MAUAJI YA KASISI (18)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
“Kwa hiyo ndio hila zako sio?” Mellina akamuuliza Wambugu huku bado akiwa anaangalia mbele.

“Nilishapewa kazi na Bill nikumalize ili kuondoa ushahidi wowote usio na tija,”

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI

ENDELEA...
Wambugu alijibu kijeuri.

“Kwa hiyo katika orodha uliyopewa, umeshaua wangapi?” Mellina aliuliza, alitumia mbinu ya kuongea ikiwa ni moja ya kumzubaisha Wambugu kabla hajapanga ni nini cha kufanya katika hali kama hiyo amabayo kwayo hakuna masikhara kwani maisha yako yapo kwa adui yako.

“Bill alishamaliza kazi yake, na alishapata kile anachokitaka, hivyo basi ninyi mlioshiriki ambao mnaweza mkatoa siri hii lazima msiwepo katika uso wa dunia, Gichui amekwenda, Cheetah hayupo, umebaki wewe na Kahaba Rose ambaye muda si mrefu roho yake itakuwa mikononi mwangu,” Wambugu aliongea kwa pozi, wakati Mellina alikuwa akifikiri juu ya shambulizi linalofuata, shambulizi la ghafla ambalo akili yake ilikuwa ikiushawishi mwili nini cha kufanya ambacho madhara yake yatakuwa kwa adui.

“Na katika hao wanaojua hiyo siri, wanaotakiwa kuuawa, unafikiri wewe haumo?” Mellina alimwambia Wambugu kauli ambayo ilimfanya kustuka kidogo, na kukumbuka kuwa kumbe hata yeye mwenyewe yupo kati ya wanaojua, akiwa katika kiutafakari hayo mara Mellina aligeuka kwa ghafla na mkono wake wa kulia ukakamata korodani za Wambugu.

“Aaaaaaaaiiiiggghhhh!!!!!” yowe la uchungu likamtoka Wambugu na kuitoa ile bastola kichwani mwa Mellina. Sasa Mellina na Wambugu walikuwa wakitazamana, sura ya Mellina iliyogeuka kutoka katika uzuri wa kike na kuwa ya kikatili kama mnyama ilikuwa imekaza macho kwa Wambugu aliyekuwa akilia kwa maumivu.\

“Sikia wewe mwanaume mjinga, Bill anataka kukuua na wewe vilevile, sasa kabla hajakuua yeye mimi naanza,” Mellina aliunguruma huku akizidi kuziminya korodani za Wambugu na kuzizungusha, maumivu makali yalikuwa yakimpata Wambugu kabla hajatulia, Mellina alimpiga kichwa kimoja cha nguvu na kumuachia Wambugu alipepesuka na kudondoke kwenye kijimeza kidogo kilichokuwa ndani ya chumba hicho hukun ile bastola ikiwa chini sakafuni, Mellina akaiokota, kulichukua lile koba lenye fedha na kuanza kuondoka.

“Mellinaaaaaa!” Wambugu alipiga kelele hasa alipoona Mellina amenyanyua koba la fedha, Mellina aligeuka na ile bastola mkononi, “Kelele wewe kubwa jinga,” alimtuliza kwa mtindo huo huku akifyatua risasi kadhaa pembeni kabisa mwa pale alipoangukia Wambugu na kuchimba sakafu na ukuta kuacha mashimo, akatoa sonyo refu na kumuacha Wambugu hoi katota kwa mkojo.

Mellina akaubamiza mlango nyuma yake na kukamata tax iliyokuwa ikipita hapo muda huo na kutokomea zake. Huku nyuma Wambugu alipopata akili alinyanyuka haraka na kukimbilia mlangoni hakuna alichoshuhudia zaidi ya vumbi jekundu lililobakisha hapo na ile gari, Wambugu alilikimbiza kwa miguu lakini hakufanikiwa alianguka chini na kuanza kulia akijigalagaza kama motto na mwili wote kuwa mwekundu kwa lile vumbi.

“Bingo!” Mellina alijikuta akitamka neon hilo alipokuwa katika siti ya nyuma ya ile tax baada ya kupekuwa na kukuta maburungutu kadhaa ya pesa, “Wapi dada?” ilikuwa sauti ya dereva tax ikimuuliza Mellina, ndipo Mellina alipokumbuka kuwa yupo kwenye tax, “Nipeleke Nakuru,” Mellina alijibu. Yule dreva tax alikuwa kama kichaa vile, akakanyaga mafuta na kuchukua barabara ya kuelekea Nakuru,”

§§§§§

Madam S alikuwa amesimama karibu na dirisha la ofisi yake, dirisha kubwa lililokuwa likikupa mandhari nzuri ya bahari ya Hindi, alitazama upande huo wa bahari, alipotosheka akageuka na kurudi kitini kwake pale ambapo aliwaacha wageni wake wameketi.

“Ndio Madam, unaonekana mtu mwenye mawazo sana,” mmoja wao alianzisha mazungumzo.

“Yeah na ndilo swala hasa ambalo nimekuitieni hapa,” Madam S alijibu, akainua bilauri yake yenye maji na kunywa kisha akaitua mezani, “Kamanda Amata ametoweka hospitalini na haijulikani wapi alipo, mkiwa kama wanaintelijensia nataka mnipe maelezo ya kina labda nini mnakihisi kimetokea, maana leo ni karibu siku ya tatu, na hatuna maelezo yakutosha, hapa ninavyokuambieni mzee katuma fax na inabidi ifanyiwe kazi haraka. Nyote mnajua umuhimu wa Amata, kichwa chake kimejaa siri asilimia 99 za serikali, hivyo haiwezekani apotee tu namna hii,” Madam S alianza kuzungumza akionekana wazi kuwa swala hilo limemuumiza kichwa kuliko maelezo. Aliwatazama wale vijana wanne waliokuwa mbele yake waliotulia kama vinyago vya mmakonde maana hawakuwa wakitisika wala kupepesa macho.

“Madam, Kamanda ni mtu wa kisasi sana asiyekubali kushindwa, je hatokuwa amerudi Nairobi kumsaka mbaya wake?” mmoja wao aliuliza. Madam S alionekana akiandika vitu Fulani kati kijidaftari chake cha kumbukumbu, kisha akainua uso na kumwangalia yule aliyeuliza, “Yote yanawezekana, tumetoa taarifa ofisi husika ya usalama pale Nairobi, nao wanajaribu kumwangalia kama yupo huko lakini bado hawajatupa jibu, ila sijui kwa maana hata yule msichana wake hakuna anachojua juu ya hili na hii si kawaida.” Alijibu Madam S.

“Ukicheki namba zake za siri kwenye mtandao vipi hazionekani?” mwingine aliuliza.

“Namba zake nazo hazioneshi chochote, maana nimempa hiyo kazi Chiba lakini mpaka sasa anasema hamuoni kwa namba zake, akijaribu juelekeo wa simu anasema pia hazisomi kwa maana simu zake zote zilizimwa juzi pale airport na ndio signal ya mwisho inasoma hapo,” Madam S alishusha pumzi ndefu na kujiweka sawa kitini, “Dah, Kamanda!’ alijiwazia huku akifikicha jicho lake.

“Kwa hiyo Madam unasemaje?” yule watatu aliuliza

“Nataka mfanye kila njia mumtafute na hakikisheni mmempata kisha mniambie yuko wapi,” Madam S alimjibu, akawapa kazi ya kumsaka Amata kwa kuwa yeye hatakiwi kupotea mbele ya macho ya wakubwa wake kutokana na kazi na cheo alichonacho.

Siku tatu nyuma…

TAARIFA za kushushwa cheo kwa Kamanda Amata hazikumfurahisha hata kidogo, baada ya Madam S kutoka pale hospitali, Amata alitafakari sana na kuumia moyoni, alijikuta anamchukia kila mtu. Alipogundua kuwa wauguai wote wametoka na yuko peke yake katika kile chumba akatoka kitandani na kutorokea upande wa nyuma ambako alipitia katika dirisha kubwa la alluminium. Akachukua tax na moja kwa moja alielekea nyumbani kwake maeneo ya Kinondoni.

Akiwa nyumbani kwake alijua wazi kuwa lazima atatafutwa kwa mtindo wowote ule, alijaribu kuangalia kila kitu ambacho kingemfanya ajulikane alipo, simu, saa ya mkononi, headphone set na kila kitu, kitu kimoja alitaka kukisahau ‘micro chip’ ya kielektroniki ambayo alipandikizwa katika kwapa lake la kushoto ambayo inawasiliana na satellite moja kwa moja hivyo kutoka ofisi ya mawasiliano ya kitengo chao wanaweza kumuona muda wote kwa namba maalum ambazo zinamtambulisha. Kamanda Amata alijua wazi kuwa hiyo chip sasa ndiyo inayomweza kumuharibia, akaona isiwe tabu, alijaribu kuminyaminya katika kwapa lake na kugundua wapi ipo kutokana na umbo lake la mcheduara lenye ukubwa kama punje ya mchele, akavuta mtoto wa meza na kutoa kisu kidogo pamoja na forceps, akiwa anajiangalia katika kioo kikubwa kilicho mbele yake alinynyua mkono na kujichana pale alipohisi chip ile imewekwa, hakukosea, kwa kutumia ile forceps akakibana sawia na kukichomoa, damu zilimwagika lakini alidhibiti hali hiyo kwa shashi iliyokuwa hapo ndani kwake na kutia dawa kidogo aina ya Iodini au wengi tunaaita dawa ya joto, aliichukua ile chip na kuitia moto ikateketea kabisa, kisha akajipanga kwa safari. Gina alimfuata na kumpeleka uwanja wa ndege ambako alichukua ndege na kurudi Nairobi kwa kificho bila mtu kujua. Aliapa kumtia mkononi kila aliye jirani na Bill mpaka ampate Bill ili kazi yake aiache kwa heshima na si kwa dharau. Ndipo aliporudi Nairobi kwa hasira ya kumsaka Bill na vibaraka wake.

Nairobi

GARI aina ya Vogue iliegeshwa nje ya kanisa la Familia takatifu, kijana mmoja aliyevalia nadhifu, suti nyeusi iliyotanguliwa na kaba shingo la rangi ya cream aliteremka na kuufunga mlango wa gari hiyo kwa madaha, kisha akaingiza mkono wake mfukoni na kutoa miwani myeusi akaipachika usoni mwake, naam, ushababi wake ulijitokeza waziwazi, akazunguka upande wa pili na kufungua mlango. Mwanamke mwenye umbo la wastani, lililojaa vizuri, anayevutia ukimwangali kuanzia kifuani mbala chini ya kiuno mashaalah taarabu ipo ya kuvutia, akiwa ndani ya suti ya kike ya kijivu, na uso wake ameuficha kwa miwani safi ya rangi ya udongo. Haikuwa rahisi kugundua kuwa huyu ni Kahaba Rose ambaye akiwa pale mtaa wa Koinange huvalia kijisketi kifupi kilichobana na chepesi ambacho huuacha mwili wake sehemu kubwa wazi. Alishikana mkono na kijana huyo kisha wakavuka geti mpaka kwenye kibanda cha mlinzi na kuomba kuonana na Paroko kama yupo, baada ya itifaki zote kufanyika ikiwa kutazamwa kama wana silaha yoyote kukamilika waliruhusiwa.

Kati ya viti sita ni vitatu vilikaliwa, upande huu Kahaba Rose na Kamanda Amata na upande mwingine ni Fr Joe Smith, babu.

“Karibuni sana, mumekuja kuandikisha ndoa?” alianza kuuliza yule kasisi.

“Hapana, tumekuja kwa maswala ya kikazi, tunahitaji kuongea machache juu ya tukio zima la Fr Gichuru,” Amata alitonesha kidonda cha kasisi huyo mzee raia wa Marekani.

“Mimi nimechoka na kuulizwa maswali kila wakati na wala sioni maendelea yake, mara Kenya Polisi, mara FBI, Mara MOSSAD, mara sijui nini, ah, nihurumieni jamani, kama kazi imeshindikana basi acheni mbona Gichuru amekwishakufa hawezi kufufuka hapa duniani tena, haya niambie na wewe unatoka wapi?” Fr Joe alilalama na mwisho kuomba utambulisho.

“Naitwa Kamanda Amata, kutoka Tanzania.” Akampa na kitambulisho kidogo cha plastiki, yule kasisi mzee alionekana kama kupigwa na shock baada ya kusikia kuwa aliye mbele yake ni Kamnda Amata, mara nyingi alimsikia mtu huyu tu na kusoma baadhi ya visa vyake ambavyo vingine vimeandikwa kama riwaya, hakuawahi kufikiri kama bonadamu huyu yupo kweli au ni hadithi tu, sasa mbele ya macho yake anakutana na kiumbe huyu, alimkazia macho kana kwamba sijui kakutana na Malaika Gabrieli.

“Wewe ni Kamanda Amata?” aliuliza huku akimnyoshea kidole na kumrudishia kile kitambulisho chake.

“Ndiyo ni mimi,” Amata alijibu huku akikiweka kitambulisho chake katika mfuko wake maalumu ndani ya koti lake.

“Kamanda Amata karibu sana,” alimkaribisha.

“Asante sana nafurahi kukutana na wewe, sasa kilichonileta hapa ni juu ya mauaji ya kasisi, Fr Gichuru. Ningependa kujua juu yake kwa kifupi ili nijue wapi pa kuanzia,”

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni