Mwandishi: Andrew Mhina
SEHEMU YA KUMI NA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Na mimi vilevile aliagizia Mudy na mara hiyo mhudumu akaenda kuwachukulia vinywaji. “Habari za Lushoto rafiki yangu?” Mudy aliuliza wakati akijiweka sawa kwenye kiti. “Habari sio mbaya ni nzuri sana rafiki yangu.Lushoto ni kuzuri sana baridi ya kule kama Uingereza nilikotoka.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Mazingira ya kijani na misitu vimenifanya nijisikie vizuri sana kwa siku hizi mbili. Ninatamani baada ya kustaafu kazi ya udokta nihamie Lushoto nikamalizie uzee wangu huko.” Alisema Dr. Jackson kwa hisia kali. Mara mhudumu alifika na makopo mawili ya Malta Guiness na kuwawekea na glasi kisha akaondoka. “Haya rafiki yangu nimekuja unipe habari ulizosema kuwa ni nyeti.
Kiukweli nimechoka sana nilitakiwa niwe niko kitandani nimepumzika saa hizi.” Alisema Jackson. “Sawa kabisa naona ni vizuri kwenda katika jambo lenyewe.” Alisema Mudy kisha akakohoa kisha akaendelea….”Nina jambo ambalo kwa siku nyingi nimelifanyia utafiti na baadaye nikaona kuwa sio vema kukaa nalo bila kukuambia.” Alitulia kidogo kuona kama maneno yake yanapokelewa namna gani.
kisha akaendelea tena… “Unajua yule Beach Man sio mtu mzuri kwako? Alianza kwa swali ili kuchokoza shauku ya Jackson ya kutaka kujua zaidi. “Sio Mtu mzuri kwangu kivipi?… Usizunguuke sema moja kwa moja hivyo ndivyo ninavyokuambiaga mara nyingi, kuwa kama una habari niambie kabisa. Namna hiyo unaweza kumsababishia mtu shinikizo la damu bila sababu ya msingi sawa?” Aling’aka Dr. Jackson kwa sauti ya juu kidogo. “Nimekuelewa ndugu yangu ila usiwe mkali. “ Habari yenyewe ni kwamba yule Jamaa ana uhusiano wa kimapenzi na shemeji yaani mkeo!” Alisema Mudy huku akimtazama Jackson jinsi atakavyozipokea habari zile.
“Nashukuru rafiki yangu kwa kunipa hizo habari.” Alisema Jackson kwa kujikaza na kuzuia hasira ambayo haijulikani ikiwa ni kwa ajili ya Mudy, au huyo Ramson aliyeambiwa. “Lakini habari zenyewe hizo kwangu siwezi kuziamini kabisa, hata ungeniambia kwa Lugha gani. Mimi na Mary tumetoka mbali sana! Mbali kiasi kwamba chochote unachokisema kuhusu yeye kunisaliti ni kama unaongea Kichina, ambacho sikielewi hata ungefafanua namna gani! Labda nikuage kwa sababu sitaki kusikia zaidi kuhusu hilo ngoja nikapumzike…
”Kwa heri.” Alisema na kunyanyuka kwenye kiti na kuelekea kwenye gari lake. Dr. Mudy alijisikia vibaya sana kwa kutokueleweka kwa rafiki yake. Alijaribu kumzuia lakini haikusaidia lolote. Hata kinywaji Dr. Jackson alikiacha hapo bila hata kukifungua. “Rudi rafiki yangu sijawahi kuzusha jambo lolote kwako na habari hii nina ushahidi nayo.” Alisema Mudy lakini ilikuwa kama anayempigia mbuzi gitaa ili aserebuke, badala yake mbuzi aliendelea kula majani!
Dr.Jackson alielekea kwenye gari yake, kisha baada ya kuingia aliiwasha na kuiondoa kwa kasi kuelekea nyumbani kwake. Njiani alikuwa anafikiria mengi sana kuhusiana na taarifa ile. Upendo wake kwa mkewe ulikuwa juu sana. Yuko tayari kupigana na mtu kama tu wataongea kinyume na mkewe. Dr. Mudy kwake aligeuka adui baada tu ya kumsikia akisema habari kuhusu mkewe.
Maneno yake yalijirudia kwenye mawazo yake kama jinamizi: “Habari zenyewe ni kwamba yule jamaa ana uhusiano wa kimapenzi na shemeji yaani mkeo.”Maneno haya yalikuwa mafupi lakini yanayoumiza sana kuliko hata risasi. Moyo unaumia vibaya sana kuliko maumivu ya mwili. Moyo unapoumia kila kitu kinasimama, maana maumivu yake hushirikiana na kichwa chenyewe. Mudy alimuumiza sana kwa habari zake hizo. “Ningejua kuwa habari zenyewe ni za hivyo nisingeitikia wito wake.” Alijisemea moyoni wakati alipokuwa akipiga honi ya gari kwa ajili ya kuingia ndani ya nyumba yake.
Mazungumzo kati ya Dr. Jackson na mkewe yalifikia mwafaka kuwa Mary atapewa shilingi milioni kumi, kusudi aongezee mwenyewe kiasi kilichobakia; ili Irene aende kufungasha bidhaa nchini China. Hii ni baada ya Mary kujieleza sana na kuonyesha mchanganuo wote wa biashara hiyo. “Fedha yote nitakupatia kesho kutwa maana kesho nitakuwa kazini kuna mwanamke ambaye nimepangiwa kumfanyia upasuaji. Na kama zoezi hilo likimalizika mapema saa saba kamili nitakuwa na kikao na uongozi wa Hospital, kuna mambo muhimu ya kuweka sawa kikazi.
“Ninakuahidi kuwa kesho kutwa mapema sana nitakwenda kukutolea hela hiyo kwenye Akaunti ya Hotel sawa?” Alisema Dr. Jackson kwa upole.“Sawa mume wangu mpenzi asante sana kwa kunijali.” Alisema Mary akifurahia mafanikio hayo na kumpongeza rafiki yake Irene kwa ushauri wake.
“Usijali wewe ni mke wangu. Unadhani mali hizi zote ni za nani kama sio zetu wote pamoja na mtoto wetu?” Alisema Dr. Jackson kwa sauti ya upole sana. Alipotaja habari za mtoto alikuwa kama ametonesha kidonda kwa Mary. Mary alikumbuka vizuri tahadhari ya Ramson, isitoshe kesho yake ndio ulikuwa mwisho wa kumpelekea fedha zake.
Ila alijipa moyo kuwa mara tu ifikapo keshokutwa majira ya saa sita, atakuwa mbele ya Ramson akimpatia Fedha zake zote. Alijua tendo hilo litaondoa shida zote na kumfanya ayafurahie tena maisha yake na mumewe. Hilo ndilo jambo la muhimu sana kwa kuirejesha furaha yake na uhuru moyoni mwake.
Dr. Jackson naye alihuzunika sana moyoni mwake kwa kupata habari za ajabu ajabu kutoka kwa Rafiki yake Mudy. Japokuwa hakuziamini kabisa lakini zilikuwa zinamsumbua kila saa. Moyo wake ulimwuma kwa uchungu kila anapofikiri kuhusu habari zile. Kila wakati alikuwa akijiuliza kama ikitokea kuwa ni kweli mkewe anamsaliti kwa Ramson angejisikiaje? Mahesabu hayo ya ndani kwa ndani yalimfanya kila wakati kukosa raha kabisa.
Naye alijiwekea ahadi ya kutafiti habari zile kwa kina.Kwa fikra zake aliamini kuwa habari zile ni uongo mtupu hazina ukweli wowote. Lakini kwa kujiridhisha ilikuwa ni lazima azifanyie utafiti. Kila mmoja kati yake na Mary alikuwa na fikra zake tofauti na mwenziye.
Fikra zao zikilenga kutafuta ubora wa maisha yao ya ndoa. Mawazo hayo yaliendelea hadi pale walipopotelea ndani ya usingizi mzito. Kila mmoja aliingia katika ndoto mbalimbali zilizousukuma usiku ule hata ikafikia asubuhi. Waliamka wenye mawazo tofauti japo kila mmoja alionyesha furaha kwa mwenzake. Kila mmoja alimpenda mwenzake, kwa dhati.
Jackson aliona ili furaha yake itimie ni pale atakapofanya upelelezi na kugundua kuwa maneno ya rafiki yake yalikuwa ni majungu tu. Hakutaka kuyakubali moja kwa moja na pia hakutaka kuyachukulia mzaha. Kwa upande wa Mary alitaka amlipe Ramson hela zake, kusudi awe huru na vitisho vyake. Hakutaka ndoa yake iingie kwenye matatizo. Alijua kuwa pindi tu atakapomlipa Ramson itampa nafasi ya kuhama kama alivyomweleza mwenyewe. Ikitokea hivyo itampa nafasi nzuri ya kuyafurahia mapenzi yake huku moyoni akiwa huru kwa asilimia nyingi na mumewe.
Ulikuwa ni usiku wa matumaini kwa Mary. Usiku mwingine uliotanguliwa na mchana uliokuwa na mishemishe nyingi, zilizoambatana na kikao kati yake na Irene. Kikao hiki kilikuwa ni kwa ajili ya kutoa asante kwa ushauri alioupokea kutoka kwake. Ushauri uliosababisha Mumewe kuahidi kumpatia kiasi cha shilingi milioni kumi.
“Rafiki yangu sina cha kufanya kwako zaidi ya kukushukuru kwa kunisaidia mbinu hizi. Shinikizo la damu liliniandama wakati wote, hivyo mawazo yalipandana kiasi kwamba sikuweza hata kuwaza kiusahihi.” Alisema Mary kwa furaha na matumaini. “Usijali rafiki yangu ni jukumu langu kukusaidia wakati wa taabu.” Alisema Irene.
Kuna ule msemo usemao: “Akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki wa kweli, Leo nimedhibitisha maneno hayo kwako. Alisema Mary.. Ila sasa mwenzangu leo ndio siku niliyotakiwa kumpelekea Ramson mzigo wake, wakati ahadi yenyewe nimepewa ya kesho. Sijui nifanyeje?” Alisema Mary kwa wasiwasi kidogo. “Usiwe na wasiwasi kesho sio mbali. Mtengenezee Mshtukizo au kwa lugha ya wenzetu Surprise!
Vile anavyofikiri sivyo wakati anafikia kuona kama mambo yamekwama ndipo unapomtokea kwa ghafla na kumkabidhi mzigo wake sawa?” Alisema Irene na Mary akaona ushauri huo ni sawa tu kwa sababu hakukuwa na njia nyingine zaidi. Baada ya mazungumzo hayo waliagana. Mary alirudi nyumbani ikiwa tayari jioni imeshafika. Alimkuta msichana wa kazi akimwogesha mtoto naye aliingia jikoni na kuandaa chakula kwa ajili ya familia.
Mengi yaliyofanyika ndani ya siku hiyo yalimchosha na kumfanya awe na usingizi. Lakini ilibidi ajikaze kwa ajili ya kumsubiri mumewe mpaka atakaporudi. Mnamo saa tatu kamili mumewe alirudi akiwa amebeba zawadi mbalimbali. Vitu hivyo walisaidiana kuviingiza ndani na baada ya kutulia alimwandalia mumewe chakula.
Baada ya kumaliza kila kitu waliingia chumbani kwa ajili ya kupumzika. Hali ya uchomvu ilikuwa imemwandama Mary hivyo alitangulia kupitiwa na usingizini wakati mumewe akiingia kazini katika kupanga malengo yake ya miradi. Dr. Jackson alitaka kuanza mradi mwingine mkubwa lakini alikuwa hajapanga kuwa ni mradi gani.
Usiku huo aliamua kupanga na kuamua kuwa ni mradi gani auanzishe baada ya kupata faida zilizojilimbikiza kwa miaka mitatu. Fedha za Hoteli zilikuwa ni nyingi hivyo zilitosha kufanyia mradi wowote mkubwa. Usingizi ulikata na pale ulipojaribu kuja aliuzimisha na kahawa chungu. Mawazo yake yaligombana ndani kwa ndani wakati alipokuwa akifikiria aina tofauti ya miradi, alizidi kuzama ndani ili kufanya uamuzi sahihi.
Ilipofika saa sita na nusu alishtuliwa na mlio wa simu ya Mkewe. Alivumilia kuona kuwa mwenyewe ataamka kuipokea lakini Mary alikuwa amelala usingizi mzito. Ili kuondoa kero kutokana na kelele hizo aliamua kuichukuwa ili aone ninani mpigaji. Mwanzoni alidhani Irene anampigia rafiki yake kwa ajili ya mpango yao ya kibiashara. Lakini alishtuka alipoona Jina la Ramson kwenye kioo cha simu!
Mawazo ya Dr. Jackson yalienda mbali sana! Iweje Ramson ampigie mkewe simu usiku huu?! Kabla hajaipokea akawa amekubaliana na maneno ya Mudy. Taratibu aliminya kitufe cha kupokelea na kuwa kimya ili asikie mpigaji anataka nini. Mara Sauti ya Ramson ikasikiika upande wa pili:
“Mary Mpenzi hii ni mara ya pili kuniahidi na matokeo yake kumbe umeamua kunidanganya! Patano letu lilikuwa leo mchana uniletee shilingi milioni kumi zangu ili niondoke katika mji huu. Kumbuka nilikwambia kuwa zile Milioni kumi ulizonipatia miaka mitatu iliyopita bado nimeziweka kusudi zinisaidie huko nitakakokimbilia kuanzisha mradi mwingine.
Tatizo ni kwamba huelewi kuwa ninakabiliwa na hatari kiasi gani nikiendelea kuwepo hapa. Sasa ninataka uchague mawili kwa sasa, kuniletea Fedha zangu mchana wa siku ya kesho au uniletee mtoto wangu. Sitanii Mary!..Labda utajua kuwa sifanyi utani pale utakaposhindwa kuniletea hela zangu hapo kesho kwaheri!”
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi