
Mtunzi: George Iron Mosenya
SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Huyu alikuwa mrefu wa haja mweusi na ambaye alionekana kuwa mwingi wa mazoezi kwa jinsi umbile la kifua chake lilivyogawanyika.
"Nguzu, hapa nd'o ninapojilaza walau siku ziende..."
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Alizungumza mwanadada ambaye Nguzu alipaswa kumtambua kama Zubeda na kusahau kabisa kama aliwahi kulijua jina la Janeth maishani mwake.
Nguzu alikuwa amejiandaa kisaikolojia kuanzia awali kuwa yule Janeth wa Mwanza aliyeswekwa rumande kwa sababu ya kumzongazonga mke wa inspekta atakuwa amebadilika mno. Lakini hakudhani kuwa angeweza kuwa anaishi katika nyumba nzuri kiasi kile, kuendesha gari zuri namna ile.
Umbo lake nalo lilikuwa limenoga, hakuwa yule kimbaumbau wa Mwanza mabatini.
Mate ya matamanio yakamruka Nguzu.
Akatamani gari, akatamani nyumba na maisha mazuri kwa ujumla.
Lakini angeyapata kwa wepesi gani ilihali alikuwa amegotea katika cheo cha ukonstebo katika jeshi la polisi na hapo alikuwa na majukumu lukuki yaliyojua kuutafuna vyema mshahara wake mdogo kila ulipokuwa unaingia.
Alipoingiza mguu wake sebuleni akazidi kughafirika, maisha ya Zubeda yalikuwa yanamkera si kwa sababu ni mabaya la! alikuwa na maisha mazuri kupindukia.
Akajaribu kuanza kujifananisha naye walau kidogo, Zubeda anamiliki luninga bapa yeye anamiliki ile modeli ya zamani yenye kisogo mfanowe mlima kilele cha mlima Kilimanjaro.
Nguzu akasonya na kupuuzia uwiano aliotaka kuuweka.
"Huenda ameolewa na kibopa hapa mjini! Acha matamanio Nguzu!" alijionya Nguzu na hapo akamuuliza Zubeda juu ya masuala ya mahusiano.
Upesi Zubeda akajibu kuwa hajaolewa na hatarajii kuolewa hivi karibuni.
Matamanio ya Nguzu yakarejea upya!.
"Njoo uione nyumba yangu Martin, Konstebo Martin Nguzu!" Zubeda akaiga namna Nguzu alivyokuwa akijitambulisha.
Nguzu akatokwa na cheko la haja!
Wakapita huku na kule hadi wakakifikia chumba cha Zubeda. Hapa ndipo Nguzu akahisi kuwa Zubeda ni mwongo tu hakuwa akiishi peke yake, na hii ni baada ya kuiona sare ya jeshi la polisi katika chumba kile.
"Hivi wanawake wataacha lini uongo wao jamani! kwani akiniambia kama ameolewa mimi nitapoteza fahamu ama?" Alijiuliza huku hamu ya kukisaili chumba ikimwisha.
"Zubeda una uhakika haujaolewa?" Kwa ghadhabu kiasi fulani akahoji.
"Eeh! sijaolewa vipi unataka kunitolea mahari." akajibu na kutupa utani juu yake.
"Na hizo sare.." Akahoji huku akikodoa macho ya kumsuta Zubeda.
"Ooh! sijakueleza kumbe, unapaswa kunipigia saluti Konstebo Martin Nguzu, mimi ni koplo Zubeda Msangi." alijibu kiuchangamfu sana.
Nguzu akabaki mdomo wazi, moyo ukaingiwa uchungu asiamini kuwa yule binti ambaye miaka kadhaa nyuma hakuwa akijua hata nini maana ya Konstebo leo hii ni Koplo. Cheo kimoja juu yake.
"Nadhani mwakani naweza kuwa ssajenti kama Mungu akipenda!" Alimalizia Zubeda.
Mungu akipenda?? akajiuliza Nguzu, ina maana Mungu haoni kuwa mimi ninahitaji zaidi kuliko huyu mwanamke au? akajiuliza katika nafsi yake na asipate majibu mjarabu.
Zubeda akatoa picha mbalimbali na kumwonyesha Nguzu, siku akiwa anaapa na picha kadhaa akiwa mafunzoni.
Nguzu akapwaya!
Kumbe kweli!! Akagutuka
Akapigia mstari kuwa hana hadhi yoyote mbele ya Zubeda.
Kikubwa alichomzidi ni kwamba yeye alikuwa mwanaume na Zubeda mwanamke, lakini hata akijitoa ufahamu kuhusu hilo bado Zubeda naye angejitapa kuwa yeye ni mwanamke na Nguzu hajawahi wala hatakuja kuwa mwanamke.
Nimepatikana leo! Alikiri Nguzu huku kijasho chembamba kikiulowanisha mgongo wake.
Bahati iliyoje kiyoyozi kilikuwa kinapepea, la sivyo kile kijasho cha usoni kile kinachoibuka ghafla mtu akiwa katika taharuki kingemuumbua Nguzu.
Zubeda alijitahidi kadri alivyoweza kumfanya Nguzu ajisikie yu huru lakini haikuwa heri katika moyo wa Nguzu.
Lakini jitihada za Zubeda kuujenga ukaribu baina yake na Nguzu hatimaye ile safari yao ambayo ilianzia jijini Mwanza ikafikia palipotarajiwa.
Ilikuwa ni siku nyingine ya kukutana kwao, walianza kwa kukumbushiana juu ya lile sakata la shida ya maji kota za polisi jijini Mwanza wakaunganisha na sekeseke la Zubeda kukabana na mke wa Inspekta. Wakafikia lile tukio la Nguzu kujitolea kumsaidia Zubeda kuanzia maji ya kuoga na baadaye chai.
Sasa Zubeda akamtaka Nguzu amtengenezee tena chai, Nguzu akafanya zaidi ya chai akampikia Zubeda ugali wa dona, nyama na mboga za majani.
Pishi likamnogea Zubeda akajikuta anataka tena na tena......
Mwishowe mapishi yakawa mapishi.
Uhusiano wa kimapenzi ukaibuka.
Lakini ulikuwa uhusiano wa kisasa uliotawaliwa na lugha za kisiasa.
Uliojaa masharti lukuki.
"Martin, sina la kukuficha safari yangu hadi hapa nilipo imetawaliwa na mikato mingi. Hadi sasa ninajihusisha kimapenzi na mume wa mtu, sio kwamba ninampenda kwa dhati ila nitakosa adabu nikisema kuwa simuheshimu. Ninamuheshimu sana moyo wangu unanishuhudia katika hili. Ujue niliwapuuzia vijana vijana hawa ama niwaite watoto, wao wanachoweza kukufanyia kwa ustadi mkubwa ni kukuburudisha mwili tu lakini kwenye masuala ya maisha wanakudumaza. Halafu wanabana sana yaani, ikitokea amekulipia kodi basi anataka kila siku aje kuifaidi kodi yake chumbani... looh!" Martin Nguzu akajikuta anatokwa na kicheko kwa jinsi Zubeda alivyokuwa analalamika.
Ni kweli lakini haikuwa masihara!
"N'do hivyo Martin yaani inafikia hatua unajuta, na vile damu inachemka anaweza akakuvunja mgongo. Nikaona hapana siwezi, nikajiweka kwa kile kibabu kina pesa na kuja hapa ni mara moja moja..... Jiulize Martin, kibabu kimenitafutia cheti cha fomfoo kwa jina hili la Zubeda, kimepambana nimeenda jeshini, kimepambana sijapitia msoto jeshini na hatimaye nimepata kazi. Kwanini nikidharau..... nakuapia kwa mizimu yote Martin, katu sijawahi kujihusisha na mapenzi na mwanaume mwingine tangu nianze kuwa na Inspekta. Wewe unakuwa wa kwanza tafadhali nakuomba sana usije ukaniharibia, usijekuwa kama vijana wenzako wanaopenda ngono kama walitangaziwa kuwa ukifanya sana unaongeza umri wa kuishi....." Akamalizia kwa utani kisha akampiga busu baridi kabisa Konstebo Nguzu katika papi za midomo yake.
Konstebo akajiona yu daraja moja na inspekta ama ikibidi hata mkuu wa majeshi.
Busu pekee!
Mahusiano yakaanza.
Hawakuliona giza lililokuwa linawanyemelea.
Wakapumbazwa na mwanga wa mwishomwisho wa mshumaa!.
Mbaya zaidi Nguzu hakutaka japo kulijua jina la inspekta ambaye anammiliki Zubeda.
Penzi likanoga Nguzu akambatiza Zubeda jina maridadi la kimahaba. Jina linalotamkika kwa sauti tulivu ya kiume na kuleta hamasa panapo faragha.
Akamuita Zuu!
_____
MUHARIRI wa gazeti la SIRI KALI alikuwa akiiendesha gari yake kwa mwendo wa kasi isiyohatarisha maisha yake ili awahi nyumbani. Kuna kitu alihitaji sana kupata uhakika kama kinaenda sawa na anavyodhania.
Ilikuwa kawaieda yake kutopenda kuwa mtu wa kuacha mambo juu juu kama ilivyokawaida ya wengine. Tangu akiwa shuleni alitambulika kwa waalimu wote kutokana na usumbufu wake, alikuwa hakubali kitu kimpite asikielewe kisha akae kimya tu.
Aliwasumbua sana waalimu kiasi kwamba ada yake ilikuwa inakwenda kihalali kabisa.
Tabia yake hii ikaendelea hata katika utu uzima wake akiwa kazini, aliifanya kazi yake kiustadi pasi na kubahatisha na pale alipohisi kuna utata aliwahi kutafuta uhakika kwa wanaojua zaidi yake.
Kutokana na gazeti alilokuwa anafanyia kazi kujihusisha sana na masuala ya siasa muhariri huyu alijiundia urafiki na na vitabu vya siasa ya afrika na dunia kwa ujumla lakini hakuwa mbali na masuala yahusuyo jeshi la polisi ambalo aligundua kuwa lipo jirani sana na siasa kuliko majeshi ya nchi za bara la ulaya ama Amerika.
Utendaji kazi wake wa kiwango cha juu ukamsababisha apewe jina ambalo hakuwahi kulisikia waziwazi zaidi ya tetesi pekee.
Wafanyakazi wenzake wakamuita Juma kimbelembele badala ya jina lake la kuzaliwa Juma Kiwele.
Hakujali maisha yakaendelea.
Alipofika nyumbani akabadili nguo zake na kisha bila kupumzika akamuaga mkewe akaondoa hadi mtaa wa tatu, akaimalizia safari yake kwa mzee wa kale ambaye alikuwa na rundo la magazeti ya miaka ya nyuma. Kuna kitu aliwahi kukiona akahitaji kukiona tena kiuhakika.
Mzee akamwachia ukumbi, akafukunyua kwa juhudi bila papara hatimaye akalipata gazeti la mwaka 1982. Kuna waraka ulikuwa umechapishwa.
"Kwa macho yangu nilitazama mwanangu wa kwanza akiuwawa mbele ya macho yangu, niheri angefyatuliwa risasi moja na kupoteza uhai. Alinyanyasika kabla ya kupoteza uhai, walimkata sikio lake ili akiri kuwa tumehifadhi bunduki ndani ya nyumba yetu, walimvunja magoti yake ili akiri kuwa sisi si raia wa Tanzania. Roho iliniuma sana haswa nilipokumbuka zile harakati za kugombea uhuru angali nikiwa kijana mbichi sana, nilipigana kufa na kupona kwa ajiri ya nchi yangu leo hii mwanangu anavunjwa miguu ili akiri kisichokuwa na ukweli. Sikuwa na la kufanya, akapoteza maisha wakatangaza kuwa alijaribu kutoroka akatandikwa risasi akapoteza damu nyingi kabla ya kugeuka maiti. Haikutosha hii, wakamwendea mke wangu kipenzi, bahati nzuri kwake hakupitia mateso bali alipoteza maisha baada ya kugundua kuwa mwanaye angali mfu!
Sikuwahi kuwa na bunduki lakini sasa ninayo, sikuwahi kuwa na roho mbaya lakini niliyonayo ninakaribiana na ibilisi, ninapoandika waraka huu bila kujalisha kuwa utachapishwa ama la nitakayoyafanya naomba nisilaumiwe na ninajua kuwa ipo siku nitakufa. Mkibahatika kuyaona maitiyangu na myape adhabu kwa kushindwa kuwa na moyo wa kusamehe!
Wakati mnayaadhibu maiti yangu mjiulize kila mmoja kwa nafsi yake.
Je? ungelikuwa wewe ungelistahimili uliyoyashuhudia??
Walidhani mimi ni mfu kwa mabaya waliyoutenda mwili wangu, lakini Mungu akawa upande wangu nikabaki hai...
Florian Ngengekuzenza Nguzu, 1982."
Waraka ule wa aina yake ukakomea pale, na baada ya hapo ukimya ukatanda mpaka miaka mitatu baadaye ambapo liliibuka kundi lililotikisa nchi, ujambazi ukakithiri utekaji na mambo yote ya kutishia amani.
Waraka ule ukiwa umesahaulika mmoja kati ya watekaji anakamatwa anabanwa na kusema kuwa kiongozi wake anaitwa Nguzu Ngengekuzenza lakini katu hajawahi kumtia machoni.
Msako unapita lakini hakuna walichoambulia. Hakuna aliyetambua ni wapi mzee yule alikuwa amejificha....
Mtindo wa matukio aliokuwa akiutumia Ngengekuzenza ambaye alisadikika kuwa mkuu wa oparesheni hiyo isiyokuwa na jina ulikuwa mtindo wa akili nyingi kuliko nguvu. Wakilinda huku analipua kule,
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi