CHUZI NDIO HILO, HAKUNA KUONJA (11)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Alijiuliza mengi moyoni.

Jua lilichomoza, mama Shua akapata wazo kwamba achukue simu ya Musa, ampigie baba Shua na kumwomba afungue mlango atoke,

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
achukue mizigo yake na kuondoka kabisa lakini Musa akagoma kumpa simu yake…

“Noo mama Shua…siwezi kukupa simu yangu wakati najua yule ni adui yangu…siwezi. Kama anataka tufie humu ndani poa tu. Kama amepanga kuniua mimi sasa nitafanyaje?” alisema Musa akiwa amekasirika sana. Kwake, ilifika mahali ikawa liwalo na liwe.

Jua lilitoka kabisa, baba Shua alitoka chumbani na Shua, akaenda kuufungua mlango na kumwingiza Shua ndani…

“Nenda kwa mama yako.”

Mama Shua alishtuka sana kumwona mtoto wake akiingia na mlango ukiwa umefunguliwa. Alimkumbatia na kuanza kulia huku akisema…

“Mwanangu, nimekutenda vibaya sana. Utahangaika sana kwa sababu ya akili mbaya ya mimi mama yako.”

Shua hakujua lolote. Alibaki akimwangalia mama yake kwa macho ya mshangao…

“Mamaa,” aliita Shua, mama Shua akazidisha kilio kumsikia mtoto wake akimwita mama.

Shua aliachana na mama yake, akamfuata Musa…

“Chumba…”

Musa alikasirika sana, akatamani kumpiga. Shua alimwita Musa chumba kutokana na maneno yake siku za nyuma akimtania Shua kwa kumwita mchumba.

***

Baba Shua alikwenda kuoga, akavaa na kuondoka zake huku pesa za matumizi akiwa amemwachia msichana wa kazi.

***

Muda f’lani, mama Shua alisimama mlangoni akimlia taiming msichana wake wa kazi akipita…

“Dada,” alimwita alipopita…

“Abe…shikamoo dada…eti kwa nini upo huko?”

“Hayakuhusu…baba Shua ameondoka au yupo?”

“Ameondoka.”

“Kweli?”

“Kweli ameniaga, ameniachia pesa za matumizi.”

Mama Shua alirudi chumbani, akamchukua Shua na kutoka akiwa hana hamu tena na Musa.

Aliingia chumbani kwake. Kitu cha kwanza ni kuangalia simu yake, akaikuta. Akashangaa sana kwani aliamini jambo ambalo angelifanya baba Shua ni kuondoka na simu hiyo.

Aliipekua ndani na kubaini kwamba, haijachunguzwa kwani baadhi ya meseji zilikuwa za jana yake usiku na hazikusomwa.

“Mh! Sasa hapa dawa ni kumwomba radhi baba Shua. Mimi ni mkewe wa ndoa, binadamu hukosea, hiyo ni kawaida. Naamini atanisamehe tu. Nitamwambia sirudii tena, nimwahidi uaminifu,” alisema moyoni mama Shua.

Amwombeje samahani? Aliamua kumwandikia ujumbe wa simu badala ya kumpigia akiamini kwa kusoma atamwelewa vizuri zaidi kuliko kumwendea hewani. Kwanza anaweza asipokee hata hiyo simu yake. Aliandika:

“Baba Shua, najua kosa langu, nimekutenda vibaya sana mume wangu. Nakiri kosa moja kwa moja. Niko chini ya miguu yako mume wangu, nisamehe sanasana! Sitarudia tena, ni shetani tu alinipitia. Sasa nimejitambua ujinga wangu. Please mume wangu. Nisamehe saba mara sabini.” Akatuma.

Baba Shua hakujibu meseji hiyo. Ilifika mahali, mama Shua akaamini kuwa, mumewe alikuwa bize hivyo hajaona meseji yake, akaamua kubipu. Lakini licha ya kubipu, bado mumewe hakumpigia…

“Sijui kama nina ndoa tena! Ina maana baba Shua amebadilika kiasi hiki? Yaani ajue jambo zito kama la mimi kulala na mwanaume mwingine halafu aendelee na shughuli zake? Lazima kuna jambo baya sana anataka kunifanyia,” alisema moyoni mama Shua.

Siku hiyo aliamua asiende kazini. Aliamua kukaa nyumbani huku kazini kwake akiaga kwa uongo kwamba anasumbuliwa na kichwa.Kingine kilichokuwa kikimpa wakati mgumu mama Shua, aliamini kwamba mume wake atapeleka habari zake nyumbani kwao kijijini jambo ambalo anajua linaweza kusababisha kifo cha ghafla cha mama yake mzazi…

“Yaani afadhali haya mambo tuyaongee wenyewe, akisema anampigia simu mama kumwambia nimempoteza mama yangu. Lakini hivi mimi hii tabia nimerithi kutoka kwa nani? Kwa baba au mama?

“Mbona sijawahi kusikia hadithi yoyote inayosema mama alikuwa mhuni au baba alikuwa mhuni. Au wananificha? Au mimi nimeathiriwa na mazingira?” alijiuliza yote mama Shua.

***

Kule kazini, baba Shua muda mwingi alikuwa mwenye mawazo. Aliiona meseji ya mke wake, lakini hakutaka kumjibu. Na aliona alipobipu lakini pia hakutaka kumpigia.

Mara simu yake iliita, akaangalia skrini na kushtuka sana baada ya kuona jina la Maua.

Maua ni msichana aliyekuwa na uhusiano na baba Shua kabla ya kukutana na mama Shua.

Baba Shua alimpenda sana Maua kiasi kwamba, alikuwa tayari kwa ndoa naye lakini alipotokea mama Shua, alijikuta akitekwa na kumsahau Maua.

Uhusiano wao ulikufa polepole mpaka kila mmoja akajikuta akichukua hamsini zake. Baadaye, baba Shua akamuoa kwa ndoa mama Shua…

“Haloo,” baba Shua aliipokea simu ya Maua…

“Haloo…mzima wewe?”

“Mimi mzima. Sijui wewe?”

“Mimi pia mzima. Niko hapa kwenye mgahawa jirani na kazini kwako, nikasema nikupigie ili kama hutajali uje tushiriki kifungua kinywa cha pamoja.”

“Wapi? Hapo Bianca?”

“Ndiyo.”

“Nakuja Maua.”

“Karibu sana.”

Baba Shua alifunga mlango wa ofisi, akaenda Mgahawa wa Bianca na kukutana na Maua.

Ni Maua bila kujali kuachwa, alipomwona baba Shua alisimama, akamkumbatia na kumpiga mabusu mawili ya nguvu…

“Mmm…mwaa….mmmwaa.”

“Asante Maua…za siku nyingi?”

“Njema, sijui wewe?”

“Mi mzima sana Maua.”

“Nakuona umenawiri mpenzi…ni hiyo ndoa au nini?”

“Ah! Maua…nadhani ni wakati wa mwili wenyewe tu. Ndoa si sababu…”

“Kwa nini Benny?”

“Ah! Nimeingia chaka Maua.”

“Umeingia chaka! Kivipi Benny?”

“Maua…nimeoa malaya.”

“Ha..! Benny…unajua hilo neno ni zito sana…umeoa malaya?”

“Niamini mimi Maua…ngoja nikupe mkasa mzima,” alisema baba Shua na kuanza kumsimulia mkasa mzima Maua kuhusu mke wake, mama Shua.

Baba Shua alitumia kama nusu saa nzima kusimulia kisa cha mama Shua na Musa. Hata alipomaliza, alihema kwa kasi kubwa ya kusimulia…

“Lo! Asee! Kwa hiyo huyo kijana Musa ndiyo mwiba kwenye ndoa yako? Sasa umeamuaje?” aliuliza Maua.

“Maua, ungekuwa wewe ndiye umekumbana na kisanga hiki hata kwa jinsia yako ungeamuaje?”

“Ningeamua kusamehe.”

“Hapana! Ni ujinga wa hali ya juu. Haiwezekani.”

“Sasa wewe unataki kufanyaje?”

“Hakuna ndoa Maua. Mwanamke anakuletea mwanaume mpaka ndani, wewe upo. Unamsema lakini bado anaendelea tu!?”

“Niachie mimi, nitaamua,” alisema baba Shua uso wake ukionekana kuwa makini sana.

“Da! Pole sana Benny. Mambo mengine vipi lakini?” Maua aligeuza kibao cha mazungumzo…

“Poa sana. Sikutegemea kama leo utanipigia, nimefurahi sana.”

“Kweli? Hata mimi nimefurahi sana wewe kukubali mwaliko wangu. Maana bwana, mtu akishakuwa kwenye ndoa, hataki tena ahadi, hataki mtoko.”

Baba Shua alicheka, akamuuliza…

“Bado unaishi Temboni?” baba Shua alimuuliza Maua…

“Kulekule lakini nyumba kama ya tano toka pale nilipokuwa nikikaa zamani. Karibu sana Benny…”

“Nitakuja siku moja…”

“Lini nijiandae.”

“Ujiandae kwa kufanyaje? Umfukuze shemeji uliyenaye sasa hivi?”

“Ha! Wala! Mimi pale haingii mwanaume labda awe ndugu yangu.”

“Mbona mimi unaniruhusu nije kuingia?”

“Sasa wewe historia yako kwangu ni tofauti na wengine. Wewe ni kama mtalaka wangu. Kwa hiyo una nafasi yako ya pekee.”

“Basi nitakuja wikiendi hii,” alisema baba Shua…

“Mimi sitaki uje wikiendi hii…”

“Unataka lini?”

“Leo!”

“Mh! Mbona ghafla sana Maua?”

“He! Jamani! Kwani nyie wanaume mna ghafla?”

“Eee! Ratiba zikiingiliana ni ghafla tu.”

“Ina maana Benny huwezi kuua ratiba zako kwa mwaliko wangu mimi?”

“Kwani umenialika au umeniomba nije nikutembelee?”

“Haya, nakualika sasa. Leo naomba uje nyumbani kwangu.”

“Sawa, kuna siku nitakuja…”

“Mimi nataka uje leo bwana.”

“Mh! Maua bwana…nikisema ghafla ndiyo hupendi…oke, nitakuja leo.”

“Saa ngapi?”

“We unataka saa ngapi?”

“Mimi nataka ukitoka kazini nikufuate twende wote mguu kwa mkono.”

Baba Shua hakuwa na jinsi, alikubali…

“Basi nitakujulisha nikiwa natoka,” alisema.

“Sawasawa.”

Walipomaliza kupata chochote, walisimama wote, wakatoka huku Maua akiwa ametangulia mbele.

Baba Shua alishangaa sana kwa namna Maua alivyobadilika. Alikuwa akitembea kwa mwendo wa kujisikia, alinawiri, alinenepa kidogo na alitakata…

“Da! Huenda ningekuwa na Maua mambo yasingekuwa hivi yalivyo sasa na mama Shua. Halafu demu kapendeza ile mbaya, suruali imemkaa kama amezaliwa nayo,” alisema moyoni baba Shua huku mwili ukianza kumsisimka kwa kumfikiria Maua alivyo kwa siku zile na moyoni akawa anakumbuka zamani za mapenzi yao motomoto.

Nje, waliachana. Maua akaingia kwenye gari lake na kuendelea na safari zake lakini huku akimsisitiza baba Shua kumfuata baadaye, baba Shua alikubali akarudi kazini kwake huku akisema moyoni…

“Kumbe Maua ana gari! Aisee! Lakini huenda huyu Maua akanisaidia kunipunguzia stresi. Kama tutaishi kama zamani itakuwa poa sana. Naweza kuendelea na mama Shua kwa vile nimefunga naye ndoa lakini huyu Maua akawa ndiye chaguo langu.”

Kusema kweli kwa muda wa siku kadhaa nyuma za mshikemshike wake na mkewe mama Shua na Musa wake, siku hiyo baba Shua alijisikia ana amani sana baada ya kukutana na kipenzi chake Maua.

***

Kwa upande wake, Maua aliondoka naye barabarani akiwa na mawazo kibao kuhusu baba Shua…

“Naamini sasa Benny anajutia uamuzi wake wa kunimwaga mimi na kumchukua huyo malaya wake,” alisema moyoni Maua…akaendelea…

“Na safari hii nikimdaka, hachomoki, kweli kabisa.”

***

Saa kumi kamili ya alasiri, Maua alimpigia simu baba Shua…

“Mm…vipi Benny? Hujatoka tu?”

“Ndiyo natoka Maua.”

“Kwa hiyo?”

“Njoo basi twende.”

Maua alichoma mafuta mpaka ofisini kwa baba Shua, akamchukua kwenye gari lake mpaka nyumbani kwake.

Walishuka wote, wakatembea kwenda ndani huku Maua akiwatambulisha majirani kwa baba Shua…

“Jamani! Mama Kise, huyu anaitwa Benny…ni mchumba wangu. Alikuwa nje kwa masomo, sasa amerudi.”

“Oooo! Karibu sana,” majirani walimkaribisha baba Shua.

Kwa jinsi alivyo, mwonekano na mavazi, kweli baba Shua alionekana kufananafanana na mtu aliyetoka nje ya nchi.

Ndani, walifikia sebuleni. Maua alionekana mwenye furaha sana kwani walipofika tu sebuleni, alimbusu baba Shua kisha akampa denda la mbali sana, wakakaa…

“Karibu sana baby, hapa ndiyo kwangu…dada,” Maua alimkaribisha, akamuita msichana wa kazi…

“Abee dada…”

Msichana wa kazi alitokea kutoka uani…

“Msikilize mgeni anakunywa nini? Lakini acha tu, namjua huyu nitamhudumia mwenyewe,” alisema Maua akisimama na kwenda kwenye friji.

***

Ndani ya saa moja, Maua alimkaribisha baba Shua chumbani…

“Njoo upaone mahali anapolala ubavu wako,” alisema Maua.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni