KONSTEBO NGUZU (5)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA TANO
ILIPOISHIA...
Akapanga kukabiliana na hili jambo kabla halijakomaa, akasimama imara akapiga saluti na kujiapiza kuwa hatalala tena na kulialia kama mtoto badala yake atapambana kiume.

Hakujua kuwa wakati yeye akiamua kusimama, kuna ambao walikuwa wakikimbia mbio kali kwa nia ya kumzamisha katika shimo lenye kiza kinene.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
"WAKATI mzuri zaidi wa kufanya mabadiliko katika maisha yako ulikuwa ni miaka kumi iliyopita..... WAKATI mwingine mzuri zaidi ni SASA! Usije ukathubutu kusema kuwa umechelewa kufanya mabadiliko katika maisha yako......fanya SASA"

ALIJARIBU kujiaminisha kuwa huenda amesikia vibaya, akazidi kujikunja kitandani ili asinzie vizuri. Lakini mlango ulipiga kelele tena, kuna mtu alikuwa anaugonga.

Akiwa na mawenge ya usingizi aliufikia mlango na kuufungua bila kuuliza ni nani alikuwa anahitaji kuingia. Hakuwa katika fahamu zake taslimu.

"Nani?" aliuliza baada ya kuwa ameufungua mlango na kukutana na kiza kinene.

Badala ya kujibiwa akasukumwa ndani, kisha tochi kali ikayamulika macho yake akashindwa kutambua kunani mbele yake.

Akajaribu kutokwa na pigo la 'Karate' aliyojifunza akiwa kambini lakini akaishia kupiga ukuta na kutokwa na ukelele wa maumivu.

Mwanga ule ukapotea na kisha taa ya chumbani kwake ikawashwa. Akayapikicha macho yake na hatimaye aliweza kuona ni nani alikuwa mgeni wake asiyetoa taarifa.

Mkojo ukatoka mbio katika kibofu usiangalie kuwa pale si maliwatoni ama msalani. Ulipofika karibu na mlango wa kutokea ukamstahi.

Haukutoka!

"Nguzu, mbona unawahi sana kulala." Ilikuwa sauti tulivu kabisa ya Inspekta Kobo ndani ya nyumba anayoishi Konstebo Nguzu.

Konstebo Nguzu aliishiwa hamu zote, akabaki katika hali isiyoeleweka.

Inspekta Kobo akaketi. Nguzu akajilazimisha akapiga saluti.

"Nguzu, ni masaa mangapi yamepita tangu tuzungumze?" aliuliza kwa utulivu uleule. Kabla Nguzu hajajibu yeye aliendelea.

"Umenogewa na mali yangu ama? Yaani kweli nimekuita kwa upole na ustaarabu wa hali ya juu kiasi kile lakini kumbe usiku huu umepanga tena kukutanana Zubeda! Mbona unanifanyia hivyo konstebo...." Alizungumza kwa kulalamika Inspekta.

Nguzu kimya!

"Naomba unitazame machoni wakati unajibu swali hili." Akasita kisha akaendelea baada ya NGuzu kumtazama.

"Unampenda Zubeda kwa dhati ya moyo ama unampenda kwa sababu ni yule mwanamke ambaye hawezi kukulilia shida badala yake wewe nd'o waweza kumlilia shida?" Swali zito likamponyoka inspekta Kobo.

Nguzu akabaki kimya tena huku akionekana wazi kuzidiwa na uzito wa swali lile na pia alikuwa hajaizoea hali ya inspekta kuwa ndani ya nyumba yake.

"Martine Nguzu kwa kumbukumbu zako unafahamu inachukua muda gani kupanda kutoka cheo kimoja kwenda kingine katika jeshi la polisi?"

"Miaka mitatu.." Sasa alijibu huku amani ikiwa imetoweka.

"Unajua kuwa yaweza kukugharimu miaka walau kumi na nane kufikia cheo changu.... lakini mimi sikutumia miaka kumi na nane kuwa inspekta, nilifanya makubwa sana... nilikuwa nina roho mbaya mno na nilikuwa nikiikamata bunduki nakuwa shetani kamili." akaupitisha mkono wake na kuichomoa bastola yake kutoka mahali alipokuwa ameihifadhi.

Sasa Martin Nguzu aliweza kuzungumza hata ambayo hajaulizwa. Mara aseme Zubeda ndiye alimlaghai mara aseme hatarudia tena...

"Sina maana mbaya kuiweka bastola hii katika mkono wangu, ninajaribu kukueleza na unielewe vyema. Ningekuwa nimekuvamia hapa kwako kwa sababu unahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya ama ujambazi, muda huu mguu wako mmoja ungekuwa unasubiri muda tu ukakatwe. Lakini sipo hapa kupambana na wewe Nguzu nipo hapa kukusihi tu, kama inawezekana naomba uniachie Zubeda wangu, nasisitiza ninajaribu kukusihi tu na wala sio kukulazimisha. Niachie huyu binti, amepitia mengi magumu nimejaribu kuitafuta furaha yake walau kidogo tu, nimewaumizawengi kwa kutumia bunduki sitaki kuumiza tena kwa kutumia moyo." akasita na kumwomba Martin maji ya kunywa, bahati nzuri hayakuwa mbali.

"Konstebo mfano mimi najitoa katika maisha ya Zubeda nakuachia wewe, je? utaweza kumjazia mafuta ya gari lake? utaweza kumnunulia nguo za gharama kiasi kile, utaweza kumbadilishia samani za ndani ya nyumba yake? utaweza kuwalipa wafanyakazi wake? Utaweza Nguzu?. Kama jibu ni hapana basi nikikuachia Zubeda kuna watu watakuja kukusaidia majukumu nawe utajikuta unaumia moyo huku ukilia kama mtoto.

Kwanini nikuache uyapitie hayo sasa.... kwanini nikuone upo katika njia mbovu nisikueleze ukweli. Nguzu kama Zubeda anakueleza ukweli, atakuwa amekueleza kuwa ninaenda kwake mara ngapi na ninashiriki naye tendo mara ngapi..... nadhani huwa anahisi mimi nimezeeka, ila sijazeeka Nguzu nipo imara mno tatizo ni moja tu, sio ngono iliyoniweka pale..... sio ngono Nguzu" Akashindwa kuendelea kuzungumza, chozi la mtu mzima likaiangukia sakafu ya Nguzu.

Huruma kali ikamshika Nguzu, akataka kusema neno lakini Inspekta akamzuia na hapo akaaga na kuondoka zake bila kuhitaji hitimisho.

Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa Nguzu, akaitazama saa yake tayari ilikuwa saa nne kasoro dakika chache usiku.

_____

JUMA KIHWELE alikuwa nje akipunga upepo huku akingojea kwa hamu simu kutoka kwa Koplo Zubeda ili waweze kumaliza zoezi lao. Alikuwa nje kwa maksudi makubwa, hakutaka mkewe ajue kuwa ameendelea na ule mpango wa kuitumia ile habari ya Zuu kujihusisha na wanaume wawili kujiingizia kipato jambo ambalo mkewe hakuwa ameliunga mkono kabisa.

Kila mara alitazama simu yake kama kuna ujumbe wowote kutoka kwa Zuu, lakini hadi majira ya saa tatu usiku bado hali ilikuwa ya ukimya. Moyo wa subira ukaanza kuingiwa uchovu akafikiria kumpigia simu na kumchimba mkwara kuwa iwapo hatafanikisha kuonana kwao basi asimlaumu pakikucha.

Akiwa katika kusubiri kule akaliona gari likipaki eneo fulani jirani na upeowa macho yake kisha akashuka mtu ambaye anamfahamu vyema.

Kimbelembele kikachukua nafasi yake. Akataka kuhakikisha kuwa anamfahamu vipi mtu yule.

Inspekta! akastaajabu.

"Jamani si inspekta Kobo huyu." akajiseme huku akisubiri kuona anaenda uelekeo gani, alipopita naye akafuata nyuma. Moyoni alijua wazi kuwa Zuu atakuwa amemweleza kila kitu inspekta, ile mipango yake ya kuvuna chochote kitu akaiona inapoteza uelekeo.

Macho yake yaliyolizoea giza yakamwona inspekta akienda moja kwa moja nyumbani kwa Martin Nguzu.

"Wanaenda kukubaliana nini hawa viumbe eeh!" alijiuliza hukiu akitamani kujisogeza hadi jirani na ile nyumba aweze kuvuna mawili matatu. Lakini alihofia kufumaniwa kisha kudhalilishwa.

Akarejea ndani ya nyumba yake, alipofika nakuiona kamera yake akapata wazo jipya.

"Hawa wawili wanajihusisha na mwanamke mmoja, kwa namna yoyote ile kuna namna fulani ya kutoelewana itajitokeza. Na kama wakipigana basi nitanasa picha nyingine muhimu kwa ajiri ya gazetini." Wazo hili jipya likamfanya atoke nje na kamera yake akaenda hadi chini ya mti akaketi huku akiiona vyema nyumba ya Nguzu.

Kiupepo chenye ubaridi wa wastani kikaungana na mawazo tele ya Juma Kihwele na kuunda usingizi.

Jumaakajikutaamesinzia akiwa eneo lile.

Alikuja kushtuka baada ya kusikia makelele... akakurupuka akidhani kuna wizi umetokea mahali.

Macho yake yakakutana na moshi ukifuka katika nyumba ya Nguzu.

Nyumba ilikuwa inatetekea katika namna ya kutisha sana. Moshi mweusi tii uliichafua anga.

Mungu wangu! akahamaki Juma, kisha akaiweka sawa kamera yake na kwenda kupiga picha kadhaa jinsi tukio lilivyokuwa likiendelea.

Moyo wake ulikuwa unadunda sana. aliulaumu usingizi uliompitia chini ya mti na kusababisha asiweze kuona tukio lilitokea katika mazingira ya namna gani.

Akatimua mbio mpaka pale lilipokuwa limeegeshwa gari alilokuja nalo Inspekta. Hapakuwa na kitu.

"Inspekta amemchomea ndani Nguzu?" alijiuliza Juma huku akiwa na kimuhemuhe kipya kuliko kile cha awali cha kugundua kuwa wawili hawa wanajihusishakimapenzi na mwanamke mmoja.

Magari ya zimamoto hayakufika usiku ule... nyumba ikateketea yote na kusalia majivu.

Juma alirejea nyumbani kwake akiwa hayuko sawa kabisa, alimfikiria mkewe na kutaka kumshirikisha juu ya kitu kilichokuwa kimetokea lakini alikumbuka majibu yake wakati anataka kufuatilia mkasa ule yalivyokuwa. Akasita kumshirikisha, hili la sasa lilikuwa zito mno na lingeweza kumtia hatiani angefanya kuliropoka.

"Kwa hiyo kulikuwa na watu ndani?" Mkewe alimuuliza juu ya hiyo nyumba iliyoungua, kwani tayari alikuwa amesikia kwa majirani na alijua wazi mumewe hawezi kupitwa na habari ile.

"Yaani hapa sina moja wala mbili." alijibu kwa ufupi. Na hakutaka kuzungumzia tena jambo lile akaingia bafuni kuoga kisha akalala.

Kitu cha kwanza asubuhi ni kujua kama habari ile tayari imepata mwanga.

Naam! Ikatangazwa kuwa nyumba imeungua kwa chanzo ambacho bado hakijajulikana na inasadikika kuwa askari mmoja amepoteza maisha akiwa ndani ya nyumba hiyo.

Nambari ya askari yule ikatajwa na kisha jina likatambuliwa baadaye.

Konstebo Nguzu alikuwa katikati ya moto ule na alikuwa ameangamia.

_____

Taarifa hii ya habari ikasikilizwa na masikio ya Koplo Zubeda Msangi aliyekuwa anaendesha gari lake kuelekea nyumbani kwa Nguzu ambaye alikuwa hapatikani katika simu ilihali walipanga kuonana usiku ule.

Zubeda akiwa amevimba kwa hasira alikuwa anaenda kumlaumu waziwazi Nguzu kuwa si mtu anayejali hata chembe.

Kulisikia jina lake likitajwa kuwa hayupo duniani tena, Zubeda akajikuta akikanyaga pedeli ya kuongezea mwendo wa gari badala ya kupunguza mwendo na mara akajikuta akikwepa kitu asichokijua gari ikatumbukia mtaroni, Zubeda ambaye hakuufunga mkanda wake akajibamiza katika kioo na kupoteza fahamu palepale huku damu nyingi ikimtiririka.

Kwa sababu ilikuwa asubuhi, askari waliokuwa barabarani waliwahi sana kumtambua koplo Zubeda ambaye alikuwa ndani ya sare zake za kazi. Simu za upepo zikapigwa upesi kutoa taarifa ile.

"ANZIA hapo ulipo, TUMIA hicho ulichonacho, FANYA kile unachoweza...."

KILIANZA kitanda kumsaliti, kila mtindo aliojaribu kukilalia ukagoma kumburudisha. Akastaajabu kitanda chake mwenyewe lakini amtii. Akasimama wima na kukitazama kwa sekunde kadhaa jinsi kilivyokosa nidhamu.

Akaondoka bila kukiaga na kuelekea sebuleni,huko akajibwaga katika kochi kubwa lililokuwa sebuleni, hili likampokea vyema na ule mbonyeo ukamfurahisha.

Heri yako bado unanitii! akajisemea, huku akiukunja mguu wake na kujaribu kuvuta taswira ya kitu kilichomfanya ashtuke usiku wa manane na kuanza kubabaika.

Moshi mnene! hiki nd'o kitu kilichokuwa kikitishia afya ya akili yake kwa wakati ule.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni