MAUAJI YA KASISI (4)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
Siku moja alitembelewa na mtu asiyemjua, baada ya mazungumzo marefu sana walifahamiana kuwa kumbe wao ni ndugu, na sasa huyu ambaye angetakiwa kumwita kaka alikuwa ni mtu mkubwa kwatika mji huo wa Achen.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
“Ndiyo, mimi ni Andreas Schurmman, baba yangu mimi mzee Ernst Schurmman alizaliwa tumbo moja na mama yako Angela Schurmman, wakati wa vita ya pili ya duni ndipo walipopoteza maisha katika mazingira tofauti na wewe ulichukuliwa ukiwa mdogo na babu yako aliyemzaa mama yako, mimi nililelewa na msamalia mwema tu mpaka nimekuwa hivi nilivo.”

Gustav alitikisa kichwa juu chini kuonesha kuwa aliielewa hiyo safari ya maisha jinsi ilivyokuwa.

“Umejuaje kama nipo hapa?”

“Nina rafiki yangu ambaye ni mfanya kazi hapa ndiye aliyeniambia lakini hata yeye hajui kuwa mimi na wewe tuna undugu, ila mimi nilijua kwa kuwa ninalikumbuka jina hili Gustav Macker, karibu sana nyumbani uje unitembelee”.

Baada ya mazungumzo yao waliagana na kila mtu kubaki na na hamsini zake, ‘Sasa ishu yangu itakamilika’, Don Andreas Schurmann alijiwazia wakati akiingia kwenye gari yake aina ya Mercedes Benz na kuuacha uwanja wa seminari hiyo.

* * *

“Hutakiwi kushangaa wala kushtuka” Don Andreas alimweleza Gustav Macker.

“Sishangai kwa unachoniambia, bali nashangaa kwa nini babu aliweka utajiri huo huko?! Inatia uchungu”

“Hapana babu yangu alikuwa na akili sana, alikuwa anatafuta mahali salama pa kuihifadhi siri ile ya utajiri kwa kizazi chake cha sasa” Don Andreas akajimiminia glass yake ya pombe kali na kusafisha koo kwa kujikohoza kidogo, kisha akaendelea, “Vatican, ni sehemu yenye usalama sana duniani, na si uongo. Mzee Peter Schurmann aliiweka pale siri ile ya utajiri mkubwa kwa ukoo wake. Sikia Gustav, utakapokuwa Padre nitafanya kila njia uhamishiwe Vatican ili ufanye uchunguzi ujue jinsi gani tunaweza kuipata Monstance ile irudi mikononi mwetu.”

Gustav aliinama kwa sekunde chache akiangalia sakafu ile ya marumaru safi ambayo ilimruhusu kuiona taswira yake mwenyewe kwa jinsi ilivyokuwa safi.

“Gustav!” Don aliita, “Usihofu, haya ni mambo madogo sana, na nina hakika tutafanikiwa na kuishi kifalme”. Maneno matamu ya Don Andreas yalianzisha mapigano ya nafsi na roho ndani ya kijana huyu ambaye kanisa liliridhia kumpa ukasisi miezi michache ijayo, ama kweli kwenye mkono wa Mungu hapakosi mguu wa shetani. Mazungumzo ya wawili hao yalikuwa marefu sana na mwishowe makubaliano yalifanyika na mpango mahsusi ukapangwa na tajiri huyo, Don Andreas, kama alivyojulikana.

Baada ya miezi sita Gustav Macker alipewa daraja la upadre na kuwa kasisi rasmi katika kanisa Katoliki, hakuamini masikio yake alipopata taarifa kuwa kituo chake cha utume kitakuwa Vatican, katika makao makuu ya kanisa hilo.

* * *


Black Cheetah alinyanyuka na kusimama wima na wengine wakafanya hivyo hivyo.

“Vijana tuingie kazini, tutengeneze pesa” Cheetah aliwaeleza wenzake na wote wakahafiki.

Walipomaliza vinywaji hivyo waliliendea gari ya Black Cheetah aina ya Subaru na kupotelea mjini. Ilikuwa tayari majira ya saa nne usiku Subaru ile ilipoegeshwa katika maegesho ya viwanja vya Uhuru, wote wakateremka na kupotelea katika club kubwa inayojulikana kama Nairobi by night, humo starehe za aina zote zilikuwa zikipatikana, walijichanganya na wadau wengine wakisubiri mida yao ya kazi ifike ili wafanye wanalolihitaji.

* * *

Ilitimu saa sita ya usiku, Cheetah na wenzake walipoegesha gari yao karibu kabisa na jingo la kanisa hilo na kushuka.

“Hivi nyie mnaosali, hiyo monstrance sijui nini huwa inahifadhiwa wapi?” Cheetah aliwauliza wenzake

“Kawaida kwenye chumba cha kuvalia makasisi, ambacho huwa ni kanisani” alijibu Mellina wakati Gicui akiliangalia jingo lile kubwa lililojengwa kwa kuta nene ajabu likiwa katikati ya mji wa Nairobi.

“Ok, nafikiri mmoja wetu aingie huko kwenye hicho chumba halafu wengine waangali usalama wa ndani na nje” Cheetah alitoa oda.

“Sawa Cheetah!” Gichui aliitikia kama aliyekurupushwa usingizini.

Dakika chache baadae Gichui alikuwa ndani ya wigo wa kanisa hilo akitalii hapa na pale, akiangalia hiki na kile, usiku mnene usio na mbala mwezi, aliifanya kazi hiyo kwa ustadi hata walinzi hawakugundua chochote, Mellina na Cheetah walibaki nje lakini kila mmoja upande wake, Mellina katika ulinzi wa nje na Cheetah akiwa makini na tayari kumuokoa Gichui kama itatokea la kutokea. Akiwa ndani ya wigo ule Gichui alitembea kwa uangalifu sana akichungulia kwenye vitundu vidogo vilivyojengewa kwenye ukuta huo wa kanisa, ndani aliona tu kataa kekundu kakiwakawaka mithili ya mshumaa, alikaangalia na kukumbuka kuwa pale huwa makasisi wanawekaweka vikombe Fulani, labda ni penyewe. Aliendelea na kutokea upande wa nyuma wa kanisa hilo, milango kadhaa ilikuwako hapo na yote imefungwa imara kabisa kwa vitasa vya kiitaliano, kila aliyoutikisa ulikuwa imara kabisa, akatoa funguo zake zinazofungua kotekote akatumbukiza moja na kujaribu ikagoma, akachukua nyingine akatumbukiza mlango ukakutii amri na kufunguka, akiwa na sox yake kichwani akaingia ndani ya chumba hicho ambako alikutana na makabati mengi ambayo yalimchanganya, kabati kubwa la mbele liliunganishwa na meza kubwa sana iliyofunikwa kwa Formica safi, akatulia na kuatafakari, kabati lipi hasa analolihitaji, kwake aliiona kazi hiyo ikiwa rahisi kabisa ni kiasi cha kufungua makabati tu na kubeba anachotaka kisha kuondoka. Alilijongea kabati hilo kubwa na kujaribu milango yake, ilikuwa wazi, ndani kulikuwa na nguo tu za ibada zinazotumiwa na makasisi....

* * *

Fr Frederick Gichuru, alishtuka usingizini, ndoto mbaya ilimsongasonga hata kuufanya moyo wake kwenda mbio, alikaa kitandani na kuitafakari ndoto hiyo hakupata maana, machozi yalimtoka, alipiga magoti mbele ya msalaba na kutulia kimya, baada ya dakika kadhaa alishtuka na kusikia kelele za mlango kama mtu anaufungua kwa kutumia nguvu, alisikiliza kwa makini na kukuguundua kuwa ulikuwa mlango wa Sakristia (sakristia ni chumba kinachojengwa pamoja na kanisa ambacho uhifadhiwa mavazi na vitu mbalimbali vya ibada), mlango ambao Gichui alikuwa akiufungua taratibu sana lakini Fr Gichuru aliusikia kwa kelele. Aliinuka na kuchuku kanzu lake zito jeusi ili kujistiri na baridi kali ya Nairobi, alienda mpaka chumba cha Fr Joe, akamkua mzee huyo anakoroma kwa usingizi mzito akaamua kumuacha, akatoka nje kuelekea kanisani kushuhudia nini kinafanyika, alishtuka na kusimama ghafla alipoona mlango wa sakristia uko wazi, alikibanza kwenye ua kubwa la yugiyugi lililomficha vizuri, ‘wanataka nini?’ alijiuliza asipate jibu, aliangalia lakini hakuona mtu kutoka, alivuta hatua ndogindogo na kuufikia mlango huo, akazipanda ngazi na kuingia ndani, aligeuka huku na huku hakuona mtu isipokuwa milango wazi ya makabati.

“Tulia apo hapo, usijitikise” sauti ilitoka upande wa makabati ya nyuma.

Fr Frederick alitulia na kunyoosha mikono yake juu kujisalimisha.

“Wanaume wanapokuwa kazini wewe hutakiwi kuamka amka” Gichui alimwambia Fr Gichuru, Fr Gichuru aling’ata meno kwa hasira, hakujali kama mtu huyo ana silaha gain alishusha mikono na kugeuka na kutazamana na domo la bastola aina ya Smith and Wesson.

“Wewe ni nani?” Fr Gichuru aliuliza

“Usitake kujua” alijibiwa

Fr Gichuru alimkazia macho Gichui, Gichui alijikuta akiishiwa nguvu na kushusha bastola yake.

“Kwa nini mnataka kulidhulumu kanisa?” akauliza Fr Gichuru, “Nani aliyekutuma? Na mnataka nini?” kimya kilitawala kati yao, “Sema nitakusaidia, kazi ya kanisa ni kusaidia wahitaji na wenye shida, sema.” Gichui aliinua bastola yake tena na kuondoa kiguu cha usalama kuruhusu risasi ipande juu tayari kabisa kufyatuliwa.

“Siogopi risasi, maana risasi itaua mwili lakini kamwe haiwezi kuuwa roho” Fr Gichuru alimueleza jambazi yule. Gichui alishusha pumzi bado akimnyoshea bastola kasisi huyo.

“Sikiliza kijana, weak bastola yako mahali pake uende kwa amani, maadam sijakuona sura yako na hii itabaki kuwa siri yetu mimi na wewe tu,” Fr Gichuru alimaliza na kuanza kufunga makabati yake. Alipogeuka baadae hakumuona yule jambazi mahali pale, akafanya ishara ya msalaba na kurudi nyumbani kwake. Usingizi haukuwako tena mpaka kulipokucha.

* * *

“Uuuuh!” Gichui alipumua kwa nguvu baada ya kuingia kwenye gari yao akiwa na wenzake tayari kuondoka.

“Tupe ripoti” Cheetah alitoa ombi kwa Gichui

“Haaaa, siamini”

“Huamini nini, umeona nini huko?” Cheetah alidadisi

“Makabati makubwa na nguo za kasisi, sijaona monstrance”

“Lakini Gichui unaonekana kuna kitu hutaki kusema” mellina alidakia kutokapale nyuma ya usukani alikpokaa.

“Kanisani, si pa kuiba” alijibu, “Nimekutana na Kasisi Gichuru ana kwa ana pale kanisani” akaweka tuo kidogo na kuendelea “Nilijikuta naishiwa nguvu, sikuweza kufanya lolote, akaniruhusu kuondoka”.

“We bwege kweli, ungembana huyohuyo akueleze” Meliina aling’aka.

“Mellina mi nashindwa kukueleza, wale jamaa sijui wana dawa!” aliongea kwa mshangao Gichui.

“Basi, tutarudi kwa nguvu mpya” Cheetah aliwapoza wenzake na kuondoka zao.

“Una uhakika kuwa hiyo monstrance ipo huku?” Cheetah alimuuliza mtu mnene kwa njia ya simu.

“Mi siyo mtoto Cheetah, najua na nina uhakika na hilo, hakikisha tunaipata” alijibiwa.

“Maana jana tumefanya upekuzi mle kanisani hatukuiona” aliendelea kuongea Cheetah

“hata kama haipo kanisani, lakini ipo maeneo hayo, fanya kila unaloweza uipate” alimaliza mtu mnene na kukata simu.

“Sasa wajukuu, hapa kilichobaki ni kufanya mbinu zote kumteka Fr Gichuru tumbane mpaka atueleze maana yeye ndiye aliyeuleta ule mzigo” Cheetah aliwaelezawenzake na wote wakaafikiana na kupanga mikakati.

* * *

“Baba Joe, leo usiku nimeota ndoto mbaya sana hata nikaamka usiku kusali” Fr Frederick alimueleza Fr Joe walipokuwa mezani wakipata chai.

“Ni nini tena umeota Fr?” Joe aliuliza

“Ah, ndoto mbaya sana” alisema huku akitua slesi za mkate katika sahani na kuiinamia meza akitegemeshwa na mikono yake miwili. Fr Joe aliona matone kama matone ya maji yakidondoka juu ya meza hiyo.

“Fr, ni nini, nieleze nikusaidie” Fr Joe aliinuka kitini na kulmuendea Fr Gichuru huku akimueleza maneno hayo, alitoa kitambaa chake na kumfuta machozi. Fr Gichuru aliinuka kitini pamoja na Fr Joe wakatoka nje kwenye kabustani kadogo na kutembeatembea wakiwa na rozali zao mikononi.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni