KONSTEBO NGUZU (12)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
ILIPOISHIA...
"Ni akina nani hawa? na wanataka nini?" Alijiuliza huku akiendeleza bidii katika kupapasa.

"Mamaaaaaa!" kelele kubwa zilisikika ghafla mbele yake na hapo akasikia vishindo vikiambaa kwa kasi.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Mungu wee! nini hiki? alijiuliza huku kwa mara ya kwanza akianza kupatwa na wasiwasi moyoni.

Akatulia tuli katika giza lile akisubiri kitakachojiri.

Hakuna aliyesogea, akasikia gari likiwashwa na kisha akauona mwanga kwa mara ya kwanza.

Mwanga ulipenya katika mboni ya macho yake katika namna ya kumsumbua.

"Tulia hapohapo mwanga mkubwa wewe!" sauti ikamuamrisha. Akatulia tuli huku akikumbuka nidhamu ya kunyoosha mikono yake juu.

Hatua zilizizidi kusogea hadi alipokuwa.

"Toa hicho kitambaa" Akaamrishwa.

Akaanza kujitazama.

"Toa kitambaa usoni!!" sauti ikaamrisha tena.

Ni hapa ambapo akili ya daktari Kobo ilifanya kazi.

Wakati wote aliokuwa akipapasa katika kiza kinene alikuwa na kitambaa usoni.

Ajabu!

Akajipapasa na kukifungua kile kitambaa. Ndio palikuwa na giza lakini sio kiza totoro kama alichokuwa akitembea kwa kupapasa.

Taa za gari zilikuwa zinammulika, akaendelea kunyanyua mikono yake juu hadi alipofika mwanaume mmoja akiwa na mkuki na rungu.

"Wewe ni nani usiku huu hapa na umefika vipi hapa. Tiketi yako ipo wapi? na kwanini haujatoka ndani hadi wakati huu..." Maswali debe yalitiririka.

"Sijui kitu chochote jamani." alijibu kwa shida, koo lake lilikuwa limekauka.

"Unajua hapa ni wapi?"

"Sijui lolote, sijui hata nilipotoka mpaka kufika hapa." aliendelea kusisitiza.

Taa zikazimwa! sasa aliweza kuwaona watu wawili zaidi, wote wanawake na kwa mbali akauona ufukwe.

Alikuwa jirani kabisa na bahari.

Kuhusu ni kitu gani kimetokea hakujua pa kuanzia lakini bado alihisi kuwa hajapaa hadi kufika katika ufukwe ule asioufahamu.

"Nipo wapi hapa jamani?" aliuliza ili apate mwanga.

Kabla jibu halijatoka, vikasikika vishindo na miale ikaanza kuonekana kuanzia mbali. Wote wakageuka nyuma kutazama kinachojiri.

"Kuna hatari hapa ndugu zangu. Ikiwa vyema tuondoke hapa" Yule bwana aliyefanania na mlinzi alitoa shauri.

Na hapo wale wanawake wawili wakaingia garini, kisha akafuata mlinzi na katukatu wakagoma kumbeba Dokta Kobo hata alipowasihi zaidi kuwa huenda alikuwa ametekwa.

Gari ikaanza kuondoka taratibu ikipambana na ule mchanga mwingi wa ufukoni mwa bahari.

Tulivu haikudumu, risasi zikaanza kufyatuliwa kuelekea lilipokuwa gari.

Dokta Kobo, akakimbia kwa kasi sana kuelkea yalipokuwa maji.

Shukrani za dhati zilikuwa kwa tabia yake ya kupenda kufanya mazoezi ya viungo kila siku.

Aliyafikia maji na kujirusha upesi ndani yake. Risasi ziliendelea kurindima huku gari lile ambalo sasa tairi moja lilikuwa limepasuliwa tayari likipambana kujinasua kutoka katika eneo lile.

Akiwa ndani ya maji dokta Kobo aliliona balaa jingine likimnyemelea, aliiona mbwa yenye afya ikijongea kule alipokuwa yeye huku ikibweka sana.

Mbwa ilizama majini, sasa haikuwa ikibwrka tena lakini ilikuwa na usongo wa hali ya juu.

"Come on lazy dog!!" alijisemea huku akijaribu kufanya hichoalichopanga kufanya.

Akaendelea kuyakata maji huku kila mara akikumbuka kuiita ile mbwa.

Alijua hawezi kuendelea kuogelea tu bila kupambana. Na alichokipanga wakati wake ukafika.

Mbwa ikamrukia na kumrarua na makucha yake.

Dokta Kobo akaukumbuka utoto wake akaujumlisha na ujana wake jinsi alivyokuwa fundi katika kukata maji. Wakati akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi alikuwa akiwazidi hadi wanafunzi wa kiume katika kukata maji.

Sasa yu katika maji kwa sababu maalumu sio mashindano ya kawaida ya mshindi kutunukiwa cheti, katika hili mshindi angetunukiwa uhai.

Dokta Kobo anayeyajua maji akavuta pumzi na kutoa nje mara kadhaa kisha akajigeuza na kumweka mbwa chini yake kisha wote wakazama.

Kilichofuata yalikuwa mashindano ya nani awezaye kuzitunza pumzi zake kwa muda mrefu awapo ndani ya maji.

Ni mbwa ama ni dokta Kobo.

Mbwa alisahau kuwa alikuja pale kwa lengo la kushambulia, sasa alikuwa anahaha huku akinywa maji mfululizo bila mpangilio.

Dokta Kobo alikuwa makini katika kuzitunza pumzi zake na wakati huo alimdhibiti yule mbwa asiweze kupanda juu kuvuta hewa.

Sekunde zake za uvumilivu zilipofikia ukomo. Akaiunganisha mikono yake miwili katika shingo ya yule mbwa kisha akairuhusu ile mbwa ifurukute.

Ikafurukuta na kumleta juu, akavuta pumzi za kutosha. Mbwa asiye na akili kama za Dokta Kobo akabaki kuhema hovyo.

Dokta Kobo akazama tena ndani ya maji, na hii ikawa safari ya mwisho.

Alipoibuka alikuwa hai peke yake, mbwa iligeuka mzoga wa ajabu unaoelea ndani ya maji kwa mara ya mwisho.

Dokta Kobo katika kichwa chake mpambano wa uhai ulikuwa haujamalizika nd'o kwanza ulikuwa unaanza.

Aliwaza na kuwazua akaukumbuka ule usemi wa wanamtaa usemao mume/mke si ndugu yako.

Akajaribu kuuhalalisha usemi ule katika hili linaloendelea.

"Ina maana Kobo mume wangu amemuua Nguzu na sasa anataka kuniua mimi kwa sababu nimejua ama?" alijiuliza huku akiendelea kuyakata maji kwa makini kabisa kujiweka mbali na hatari.

Akayakumbuka mema yote waliyoyapitia katika ujana wao, na sasa katika utu uzima huu yasahaulike?? Alijiuliza na kuingiwa na ukakasi mkubwa sana katika kuupata usahihi.

Zubeda!

Jina hili likamshambulia ghafla, akahisi wawili hawa lao ni moja. Wamekolezana kimahaba wamemuua Nguzu na sasa hawataki usumbufu wowote ule wanataka uhuru wameamua kumtokomeza.

"Koboko mume wangu? Hapana.... hawezi kunifanyia hivi mimi." Alijiuliza na kujipatia jibu japokuwa hakutaka jibu lile limuathiri na kuwa jibu la uhakika.

Baada ya kukatab maji kwa juhudi zote na kuamini kuwa yu mbali na ile shari. Alienda hadi ufukweni akajinyoosha na kuvuta pumzi za kutosha.

Hakujua ilikuwa ni saa ngapi na mbaya zaidi hakujua maadui wake walikuwa upande gani kwa wakati ule.

Subira! ndo kitu pekee kilichohitajika kwa wakati ule pale alipokuwa.

Akaendelea kutulia mtaalamu yule wa magonjwa ya moyo.

Dakika takribani arobaini zilitimu bila purukushani yoyote, lakini hapakuwa tulivu zaidi.

Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika maeneo mbalimbali.

Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake, asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila kuanguka.

Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.

Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake katika hili tukio.

Akayafumba macho yake na kutazama angani. Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.

Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.

Miale ikaanza kuonekana, akiwa ametuliapalepale akajigeuza upande wake wa kushoto na kuona kundi la watu wakirandaranda huku wakimulika maeneo mbalimbali.

Daktari Kobo akajipima nguvu katika mwili wake, asingeweza kukimbia walau mita mia mbili bila kuanguka.

Maji yalikuwa yamemdhaifisha sana.

Mapigo yake ya moyo yakaongeza kasi na kujiona kuwa ule ulikuwa mwisho wa ujanja wake katika hili tukio.

Akayafumba macho yake na kutazama angani. Akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana.

Hofu ya kifo ilikuwa jirani yake.

_______

UMATI mkubwa wa watu ulikuwa unasukumana kutazama tukio lile la kustaajabisha.

Huyu alisema hivi yule naye akapinga na kusema vile.

Baadaye majira ya saa nne asubuhi umati ulitawanyishwa baada ya askari kufika eneo lile na kuwasihi wasogee mbali.

Wakiwa wametangulizana na wataalamu wa afya, polisi waliwaacha wataalamu wale wawapatie majibu ikiwa mwili uliolala pale chini ulikuwa hai ama tayari kwa kuzikwa.

Ule ubishani uliokuwa kwa raia juu ya mwili ule ukahamia kwa maaskari watatu, na wao wakaanza kubishana chini chini juu ya mwili ule.

Askari mmoja alisimamia upande mmoja na wawili wakiunganisha nguvu kutetea hoja yao.

"Yupo hai lakini moyo wake unapiga kwa tabu sana." Mtaalamu wa afya alitoa majibu, askari wakafuata taratibu zote na kuuingiza mwili katika gari ya wagonjwa huku wakikumbuka kupiga picha eneo lote ambalo waliukuta mwili ule.

Waliondoka pale na kuucha ubishani ukiendelea, na wale askari nao waliendelea kubishana lakini hii ya sasa ilikuwa katika namna ya utani tu.

Gari likaingia barabarani huku likipiga ving'ora.

Kutoka Kariakoo sokoni hadi Muhimbili sio kitambo kirefu sana hasahasa kwa gari hili ambalo linapishwa njia na magari mengine.

Hivyo hata msafara huu haukuchukua kitambo kirefu kuifikia hospitali.

Mwili ukashushwa huku ukipokelewa na wauguzi. Askari wakiwa bado na wawakilishi wao katika hili.

Hapa sasa hapakuwa na kufananisha tena, ulikuwa ni mwili ulioibeba sura iliyokuwa ikifahamika vyema katika hospitali ile ya taifa.

Sura ya dokta Kobo!

Jina ambalo umaarufu wake sasa ulikuwa umezidi tangu apotee kazini pasi na taarifa yoyote ile, kupotea huku kukakifanya kitengo kinachohusika na masuala ya moyo kupwaya sana.

Dokta Kobo alikuwa mtaalamu sana, lakini ucheshi wake na moyo wa upendo vilimfanya kuacha pengo alipokosekana.

Sasa anarejea akiwa katika machela, hana fahamu na hajulikani kama atapona.

Wauguzi na madaktari walilia huku wakimwombea dua aweze kupona.

Kutokea hospitali ya Muhimbili, simu ikapigwa kwa mume wa dokta Kobo yaani Inspekta Kobo.

SIMU hii ilifika katika wakati mbaya sana. Inspekta Kobo alikuwa amechanganyikiwa mno. Walinzi wa siri aliowaweka kumwangalia mkewe na nyendo zake walikuwa wamemueleza kuwa dokta alikuwa ameshindia siku nzima ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia, walipojaribu kupeleleza chumba kile wanatanabai kuwa dokta Kobo alipitia mlango wa dharula kutoweka ndani ya chumba kile hivyo hawakujua ni wapi ameelekea.

Jitihada za kumsaka zikagonga mwamba.

Asubuhi akiwa bado hajajua nini hatma ya mke wake kipenzi anapokea ujumbe wa kitisho.

"MKEO AMETAPIKA KILA KITU." Ujumbe huu ulimaanisha kuwa mkewe amesema kila kitu.

Kuhusu hili hakushtuka sana kwa sababu alikuwa akimuamini sana mkewe jinsi alivyokuwa jasiri pengine kuwazidi wanaume wengi tu.

Hofu yake ilikuwa usalama wa mkewe ambaye kufikia hapo alijua kuwa alikuwa ametekwa tayari.

Mawazo yake yalizunguka huku na kule na kumlazimisha kuwa watu hao wamemuua mke wake.

"Kama mmemuua mke wangu, mtaijua gharama halisi ya mguu wangu uliopotea kwa sababu ya kupambana..." Akamalizia na tusi lake la kiitaliano. Lakini kwa mara ya kwanza akajikuta akilitoa tusi hilo kinyonge sana.

Inspekta Kobo akagundua kuwa alikuwa yu na uoga wa ajabu mno,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni