Mwandishi: Andrew Mhina
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Karibu Mary ukiweza waalike na marafiki zako ili waje kupunga upepo na kuogelea.”Alisema Ramson. “Kwa hilo usiwe na wasiwasi nitafanya hivyo.” alisema Mary wakati akiingia kwenye gari lake na hatimae kuliondoa taratibu.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Mwenyekiti wa kijiji cha Tabu yanini siku moja nyakati za Asubuhi alimtembelea Mzee Kihedu. Alikuwa na mazungumzo mengi lakini moja ya mazungumzo hayo lilikuwa juu ya Ramson. “Bwana Kihedu habari za kijana wetu Ramson? Nilimwona wakati wa msiba wa bibi yake lakini baada tu ya kumaliza mambo yote aliondoka, japo nilihitaji sana kuongea naye.”
Alisema Mwenyekiti. “Kwa kweli ndugu mwenyekiti kijana Ramson anaendelea vizuri sana huko aliko. Sijasikia tatizo lolote juu yake na pia maisha yake yanaendelea vizuri.” Alijibu Mzee Kihedu huku akimimina kahawa kwake na kwa Mwenyekiti. “Unajua bwana Kihedu moyo umeniuma sana baada ya kugundua kuwa Ramson hakuwa mwizi.
Kubwa sana linaloniumiza ni jinsi nilivyomfukuza hapa kijijini, nikishirikiana na wanakijiji. Nilitafuta sana nafasi hii ili nije tu kuzungumza na wewe, ili unikutanishe na Ramson nimwombe msamaha na kuitisha mkutano wa kijiji. Ninakusudia kumtakasa kwa wanakijiji kwa ubaya tuliomzushia.” Alisema mwenyekiti kwa unyenyekevu sana. “Ndugu mwenyekiti ninashukuru kwa kusikia kutoka kwako kuwa Ramson sio mwizi!
Hicho kilikuwa ni kidonda ndani ya moyo wangu, kwa mjukuu wangu kuitwa Mwizi na kukataliwa na kijiji. Ilinigharimu sana kufikiri na kuvumilia maumivu hayo kwa muda mrefu. Ila niseme tu kuwa Ramson kwa sasa yuko vizuri na hana kinyongo chochote na wewe wala wanakijiji. Niligundua hili pale alipokuja kwa ajili ya msiba wa bibi yake.
Baada ya kumaliza msiba alisifu ushirikiano ulioufanya wewe na wanakijiji kwa ajili ya mambo yote ya mazishi. Alikusifu kwa mambo yote hasa jinsi ulivyokuwa mstari wa mbele katika shughuli nzima ya msiba.”“Enhee! alisemaje kuhusu tatizo lile?” Alidakia mwenyekiti! “Nilipozungumzia masaibu yaliyompata, alichosema Ramson ni kwamba kijiji kilitumika kumpeleka mahali ambapo alipaota siku nyingi, ili akaweke makao yake. Aliongeza kuwa kama kijiji kisingefanya hivyo asingefikia ndoto zake hizo. Kwa sasa Ramson anamiliki biashara zake ufukweni huko Tanga. Maisha yake yanaenda vizuri na tayari ameajiri watu kadhaa wa kumsaidia katika biashara na miradi yake.
Katika ufukwe huo anapata wageni wengi sana mpaka wazungu. Kwakweli ndugu mwenyekiti hata Ramson angepewa magari na hela nyingi, hawezi kuja tena kukaa hapa kijijini. Hayo ndiyo niliyoyaona kwake.” Alihitimisha Mzee Kihedu kutoa maelezo. “Hayo ni sawa bwana Kihedu. nafurahishwa na maendeleo yake pia, lakini nitahitaji siku moja aje ili niitishe mkutano na kumwondolea shutuma zile.
Hilo ni deni ninalodaiwa kulilipa kwake na utu wake niliouharibu kwa maneno yasiyo ya kweli.” Alisema mwenyekiti kwa msisitizo. “Sawa ndugu Mwenyekiti nitafanya hivyo, akirudi kuniangalia nitamwambia aje mwonane wenyewe.” Alisema Mzee Kihedu. “Sawa sawa kabisa bwana Kihedu, nitashukuru nikionana naye mwenyewe ili kulizungumzia hilo.”
Alisema Mwenyekiti huku akiweka kikombe cha kahawa mezani na kunyanyuka. “Mbona unasimama ndugu mwenyekiti, bado kahawa ipo tuendelee kunywa kuna mengi ya kuzungumza.” Alisema Mzee Kihedu. “Bwana Kihedu ngoja niende mazungumzo hayaishi. Tutakuwa na muda mzuri wa mazungumzo hayo. Kwa sasa ngoja niwahi shamba, kuna vijana wametangulia na mke wangu kwa kazi ya kuangua nazi. Mama Batuli ana kazi nyingi, naenda kusimamia maswala ya nazi pamoja na ubebaji.”
Alisema Mwenyekiti huku akiusogelea mlango. Mzee Kihedu alinyanyuka na kumsindikiza mpaka nje ya nyumba yake. “Sawa Mwenyekiti wangu nikutakie siku njema.” Aliaga Mzee Kihedu. “Na wewe pia.” Alisema hayo na kuondoka kisha Mzee Kihedu alirudi ndani na kujiandaa kwa majukumu ya siku hiyo mpya.
Asubuhi hii ilikuwa ya harakati nyingi kwa Mary. Alikuwa akipanga hiki na kupangua kile ili mradi alikuwa yuko na shughuli nyingi sana. Mawazo pia yalikuwa mchanganyiko kwenye kichwa chake, ndio maana akajipatia shughuli nyingi hata ambazo hazina umuhimu. Mawazo yake yalikuwa juu ya Beach Man! Mtu huyu wa Ufukweni alimchanganya kwa aina ya maisha yake. Alisikia kuwa pale Ufukweni ni yeye aliyepatengeneza.
Cha kusisimua ni kwamba Kijana huyo alianzisha sehemu hiyo akiwa hana hata hela. Alihamia tu mahali hapo akitokea kijijini kwao, kidogokidogo akajikongoja mpaka kufikia hatua hiyo. Mawazo yake hayakuwa na sababu ya msingi katika kuyachukulia umuhimu wa kiasi kile! Hata siku moja hajawahi kufikiri kuanzisha mradi unaofanana na ule.
Hata yeye angeulizwa ni kwanini anafikiri kwa kiwango hicho juu ya mradi wa Ramson, asingekuwa na jibu la maana. Ila alipokuwa katikati ya mawazo hayo alishtuliwa na simu iliyokuwa inaita. Alipoangalia kwenye kioo cha simu alikutana na Jina la Irene!..“Halo Irene habari za asubuhi? Aliitikia Mary kwa bashasha! “Habari ni nzuri sana Mary nimekumiss sana ndio maana nikakupigia, kama una nafasi uje tujumuike wote kwa chakula cha mchana.” Alisema Irene.
“Asante rafiki yangu ni kama uliyejua kuwa niko mpweke sana leo.” Alisema Mary. “Sawa basi karibu sana ndugu yangu” Alisema Irene na kukata simu. Mary akakusanya nguo na kuzirudisha mahali pake taratibu huku akijiandaa kuelekea kwa Irene. Baada ya kuoga na kujiweka sawa alitoka na kumwaga msichana wake wa kazikuwa anatoka kidogo, angerudi baada ya muda si mrefu sana. Kisha akazama ndani ya gari yake na kuiondoa kwa mwendo wa taratibu.
Mwendo wake ulimfikisha nyumbani kwa rafiki yake kwa muda muafaka, kwani alimkuta akiwa anaandaa chakula mezani. “Woooooow rafiki yangu!” Alisema Irene baada ya kumwona Mary akiingia ndani ya sebule. “Wooooow! Irene mambo vipi?” Aliuliza Mary wakikumbatiana. “Kwa kweli mambo ni mazuri karibu sana Mary. Nimekukumbuka sana asubuhi. Sababu ya kukukumbuka ni juu ya biashara yetu. Niliona kama tunaweza kuiboresha zaidi ingetuingizia faida kubwa sana.”
Unajua ni siku nyingi zimepita bila kukaa kikao cha kujadili habari ya maendeleo ya biashara?” Alisema Irene. “Ni kweli kabisa Irene! Wazo lako ni la manufaa makubwa sana.” Alisema Mary huku akiliendea sofa na kujikalisha. “Mary naona ungekaa mezani kabisa kwa sababu umekuja kwa wakati chakula tayari.” Alisema Irene na Mary alinyanyuka na kusogea mezani taratibu.
“Mwanamke kwa kwenda na wakati wewe! Saa saba kamili chakula tayari mezani!” Alitania Mary huku akijikalisha kwenye kiti kinachokabili meza kubwa ya duara. “Si unajua tena rafiki yangu miili yetu haijengwi na matofali! Chakula ndio kinachotengeneza kila kitu katika mwili wa mwanadamu, usipojijali unafikiri utakuwaje?” Alisema Irene wakati akifunua bakuli la chakula maarufu kama hot port. Baadaye alimsogezea Mary pamoja na mboga, kusudi ajipakulie mwenyewe. Mary alifanya hivyo na baadaye wakaingia katika mazungumzo yao, wakati wakipata chakula.
Mazungumzo ya biashara yalipokwisha waliingia kwenye mada mchanganyiko. Waliongelea lolote waliloona linafaa kuliongelea ilimradi kusogeza muda.“Unajua Irene unapitwa na mengi?” Alisema Mary katika kuanzisha mada mpya. “Yapi rafiki yangu?” Aliuliza Irene huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.“Hivi ulishawahi kufika Mwahako Beach?” Aliuliza Mary kiushabiki. “Wala sijawahi kufika kwani kuna nini cha ajabu huko?” Aliuliza Irene.
“Si ndio rafiki yangu ninakuambia kuwa unapitwa na mambo mengi? Mwahako kuna bonge la Beach! Si unasema hapa Tanga hakuna ufukwe uliotulia? Basi nenda kauangalie Ufukwe wa Mwahako utaupenda mwenyewe!” Alisema Mary kwa namna ya mpiga debe! “Tanga kuna ufukwe wa maana kweli kama fukwe za wenzetu?” Aliuliza Irene. “Kama wapi?” Mary aliuliza pia. “Kama Mombasa?” Unajua Mary mimi nimependa sana fukwe za Jirani zetu wale.” Wamefanya ubunifu wa hali ya juu sana na kujaribu kuwekeza kwa nguvu zote, hadi watalii wakatamani kuwa wanatembelea fukwe hizo.
Mombasa wamepiga hatua kubwa sana kwa njia hiyo.” Alisema Irene. “Ni kweli Irene sio wewe tu hata mimi ni mmoja wa washabiki wa Fukwe za jirani zetu Wakenya. Mara kwa mara mapumziko yetu na Dr. tunapenda kutembelea kwenye Fukwe hizo. Ila wiki kama mbili zilizopita Dr. alinipa habari za kuwepo kwa ufukwe mzuri maeneo ya Mwahako. Na mimi sikuamini kwa kuambiwa tu bali siku tuliyoenda ndipo nilipoamini kwa macho yangu.
Labda wewe pia siku tukienda utakubali baada ya kuona mwenyewe mandhari yaliyopo hapo.” Alisema Mary. “Okay Twende lini? maana umenihamasisha mpaka nimehamasika! natamani nipaone mahali hapo.” Alisema Irene. “Hakuna shida nitakupeleka huko hata kesho ukitaka. Nitaangalia nafasi kisha nitakuambia jioni ratiba yangu.
Itakuwa nzuri sana Irene utafurahi pia kumwona The Beach Man, ni mtu mwenye bidii na mtanashati sana muda wote. Anapendeza sana kama ufukwe wenyewe unavyopendeza!” Alisifia Mary.Nafikiri wewe umeshampenda huyo The beach Man unayemsema, maana unavyomsifia!
Alisema Irene kwa mashaka huku akionyesha mshangao. “Umejaribu kuwa karibu na ukweli, sina la kukubishia ila nahitaji ushauri wako juu ya hili.” Alisema Mary kwa aibu kidogo. “Unataka kuvunja ndoa yako? Mimi simo siwezi kuwa mshauri wako katika hili.” Alisema Irene kimbea huku akijichekesha kwa sauti.
“Hakuna neno rafiki yangu mimi naona ni vizuri kesho tufike huko kusudi ukashuhudie mandhari ya ufukwe mambo mengine tutayaongelea tukiwa katika eneo hilo sawa? Kwa sasa sina maneno mengi ya kuongea.” Alisema Mary. “Vipi wewe kuhusu Shemeji? mmekubaliana ndoa ikafungiwe wapi?” Aliuliza Mary. “Kwakweli rafiki yangu mpaka sasa nimechanganyikiwa.” Alisema Irene wakati akiweka juice mezani.
“Jiwekee juisi unayoipenda kati ya hizi hapa na kama huna chaguo lako hapa sema nikutolee nyingine.” Alisema Irene. akiwa kapanga chupa mbalimbali za Juisi mezani. “”Hizi zote nazipenda nitakunywa yoyote kati ya hizi usisumbuke kutoa nyingine. Alisema Mary. Mwenzangu uko juu kuhusu mambo ya matunda. Juisi zote hizo ni kwa ajili yako tu na msichana wako wa kazi?” Alisema Mary kwa mshangao.
“Kwakweli mimi kuhusu matunda mtu haniambii kitu. Ninatengeneza Juisi za matunda ya kila aina, kusudi kujenga na kulinda mwili. Si unajua kuwa Miili haina spea kwa hiyo tunapaswa kuilinda na kuitunza ili isipatwe na uharibifu.” Alizungumza hayo huku akisogeza glasi kwa rafiki yake. “Nimekuelewa rafiki uko sawa kabisa. lakini nimekuuliza habari ya ndoa yenu mmepangaje naona bado hujanijibu vizuri.” Mary alikumbusha. “Ni kama nilivyokuambia rafiki yangu kuwa ndoa yenyewe ina mambo ya kuchanganya tu.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi