Mtunzi: Richard Mwambe
SEHEMU YA KWANZA
HOLY FAMILY BASILICA
HAKUNA mtu aliyeamini anachokiona mbele yake, kila aliyepita njia alitikisa kichwa na wengine kuangusha machozi. Polisi kutoka kituo cha kati cha Nairobi walikuwa hapo mbele ya kanisa hilo kubwa wakifanya uchunguzi wa hili na lile. Mwili usio na uhai ulikuwa umelala chini na majeraha makubwa kifuani yakiwa yameganda damu nzito. Hakuna asiyejua mwili ule ni wa nani, kila aliyepita alisikitika, wengine hata walighairisha safari zao za kazini, vilio vilitawala eneo lile. Kila mtu alionekana kuguswa kwa namna moja au nyingine na mauaji ya Kasisi huyu wa kanisa la Roman Catholic, Rev Fr Frederick Gichuru, hakuna aliyejua kwa nini na ni nani aliyetekeleza mauaji haya ya kinyama. Baada ya kumsachi hakuna cha ziada walichokikuta katika kanzu ya kasisi huyo zaidi ya rozari iliyokuwa mkononi mwake.
“Bila shaka alikuwa katika sala zake za asubuhi” sauti ya kukwaruza kutoka kwa koplo Otholong’ong’o ilipenya sikioni mwa sajenti Maria Kariuki ambaye kwa muda huo alikuwa bado amepigwa na butwaa. Sajenti Maria alisikitika na kujutia nafsi yake, alijiona kama mwenye makosa mbele ya Mungu kwa kifo hicho.
“Ndiyo, afande, daima asubuhi kabla ya misa makasisi wa kikatoliki huwa na wajibu wa kusali kwanza wao weyewe” Sajenti Maria alimjibu koplo Otholong’ong’o huku ukungu mzito ukimtoka kinywani mwake kuashiria baridi kali ya mwezi wa sita hapo Nairobi. Bado sajenti Maria alikuwa kajiinamia jirani kabisa na mwili ule akiuangalia kwa makini jinsi ulivyoharibiwa kwa risasi, maganda saba ya Colt 45 yalikuwa mkononi mwake, huku akiyarusharusha alijinyanyua taratibu na kuamuru mwili ule uondolewe na kupelekwa chumba cha maiti cha hospitali ya rufaa.
Inspekta Simon Saitoti alimkazia macho sajenti Maria aliyekuwa ameketi mbele yake akiwa na jalada moja la khaki lililoandikwa juu ‘MAUAJI YA KASISI’, alionekana kama mtu ambaye haelewi anachoelezwa, alilivuta jalada lile na kuliperuzi kurasa zake chache kwa dakika kadhaa, kasha akainua macho yake kutazama ukutani ambako kulipambwa kwa picha ya muasisi wa taifa hilo, hayati Jomo Kenyatta.
“Umesema paroko wa kanisa hilo hamjamkuta, sivyo?” Inspekta Saitoti alimtwanga swali sajenti Maria.
“Ndiyo afande, na tulipowauliza masista walisema kuwa kawaida wanakuwa na zamu ya kufanya misa za asubuhi vigangoni, hivyo paroko alikuwa amekwenda kigangoni” Maria alijibu kwa ukakamavu wa kipolisi.
“Ok, mauaji kama haya hayajawahi kutokea hapa kwetu hii ni mara ya kwanza, na naomba sana iwe mara ya mwisho, endelea kufanya uchunguzi wa tukio hili kwa kina ukishirikiana na koplo Otholong’ong’o na mnipe taarifa za kina, ili tuwatie mbaroni wauaji.”
“Sawa afande” sajenti Maria alisimama na kurudi nyuma hatua mboli na kupiga saluti ikiwa ni kitendo cha kuonesha heshima kwa mkubwa wake kadiri ya nidhamu za kipolisi.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Kijua cha haja kililing’aza jiji kubwa la Nairobi, jiji lenye pilikapilika za kila aina katika ukanda wa Afrika ya Mashariki. Watu walionekana wakitembea na kuvuka barabara kwa haraka haraka kuashiria kuwa ukichelewa tu matatu itakugonga. Bado hali ya ubaridi ilikuwa ikiendelea na kila mtu alionekana kujidhatiti kwa hali hiyo.
Kwenye kituo kimoja cha basi, mwanaume mmoja mrefu alikua amesimama akisubiri matatu, mara tu matatu moja ikafika na muziki mkubwa ndani yake, akaikaribia na kupanda ndani yake, mkononi alikuwa na mfuko wa plastiki ulioandikwa UCHUMI, bila shaka alikuwa akitoka supermarket, safari yake kwa matatu hiyo iliishia katika kitongoji cha Uthiru Kenoo barabara kuu ya kwenda Uganda. Kwa mwendo wa wastani alivuka kwa kupitia daraja kubwa na kufika upande wa pili wa barabara hiyo ambapo kuna biashara nyingi, aliliendea gari aina ya Hammer lililokuwa limepaki hapo, ndani yake hakukuonesha dalili yoyote ya kuwapo mtu, alifungua mlango kwa kidubwasha maalum na kuuweka ule mfuko katika kiti cha mbele kasha akatokomea kusikojulikana.
Takribani nusu saa hakuna aliyeisogelea gari ile, mara akaja mtu mwingine mnene wa haja pamoja na mwanamke mmoja mrefu na mwenye mwii ulioumbika vizuri, wakaingia ndani ya gari ile na kujifungia milango.
“Shit, washakosea tena” alisikika Yule mtu mnene akimwambia Yule mwanamke
“Nini tena?”
“Hawako makini na kazi yao, tunawalipa pesa nyingi lakini hawajui nini cha kufanya, nguruwe wakubwa hawa”
“Kwani nini?” Yule mwanamke alizidi kudadisi
“Ah, we yaache tu, hutakiwi kujua”
“Aaa jamani, yani umelala na mimi umenambia vingapi mapaka hili usinambie?”
“Mambo ya kazi haya, achana nayo”.
Ile gari ilitiwa moto na kurudi mjini, hakuna ambaye angekaa bila kulitupia macho gari ilo ka jinsi lilivyo na uzuri wa aina yake na gharama yake ndiyo iliyotia kiwewe.
Moja kwa moja gari ile ilisimama karibu kabisa na mtaa wa Koinange, mtaa unaosifika kwa machangudoa hapo Nairobi.
“Nitakucheki usiku twende club” mtu mnene mwenye asili ya kihindi alimwambia Yule mwananmke na kumpa noti za shilingi elfu moja moja tano za Kikenya.
* * *
Askofu mkuu wa jimbo kuu la Nairobi, Mhashamu Gregory Julius Maina, akiwa ofisini kwake alishikwa na huzuni kubwa kwa habari ya mauaji ya fr Gichuru, alimlilia na kumuombea lakini hakujua ni nini hasa chanzo cha kifo hicho. Alitafakari na kuumiza kichwa, kasha akainua macho yake na kutazama jopo lile la makasisi lililokuwa mbele yake, kila mmoja alikuwa ama akiangusha au akijifuta machozi, ukumbi wa parokia ya Maria Consolatha katika eneo la Westland ulikuwa umetulia kimya kabisa kana kwamba hakukuwa na watu ndani yake.
“Nawasalimu katika jina la Bwana” Askofu aliwasalimu makasisi wale wapatao kama mia mbili weupe kwa weusi.
“Amen” waliitikia.
“Nina masikitiko moyoni, kuwatangazia rasmi kifo ca kasisi mwenzetu padre Frederick Gichuru, paroko msaidizi wa parokia ya Familia Takatifu, kilichotokea leo alfajiri kwa kupigwa risasi saba za kifuani na kupoteza uhai papo hapo” alifuta machozi na kukaa kimya kidogo, kasha akaendelea “Tunalaani vikali kabisa mauaji haya yasiyo na sababu inayoeleweka, hatuna cha kusema zaidi ila sisi kama kanisa tunaiomba serikali na vyombo vyake vya dola vifanye kazi ya kuwatia nguvuni wote wanaohusika, na tunawaomba raia wema wanaojua tetesi yoyote ya kifo hiki kutoa taarifa polisi au hata kwetu ili kusaidia katika kupambana na kadhia hii. Zaidi ya yote Bwana awasamehe kwa maana hawajui watendalo. Ibada ya mazishi itafanyika keshokutwa katika Basilica la Familia Takatifu” alimaliza Askofu kutoa tamko kwa niaba ya kanisa, kisha kuwapatia Baraka na wote wakatawanyika.
“Baba, pole kwa msiba” Kasisi mmoja alimsalimu paroko wa Basilica la Familia Takatifu ambaye msaidizi wake ndiye aliyeuawa asubuhi hiyo.
“Tumeshapoa, Mungu mwenyewe anajua”
Mara gari ya polisi aina ya Land Cruiser iliingia katika viwanja vya kanisa hilo la Conslata, sajenti Maria alikuwa wa kwanza kuteremka, akiwa ndani ya suruali yake ya buluu na shati la buluu bahari alipendeza kwelikweli. Alifanya juu chini kumpata Padre Joe Smith, raia wa Marekani ambaye ni paroko wa Basilica lililotokea mauaji, alipompata alimuomba kuongea naye machache na wote wakaelekea katika ofisi ya parkia hapo Consolatha.
“Pole sana baba kwa msiba, naitwa sajenti Maria kutoka kituo cha polisi cha kati Nairobi”
“Asante, tumeshapoa” alijibu Fr Joe Smith kwa Kiswahili chake kinachopendwa na wengi hasa anapotoa mahubiri.
“Wakati tukio linatokea, wewe ulikuwa wapi asubuhi hiyo?”
“Mimi nilikuwa nimekwenda kufanya misa ya asubuhi kigangoni”
“Siku hiyo ni wewe ulitakiwa uwende kigangoni?”
“Hapana, kadiri ya ratiba siku hiyo haikuwa zamu yangu”
“Enhe sasa ilikuwaje ukaenda?”
“Fr Gichuru, usiku wa jana alinambia kuwa yeye hajisikii vizuri, hivyo angependa kubaki parokiani” alimjibu sajenti Maria ambaye alionekana kuandika vitu Fulani kwenye kitabu chake.
“Je unafahamu lolote kama marehemu alikuwa na ugomvi na mtu, au hali yoyote tofauti iliyokuw katika maeneo yenu kama wachungaji?”
“Kwa kweli katika siku hizi, kumekuwa na mambo ya ajabu kabisa, kuna watu walikuwa wanakuja sana pale parokiani na kuuliza mambo mengi kwa watoto watumishi, wakati Fulani tulimkuta mtu anapekua Sacristia, walipomuuliza akawachapa makofi.”
“Mlichukua hatua gani?”
“Niwaulize ninyi polisi, mimi nilipiga simu polisi na mkaahidi kuja kufanyia uchunguzi lakini bho! Sikuwaona”
“Sawa, msaidizi wako alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu yeyote awe sista au mwingine yeyote?”
Fr Joe alishtuka kidogo kwa swali hilo. Sajenti Maria akatoa tabasamu lake lisilo nahisia hata kidogo mbele ya watu.
“Mbona umeshtuka baba?”
“Eh nikikuuliza wewe kama una mahusiano na kasisi hautashtuka?” wote wakacheka kasha Joe akaendelea “Hakuna kitu kama hicho, kama kipo basi mimi sijui”
“Haya, asante sana baba, kama nikikuhitaji nitakutafuta” wakapeana mikono na kuagana.
Sista Rose alikuwa akibubujikwa na machozi mbele ya sajenti Maria.
“Usilie Sista, ni maswali machache tu nataka kukuuliza”
“Sawa afande”
“Wakati mauaji yanatokea wewe ulikuwa wapi?”
“Muda huo mimi nilikuwa natoka nyumbani kwetu naenda kuandaa misa kanisani…
Ilivyokuwa
…Ilikuwa yapata saa kumi na moja na nusu alfajiri, sista Rose alikuwa na zamu ya kwenda kuandaa misa, aliamka na kujiandaa, kisha akiwa ndani ya mavazi ya kitawa alitoka nje ya nyumba ‘coventi’ yao na kwa mwendo wa taribu na rozari yake mkononi alikatisha kauwanja kanakotenganisha nyumba yao na kanisa, mara alisimama ghafla moyo wake ulifanya paaah! Hakujua kwa nini, kwa mbali alimuona Fr Gichuru akiingia kwenye uwanja wa kanisa hilo akiwa kwenye vazi lake jeusi na kofia nyeusi yenye nyoya katikati, alivaa kikasisi hasa na si mara nyingi kuonekana kaika mavazi haya.
Alikuwa akitembea taratibu na mara walikutana na sista Rose katikati ya uwanja, wakasalimiana kwa ishara lakini Fr Gichuru alibaki kasimama akimwangalia sista Rose, akamuonesha ishara ya kuwa ainamishe kichwa chake, sista Rose akafanya hivyo na Fr Gichuru akamuwekea mikono kichwani kumbariki, mara mwanga wa taa za gari ukawamulika kutoka getini, hakuna liyejua ni gari ya nani, Fr Gichuru akamuacha Sr Rose aendelee na shughuli yake yeye akaliendea geti…
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi