KONSTEBO NGUZU (6)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA...
Heri yako bado unanitii! akajisemea, huku akiukunja mguu wake na kujaribu kuvuta taswira ya kitu kilichomfanya ashtuke usiku wa manane na kuanza kubabaika.

Moshi mnene! hiki nd'o kitu kilichokuwa kikitishia afya ya akili yake kwa wakati ule.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Akainyanyua simu yake na kujaribu kupiga katika nambari alizokuwa amepiga awali na hazikuwa zikipatikana.

"Ni kweli Sule anavuta bangi tena sana tu, lakini sidhani kama bangi yake inaweza kumfanya akafanya upuuzi mkubwa namna hii..." Akajisemea huku akiketi.

Alipoketi na kuwa kimya kwa muda kidogo akakumbwa na kitu ambacho kilimfanya ashindwe kuketi bali kusimama wima kabisa.

Kuna vitu viwili vilikivamia kichwa chake, ulikuwa ni mfano wa picha ambazo zilikuwa gizani na sasa akabaini kuwa aliziona lakini pasi na uhakika.

Picha ya kwanza ilikuwa ni mtu chini ya mti.

Ni nani yule? akajiuliza huku akijilazimisha kuing'arisha picha ile katika kumbukumbu zake.

Haikung'aa!

Picha ya pili ni ya mwanaume akizungumza, na haikuwa ngeni sauti ile katika masikio yake. Haikuwa sauti aliyokuwa akiishikia mara kwa mara kama ilivyo sauti ya mkewe ambaye ni daktari. Hii ilikuwa sauti ambayo aliwahi kuisikia asijue mwaka wala tarehe, hakukaribia kukumbuka hata mahali alipowahi kuisikia.

Ila aliwahi kuisikia.

Baada ya miaka mingi ya mapambano na kisha kuamua kutulia tuli baada ya kuvunjika mguu wake, akabaki katika mapambano ya kalamu na karatasi huku akiwa yu katika chumba tulivu chenye urafiki wa dhati na kiyoyozi.

Kwa jicho lake pevu kabisa Inspekta Kobo akajiona anaungiza mguu wake mbovu katika mapambano mapya.

Licha ya mkewe kuwa daktari inspekta alipendasana kumshirikisha masuala yake pindi yanapomwendea kombo.

Na hili lilikuwa limemnyima usingizi, akabofya simu yake na kumpigia mwenza wake, simu ikaita lakini haikupokelewa.

"Yupo chumba cha upasuaji huyu..." alijisea na hakujaribu tena kupiga.

Akafikiria kumpigia mpenzi wake wa siri, koplo Zubeda, akajiuliza mara mbilimbili kisha akaikumbuka ile kauli mbiu ya 'ukivuka mipaka basi siri mweleze mkeo unayempenda kwa dhati lakini kamwe usitapike siri zako mbele ya hawara. HAWARA hana dhamana...

Inspekta akakiri kuwa anampenda sana Zubeda lakini tahadhari lilikuwa jambo la muhimu sana.

Akarejea katika kochi akaketi.

"Nguzu atakuwa amekufa ama? na kama hajafa itakuwaje upande wangu..." alijiuliza Inspekta asipate wa kumjibu.

Watoto wake walikuwa wanaelea katika dimbwi la usingizi mzito.

Mawazo juu ya mawazo hatimaye usingizi ukamwonea imani, ukamsomba na kumuunganisha katika dimbwi walilokuwqa wakisafiri watoto wake kwa wakati ule.

Dimbwi la usingizi.....

Asubuhi akaamka akijisikia ahueni na akijaribu kujisahaulisha kuhusu kiza kilichojiri usiku uliopita.

Akiwa anafanya jitihada za kuyafuta haya akaipokea taarifa juu ya kuchomwa kwa nyumba aliyokuwa akiishi konstebo Nguzu, kilichosalimika ni nguo zake zilizokuwa zimeanikwa katika kamba iliyokuwa mbali kidogo na nyumba.

Si kichwa wala fuvu lake kilichosalia katika moto ule wa kutisha.

Inspekta akazishusha pumzi zake, akaanza kutembea huku na kule katika himaya ya nyumba yake. Akaunda mfano wa mzazi mdogo katika kichwa chake, akahisi uhai wa Nguzu ungeweza kuwa hatari sana kwake.

Hatari kwa sababu alikuwa na ubaya naye nafsi ya Kobo ikakiri kuwa ilikuwa imechefukwa haswa kutokana na uwepo wa Nguzu.

Kwa hatua hii ya kuzimika moja kwa moja akahisi kuwa itakuwa ni nafuu kubwa kama mtu aliyeingiliwa na mchanga jichoni akifanikiwa kuutoa na kisha jicho lake kubaki huru.

Lakini uhai huohuoungeweza kumweka matatani kwa sababu Nguzu angehojiwa juu ya nani amehusika katika moto ule, angwataja watu ambao ana ubaya nao, kwa nini asilitaje jina la inspekta Kobo kama jina la muhimu zaidi!!

Ni heri amezimika. Alihitimisha Inspekta Kobo.

Akahamia upande wa pili wa mzani, Nguzu amekufa vipi?

Je? ninahusika? akajiuliza, kisha akachukua simu na kupiga tena nambari aliyokuwa akihangaika nayo usiku uliopita.

Haikuwa inapatikana...

Hapo akarukia sehemu ya pili, ni nani alikuwa chini ya mti, na ni sauti ya nani aliisikia upande mwingine...

Haya yalikuwa maswali magumu zaidi. Maswali yaliyosababisha aamue kuwa upande wa yeyote yule ambaye amefurahia kifo cha Konstebo Nguzu.

Akaufunga ukurasa wa mawazo mazito juu ya ni nini atafanya ili Zubeda atulie na kuachana na Nguzu. Sasa aliwaza ni kitu gani amfanyie asije akazama kwa mwanaume mwingine kama ilivyokuwa kwa Nguzu.

Akaamua kumfanyia ugeni wa ghafla utakaotawaliwa na upya mkubwa sana kutoka kwake...

Akiwa mwenye kubwa tabasamu aliingia maliwatoni kujisafi mwili wake.

Kisha akalivamia jokofu na kutoa maji ya matunda. Akaigida kwa fujo glasi ya kwanza mpaka ikamalizika. Kisha glasi ya pili akainywa taratibu huku akiwa anaipanga ratiba yake kwa siku hiyo.

Simu yake ya mkononi ikatoa mlio kumaanisha kuwa kuna ujumbe mpya umeingia.

Akaifungua upesi kwa sababu simu ilikuwa kiganjani kwake.

"Bosi, shemeji kapata ajali yuko Temeke hospitali. Amekula mzinga na Suzuki yake"

Ujumbe ule wa maandishi ukawa kama ulioambatana na umeme mkali kuzidi kipimo, ukautekenya mkono wa inspekta glasi ikamtoka mkononi, kisha akaanguka chini kama mzigo baada ya miguu kuelemewa.

Mpasuko wa glasi na kishindo cha mwili mzito wa inspekta vikawashtua watoto waliokuwa wameamka tayari.

Balaa jingine likaibuka.

Walipiga mayowe huku wakiiitana kwa kusisitiza kuwa baba yao angali katika tatizo kubwa.

Inspekta Kobo alijaribu kusimama ili alete amani kwa watoto wake lakini akabaini kuwa hawezi kusimama, ule mguu wake ulioungwa kwa vyuma ulikuwa umeyumba.

Tusi pekee katika lugha ya kiitaliano alilolifahamu likamponyoka huku akiipigapiga sakafu.

Kelele zilivyozidi akatoa onyo, akawafokea watoto wake huku akijinadi zaidi ya mara mbili kuwa yeye ni mwanajeshi kamili wasihamanike.

Maneno ya shujaa huyu yakatuliza munkari, akafikishwa hospitali katika hali ya utulivu kabisa bila papara za kuwafanya majirani watambue kuwa inspekta Kobo amekumbwa na balaa.

_______

MAJIRA YA saa nne usiku kiwiliwili cha kiume kikiwa katika koti kubwa lililoungana na kofia yake kilikuwa kikikatiza katika wodi ya wanawake kwa mwendo wa haraka huku kichwa chake kila mara kikinyanyuka juu kutazama uelekeo wa mbele na kisha kuinama tena.

Safari ile iliyojaa umakini iliishia katika chumba kilichojitenga mbali na wodi za wanawake.

Watu wawili walimpokea kimyakimya na kumwingiza chumbani, akamwona mgonjwa wake.

"Nakupenda sana Zubeda." Lilikuwa neno la kwanza kumnong'oneza yule mgonjwa kisha akainama na kumbusu.

Zubeda akajaribu kutabasamu kidogo.

Inspekta Kobo alizungumza machache na Zubeda kisha akamweleza kuwa siku inayofuata atakuwa na muda mrefu zaidi wa kuzungumza mengi.

Akaaga na kuondoka!

Alitumia usafiri wa pikipiki, upesi akarejea nyumbani kwani kwa ratiba ya mkewe ilivyokuwa siku hiyo alipaswa kuwa nyumbani majira ya saa tano usiku.

Inspekta aliwasili baada ya dakika chache tangu saa tano ilipotimia. Hofu ilimtawala kidogo kwa sababu ya maswali ambayo angepokea kutoka kwa mkewe lakini pia angelaumiwa sana kwa kuanza mizunguko mapema kiasi hicho badala ya kupumzika.

Hakumkuta mkewe nyumbani, akaanza kujilaumu sana kwa kuhofia ujio wa mkewe, huenda angeweza kuendelea kuzungumza na Zubeda kwa muda mrefu zaidi.

Wakati akiwaza haya, Daktari Kobo ambaye ni mkewe alikuwa katika chumba cha mgonjwa akijaribu kuzungumza naye kwa lugha ya upole kabisa, ni kawaida ya madaktari kuitumia lugha inayoleta tumaini kwa mgonjwa.

Tofauti na ulivyokuwa utaratibu wa siku zote aliouzoea mgonjwa yule alistaajabu kuona mlango wa chumba kile alicholazwa unafungwa kwa ndani na yule daktari mwanamke.

Kisha mwanamama yule akakisogelea kitanda na kumjulia hali.

Mapigo ya moyo ya yule mgonjwa yakaanza kwenda mbio kupita kawaida.

"Bila shaka sina haja ya kujitambulisha.... na hakika sijaja kwa ubaya humu ndani. Unaitwa Zubeda na unajihusisha kimapenzi na mume wangu wa ndoa Inspekta Kobo." Akaweka kituo kisha akamwinamia mgonjwa yule.

"Nimekusudia kuzungumza na wewe kwanza kwa sababu wewe ni mwanamke mwenzangu, unafahamu nini kuhusu kifo cha Konstebo Nguzu?" Swali lile lilikuwa kama upinde wenye moto mkali mbele yake. Likamchoma haswa Zubeda.

"Sijui lolote." alijibu kwa ufupi mno.

"Zubeda, narudia tena, sipo hapa kwa sababu ya wivu wa kimapenzi, nina umri wa miaka thelathini na tisa sasa, nimeishi na inspekta kwa zaidi ya miaka kumi na nane. Nilikuwa ninao wivu zamani sio sasa.... ninawapenda sana watoto wangu sitaki wakose huduma zababa yao na huenda katika hili ni msaada pia kwako.Kuna taarifa ambayo haijazagaa kuwa wewe na inspekta mmeshirikiana kuichoma nyumba ya Nguzu huku yeye akiwa ndani na kusababisha mauti yake. Hili nd'o lililonileta hapa..... ungekuwa ni wivu wa mapenzi ningeagiza wakuchome sindano moja tu na siku inayofuata ungehamishiwa mochwari tayari kwa maziko, na mwili wako unmgeoza licha ya kupigwa na ubaridi wa mochwari. Sina nia mbaya... naomba unipe ushirikiano. Wewe na inspekta mpo matatani. Kumbuka kuwa IGP hapatani na inspekta Kobo sana, atawanyoosha katika hili. Niambie kama mmehusika ili tuweke kando masuala ya mapenzi kisha tuketi pamoja na kuitafuta suluhu kabla vithibitisho havijatapakaa."

Maneno ya dokta Kobo yalikuwa mazito mno, Zubeda hakuamini kile alichokisikia, hakuwahi kuzungumza na inspekta Kobo hata siku moja juu ya mpango huu wa kinyama kiasi hicho.

"Ukiachana na hiyo njama, sijawahi hata siku moja kuzungumza na inspekta juu ya konstebo Nguzu."

"Sema hayati..." Dokta alimrekebisha.

Marekebisho haya yakamuumiza Zubeda katika moyo wake, alikuwa amemzoea mno Martin Nguzu. Sasa anaambiwa amepoteza maisha.

"Inspekta Kobo nd'o mtu wa mwisho kuingia nyumbani kwa marehemu kabla moto haujaimeza nyumba ile. Hivi unadhani wakuijumlisha na tatizo la wewe kuwa na wapenzi wawili kwa waikati mmoja kuna mtu atahitaji ushahidi wa ziada. Zubeda utapotea vibaya mno, mimi sijui sana sheria lakini kama nikichaguliwa kutoa hukumu katika hili basi nikiwapeleka gerezani miaka michache kabisa ni thelathini thelathini. Wauaji wakubwa nyinyi.." Jazba ikataka kuchukua nafasi akatulia kwa muda kujizuia na hali ile.

"Shangazi, sijui lolote kuhusu huu mpango unaousema, sijawahi kuzungumza na Inspekta juu ya lolote kuhusu Nguzu. Hii ni kweli ya moyo wangu..."

"Sawa kama haujui. Mimi naondoka..." alizungumza doktahuku akiyanyanyua mabega yake juu.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni