KONSTEBO NGUZU (11)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Hata tukio la kukuta pesa katika nguo aliyoianua katika kamba usiku ule baada ya kujinasua katika kifusi katika nyumba iliyokuwa imeanguka bado kilimtatanisha.

"Nani wa kusahau pesa katika nguo ndani ya jiji la Dar es salaam!!"

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
alijisemea na kujikuta akitokwa na tabasamu kubwa sana kulikumbuka jiji lile na vituko vyake.

"Mzee Majenga kuna kitu anapaswa kunieleza, sidhani kama nipo kawaida." aliweka hitimisho lile.

Wakati anarejea katika chumba chake akaanza kumuwaza tena mama yake mzazi.

Nini kinatokea? alijiuliza huku hofu ikianza kumwingia.

Hakutaka kupuuzia hii hisia iliyomjia ghafla, akajiahidi kuwa siku inayofuata atalazimika kurejea jijini Mwanza.

Akarejea katika kile chumba chenye kunguni wapenda sifa. Akajilaza na kusinzia.

Alfajiri ilimkuta barabarani, akadandia gari na kurejea jijini Mwanza.

Ilikuwa kama hisia zake zilivyomuelekeza, alipoingia jijini Mwanza hata kabla hajajikita katika upelelezi wa chinichini akatambua juu ya kamakakamata ya wakazi wa Shamaliwa nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Akajipeleka Shamaliwa kuhakikisha tu!

Mama yake alikuwa mojawapo kati ya watu waliokuwa mikononi mwa polisi.

Cheko la hasira likamponyoka, akatembea hadi katika kituo cha mabasi akajiweka katika basi ndogo iliyokuwa inafanya safari zake kuelekea Nyegezi. Akatulia katika nafasi iliyokuwa wazi. Mkononi akiwa na pesa kamili kwa malipo ya nauli ya kutoka Shamaliwa hadi Mabatini.

Alishuka mbali kidogo na kutembea kwa miguu taratibu hadi zilizopokuwa nyumba za polisi. Nyumba zilezile alizoishi pale miaka kadhaa nyuma.

Nyumba zile zikaikamata akili yake, akaukumbuka ule ugomvi kati ya Janeth ambaye baadaye alibadili jina na kuitwa Zubeda jinsi alivyokwidana na mke wa inspekta na mwisho kujikuta akitupwa rumande kwa siku kadhaa.

Kumbukumbu zaidi za kumwandalia binti yule kifungua kinywa zikamfanya ayakumbuke mapenzi yao motomoto baada ya kukutana jijini Dar es salaam huku Zubeda akiwa ni Koplo na yeye akisalia katika nafasi yake ya ukonstebo.

Tabasamu liliunda kibanda katika uso wa Martin, akatembea upesiupesi hadi katika nyumba mojawapo akaitazama kwa sekunde kadhaa, kisha akapita kwa kasi akaelekea nyumba nyingine, hii nayo akaitazama upesi upesi.

Akafanya vivyo hivyo katika nyumba nane. Baada ya kuridhika kuwa alikuwa makini kabisa kwa kila hatua aliyopita katika makazi yale pasi na mtu kumshtukia akaamua kuzua balaa alilopanga kulizua.

Lilikuwa balaa haswa!

MARTIN Nguzu hakuwa mgeni eneo lile la kota za polisi Mabatini, hivyo hata sasa hakutembea eneo lile kama mgeni.

Udhaifu wa ulinzi aliufahamu vyema na uwepo wa kiwanja cha mpira katika maeneo yale ya kota yalisababisha iwe ngumu sana kwa mtu kupatwa na hisia zozote za kutisha juu ya ugeni wa hapo kota.

Nguzu alilifikia upesi eneo alilohitaji kufikia kisha akatazama kama kuna mabadiliko.

Hapakuwa na mabadiliko ya aina yoyote ile, akatabasamu na kujiwekea alama za ushindi waziwazi.

Majira ya usiku wa saa mbili akarejea eneo lile kwa ajili ya kutekeleza agano lake la kuhakikisha kuwa mama yake anakuwa huru kwa namna yoyote ile.

Wakati huo alikuwa ameanza kupata majibu kuwa mtihani uliopo mbele yake haukuwa mdogo hata nukta.

Mfumo wa umeme eneo la kota ya polisi Mabatini ulikuwa mbovu kupindukia, nyaya za umeme zilipita chini kwa chini katika namna iliyotia kero kutazama.

Wazazi wenye watoto nd'o walijitahidi kupigia kelele hili suala lakini majibu yalikuwa yaleayale ya siku zote.

"Kilio chenu kimesikilizwa!"

Hiki kilio kikaenda miaka nenda rudi huku kikigeuka kuwa kichekesho na si kilio tena.

Hakuna jema lililoboreshwa.

Kama nyumba zenyewe zinatia kichefuchefu vipi kuhusu huo umeme??

Nguzu aliikuta hii hali katika safari yake ya kutoka kuzimu na kurejea tena duniani na sasa yupo katika ile ardhi aliyozaliwa miaka mingi iliyopita.

Zile kota za polisi alizoziona angali akiwa anasoma, sasa hazitamaniki zinazidi kukera kuzitazama.

Anarejea katika anga zile kwa sababu maalumu.

Anatazama pande zote na kuzichimua kwa umakini zile waya. Akautazama uelekeo na kuchagua dakika ya kufanya balaa alilopanga kulifanya.

Akazihesabu dakika akachuchumaa kisha akaziachanisha nyaya kadhaa.

Giza likaingia katika eneo lile ghafla.

Sauti za manung'uniko zikasikika huku na kule.

Manung'uniko yale hayakudumu kabla Nguzu hajazua taharuki kubwa.

Akazigusanisha zile waya na hapo mlipuko mkubwa ukasikika eneo la chooni.

Akatimua mbio na kwenda upande mwingine na huko akagusanisha nyaya ukatokea mlipuko wa kushtukiza eneo ambalo zamani lilikuwa likitumika kama bwalo la chakula.

Sasa hali ikawa mbaya, wapo waliotoka nusu uchi ndani ya nyumba zao, wengine wakabeba vigoda badala ya watoto.

Hali ilikuwa tete!

Nguzu naye akachanganyikana katika ile taharuki na kujifanyaamepotea njia, akaingia katika nyumba mojawapo ambayo watu walikuwa wametoka kwa hofu.Akaikwapua simu na kuondoka nayo, upesiupesi akaitumia simu ile ya upepo kutoa taarifa ya kutisha kwa maneno machache mno.

"NINGEWEZA KULIPUA HIZI KOTA NA KUUA KILA KIUMBE HUMU NDANI. SIJASHINDWA ILA NI SALAMU TU. WAACHWE HURU WOTE WALIOKAMATWA BILA MAKOSA. OVA!"

Hakujitambulisha jina akaiacha simu ile ikizungumza peke yake huku akiuliza yeye ni nani.

Kama salamu za kivita hii ilikuwa imetangazwa katika namna ya kutisha kutoka kwa adui.

Ule upande uliofanya ukatili huu wa kuwakamata watu wasiokuwa na hatia ukaanza kutetemeka huku kila mmoja akijutia maamuzi haya ya ajabu.

Na hapo likaongezeka swali jipya juu ya adui mpya aliyejiamini kiasi kile cha kupitiliza akavamia kota za polisi na kuchafua hali ya hewa.

Wakati wanaukosa usingizi, Martin Nguzu alikuwa amelala katika nyumba ya kulipia yenye hadhi ya kawaida.

Uzuri wale ndugu zake wa Shinyanga hawakumtembelea usiku huu.

Hapakuwa na Kunguni!

______

GARI iliingia kwa mwendo wa kawaida na kulikaribia geti la nyumba aliyokuwa akiishia Juma Kihwele. Namna gari ilivyoingia haikutisha hata kidogo, lakini namna alivyoshuka aliyekuwa ndani ya gari ndiyo iliyovuta umakini wa watu waliopendezwa na kujua yasiyowahusu.

Ni wachache tu yaliwahusu.

Alishuka mwanamama na kuubamiza mlango, kisha kwa mwendo wa harakaharaka alitembea kulielekea geti kuu la kuingilia ndani.

Mlangoni akamkuta mlinzi, kwa mbali wakaonekana kuzozana. Mlinzi anamzuia asiingie naye analazimisha kuingia.

Mlinzi akazidiwa nguvu, yule mama akaingia mbiombio ndani ya ile nyumba.

Akaufikia mlango na hapo akakutana na mwenye nyumba.

Ujio ule wa ghafla ukampagawisha Juma Kihwele. Lakini hakupata nafasi ya kujiandaa kabla yule mama hajamvamia na kumkwida shati lake.

"Nipatie pesa zangu Kihwele, muda huu nazihitaji." Alikoroma yule mama aliyekuwa na misuli imara.

Juma Kihwele huku akitweta akajaribu kumtuliza yule mama, lakini ilikuwa kazi bure kabisa. Mama alizidi kufoka kwa sauti ya juu sana. Hatimaye mke wa Juma akatoka akiwa amembeba mtoto wake. Kulikuta sakata lile akamtua mtoto wake na kuingia katika tukio lile moja kwa moja.

Wivu wa mapenzi!

Hicho ndo cha kwanza kilichovamia kichwa cha mke wa Juma!

Mke mwenza...

Hili nalo likamvamia na kumsulubu, ni kitu ambacho hakutaka kitokee japokuwa dini ilikuwa inaruhusu kabisa. Lakini ingekuwa kwa amri yake angezuia hili jambo kwa mume wake pekee, kwa wengine angeliacha kama lilivyo.

"Huyu ni nani Juma?" Aliuliza kwa shari kiasi.

Juma akashindwa kujibu.

"Wewe ni nani mama, na nini kinatokea hapa?" Akamgeukia yule mwanamke mpenda shari.

"Naitwa Dokta Kobo, ninamdai mumeo. Naomba anipatie pesa zangu nijiondokee hapa." Alijibu kwa kirefu.

Juma Kihwele akafanya kosa kubwa kupinga kuwa hadaiwi kitu chochote na yule mwanamke.

Dokta Kobo hasira zikamjaa, akamkwida vyema zaidi Juma. Na hapa sasa ukazuka ugomvi, mlinzi akasogea eneo la tukio kwa ajili ya kumsaidia bosi wake.

Kuona kuwa wanaompinga wamekuwa wengi, Dokta Kobo akaingiza mkono katika pochi yake kubwa kiasi. Akarudi nyuma na hapo akatoa bunduki.

Wacha wee!

Wivu ukasahaulika, ubabe wa mlinzi nao ukaenda likizo huku rungu lake likimtoka mkononi, Juma akakaza mwendo wakamfuatia wenzake wakitimua mbio. Huyu akiita mama yule anaita Mungu wangu na mwingine haongei.

Mbio!

Dokta Kobo akamtazama vyema Juma Kimbelembele anavyokimbia kwa uoga huku akipiga mayowe, ndani ya sekunde chache akayahesabu maovu yote kutoka kwa bwana huyu na hapo akaufikia uamuzi wa kumuhukumu.

Akaielekeza silaha yake kule alipokuwa Juma Kimbelembele, kisha akaanguka chini na kutua kwa kutumia goti moja, akamweka Juma katika shabaha. Vilevile kama alivyowahi kufundishwa na mume wake ambaye ni ana cheo cha inspekta katika jeshi la polisi.

"Kafie mbele mwanaharamu mkubwa wewe..." Likamtoka neno lile na kisha akakifikia kitufe cha kufyatulia.

Mlio mkubwa ukasikika!

_______

GIZA lilikuwa limetanda wakati fahamu zikirejea kinyonge katika mwili wa dokta Kobo. Alijihisi maumivu kwa mbali lakini alipojipapasa hakuwa na jeraha.

Akatulia kwa muda kisha akakumbuka kwa juhudi zote ni wapi alitoka hadi kulifikia giza lile.

Kama kawaida yake hakuwa mwenye papara, hili ni moja kati ya jambo lililopelekea inspekta Kobo kumtolea mahari upesi na kumuoa moja kwa moja.

Akazikusanya fikra zote na tabasamu hafifu likamtoka.

"Nimetekwa!" alijisemea huku akijiandaa kukabiliana na huo ukweli.

Akaukumbuka mlio mkali wa risasi uliopelekea ashindwe kukivuta kitufe cha kufyatulia na kumwondoa duniani Juma Kihwele.

Kwa maksudi akaanza kukohoa ili wenyeji wake waweze kujisogeza karibu yake.

Kimya! akabaki kuusikia mwangwi wa kikohozi chake mwenyewe.

Akakohoa tena, bado hali ilikuwa ileile.

Akasitisha zoezi lile akasimama na kuanza kupapasa gizani akijaribu kutafuta mwanga wa kutoka katika eneo lile ikiwa ni kweli hajatekwa.

Aliendelea kupapasa bila kukutana na kitu chochote kile.

Akajipapasa na kukuta amepungukiwa bunduki pamoja na mkoba wake. Akatambua wazi kuwa alikuwa amepekuliwa. Hakuwa na hofu kubwa.

Hiyo ilikuwa ni asili yake. Katika kazi yake ya udaktari alishuhudia wagonjwa wengi wakipoteza maisha, wengine mikononi mwake wengine katika mikono ya madaktari wengine.

Hivyo hakuwa akikihofia sana kifo. Alijua ipo siku atakufa...

Na sasa alijiona katika mdomo wa kifo. Aliendelea kutembea zaidi akipapasa huku na kule.

"Ni akina nani hawa? na wanataka nini?" Alijiuliza huku akiendeleza bidii katika kupapasa.

"Mamaaaaaa!" kelele kubwa zilisikika ghafla mbele yake na hapo akasikia vishindo vikiambaa kwa kasi.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni