MTU WA UFUKWENI (18)

0
Mwandishi: Andrew Mhina

SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
Tatizo ni kwamba huelewi kuwa ninakabiliwa na hatari kiasi gani nikiendelea kuwepo hapa. Sasa ninataka uchague mawili kwa sasa, kuniletea Fedha zangu mchana wa siku ya kesho au uniletee mtoto wangu. Sitanii Mary!..Labda utajua kuwa sifanyi utani pale utakaposhindwa kuniletea hela zangu hapo kesho kwaheri!”

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Baada ya maneno hayo makali simu ikakatika. Dr. Jackson alishituka sana kusikia maneno hayo! Moyo wake ulimuuma sana baada ya kugundua hata mtoto Lameck ni wa Ramson! Ujasiri na uvumilivu ndio uliomfanya asimwamshe mkewe wala yeye mwenyewe asifanye jambo la ajabu katika kipindi hicho kigumu kwake!

Taratibu hasira zake zilitengeneza machozi huku moyo wake ukiachia maumivu ya aina yake! “Kumbe Lameck sio mtoto wangu, kumbe fedha nilizoambiwa kuwa ni za biashara ni kwa ajili ya kumpatia Ramson ili kuficha siri kuhusu mtoto! Kweli nimefanywa bwege kwa kiasi kikubwa sana!” Dr. Jackson aliendelea kujiwazia huku akiuguza moyo wake uliokuwa na maumivu kama kidonda.

Mawazo ya kupanga miradi yakabadilika ghafla badala yake akaanza kupanga jinsi ya kufanya katika janga hili. Alijua kuwa busara ilihitajika kwa kiwango cha juu sana. Kuchukulia papara suala hili ilikuwa ni hatari sana. Kwa Jackson busara aliiwekea kiwango cha juu sana katika kufanya maamuzi. Aliona mengi yaliyofanywa na watu bila kufikiri jinsi yalivyoleta hasara, katika maisha ya watu hao.

Alimkumbuka rafiki yake Chido aliyeamua bila busara kuua mkewe na hatimaye kujiua mwenyewe, eti kwa sababu alimfumania na House boy wao. Mawazo yake yalimkumbusha jamaa mmoja aliyeitwa Alen aliyekuwa akimiliki biashara nyingi zikiwepo vituo saba vya mafuta ya magari. Jamaa huyu aligundua kuwa rafiki yake mpenzi alikuwa na uhusiano na mkewe na kwamba kati ya watoto aliokuwa nao wanne, wawili walikuwa wa huyo rafiki yake.

Huyo naye alichukuwa maamuzi ya kuwaua watoto wote wa jamaa yake na kumwua mkewe kwa bastola,kisha akakimbia. Baadaye Alen alikamatwa na Polisi akiwa mafichoni na kupelekwa mahakamani. Mahakama ilimkuta na hatia hatimaye alihukumiwa kifungo cha maisha Gerezani. Mali zake alizozisumbukia kwa muda mrefu kwa taabu, aliziacha huku maisha yake yakiwa nyuma ya nondo akiteseka bila kikomo. Haya yote yalipita katika kichwa cha Dr. Jackson. Alifikiria kwa kina kitu cha kufanya ili asilete madhara kwa mtu yeyote.

Mwishowe akaona vema kuwa asubuhi akatoe hela zote alizozitaka mkewe na kumkabidhi. Hizo ndizo zitakazomfanya awabambe pale watakapokutana kwa ajili ya kukabidhiana. Kwa njia hiyo Wezi wake watajihukumu wenyewe na huo unaweza kuwa ndio mwisho wa mkewe kumsaliti. Busara aliyoibuni ni kwamba baada ya kuwakuta jinsi watakavyobabaika na kuomba msamaha mwisho wa yote atatangaza msamaha kwao, bila kusababisha madhara kwa yeyote.

Moyo wa Dr. Jackson uliuma sana kwa fedheha atakayoipata hasa itakapojulikana kwa watu kuwa mtoto aliyekuwa anajivuna naye sio wa kwake. Hali hiyo tena ikaibua maumivu katika moyo wake na maamuzi ya kwanza yakatibuka na kukosa uamuzi sahihi, juu ya jambo hilo.

Machozi yalimtoka pindi alipokuwa akimwangalia mkewe aliyekuwa katikati ya usingizi. Mwisho wa yote alipitisha uamuzi aliouona ni wa Busara zaidi. Alipoangalia saa yake alikuta ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri. Alikesha hapo kitini akiwa amechanganyikiwa kutokana na mlundikano wa mambo. Mary aliamka alifajiri hiyo baada ya simu yake kupiga Alam. Ulikuwa ni wakati wa kuanza majukumu yake ya kumwandalia mumewe chai kusudi awahi kwenda kwenye mizunguko ya siku hiyo.

“Heey! inamaana leo hujalala kabisa! Mbona uko vilevile na nguo zako ulizotoka nazo kazini jana?” Aliuliza Mary kwa mshangao. “Ni kweli sijalala kabisa nimekuwa na mambo mengi sana usiku huu.” Alijibu kwa upole sana Dr. Jackson akiwa kajiinamia mezani, akijifanya kuwa anapitia mahesabu kwenye karatasi.

Lengo lake lilikuwa kuficha uso wake uliokuwa na majonzi. Sawa mume wangu pole sana kwa kazi hiyo nzito, ila ungejipumzisha japo kidogo kazi haziishi. Mwili ndio huo huo, wenyewe hauna spea unatakiwa uupumzishe, kusudi upate nguvu kwa ajili ya kufanya mambo mengine.” Alishauri Mary na kuingia maliwatoni kujiandaa, kwa ajili ya kuanza majukumu yake.

Jackson hakujibu neno ila baada ya mkewe kutoka bafuni,naye aliinuka na kwenda kuoga. kisha akajiandaa na kumuaga mkewe kuwa anaondoka. “Si usubiri kidogo nikuandalie chai mume wangu?” Alisema Mary. “Nina suala muhimu naenda kuweka sawa ofisini kusudi niwe huru baadaye kwenda Bank; nikichelewa naweza nisipate muda wa kufanya mapatano yetu.” Alisema Dr. Jackson na kutoka huku akielekea lilipo gari lake alipanda ndani na kuliondoa gari kwa mwendo wa taratibu.

Dr. Mudy alifurahi kumwona rafiki yake amemtembelea asubuhi hiyo. “Karibu ndugu yangu mbona asubuhi sana kwema huko?” Aliuliza Mudy akijaribu kuchangamka kwa rafiki yake. “Kwema tu kwani ni mara ya kwanza kuja hapa asubuhi kama hivi?” Aliuliza Dr. Jackson kisha alinyoosha mkono ili kusalimiana na rafiki yake. Walishikana mikono na kusalimiana, kisha Mudy akamkaribisha rafiki yake sebuleni.

Baada ya kukaa kwenye kiti Dr. Jackson alimwambia rafiki yake: “Rafiki yangu nimeamini kile ulichokisema. Nimefanya upelelezi baadaye nimedhibitisha jambo lile kuwa ni kweli.” Alisema hivyo kisha akatulia kidogo… kisha akamweleza kila kilichotokea usiku wa jana yake. Dr.Mudy alikuwa anasikiliza kwa makini sana.

“Lakini rafiki yangu una moyo wa uvumilivu sana. mtu mwingine angeshafanya mambo ya ajabu kwa hasira. Sasa ulikuwa unataka nikupe ushirikiano gani baada ya kugundua mambo hayo?” Aliuliza Dr. Mudy kwa utulivu. “Kwako nimekuja ili unipe ushahidi ulionao juu ya swala hili kusudi nipate nyongeza ya hayo niliyoyashuhudia jana.” Alisema Dr. Jackson. “Sawa rafiki yangu.” Alisema Mudy kisha akaenda jikoni kumwita mkewe na kumtaka awaletee kahawa. Kisha akarudi kwenye kiti chake na baada ya hapo akaendelea na mazungumzo..

”Unajua tangu mtoto anazaliwa nilijua kabisa kuwa hakuwa wa kwako. Ila nilinyamaza sikutaka kukuchanganya maana ulikuwa masomoni. Hali hiyo ilininyima rahasana na baadaye nilifuatilia ili nijiridhishe katika mashaka yangu. Kufuatilia kwangu nyendo za shemeji za kila wakati za ufukweni, kukazaa matunda.Siku moja nilienda ufukweni nikawaona Ramson na shemeji wakiwa wanaogelea. Hali hiyo ikanifanya nichukuwe picha kadhaa za ushahidi.

Haikuishia hapo niliendelea kupeleleza na kugundua mengi sana. Mengi ya kutosha ambayo nayo niliyapiga picha. Lakini pia baadaye nikakumbuka tukio la ajali mbaya uliyoipata nchini India, tulipokuwa pamoja masomoni. Baada ya ajali ile ya piki piki uliyoipata baada ya kugongwa na gari, ulipopimwa ulionekana kuwa hungeweza kupata mtoto katika maisha yako. Ushahidi wa hilo ni vyeti hivi vya Hospitali uliyotibiwa. Wakati unapatiwa matibabu ulikuwa hujitambui, kwa namna hiyo kila kitu nilihusishwa mimi kama ndugu yako.

Majibu hayo ya vipimo usingelivikumbuka kwa sababu wakati yanatolewa wewe ulikuwa mahututi kitandani. Nilipewa vyeti vyako na kwa bahati nikasahau kukupatia, nilihifadhi kwenye begi langu. Nilishanga nilipopata habari kuwa Shemeji alikuwa mjamzito. Ndipo nikakumbuka maneno ya Daktari kule India. Kumbukumbu yangu ilinipeleka kwenye cheti nikaamua kukitafuta. Baadaye Mungu sio Athumani nilikipata.

Hiki ndio cheti chako kinachodhibitisha kuwa huwezi kupata mtoto!” Dr. Mudy alimwonyesha rafiki yake cheti hicho… na kumfanya Dr. Jackson aendelee kupigwa na butwaa!..Kisha akaendelea.“Kwa hiyo mpaka hapo nyongeza yangu ni hiyo na ushahidi wangu ni huo hapo. Moyo uliniuma pindi nilipokumbuka jinsi mama alivyokuwa akimsema vibaya mkeo kuwa ni mgumba.

Hali hii ikanipa kuona kuwa labda shemeji alifikia mahali akapimwa na kuonekana kuwa hakuwa na matatizo hivyo akaamua kuzaa nje ya ndoa na kuificha siri hiyo japo kwa fedha ili kuficha aibu yake na yako katika ndoa yenu. Ndio maana akaamua kufanya hivyo!” Alisema Mudy akiwa katika hali ya kumtetea Shemeji yake kusudi rafiki yake asimchukulie maamuzi magumu.”

Hayo niachie mwenyewe acha kumtetea! Dr. Jackson alisema huku akikiangalia kile cheti na picha alizopigwa mkewe akiwa na Ramson Ufukweni. Mara alisikia nyayo za shemeji yake yaani mke wa Mudy akija mezani akaficha zile picha chini ya meza. Mke wa Mudy alimsalimia shemeji yake kwa uchangamfu sana na baadaye alimkaribisha kahawa. Baada ya kuwamiminia kwenye vikombe. Jackson alishukuru kwa kahawa na kuendelea na mazungumzo yake na Dr.Mudy.

“Jambo hilo la kuanza kumtetea shemeji yako achana nalo kabisa. Niachie mimi mchezo mzima nitajua nifanyeje sawa?” Alisema Dr. Jackson wakati akimalizia kahawa yake na kisha alinyanyuka akiwa kashikilia ushahidi wa picha na cheti chake baadaye akaaga kuwa anaondoka. “Sawa rafiki yangu lakini hupaswi kuchukuwa hatua yoyote mbaya. Ninakuamini sana kuwa wewe ni mtu jasiri unayeweza kuvumilia mambo magumu katika maisha.

Sitaamini macho yangu kama utaonyesha kubadilika katika tabia yako ya mwanzoni. Jikaze na uendelee kuwa jasiri na mvumilivu ili mambo haya yamalizike kwa usalama. Naamini baada ya hapo amani itakuwa kubwa katika maisha yenu.Ninasema hivyo kwa sababu ninajua hii ni bahati mbaya tu.” Alisema Mudy maneno ya busara sana kwa rafiki yake baada ya kumwona akiwa na hasira kali. “Okay nimekuelewa nitakuona jioni kukupa michapo kuhusu kile kitakachotokea maana nataka niwafanye wakutane leo.”

Alisema Dr. Jackson huku akiingia ndani ya gari lake na kuliondoa baada ya kuangalia saa yake ya mkononi. Neno la mwisho alilosema Dr. Jackson, Mudy hakulielewa kuwa alikuwa na maanisha nini kusema kuwa alikuwa anataka awafanye wakutane ufukweni leo. Mudy alikumbuka kumpungia mkono rafiki yake wakati akiwaamechelewa sana; badala yake aliona vumbi kiasi lililoonyesha kuwa rafiki yake alishatokomea.

Mary alifurahi sana kupatiwa mzigo wa hela na mumewe. Woooow! nafurahi sana Mume wangu kuona kwamba unanijali kiasi hiki. Asante kwa kuwa Mume mwema kwangu.” Alisema Mary wakati akizipokea hela hizo. “Usijali ni kawaida tu kwa mume kumjali mkewe.

Ila sikai kuna mahali nakimbia nimekuletea tu hizi hela kusudi umpelekee rafiki yako, awahi kufanya utaratibu wa safari ya China au sio?” Aliuliza Dr. Jackson wakati akitoka na kuelekea iliko gari yake. Kwa Mary ilikuwa ni nafuu kwake kuona Mumewe kaondoka ili apate mpenyo wa kupeleka hela zile kwa Ramson. Alijiandaa haraka haraka na baada ya muda alianza safari kuelekea Ufukweni.

Mwendo wake ulikuwa wa kasi sana wakati akienda ufukweni kwani alijua kuwa huenda mumewe angerudi mapema nyumbani asije akamkosa kisha akamfuata kwa Irene nako akamkosa ikawa taabu. Baada tu ya kuondoka Dr. Jackson alipiga simu nyumbani kwa msichana wake wa kazi aitwaye Magreth: “Halo mage mama ameshatoka au bado yupo?” Aliuliza ili kuhakikisha. “Ametoka na gari Muda si mrefu.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)