mbali zaidi kwa kuwaza ni mkosi gani unamuandama katika maisha yake kwavile amekuwa akibadili matatizo kama nguo. Yaani leo ana nyekundu, kesho nyeusi, kesho kutwa kijani.
Mawazo mazito yaliuchosha ubongo wake, mara baada ya kupata fahamu. Alijihisi mchovu na asiye na nguvu asilani. Alishindwa kuzuia hisia za uchungu zilizokuwa zinapelekea machozi na makamasi kumtoka bila breki.
Baada ya muda mfupi, mlango ulifunguliwa nesi akachungulia mule wodini na kisha akaufunga mlango tena, na kuondoka bila kuzungumza naye chochote. Zilipopita dakika tatu nesi yule alirudi huku akiwa ameongozana na daktari mmoja.
“Nyamaza kulia binti, usiwe na wasiwasi wala presha kwasababu tatizo lako linatatulika.” Daktari alisikika.
Adela alizidi kulia kwa masikitiko makubwa kwasababu alijua maneno yale ni ya kumtia moyo. Aliona safari ya matumaini imewadia bila kupenda.
“Nisikilize kwa makini, nakupatia huduma ya dharura ijulikanayo kwa jina la ‘POST- EXPOSURE PROPHYLAXIS’ (PEP) ambayo husaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI ndani ya masaa 72 baada ya maambukizi ya virusi hivyo. Huduma hii huenda sambamba na chanjo iitwayo ANTIRETROVIRAL MEDICINES (ART) yenye nguvu ya kukukinga na maambukizi ya VVU.”
“Eehuuuu!” Adela alishusha pumzi huku akitabasamu kwa mbali, baada ya maneno ya daktari kurejesha matumaini yaliyokuwa yamepotea.
“Kwahiyo dokta sitapata maambukizi?”
“Haswaaaa, bila shaka, maadamu tunakupatia kinga hii ndani ya masaa 72, ninauhakika utaendelea kuwa mzima usiye na maambukizi. Baada ya miezi mitatu nenda kapime afya yako kwa uhakika zaidi.”
“Sawa, lakini kwani huduma hii ni ngeni?” alihoji ili aweze kufahamu zaidi kwavile hakuwahi kuisikia hata siku moja. Jibu la swali hilo, halikutoka kwa daktari tena, bali Nesi alimjibu kwa kumpa simulizi fupi iliyowahi kumtokea maishani mwake.
“….Hapana, huduma hii ipo kwa miaka mingi sana, na iliwahi kunisaidia miaka mitano iliyopita wakati nilipokuwa nikimuhudumia mgonjwa mmoja wa malaria. Katika harakati za kumsaidia kwa vile alikuwa katika hali mbaya, nilijikuta nimejichoma na sindano ambayo tayari nilikuwa nimeshaitumia kwake. Nilichokifanya nilimtoa damu kisha nikapeleka maabara kucheki. Kwa bahati mbaya nikakuta yule mgonjwa ni muathirika wa virusi vya UKIMWI, nilihisi kuchanganyikiwa kwasababu ilikuwa imebaki miezi minne nifunge harusi na mchumba wangu kutoka ng’ambo. Baada ya hapo nilipewa huduma hii ya PEP hadi leo mimi ni mzima sina maambukizi ya ugonjwa huo.”
Adela alifurahi sana baada ya kusikia ushuhuda ule kutoka kwa muuguzi. Alihisi mwili wake umepata nguvu. Alimshukuru sana Mungu kwasababu hakutegemea kwamba amenusurika kupata maambukizi. Alipomaliza kuhudumiwa alikwenda hadi stendi ili aweze kurudi nyumbani kwao. Tayari ilikuwa ni jioni wakati alipopata gari linaloelekea shinyanga.
Hakuwa na hamu ya kuwahi sherehe ya ubatizo wa mtoto wa dada yake tena. Mambo yaliyokuwa yamemtokea mkoani mwanza yalimchosha mwili na roho. Alijutia uwamuzi wake wa kwenda kumtafuta mpenzi wake, kwavile amerudi na majeraha ndani ya moyo, halikadhalika katika mwili wake pia. Safarini alikuwa ni mtu wa kulia kwavile fikra zake zilikataa kung’ooka kwa Benedict.
Alitamani kupata nafasi nyingine na mwanaume huyo kwakuwa ndiye alikuwa furaha yake. Aliwaza maisha yake yatakuwaje bila mtu huyo ambaye anampenda kuliko kitu chochote humu ulimwenguni. Licha ya kwamba mwili wake ulikuwa umejaa majeraha yenye kumpa maumivu makali lakini hakujali hilo. Hakuona kabisa thamani ya mwili wake ili hali mwenye dhamana ya kuutumia alikuwa ameshatoweka katika uso wa dunia.
Usiku wa saa nne kasoro aliwasili kijijini kwao, Ibinzamata akiwa amechoka kupita kiasi. Mama alihuzunika sana kutokana na majeraha aliyoyaona mwilini mwa binti yake. Adela alieleza ukweli kwamba alivamiwa na chizi asubuhi ya siku hiyo wakati alipokuwa stendi ya mabasi Mwanza. Kuhusu habari za Benedict, hakuthubutu kuzizungumza mbele ya mama yake kwasababu alishakatazwa kujihusisha na mapenzi angali bado anasoma.
Kwahiyo aliendelea kuugulia maumivu ya msiba wa mpenzi wake ndani kwa ndani. Alikonda na kubaki kama moja kwasababu ya mawazo. Alishindwa kula na kunywa ipasavyo kwasababu ya kumuwaza mtu wa ndoto zake. Alitamani angalau apate japo dakika mbili na mpenzi wake huyo, ili aweze kumweleza jinsi ambavyo anampenda.
Baada ya miezi mitatu alikwenda hospitali kupima afya yake ili aweze kujua kama ile kinga ilifanya kazi ama la! Baada ya vipimo iligundulika ni mzima asiye na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Alimshukuru sana Mungu kwa kumnusuru na gonjwa hilo la hatari. Kufikia muda ule afya yake, ilikuwa imehimarika vya kutosha. Tatizo lake lilibaki kuwa moja tu, ambalo ni la kuonana na mpenzi wake. Hakuchoka kumuomba Mungu siku moja aweze kuonana na Benedict hata kama sio duniani, iwe hata peponi.-
Mazishi ya mama mkwe yalipomalizika, Nelson alirejea Mwanza akiwa ameongozana na familia yake. Aliwasiliana na Mr Lee na kumjulisha msiba mzito aliokuwa ameupata. Aliongezewa wiki zingine mbili kwaajili ya maandalizi ya safari. Alifurahi sana kwasababu mke wake alionekana kuchoka sana kutokana na kufiwa na mama yake. Akilini aliwaza hadi zile wiki mbili ziishe mke wake atakuwa amepata nguvu na pia wataweza kupata muda wa kuudhuria mkutano mkubwa wa injili ambao ulikuwa unaanza siku chache za mbeleni. Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na mtumishi wa Mungu Isaka akishikiana na ile taasisi ya nchini Uingereza kwa muda wa siku saba jijini humo.
Siku ilipofika, huduma ya maombezi na uponyaji ilianza rasmi. Umati mkubwa wa watu walikusanyika kwa wingi katika kiwanja cha CCM KIRUMBA. Watu wengi walipata uponyaji kwa njia ya maombi. Ulikuwa ni mkutano mkubwa na wa kiistoria kufanyika mkoani humo. Mara tu baada ya mkutano huo kuanza Vivian alianza kujifanya anaumwa ili asiweze kuudhuria. Japokuwa alielezwa, uponyaji ataupata atakapokwenda katika mkutano huo wa injili, lakini aligoma kabisa. Kwa wakati huo Nelson hakuwa amegundua kuwa ule ni ujanja wa shetani aliyekuwa ndani yake. Hata hivyo alizidi kumwomba Mungu ili aweze kumuwezesha mke wake kuhudhuria mkutano ule wa kipekee kabisa.
Siku ya mwisho kabisa ya mkutano, Vivian alijihisi kuna nguvu inamsukuma kwenda katika mkutano ule pasina kutambua ni nguvu gani. Mume wake na mwanae walikuwa tayari wameshatangulia mkutanoni. Baada ya kupingana kwa muda mrefu na nguvu ile iliyokuwa inamsukuma hatimaye alijikuta njiani, akitembea kwa mwendo mkali kuelekea kule kwenye mkutano.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni