Mwandishi: Andrew Mhina
SEHEMU YA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Mimi kesho ninataka kuhamia mahali pale ili nitengeneze sehemu ya kukaa, huku nikiangalia uwezekano wa nini cha kufanya.” Alisema hivyo kuonyesha msimamo kwa maamuzi yake. “Unataka kuniambia umeamua kujitengenezea mahali pa kukaa pale Ufukweni sivyo?”Aliuliza kwa hamaki Richard!
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
“Ndio rafiki yangu huo ndio msimamo wangu juu ya hilo.” Alijibu Ramson. “Kwa hiyo unataka uwe The Beach Man sio?” Aliuliza tena swali la kichokozi.“Ndio kuanzia sasa niite The Beach Man, maana nitakwenda kuishi ufukweni, nitafanya kazi ufukweni na nitakuwa mtu wa ufukweni kwa ujumla. Hayo ndiyo mawazo yangu na ninayaingiza kazini kuanzia sasa ili yawe ndio sehemu ya maisha yangu.” Alisema Ramson huku akijiandaa kuweka sawa vitu vyake.
Siku hii ilikuwa ni ya maandalizi ya kufua nguo na kujitayarisha kwa safari ya kwenda kwenye makao mapya. Moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kuanza maisha katika eneo lenye changamoto ya kipekee. Amejifunza kuwa mtu wa vitendo sio maneno peke yake. Tendo moja huongea zaidi ya maneno elfu moja. Amejikita kuwa mtendaji zaidi ya kusema tu.
Yalikuwa ni mazingira ya kutisha kutokana na ukimya uliozingira eneo hilo. Ni sauti ya ndege tu pamoja na wadudu waishio kando ya bahari kwenye miti ya mikoko. Vichaka vilikuwa ni vingi ila ufukwe ulikuwa ni mzuri sana. Kulikuwa na nafasi ya kuweka vibanda na kutayarisha mandhari nzuri sana ya kupendeza.
Kando ya miti mikubwa pembeni ya mwishilizio wa maji ya bahari alijenga kijumba chake kwa kikata miti imara na kuikita, hatimaye kuizungushia fito. Alikuwa na kamba za kutosha katika kufunga fito hizo, kisha alienda kijijini Mwahako na kununua makuti, kisha aliezeka kibanda chake chenye vyumba viwili.
Baada ya kukamilisha zoezi lake hilo lililochukua wiki nzima, alikaa ili ajipange jinsi ya kuanza mikakati yake.Siku moja akiwa nje ya kibanda chake alijiwa na mgeni. Mgeni huyo alikuwa ni Ringo. Ringo aliwahi kuishi katika kijiji cha Tabu yanini, lakini aliondoka kijijini hapo zamani kidogo. “Ohooo!! karibu Mr. Ringo.” alisema Ramson akimkaribisha jamaa huyo, aliyekuwa ameduwaa kwa mshangao baada ya kuona kijumba maeneo hayo.
“Asante! Ehee umenijuaje jina langu? mimi sikukumbuki.” Alisema Ringo huku akimtazama kwa mshangao Ramsoni. “Mimi ni mjukuu wa Mzee Kihedu anayeishi katika kijiji cha Tabu ya nini. Ninakujua kwa sababu ulikuwa unaishi pale kijijini, japo uliondoka zamani kidogo. Pia nilisona darasa moja na mdogo wako Bwizo.” alihitimisha maelezo Ramson. “Ni sawa ninakukumbuka sasa. ila ulikuwa hutaki kujichanganya na vijana wenzio ulikuwa ukiambatana na babu yako muda wote. nakukumbuka japo kweli ni siku nyingi sana.” Alisema Ringo. “Nashukuru kwa kunikumbuka karibu kiti Mr. Ringo.” Alimsogezea kigogo na yeye akarudi kuketi kwenye gogo kubwa la mnazi. “Asante haya na huku umekuja kufanya nini?” Aliuliza Ringo huku akijikalisha kwenye kigoda hicho.
“Ni hadithi ndefu sana kaka.” Alimhadithia habari yote hatua kwa hatua. “Ndio hivyo baadaye nimeamua kujijengea kibanda hapa, ili nianzishe maisha yangu peke yangu.“Mmmmh! pole sana dogo. Ninayajua matatizo ya pale kijijini. Watu ni wavivu sana na pia hawataki kujisumbua kwa lolote. Nashangaa kwa hatua hiyo iliyofikia kwamba pamoja na wizi unaoendelea pale bado hawataki kujishuhulisha kutafuta wahalifu, badala yakewameridhika tu kuwa wewe ndiye mwizi wao!
Kwanini wasichunguze basi kuwa katika wizi huo unaoufanya unashirikiana na nani? Maana haiwezekani wizi ukafanyika kijiji kizima, kila wakati na mhusika akawa ni mtu mmoja tu!Alisema Ringo kwa masikitiko. Kaka hii naijua ni njama za baadhi ya watu ambazo zimefanywa dhidi yangu. Njama hizi zimefanyika ili kuficha ukweli wa nani wanahusika kwenye uhalifu unaofanyika. Vijana wengi kijijini ni wavuta bangi, wanakaa tu maskani bila shughuli yoyote.
Hii inatokana na Uvivu! Watu hawana kazi ya kufanya wanasubiri nazi tu! Nazi zenyewe ziko wapi, wakati tayari minazi imeshazeeka?” Unafikiri watu watafanya nini wakati hawana kazi za kuwapatia kipato? Alisema Ramson kwa uchungu kidogo! “Hiyo ni kweli dogo ninakubaliana na wewe kwa uchunguzi ulioufanya. Tangu mwanzo yule kijana Alen alikuwa ni mkorofi na mwizi mkubwa. Alikuwa anashirikiana na baadhi ya vijana palekijijini kuiba mazao ya watu. Nafikiri kama bado yupo kijijini pale hilo ndio kundi hatari kwa wanakijiji. Nashangaa wanakutwisha mzigo ambao sio wa kwako.
Lakini kuna sababu gani ya kuja kuishi huku Ufukweni tena porini peke yako? Huoni kuwa ni hatari sana?” Aliuliza kwa mshangao Ringo. “Bwana kaka nina mpango wa pekee sana mahali hapa. Mtazamo wangu kwa haraka ukiusikia unaweza kuuchukulia kama ndoto fulani, lakini nataka niifanye ndoto hiyo kuwa kweli.” Alisema kwa hisia kali Ramson.“Ehee! ndoto gani hiyo dogo?”Alidakia na kuuliza Ringo.“Hapa nataka nipatengeneze baadaye pawe Ufukwe Utakaotembelewa hata na watalii kutoka ulaya.
“Kwa hatua ya kwanza kabisa nataka nitengeneze vibanda vingi vizuri na kununua mipira ya ndani ya magari na kuijaza upepo kwa ajili ya kuwafundishia watu kuogelea.” Ramsoni alieleza mpango wake wote kuhusu makusudi yake. “Ninakuelewa dogo na wala hilo sio ndoto ni jambo linalowezekana, mbona kwa wengine yamewezekana itashindikana kwako kwanini?
Mimi ninakupongeza na pia ninakuunga mkono mia kwa kwa mia, niko tayari pia tushirikiane ukitaka.” Alisema Ringo akimtia moyo Ramson juu ya wazo lake.“Mimi sina neno ndugu yangu, hilo ndilo ninalolihitaji angalau niwe na mtu tutakayepeana mawazo kwa kila jambo katika mikakati hii.” Alisema Ramson kwa shauku kubwa. “Mimi nilikuja mjini toka kijijini kwa nia ya kutafuta kazi. Alianza kujieleza Ringo… kisha akakohoa na baadaye akaendelea…”Nimetafuta kazi na baadaye nikapata hizi za kujenga. Nimekuwa saidia fundi kwa kipindi kirefu mpaka sasa kidogo ninajua kujenga lakini kazi kwa kweli hakuna. Nimekaa muda wa mwezi mmoja lakini bado sijapata kazi. Kutokana na kukosa kazi kwa kipindi chote hicho imeamua kujishughulisha na uvuvi.
Hiyo ndiyo kazi yangu, wakati mwingine ninanunua samaki na kwenda kuwatembeza kijijini.” Alitoa maelezo marefu Ringo, mwishowe wakakubaliana washirikiane katika kazi ya uvuvi na ujenzi wa ufukwe huo. Kaka huku ndio kufanya kazi kwa malengo. Sio unafanya kazi fedha inayopatikana unaitumia tu na kesho unarudi tena kazini kuanza moja.” Alisema Ringo akimaanisha kuwa hela yao itakuwa ikitengenezea kitu kitakachosababisha mafanikio makubwa sana katika maisha yao.
“Ni kweli kabisa. nafikiri huu utakuwa ni mradi utakaowavutia watu wengi kuiga na baadaye mabadiliko yatatokea katika Fukwe zetu zote katika pwani hii.” Ramson aliongea hivyo na baadaye alinyanyuka na kumtaka Ringo waende kutafuta chakula kwani giza linaingia.
Kelele nyingi zilisikika alfajiri na mapema katika mtaa mmoja wa kijiji cha Tabu ya nini! Kelele hizo zilivuma kila mahali kwani zilikuwa kelele zilizochanganyika na mayowe. Watu wenye masikio ya udadisi waliyatega ili kusikiliza kuwa kelele hizo ni za nini? mara haikuchukuwa muda bila kusikia sauti ya Weziiiii!! Hili lilimfanya hata mtu angekuwa mvivu namna gani kuamka kitandani na kwenda kushuhudia mwizi ninani.
Kila mtaa walisikia sauti hizo nao wakaitikiana na kujikusanya ili kuwaandama wezi hao ili kuwaadabisha. Wingi wa watu wenye hasira ulisaidia kukamatwa kwa vjana watatu waliojulikana vema kijijini hapo. Inasadikika walikuwa wameiba mbuzi wawili wa Mzee Amana, majirani wa mzee huyo ndio walioshtuka walipowaona wakiwatoa kwenye banda lake.
Kelele za mwizi ziliwashtua wezi hao na kuanza kukimbia. Lakini mara tu baada ya kusikia sauti hizo wanakijiji walitoka kwa wingi wakiwa na dhana za kila aina. Mwisho wa yote Vijana hao walikamatwa karibu na kisima cha maji wakitaka kukimbilia nje ya kijiji hicho. Hasira za wananchi zilikuwa kali sana ila baada ya kuona kuwa vijana hao ni watoto wa Viongozi wa kijiji, walisita kuwapiga zaidi na kutaka kuwapeleka moja kwa moja kwenye ofisi ya kijiji.
Karibu kijiji chote kilikusanyika Kituoni hapo, ili kushuhudia watu waliokuwa wakiwasumbua na kuwakosesha usingizi kila siku. Katika mkusanyiko huu hata Mzee Kihedu na mkewe Bi Namkunda walikuwepo. Vijana wale waliokuwa wamefungwa kamba walikuwa wamekalishwa katikati ya umati mkubwa wanakijiji, kila mmoja akiwashangaa! “Sio mtoto wa Mtendaji yule!” Aliuliza mwanamke mmoja kwa hamaki baada ya kumwona Alen, akiwa amejiinamia huku damu zikiwa zinamtoka katika majeraha machache usoni mwake.
“Na yule pale umemwona?” Aliuliza mwenzake akinyoosha kidole kwa Rama aliyekuwa amefunika uso kwa shati lake. “Mmh! yule si amejifunika? Jamani wafunueni tuwaone wanaotuhangaisha katika kijiji hiki.” Alisema mama mmoja wa makamo, Askari wakawasogelea vijana wawili waliokuwa wamejifunika na kuyaondoa mashati waliyokuwa wamejifunika. “Aaaa! kumbe ni Watoto wa Viongozi wetu wote?” Abuu alikuwa ni mtoto wa Katibu wa kijiji, Rama alikuwa ni mtoto wa Mwenyekiti ambapo Alen alikuwa ni mtoto wa Mtendaji wa Kata. Walitumwa vijana wawili kwenda kumwita Mwenyekiti. Wanakijiji walitaka kusikia uamuzi wa kiongozi wao juu ya wezi wale, mmoja wapo akiwa ni mtoto wake mwenyewe. Kwakweli ilikuwa ni aibu sana kwa viongozi wa kijiji hiki; ilikumbukwa kuwa Kijana Ramson alifukuzwa kijijini hapo akidaiwa kuwa ni mwizi, lakini leo ukweli umebainika.
Hali ilikuwa ni tete sana. Uamuzi haukuweza kujulikana mapema utakuwaje. Wajumbe waliotumwa kwa mwenyekiti walirudi na ujumbe kuwa Mwenyekiti anasema vijana hao wawekwe mahabusu. Askari waliwasweka ndani na kuwaacha wananchi kutawanyika.
Kila mmoja aliguna kivyake wengine waliridhika kwa hatua hiyo. Lakini wengine walilalamika, walitaka Viongozi hao wajitokeze mbele ya wananchi ili wasikie maamuzi yao juu ya watoto wao. Hii inatokana na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi ya Ramson, walitamani kuona kuwa hatua iliyochukuliwa kwa Ramson inachukuliwa pia kwa watoto wa Viongozi hao wa kijiji. Hata hivyo malalamiko yao hayakuweza kubadilisha maamuzi ya wakubwa wao.
Baada ya miezi mitatu tayari ufukwe wa Mwahako ulikuwa unaonyesha sura fulani. Sura waliyoihitaji itokee kusudi kuwapatia wateja wazuri watakaokuja kuogelea na kujipatia baadhi ya bidhaa ufukweni hapo. Asubuhi vijana hawa Ramson na Ringo walikuwa wakinunua samaki na kwenda kuuza kijijini. na baada ya kazi hiyo walirudi Ufukweni hapo ili kuendelea kujenga vibanda. Vibanda walivyokuwa wakijenga kwa ajili ya kazi vilifikia kumi.
Vilikuwa ni vizuri na vyenye kukidhi haja ya wateja watakaokuja kutaka huduma ya kuogelea. vibanda hivi vilikuwa ni bafu kwa ajili ya kuondoa maji ya chumvi kwa waogeleaji. Sambamba na vibanda hivi waliweka vihema vya kuweka vimvuli kisha walitengeneza vimeza vya kuwekea vinywaji. Mahali hapo palifaa sana kupumzikia hata kama watu wengine hawakutaka kuogelea, watakaa mahali pale na kununua vinywaji.Ramson na Ringo walilazimika kuweka vinywaji ili kuwavutia wateja zaidi.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi