MTU WA UFUKWENI (13)

0
Mwandishi: Andrew Mhina

SEHEMU YA KUMI NA TATU
ILIPOISHIA...
Nafurahi kusikia habari hizo endelea na vipimo kuhusu afya yako na kufuata masharti ya madaktari kuhusu kujitunza na mtoto aliyeko tumboni sawa mke wangu?” Alisema Dr. Jackson.. “Sawa Mume wangu nitafanya hivyo.” Kisha simu ikakatika.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Mawazo yalikuwa ni mengi sana kiasi cha kumkosesha usingizi. Hakujua kuwa atayakwepa vipi masaibu yaliyo mbele yake. Mawazo yake yalikosa kumpa jibu la kuepuka aibu iliyoko mbele yake. Aliona kuwa hakuwa na budi kutumia mbinu zaidi kusudi kuficha tatizo hilo. Lakini ni mbinu gani?

Hakupata jibu na hili ndilo lililokuwa tatizo lake. Mwishowe akaona atafute tena mawazo kwa rafiki yake. Irene rafiki yake alikuwa na mbinu nyingi. Alimshauri aende kumwona Ramson na kukubaliana kuwa mtoto atakayezaliwa awe wa Jackson mume wake ili kumwepushia tatizo.

Baada ya ushauri huo Mary alienda kumtembelea Ramson na kumwambia kuhusu kuficha siri ile kuhusu mtoto atakayezaliwa. “Unajua Ramson ni kweli tulishirikiana hadi mimi kupata ujauzito huu lakini kumbuka kwako na kwangu litakuwa tatizo. Mimi ni mke wa mtu. Ikiwa itajulikana kuwa mtoto huyo ni wa kwako nitakuwa nimekuweka katika wakati mbaya sana na mimi pia ndoa yangu inaweza isiwepo tena.” Alisema Mary kwa utulivu ili kumvuta Ramson amwelewe.

“Ni kweli kabisa Mary hayo unayoyasema lakini unataka kuniambia itaishia tu kuficha siri hii kwa upande wangu? Utafanyaje ili nisahau kuwa mtoto sio wa kwangu wakati ukweli utakuwa unajulikana kati yetu wawili? Unafikiri nitakuwa mjinga kiasi cha kuona mtoto wangu analelewa na baba mwingine, wakati nikijua kabisa kuwa ni damu yangu? Hebu niambie la kufanya ili ninyamaze Mary.” Alisema Ramson kwa utulivu sana lakini kwa uzito wa hali ya juu.

“Ni sawa Ramson umesema kweli kuwa huwezi kuvumilia juu ya hili lakini kumbuka utaniponza mimi na wewe pia utakuwa hatarini. Kwa hiyo nimeona ni vizuri unifichie siri, kusudi tusiingie katika shida. Wewe unaonaje labda pia naomba unipe mawazo yako.” Alisema Mary kwa mtego akihitaji kusikia kutoka kwa Ramson kuwa angesemaje. “Unajua Mary tangu mwanzo nilikataa kuingia katika uhusiano na wewe! nilijua yanaweza kutokea mambo mabaya sana mbeleni.

Lakini kwa sababu tayari mambo yametokea kama hivi ni vizuri ujue kuwa mimi ni mwanamme. Usidhani kuwa mimi ni mwoga kiasi hicho. Siwezi kuikana damu yangu, kama mtu anaweza kuhiyari kufa kwa ajili ya kuilinda familia yake, kwanini mimi niwe mwoga katika kumpigania mtoto ambaye nina uhakika kuwa ni wangu?” Alisema Ramson kwa ujasiri wa hali ya juu na kuongeza mashaka kwa Mary!

“Ni kweli lakini Ramson utaniingiza kwenye shida na mume wangu. Labda naomba sana uifiche siri hii na mimi nitakupa kiasi cha fedha.” Alisema Mary kwa sauti ya kubembeleza.“Hapo ninaweza kukuelewa Mary, lakini ni kiasi gani utanipa kitakachonifanya nisahau mtoto wangu?” Aliuliza Ramson. “Sema wewe Ramson” Alijibu Mary. “Sawa kwa kukusaidia ili usiachane na mumeo nipatie Shilingi million ishirini najua kwenu hela sio tatizo. Nafanya hivyo kwa sababu sitaki matatizo yakutokee. Alisema Ramson kwa kuonyesha huruma.

“Kama nikikupa kiasi hicho hutaifanya siri hii itoke?” Aliuliza Mary huku uso wake ukionyesha tabasamu. “Siwezi kutoa siri ila ikiwa tu utanipa hela hizo zote.” alisema Ramson kwa uhakika. “Sawa Ramson nitakupatia hela hizo lakini kwa awamu, Kesho nitakuletea nusu yake na Dr. Akirudi nitakupatia nusu nyingine maana kuna hela tuliziweka Fixid Account.

Asante sana kwa kukubali kunifichia siri hii alisema Mary huku akimkumbatia Ramson. “Ila jambo moja ukumbuke.” Alisema Ramson kisha akaendelea. “Mumeo akirudi hicho kiasi cha fedha unipatie mapema sana. Hilo ndio sharti kinyume na hapo nitaghairi makubaliano yetu sawa?” ….”Sawa Ramson nitafanya hivyo.” Alisema Mary. Baada ya mazungumzo hayo Mary na Ramson walipatana kukutana kesho yake nyakati za jioni. Kisha wakaagana na Mary akarudi mjini.

Ulikuwa ni mtihani mwingine ambao ulijitokeza tena katika maisha yake. Hakupenda kukosea ila tayari aliingia katika mtego ambao hakupenda awepo ndani yake. Akili yake ilivurugika alipofikiria kuwa itakuwaje ikiwa Dr. Jackson akigundua kuwa amekuwa na uhusiano wa Kimapenzi na mkewe.

Hakupata nafuu yoyote hata pale alipofikiria kuhusu fedha alizomwambia Mary ampe. Kilikuwa ni kiasi kikubwa sana, lakini hakikutosha kumpa amani kwenye hatia ile. Moyo wake ulikuwa hautulii wakati huo. Lengo lake lilikuwa ni kuuhama mji ikiwa mambo yatagundulika. Fedha ile atakayopewa alikusudia kuiweka Benk Dr. Akirudi, azikusanye kwa pamoja na kuukimbia mji. Hayo ndiyo malengo ya Ramson kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake.

Ilipita miaka miwili baada ya uhusiano wa Ramson na Mary. Mtoto alishazaliwa na tayari alikuwa na zaidi ya mwaka mmoja. Alikuwa ni mtoto wa kiume aliyeitwa Lameck. Mara kwa mara Mary alikuwa anaenda Ufukweni na mtoto huyo, akiwa kaongozana Irene rafiki yake. Hata uhusiano wa kimapenzi kati ya Mary na Ramson uliendelea kwa namna ya usiri. Siku moja walipokuwa ufukweni walikuwa na mazungumzo kuhusu mtoto.

“Naona mtoto amekuwa mkubwa sasa, unafikiri ni lini utanimalizia hela zangu ili nimsahau kabisa?” Alisema Ramson huku akimwangalia mtoto wake aliyekuwa amebebwa na Irene. Irene na Lameck walikaa kwenye viti umbali wa mita mia moja, wakati Mary na Ramson wakiwa kwenye mazungumzo yao. “Hilo lisikupe shida Ramson nadhani yote tulishayamaliza kwenye mkataba wetu, nilikwambia usubiri kiasi kilichobaki nikupatie wakati Dr Jackson akirudi nchini.

Ninaamini kuwa unakumbuka hilo.” Alisema Mary kwa namna ya umakini sana huku akimtazama Ramson machoni ili maneno yale yamwingie sawasawa. “Ni sawa Mary lakini jamaa amekaa sana huko au ameongeza tena muda wa masomo yake?” Ramson Aliropoka! “Ramson naamini wewe ni mtu makini sana na unajua kila kitu sina nilichokuficha! Nilikwambia kuwa Dr. Jackson atakaa nchini Uingereza kwa muda wa miaka mitatu.

Mpaka sasa ana miaka miwili na miezi saba. Miezi mitatu tu imebaki atarudi na kila kitu kitaenda kama tulivyopanga sawa?” Alisema Mary. “Sawa Mary nimekuelewa.” Alisema Ramson. “Nashukuru kwa kunielewa Ramson sasa ninaona ni wakati wa kurudi nyumbani kwaheri tutaonana siku nyingine.” Alisema Mary na kusimama kisha akaanza kupiga hatua kumfuata Rafiki yake Irene.

“Sawa nitakupigia simu tuangalie namna ya kuonana tena siku mbili hizi sawa?” Ramson Alimwambia Mary. “Sawa.” Alisema Mary bila kugeuka na baada ya hapo Mary na Irene walinyanyuka na kuelekea lilipo gari lao. Irene alimpungia Ramson Mkono wa kwaheri wakati Mary akilitoa gari ufukweni hapo.

Yalikuwa ni mapokezi mazuri sana yaliyofanywa na watu wachache na wa muhimu katika Uwanja wa ndege. Uwanja huu wa Mwalimu J.K.Nyerere, ulifurika watu wengi jioni hii miongoni mwa watu waliokuwa hapa walikuwa ni Dr.Mudy, Mary na Mtoto Lameck. Dr. Mudy ni rafiki yake Dr.Jackson alikuwepo uwanjani hapa pamoja na Mary na mtoto Lameck ili kumpokea Dr. Jackson. Leo ilikuwa ndiyo siku ya kurudi kwa Dr. Jackson nyumbani Tanzania.

Alikuwa na furaha sana kurudi tena nyumbani, baada ya kuishi kwa muda mrefu mbali na familia yake. Zaidi sana kilichomfurahisha ni juu ya kuzaliwa kwa mtoto Lameck. Shauku ya kumwona mtoto wake ilikuwa kubwa sana. Moyo wake ulikuwa na shauku kubwa sana ya kumwona mkewe mpenzi Mary.

Hakupata picha furaha atakayoipata pindi atakapowaona Mke wake na mtoto wake. Aliona kama ndoto na baraka ya pekee sana kwa familia yake kuongezeka. Shauku yake ilizidi baada ya ndege kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Aliona mchakato wa kukaguliwa mizigo kama inayochelewesha kuonana kwake na familia yake.

Uvumilivu wake ulimsaidia mpaka zoezi hilo likaisha, baada ya hapo akasogelea maeneo ya mapokezi na ndipo alipomwona mke wake na mtoto. Furaha yake ilikuwa kubwa sana kuwaona naye mkewe akiwa na mtoto wake alimkimbilia mumewe na kumkumbatia kwa furaha. “Woooooow!!! Mume wangu mpenzi! Nimefurahi sana kukutana tena.” Alisema Mary akimwachia mumewe baada ya kukumbatiana kwa muda mrefu.

“Mimi ni zaidi mke wangu. Nilikuwa ninaona kama ndege imesimama angani maana nilikuwa na hamu sana ya kuwaona na mtoto wangu mpenzi.” Alisema Dr.Jackson huku akimchukuwa mtoto toka kwa mama yake. “Vipi baba hujambo?” Dr.Jackson alimsalimia mtoto wake. Mara hiyo hiyo alijitokeza Dr.Mudy!“Mzee UK imekukubali sana!” Alisema Dr.Mudy huku akimgusa rafiki yake begani.“Oooohoo! Dr. Mudy!” Alifoka Dr. Jackson kwa furaha!“Ee bwana nimekusahau ghafla naona kitambi kinaanza kutafuta njia mzee!! Inaelekea bongo mambo mazuri sana.” Alisema Dr.Jackson kwa furaha sana baada ya kumwona rafiki yake Mudy.

“Karibu sana rafiki yangu tumekumiss sana mtu wangu.” Alisema Dr.Mudy huku wakiongozana kwenda kwenye gari aliyokuja nayo Mary. Baada ya Dr. Jackson na mkewe na mtoto wao kupanda ndani ya gari, Dr. Mudy naye aliifuata gari yake na kuingia ndani tayari kwa safari ya kwenda nyumbani kwa Dr. Jackson Ostabay mahali ambapo Dr.Jackson alipanga kukaa na mkewe kwa siku tatu ndipo warejee jijini Tanga. Walipofika walizungumza mawili matatu wakati wakipata vinywaji kisha Dr.Mudy aliaga.

“Jamani sasa na mimi ngoja nirudi nyumbani tutaonana kesho baada ya wewe kupumzika ili tuulizane habari za UK. vizuri.” Alisema Dr. Mudy. “Sawa ndugu yangu wewe nenda ukalale kesho jioni itabidi uje ili tuogee mengi.” Alisema Dr. Jackson huku akinyanyuka na kuingia ndani baada ya muda alitoka na mfuko mdogo na kumkabidhi Mudy.“Hii ni zawadi yako Rafiki yangu.

Ninajua kuwa wewe ni mlevi sana wa vitu hivi.” Alisema Dr. Jackson. “Aiiiiiisee Loptop!.. Kwakweli siamini macho yangu!” Alisema Dr.Mudy kwa mshangao wa furaha! “Ndio nimekuletea rafiki yangu japo ucheze cheze Game!” Alisema Dr. Jackson huku akicheka. “Usifanye utani rafiki yangu unajua umenipa zawadi nzuri sana? Hapa Internate kwa sana na Game inapigwa vilevile! Alisema Dr. Mudy kwa utani. “Sawa ndugu yangu tuonane kesho basi alisema Dr. Jackson huku akimtoa nje ya geti na baadaye rafiki yake huyo aliondoka akiwa na furaha tele.

Dr.Jackson na mkewe walikuwa na furaha sana hasa Jackson kwa kumwona mtoto aliyeamini kuwa ni mtoto wake. “Nafurahi sana kumwona mwanangu mpendwa Lameck. Kwakweli hatimaye leo aibu ya kuwa hatuna mtoto imefutika kabisa. Nimepata mrithi wa mali hizi na mtu muhimu wa kuendeleza mali zetu.” Alisema Dr. Jackson kwa furaha isiyo na kifani. Alikuwa akicheza na mtoto wake kwa muda mpaka akaanza kusinzia.

Alinyanyuka na kwenda kumlaza kwenye kitanda chake. Waliongea mambo mengi sana wakiulizana hiki na kile kwa zamu. Baada ya muda mrefu wote walijikuta wamepitiwa na usingizi. Kwa Jackson furaha ilikuwa kubwa sana kwa kuungana na mke na Mtoto wake. Aliyafurahia maisha kwa namna ya ajabu sana.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)