MAUAJI YA KASISI (31)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA THELATHINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Wachezaji walianza kupungua katika mchezo kwa kuwa hawakufaulu, walizidiwa maarifa na wengine, mara hii Kamanda Amata alidumu katika mchezo, japokuwa hakushinda lakini alitoka wa pili na mchezo wa mwisho alicheza na Don Andreas, ambapo alizidiwa kwa ujanja mdogo sana.

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Mr Fransisco, unaweza kucheza tena kwa kuwa umeikaribia bahati, umekaribia utajiri, weka dau lingine na ucheze tena. Kamanda Amata alijikuta hana pesa zaidi, alikuwa na kiasi kidogo ambacho hakingefaa sana kununua token. Mchezeshaji akawapa breki ya kujiweka sawa. Kamanda Amata akainuka na kuelekea kaunta ambako aliagiza glass moja ya pombe kali, akinywa taratibu huku akiandika ujumbe kwa kupitia saa yake kwenda kwa Madam S, dakika moja baadae, alipata majibu na akayafanyia kazi. Mara moja akafanya mchakato palepale hotelini kuweza kubadilisha pesa aliyotumiwa na Madam S, $ 1500 si haba kwa mchezo huo wa mwisho kwa mujibu wa Yule mchezeshaji.

Meza ilijaa tena wadau, kabla hawajaanza mchezeshaji akatoa rai yake kama ilivyo sheria ya mchezo.

“Sasa tunaingia raundi ya mwisho, tumeona wote waliofanya vizuri katika raundi zilizopita, tumeona pia uchezaji wa mgeni wetu kutoka Uganda si mbaya sana, sasa angalisho, kila mtu aweke dau ambalo hatoathirika katika akiba yake baada ya kushindwa mchezo huu,” akamaliza kusema kisha akzungusha chungu, wote wakaweka mapesa kibao, mmoja wao, Yule tajiri wa Venezuela alikuwa ameishiwa na kubaki na kiasi kidogo, akaweka dau gari yake ya thamani, Marcedes Benz CLA45 AMG 4MATIC 355-hp. Ilikuwa ni gari mpya kabisa, toleo jipya ambalo thamani yake si ya kitoto. Kamanda Amata akatupia katika chungu kile $ 1500 kama zilivyo, kila mtu akaguna tena, lakini hawakuguna kwa Yule aliyeweka gari kwa sababu walijua kuwa ana uwezo wa kununua nyingine.

Mchezo ulianza na kila mtu alikuwa makini sana mara hii, hakuna aliyetaka kupoteza mchezo huwo wa thamani kwa maana atakayeshinda atakuwa ni milionea wa kutupwa kwa pesa atakazokusanya. Lakini kamali ni kamali tu, mmoja baada ya mwingine walianza kupanguka.

Mwisho wa mchezo wakakutana Don Andreas na Kamanda Amata. Ilikuwa ni nafasi nzuri sana kwa Kamanda Amata kutazamana uso kwa uso na tajiri huyo ambaye siri ya safari yake pale Ujerumani iko ndani ya kifua chake. Don Andreas alikuwa haelewi afanye nini, mara ajishike nywele, mara shavu, mara ajikune ilimradi kutaka kushinda mchezo huo wa dhahabu, wakati Kamanda Amata alikuwa katulia kitini akimtazama kwa makini tajiri huyo anavyochachawa. Wakati mchezo huo ukiendelea, kijana mmoja aliyevalia suti safi nyeupe aliingia pale mezani na kuzunguka nyuma ya Don Andreas akamnong’oneza kitu, Don Andreas alipata mshtuko wa mbali kidogo ambao mpaka uwe mzoefu wa mambo ya kiintelijensia ndio waweza kugundua.

Kamanda Amata aliisoma hali hiyo, akapata hisia ya kitu Fulani. Mchezeshaji alimuhamasisha Andreas kucheza. Mwisho wa mchezo, Kamanda Amata akaibuka mshindi, makofi mengi yalitawala wakatia akikusanya kete zote kuwa ni ushindi wake, pamoja na funguo ya gari ile ya kisasa, aliegemea kiti chake na kumtazama Don Andreas aliyeonekana kuchoka ghafla kitini mwake. Wale wengine walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine kwa maana mchezo ulikuwa umefikia mwisho. Kamanda Amata aliiegemea tena meza na kumtazama Andreas.

“Sasa tucheze mimi na wewe, wawili tu,” Kamanda alimwambia Andreas. Don Andreas alimtazama Kamanda Amata.

“Sina dau kwa sasa la kupoteza, wewe tumia utajiri uliopata,” Don Andreas akamwambia Amata huku akijiandaa kuondoka, wapambe wake tayari walikuwa wamekwishafika. Kamanda Amata akamzuia Don Andreas kwa kumgusa kiganja cha mkono alichokisahau mezani, akastuka na kumtazama Kamanda, “Dau unalo, tena la gharama sana,” kamanda Akamwambia Don. Tabasamu la uongo likatoka katika sura ya Andreas.

“Mostrance, weka dau Mostrance,” kamanda Amata alimwambia Don. Neon hilo lilimfanya Don Andreas kukunja sura ghafla na kurudi sawia kwenye kiti chake kama awali, “Unasemaje Mr…” kabla Andreas hajamaliza kutaja jina, Kamanda Amata akajitambulisha rasmi, “…Kamanda Amata,” akamalizia. Ilikuwa ni kama tetemeko la ardhi ka Don Andreas kujua kuwa yupo na nani mbele yake. “Hutoliona jua la kesho kijana,” Andreas akamwambia Kamanda Amata.

“Kama wewe ndiwe umeweka jua liangaze mchana, sawa, ila kama si wewe nitaliona, ila wewe na Bill sijui nani ataliona kati yenu,” Kamanda Amata alinyanyuka kitini na kuanza kuondoka huku yule mchezeshaji akikusanya zile kete tayari kuzibadili kuwa pesa ili apatiwe Kamanda Amata. Kamanda Amata alipoanza kuondoka akakutana na binti mmoja mzuri wa sura, mavazi yake yalionesha asilimia 80 ya mwili wake usiokuwa na nguo, wakasimama na kutazamana nyuso zao, Yule binti akatabasamu, tabasamu la

wizi, kamanda Amata akamshika kiunoni na kuondoka naye mpaka kaunta ambako aliagiza kinywaji na kuanza kukimiminia kinywani mwake huku cheers nyingi na Yule binti, Kamanda alikuwa millionea ghafla, lakini alijua wazi hatari inayomkabili muda huo.

“Unahitaji cash au tukuwekee katika akaunti yako?” sauti ilitokea kaunta ikimuuliza Kamanda juu ya pesa zake, “Weka kwenye akaunti kisha nipe namba ya muamala wangu kwa ajili ya kuhakikisha,” alimjibu yule mhudumu wa kaunta.

“Beibi, nimekupenda ghafla,” Yule mwanamke alimwambia Amata. “Usijali leo ni mimi na wewe mpaka majogoo yawike,” kamanda Amata aliongea kwa Kijerumani cha kubabaisha, “Mmmm aliyekwambia huku kuna majogoo ni nani?” Yule binti alizidi maneno ya mtego, “Aaaaa jamani majogoo huyajui,” Kamanda Amata akawuliza Yule binti. Alipokabidhiwa kadi maalumu yenye namba za muamala wake, akamshika mkono Yule binti na kutoka nae pale kaunta, hatua mbili, mkono mmoja ukazungushwa kiunoni, wakapotelea nje ya hotel hiyo.

§§§§§

BILL VAN GETGAND alishusha mtemba wake kutoka kinywani, akapuliza moshi mwingi hewani na kusababisha mchafuo wa mazingira kutokana na huo moshi taka, akashusha kioo cha gari iliyombeba mpaka chini kabisa, kisha akatupa kipisi kilichobaki kwa kulenga katika kasha maalum la takataka liliwekwa hapo jirani na maegesho.

Alimtazama Kamanda Amata akitoka na Yule binti wa kizungu, wakiwa wamekumbatian viunoni, walipolifikia lile gari, wakakumbatiana kwa kutazamana, wakapeana mabusu ya kuinyonyana ndimi zao. Kengele za hatari zikagonga katika kichwa cha Amata, akatoa miwani yake na kuivaa, alipotazama kwenye maegesho akashuhudia kioo cha Vogue kikimalizia kupanda juu, akajua kuna kitu.

“Uko peke yako?” Kamanda Amata akamuuliza.

“Yeah, peke yangu,” Yule binti akajibu.

“Huwa unakuja kufanya nini hapa?” swali lingine kutoka kwa Kamanda.

“Mmmmm huwa nakuja kutafuta wanaume wazuri kama wewe,” akajibu Yule binti. Kamanda Amata akaminya kitufe kwenye funguo ya gari aliyopewa na Benz moja nyekundu ikawaka taa zake kuashiria kuwa ndiyo yenyewe, akaiendea na kufungua milango akajitoma nyuma ya usukani, na Yule binti akakaa pembeni.

“Unanipeleka wapi?” akauliza Yule binti.

“Beach,” kamanda akajibu huku akiondoa gari ile katika maegesho. Nyuma yake ile Vogue nayo ikaondoka, lakini haikuwafuata njia waliochukua wao. Kamanda Amata aliendesha gari hiyo taratibu sana akiizunguka mitaa ya mji huo mkongwe kabisa huko Ujerumani, huku akiwa macho yake yakitazama nyuma, mbele kwa umakini mkubwa sana kujua kama kuna anyemfuata au vipi.

Kamanda Amata aliendelea kuzunguka katika mitaa ya mji huo bila kuegesha gari popote huku akiwa hana maongezi yoyote na Yule mwanamke katika gari hiyo.

“Hey beibi, mbona huongei, na wala huniambii unanipeleka wapi? Mi nataka twende kwangu,” Yule mwanamke alimuuliza na kumwambia Amata ambaye alikuwa ametingwa na usukani wa gari hiyo.

“Najaribisha gari yangu mpya, usijali, nikichoka tutakwenda kwako,” Kamanda Amata alimjibu Yule bibie huku akiendelea kuchapa mwendo, akipita barabara hii na kutokea barabara ile. Mara nyuma yake akasikia ving’ora vya polisi vikija upande wake, akaangali kwenye kioo cha kuendeshea gari akaona gari mbili za polisi zikija kwake, akaongeza mwendo na zile gari zikawa zinakuja kwa kasi. “Polisi,”Yule mwanmke akamwambia Kamanda.

“Usiogope, hao sio polisi, kwa jinsi wanavyoendesha gari,” Kamanda Amata akajibu.

“AA 768 G weka gari pembeni!!” ilikuwa sauti kutoka katika kipaza sauti ambacho polisi wale walitumia kumsimamisha Kamanda Amata, lakini badala ya kusimama aliendelea kutimua mbio na gari lile, sasa alitembea mwendo wa hatari zaidi. Kamanda Amata kwa ujumla alikuwa akijua kuwa Andreas, Bill na vibaraka wao lazima watakuwa wakimnyemelea katika mitaa hiyo hivyo hakutaka kuuacha mji ule mapema wala hakutaka kurudi hotelini mapema ili aone nini mwisho wake, alishajua kuwa kurudi hotelini ni kujiweka kwenye hatari zaidi.

“Unaitwa nani?” ndio kwanza Kamanda Amata anagundua kuwa hakuwa amemjua kwa jina yuel mwanamke.

“Naitwa Hellen,” akajibu huku akijinyoosha kwa kujipindapinda mwili wake klitu ambacho kilimsisimua Kamanda Amata hasa alipokuwa akikiona kile kifua kilichopambwa na matiti mawili mazuri yakiyotuna kwenye kigauni hicho chepesi sana.

“Hellen, unamfahamu Don Andreas?” Kamanda Amata akauliza.

“Ndio, namfahamu sana, kwani kuna mtu ambaye hamfahamu tajiri huyo matata hapa mjini? Kibosile mpenda vimwana, vipi una shida naye?” Hellen akajibu na kurusha swali.

“Hapana siwezi kuwa na shida na mtu masikini kama Yule,” kamanda Amata akajibu huku akimtazama Hellen, wakati huo ile Mercedes Benz ilikuwa inasoma 158 km/h, mwendo mkali kwelikweli. “Mr Francisco, unajua wewe ni mgeni sana hapa Aachen,” akaanza dodoso zake za kike.

“Hapana, huwa nakuja mara nyingi sana hapa ila wewe hujawahi kuniona, kwa nini unauliza?” kamanda Amata aliendeleza mazungumzo kwa kuwa alijua nini kitafuata. “Usimwite Andreas masikini, ana masikio zaidi ya million hapa Aachen,” Hellen aliongea kwa mapozi.

“Oooh, sikujua huyo atakuwa shetani basi, maana binadamu kawaida ana masikio mawili tu,” Amata akajibu kwa utani, lakini alipomwangalia Hellen akaona hata kutabasamu hakupo usoni mwake, akajuwa kuwa sasa kaanza kumfika moyoni kwa maneno yale. Hellen alimtazama Kamanda Amata hakummaliza, akaingia za mkono wake mkobani na kutoa kitu kama kikebe cha wino wa mhuri, akakifungua, ndani yake mlikuwamo na sigara tano na kiberiti cha gesi, vyote viliweza kutosha ndani ya kikebe kile. Akachomoa sigara moja na kuiweka mdomoni, akamtazama Kamanda Amata, kabla hajafanya lolote Kamanda Amata aliitambua ile sigara,

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni