MTU WA UFUKWENI (10)

0
Mwandishi: Andrew Mhina

SEHEMU YA KUMI
ILIPOISHIA...
“Asante Mimi naitwa Jackson Kigoi kwa fani ni Dokta hivyo watu wamezoea kuniita Dr.Jackson, huyu niliyenaye ni Mke wangu mpenzi anaitwa Mrs Mary Jackson.” Alisema Jamaa huyo aliyejitambulisha kama Jackson.. kisha akaendelea..“Kuja kwetu hapa ni ili tujipumzishe na kuogelea.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Tumepata taarifa juu ya ufukwe huu kuwa ni mzuri na mmiliki wa eneo hili ni mkarimu sana na ndivyo tunavyojionea hapa.” Alimalizia kutoa utambulisho Dr.Jackson huku mkewe akitoa tabasamu kumuunga mkono kwa maneno yake. “Labda ni kweli! Karibuni sana ndugu zangu. Sijui kama mtahitaji vifaa vya kuogelea?” Aliuliza Ramson kwa uchangamfu. “Mimi sina shida ila mwenzangu inabidi umpatie puto maana asije akatupa mitihani hapa hajui kuogelea kabisa.” Alisema Dr.Jackson.

“Hamna shida kabisa Dr,” Alisema Ramson huku akiingia kwenye kibanda kimojawapo na kutoa Puto moja na kumkabidhi Mke wa Dr. nao wakaondoka na kuelekea kwenye maji. Baada ya hapo aliendelea na kazi zake nyingine. Mpaka baada ya muda wa masaa mawili alipoitwa tena na wateja wake hao kwa ajili ya kuwaelekeza bafu iliyowekwa tayari kwa ajili yao ili kujisafisha kwa maji safi. Ramson aliwaelekeza na baadaye walipokuwa tayari walimlipa kwa huduma zote.

Hapa mahali tumepapenda sana pana huduma nzuri na mazingira yake yanavutia. Alisema Dr. Jackson au unasemaje mke wangu?,” Aliuliza Dr. Jackson huku akimgeukia mkewe. “Kwa kweli ni pazuri sana,” Aliitikia na kutabasamu tutakuwa tunakuja hapa kila mara alimalizia Mrs Jackson. “Nashukuru sana kama mmependezewa na huduma zangu na wakaribisha sana,” Alisema Ramson huku akiwasindikiza wakati wakielekea kwenye gari lao.

Baada ya kuingia garini walimpungia na kuondoka taratibu. Ramson akarudi kuhudumia wateja wengine. Kwa ujumla alikuwa na mawazo mengi mazuri kwa jinsi alivyokuwa anapata wateja kila wakati. Kubwa na la kupendeza ni pale wanaposifia eneo lile kuwa ni zuri. Sifa hizo zilichangia sana kutia bidii, katika kuuboresha ufukwe huo. Ramson alikuwa tofauti sana na watu wengi katika namna ya kupokea sifa kwa jambo fulani. Wengine wanaposifiwa hukaa wakarithika na sifa hizo.

Ila Ramson huchukulia kuwa kusifiwa kwake ni changamoto za kumfanya asonge mbele kwa kufanya vizuri zaidi. Dr. Jackson na mkewe walimpa changamoto nyingine, ambayo kwake ilikuwa ni chachu ya kufanya mambo makubwa zaidi. Alipata ari nyingine ya kuboresha huduma ufukweni hapo. Mawazo yake yakawa katika kutafuta jinsi ya kufanya vizuri zaidi ili kuzifikia ndoto zake.

Ulikuwa ni mchana uliokuwa na jua kali pamoja na joto. Mchana huu ulikuwa wa faida sana kwa Ramson kwani ulivuta wateja wengi waliotaka kupunguza joto, kwa kuogelea na wengine kupunga upepo tu ufukweni hapo. Watu wengi walihitaji vinywaji baridi ambavyo vilikuwepo vya kila aina. Akisaidiana na wasaidizi wake katika kuuza aliwauzia wateja wake soda Juice na Ice cream za aina mbalimbali.

Kwa ujumla watu waliburudika sana na kutamani kuja tena katika ufukwe huo kutokana na huduma zake kuwa nzuri. Wakati Ramson akiwahudumia watu mara jamaa mmoja alimsogelea karibu, “Ramson!”Aliita jamaa huyo kwa sauti ya mshangao! Ramson alipogeuka hakuamini macho yake, alikuwa ni Richard rafiki yake. “Richard ni wewe rafiki yangu?” Ramson alisema hivyo na kumkumbatia rafiki yake.

“Kwa kweli leo ni siku njema sana, karibu Richard.” Alisema Ramson huku akimwelekeza mahali pazuri pa kukaa ili wazungumze. “Chidy njoo uchukuwe vinywaji hivi uwapelekee wale watu pale mtu na mkewe sawa?” Ramson alimwagiza kijana wake wa kazi. Njoo hapa rafiki yangu yeye na rafiki yake walikaa kwenye mwamvuli mmoja uliojengewa kwa ajili ya kuleta kimvuli.

“Hatimaye ndoto zako zimetimia Ramson,” Alisema Richard huku akionyesha kumshangaa Rafiki yake. “Ni kweli Richard nashukuru sana kwa ajili ya hatua hii, japo bado ndoto ni nyingi zinazosubiri kutimizwa,” Alisema huku akitabasamu. “Kwa kweli sikutegemea kuona haya ninayoyaona leo. Alisema Richard kisha akatulia kidogo wakati akipokea juisi yake aliyoletewa na mfanyakazi.. kisha akaendelea

“Ulipozungumzia mambo ya Beach mimi nilichukulia kwa uzito mdogo sana. Japo sikudharau maono yako lakini sikufikiri kuwa utakifikia mapema hivi. Hongera sana Ramson.” Alisema Richard huku akiangaza angaza macho kwenye maeneo mbalimbali.“Asante sana rafiki yangu, ndio hivyo maisha yalivyo… Kutumia Fursa ni jambo la muhimu sana.

Kuna Fursa nyingi sana zinazotokea katika maisha ya mtu. Afya njema ni fursa mojawapo kwa upande wake, Ujana pia ni fursa, na mawazo yenye msukumo wa kufanya jambo fulani nayo ni fursa. Kuna aina nyingi za Fursa ila nimetaja hizi chache ili niweze kuzizungumzia. Kwa ujumla wake fursa zote hizi hutokea mara moja moja na hazirudii tena . Mfano ujana: “Ujana unapokuja na mtu akashindwa kutumia ujana wake vizuri ujana huo unapoondoka hauwezi kurudi tena hata kama ungefanya nini!

Nguvu za ujana ni nyingi sana, lakini zinakabiliwa na changamoto nyingi pia. Matumizi mabaya ya ujana kwa njia ya tamaa tu huharibu fursa ya mtu. Wengi wameutumia ujana wao vibaya na kukosa kuweka kumbukumbu nzuri za maisha yao baada ya wao kuzeeka au kufa. Kwa upande wa afya njema ni moja ya fursa tuliyopewa na Mungu.

Matumizi ya afya zetu njema yazingatie kuwa kuna wengi hawajiwezi aidha ni wagonjwa ama wamepungukiwa na viungo muhimu katika miili yao. Ikiwa mtu ni mzima wa afya asipoutumia uzima huo iko siku atakuja kujilaumu; kwa kuwa hata uzee nao utakuwa kikwazo cha kufanya mambo mengi muhimu. Tunapokuja kwenye mawazo yenye msukumo wewe ni shahidi.

Ninakumbuka nilikushirikisha zaidi juu ya maazimio yangu kuhusu kufanya kazi za ufukweni. Najua ulikuwa hujanielewa mpaka tunaachana wakati ule. Ila niliambulia kwako jina zuri sana lililonifaa, kwani uliniita The Beach Man! Kweli rafiki yangu niliamua kuwa mtu wa ufukweni na kuishi ufukweni. Mahali hapa pakawa ndio nyumbani kwangu nimewekeza chochote nilichokipata katika ufukwe huu.”Ramson Alikohoa kidogo kisha akaendelea.

“Kwa kupitia mawazo hayo nimefaulu kutengeneza kituhiki, kitu ambacho kwa maneno tu hakiwezi kuonekana wala kushikika!Karibu sana Ufukweni kwa rafiki yako.” alihitimisha Ramson Hotuba yake. “Asante sana Ramson kwa fundisho lako lenye kuambatana na mfano huu mzuri na halisi. Nimevutiwa na maono yako makubwa sana, unaona mbali sana Ramson.” Alisema Richard.

“Wewe uko wapi sasa?” Aliuliza Ramson. “Baada ya kuachana nilikwenda tena kwa baba mkubwa na kumwomba anisaidie kiasi cha hela za Mtaji ambazo nilitarajia kufungua biashara fulani.Nilikuambia kuwa baba yangu huyo hawezi kuacha kunisaidia, lakini kabla hajanisaidia anatanguliza maneno mengi sana ya masimango. Baada ya masimango hayo hunipatia kiasi kile nilichomwomba au zaidi.

“Lakini safari hiyo niliyomwendea alikuja na jambo tofauti, hakunipa hela bali alinipeleka kuchukuwa kozi ya Uongozi nchini Marekani. Miaka miwili ilinitosha kuajiriwa kwenye kampuni ya usafirishaji iliyoko Jijini Dar-es-Salaam.” Alisema Richard. “Aaaaah! hongera sana rafiki! Ni hatua nzuri sana.” Alisema Ramson. “Asante na hivi ninavyoongea mimi ndiye meneja wa kampuni hiyo ambayo nimeitumikia kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.”

“Hongera sana Richard.” Ramson alimpongeza rafiki yake na kuongea mengi sana kabla hawajaachana. “Kwa hiyo umekuja kumwona baba mkubwa?” Aliuliza Ramson wakati wakiagana. “Ndiyo nimekuja kumwangalia afya yake Yeye kashakuwa mzee sasa.” Alimalizia huku akitabasamu na kupanda ndani ya gari yake tayari kwa kuondoka. “Kwaheri Ramson nitakutembelea tena wakati mwingine.” Alisema. “Asante kwaheri Richard!” Alisema Ramson huku akipunga mkono kuagana na Richard.

Ilikuwa ni siku ya Jumatano mchana Ramson alipopata mgeni. Mgeni huyohakuwa mwingine bali alikuwa ni Mary au Mrs Dr. Jackson. Mary alipoegesha gari lake alimsogelea Ramson mahali alipokuwa amekaa akipunga upepo. Wooooow Mrs Dr. Karibu sana.” Alisema Ramson akimkaribisha. “Asante sana Ramson, naona umepumzika habari za tangu tuachane?” Mrs Dr.Jackson aliuliza huku akijikalisha kando ya Ramson.

“Ninashukuru karibu Mrs. Dr. Leo umekuja peke yako?” Aliuliza Ramson. “Dr. Jackson amepata safari, amekwenda Uingereza kuongeza masomo yake ya Udaktari.” Alijibu Mary. “Atachukuwa muda gani kumaliza amasomo yake?” Aliuliza Ramson huku akijiweka sawa kwenye kiti. “Atakaa huko miaka mitatu.” Alijibu kwa hali fulani ya unyonge kidogo Mary,kisha akanyanyuka na kusimama. “Naomba puto nimekuja kuendelea kujifunza kuogelea.” Alisema Mary.

Ramson alinyanyuka na kuelekea kwenye kibanda cha kuhifadhia Maputo na kumchukulia moja, “Hili linakufaa sana unaweza kulitumia kwa njia zozote, hata kulala juu yake wakati ukichoka kuogelea” Alisema Ramson na kumkabidhi puto lililokuwa kama kitanda. “Lakini ningehitaji uje unifundishe maana kwa kweli sijui lolote kuhusu kuogelea.” Alisema Mary baada ya kupokea puto hilo.

“Sawa nitakuja tangulia kuna mambo niyaweke sawa kwa ajili ya wateja.” Ramson alijibu na kuchukuwa chombo cha kuchotea maji na kwenda kuchota maji yaliyokuwepo kwenye pipa na kujaza ndoo mbili na baadaye aliuzipeleka kwenye bafu mbili tofauti. Baada ya kazi hiyo alimfuata Mary aliyekuwa anachezea maji kwenye kina kidogo.

“Sogea kule mbele kwenye maji mengi.” Alisema Ramson wakati akianza kuinga kwenye maji. Walisogea mpaka kwenye kina kirefu cha maji na Ramson alimfundisha Mary jinsi ya kuogelea kwa muda mrefu. Kwakuwa Mary alikuwa mwepesi kuelewa aliweza kushika mitindo miwili ya kuogelea. Mpaka wanatoka kwenye maji alikuwa anajua kuogelea kiasi. “Ramson nashukuru sana kwa kunifundisha. Wewe ni mwalimu mzuri sana.” Alisema Mary akishukuru. “Asante sana Mary kwa shukrani zako, wewe pia ni mwanafunzi mzuri sana, maana ni mwepesi wa kuelewa unapofundishwa.

Kwa sasa hata nisipokufundisha tena mitindo mingine itatokana na ubunifu wako tu katika kuchezea maji.”Alisema Ramson na kumwelekeza ilipo bafu ili akaondoe maji ya chumvi.“Aaaah! Mi mbona bado nahitaji uendelee kunifundisha? siku moja tu haitoshi kunifanya nijue kuogelea mwenyewe.” Alisema Mary wakati akielekea bafuni. “Sawa Mary nitakufundisha tena siku ukija.” Alisema Ramson.

Baada ya Mary kumaliza kuoga alitoka bafuni na kumuaga Ramson. “Ramson kwaheri naweza kukutembelea siku nyingine.” Alisema wakati akielekea ilipo gari yake. “Karibu Mary ukiweza waalike na marafiki zako ili waje kupunga upepo na kuogelea.”Alisema Ramson. “Kwa hilo usiwe na wasiwasi nitafanya hivyo.” alisema Mary wakati akiingia kwenye gari lake na hatimae kuliondoa taratibu.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)