NISAMEHE LATIFAH (18)

0
Mwandishi: Nyemo Chilongani

SEHEMU YA KUMI NA NANE
ILIPOISHIA...
Huko, Latifa alijikuta akibubujikwa na machozi, hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa wakipitia mateso makubwa kama alivyokuwa watu hao. Wengi walikuwa wagonjwa, madaktari walikuwepo kwa ajili ya kuwahudumia lakini kutokana na idadi ya wakimbizi kuwa wengi, hata wale madaktari walionekana kuwa wachache.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
Siku hiyo napo akashinda hukohuko, baada ya kumaliza kila kitu, wakarudi Kigoma Mjini ambapo wakachukua ndege na kuanza safari ya kwenda Dar es Salaa, sehemu ambayo alizaliwa Latifa, sehemu kulipokuwa na watu wengi aliokuwa akiwachukia.

Ulikuwa ni muda wa kuhangaika, kujutia kile kilichotokea na pia huo ulikuwa muda wa kulia na kusaga meno. Msichana aliyekuwa amemkataa ndiye aliyekuwa gumzo duniani, ndiye aliyesemekana kuwa na utajiri mkubwa kuliko vijana wote waliokuwa na umri chini ya miaka thelathini.

Ibrahim aliumia moyoni mwake, mafanikio ya Latifa yaliuumiza mno moyo wake, akawa mtu aliyekosa raha, amani na furaha, kila alipokuwa akikaa, alijikuta akijilaumu kwa ujinga aliokuwa ameufanya.

Latifa alikuwa msichna mzuri, mwerevu, mwenye akili na kuchanganua mambo, mbali na sifa hizo zote, msichana huyo alikuwa na sifa moja kubwa kwamba alikuwa akimpenda. Alipewa upendo wote, alithaminiwa kwa kiwango cha juu kabisa lakini badala ya kuupokea upendo ule, baada ya kuona namna gani alithaminiwa, mwisho wa siku akaona vyote hivyo havikuwa na thamani, upendo haikuwa sababu ya kuendelea kumpenda, akaamua kumuacha, akaamua kumliza, akaupa kidonda moyo wa msichana huyo, pasipo kuwa na huruma, akamwambia achukue taimu yake na yeye abaki na Nusrat, msichana aliyeamini kwamba angeishi naye milele.

Kama kulikuwa na watu waliokuwa na maumivu makali duniani, Ibrahim alikuwa wa kwanza, alilia, macho yakawa mekundu, alijuta na kujuta lakini ukweli haukubadilika, kila kitu kilibaki kilekile kwamba aliacha nazi, akajiona mjanja wa kuchagua na mwisho wa siku mikono yake ikaangukia kwa koroma.

Nusrat, yule msichana mrembo, yule msichana aliyemwambia kwamba angempenda miaka yote, leo hii alikuwa akiishi naye kimagumashi, maisha na wanaume wengine yakamteka na mwisho wa siku kujikuta akitumia muda mchache sana kuwa naye.

Ibrahim hakuficha, alimwambia mzee Deo juu ya Latifa, yule msichana mrembo aliyekuwa akivuma sana, msichana aliyekuwa bilionea.

“Msichana mwenyewe huyu hapa,” alisema Ibrahim, alikuwa akimwambia mzee Deo.

“Msichana gani?”

“Yule niliyemuacha kwa ajili ya huyu fisi,” alisema Ibrahim.

“Unamaanisha Latifa?”

“Ndiyo!”

“Sasa ilikuwaje mpaka ukamuacha mwanamke bilionea?”

“Ni ujinga, kipindi kile hakuwa na kitu, alikuwa msichana aliyejielewa, ila huyu nguchiro akanishawishi mpaka nikawa naye,” alisema Ibrahim huku akishindwa kulizuia chozi lake kububujika mashavuni mwake.

“Pole sana aisee! Latifa ni msichana mrembo, kama ningekuwepo siku hiyo, hakika ningekupiga vibao, kwa mbali anafanana na Nahra kipindi kile alichokuwa msichana wangu,” alisema mzee Deo.

“Nahra huyo mwanamke uliyezaa naye?”

“Ndiyo! Ila duniani mara nyingi watu huwa wawiliwawili,” alisema mzee Deo pasipo kujua kama yule aliyekuwa akimzungumzia alikuwa binti yake wa damu.

Ibrahim alijitolea kumsaidia mzee Deo, mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, kitu cha kwanza alichokifanya ni kumpeleka nyumbani kwake huku mzee huyo akiwa na mguu moja.

Japokuwa mke wake alikasirika sana juu ya ujio huo lakini Ibrahim hakutaka kujali, alijisikia kumsaidia mzee huyo siku zote za maisha yake. Siku ambayo mzee huyo alikuja nyumbani hapo, mke wake, Nusrat alilalamika sana mpaka kufikia hatua ya kutaka kupigana lakini msimamo wa Ibrahim ukawa huohuo kwamba mzee Deo hakutakiwa kuondoka nyumbani hapo.

Baada ya siku kadhaa, wakapata taarifa kwamba Latifa alikuja nchini Tanzania na safari yake ilianzia mkoani Kigoma. Moyo wake ulifarijika mno, alitamani kuonana na msichana huyo, si kwa lengo la kumwambia wawe pamoja, kitu alichokitaka ni msamaha kutoka kwa binti huyo tu.

Alimsubiria kwa hamu kubwa, mpaka siku ambayo ilitangazwa kwamba msichana huyo aliingia jijini Dar es Salaam na watu zaidi ya elfu kumi walikwenda kumpokea uwanja wa ndege.

Ibrahmi hakutaka kukaa nyumbani, alitaka kwenda huko, naye awe mmoja wa watu waliokwenda kumpokeaLatifa. Kutokana na idadi kubwa ya watu, hakupata nafasi ya kufika mbele kabisa, alisimama kwa mbali huku akimwangalia msichana huyo ambaye alikuwa na mwanaume asiyemfahamu kabisa, moyo wake ulimwambia kwamba mwanaume huyo alikuwa mpenzi wake.

Ibrahim hakumsogelea, hakutaka kuonekana, kumuona Latifa, moyo wake ukaridhika kabisa, alichokifanya ni kugeuka na kurudi nyumbani. Njiani mawazo yalimsumbua mno, hakuamini kama kweli Latifa alikuwa vile aliyokuwa, kila alipokuwa akiufikiria ubilionea aliokuwa nao na umaarufu, aliona kwamba hata yeye pia angekuwa bilionea kwani wangechangia utajiri huo.

Alipofika nyumbani, alishangaa kuona mzee Deo akiwa nje, alikuwa akililia kama mtoto mdogo, damu zilikuwa zimetapakaa kila kona, mguu wake ambao ulikuwa haujapona inavyotakiwa ulikuwa umetoneshwa.

Ibrahim alipomuona, akamkimbilia kule alipokuwa, akainama na kumwangalia mzee huyo ambaye alikuwa na kipande cha mguu kutokana na kukatwa kwa sababu ya kansa. Alishindwa kuvumilia, akajikuta akitokwa na machozi.

“Vipi tena?” aliuliza Ibrahim.

“Mke wako.”

“Kafanya nini?” aliuliza Ibrahim huku akionekana kuwa na hasira.

“Amenifukuza kwako, kanitupa hapa nje,” alisema mzee Deo.

“Hebu subiri!”

Ibrahim akasimama na kuufuata mlango, akataka kuufungua lakini mlango haukufunguka, ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Wakati akiendelea kuugonga, hapohapo kwa chini akaona kikaratasi kikiwa kimepenyezwa chini mlangoni, akakichukua na kuanza kukisoma, kiliandikwa maneno machache sana yaliyosomeka ‘Sitaki nimuone huyo mzee mchafu nyumbani kwangu! Ukijifanya kiburi, hata wewe utaondoka, hujachangia hata tofali humu.’

Ibrahim akahisi moyo wake ukichomwa na kitu chenye ncha kali, aliumia mno, alijikuta akikunja ngumu na kukichanachana kikaratasi kile. Maneno yaliyoandikwa katika karatasi ile yalikuwa ya kweli kabisa kwamba hakuchangia hata tofali ndani ya nyumba ile.

Ibrahim akamfuata mzee Deo, akamnyanyua na kuanza kuondoka naye. Mzee huyo alikuwa na maumivu makali, bado damu zilikuwa zikimtoka katika kipande cha mguu alichokuwa nacho, alichokifanya ni kumpeleka hospitali.

Safari ya kwenda Dar es Salaam ikaanza rasmi, ndani ya ndege bado Latifa alionekana kuwa na mawazo lukuki, penzi lake kwa Dominick lilichanya kiasi kwamba akawa haoni wala hasikii.

Walipofika Dar, idadi ya watu elfu kumi walikuwa wamefika uwanjani hapo, ndege ile ilipoanza kutua, kila mmoja alionekana kuwa na furaha, vibendera vidogo vikaanza kupepewa, watu waliovalia fulana zilizokuwa na picha za Latifa wakajisogeza mbele kabisa.

Uwanjani hapo Latifa alikuwa amepewa heshima kubwa mno, Waziri Mkuu, bwana Abdallah Kibonde alikuwa amefika kwa ajili ya kumpokea msichana huyo huku kukiwa na kundi la watoto watatu ambao waliletwa kwa ajili ya kumkabidhi maua kama ishara ya heshima na kumpenda.

Kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo na pote alipopita Latifa kilikuwa kikirushwa laivu katika mashirika mbalimbali ya habari kama CNN, BBC, Aljazeera na mengine mengi kwani huyu Latifa alikuwa mtu mwenye nguvu kwa kipindi hicho, mtu aliyeleta mapinduzi makubwa mno.

Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Dominick alikuwa akikifuatilia kwa karibu zaidi. Alifurahi kuwa karibu na Latifa, kwake, alionekana kuwa msichana mwenye nyota kubwa ya kupendwa.

Miongoni mwa watu wengi waliokuwepo mahali hapo, walikuwa waandishi wa habari ambao mikono yao ilikuwa na kamera na walikuwa wakiendelea kufanya kazi yao ya kupiga picha kwa kila kilichokuwa kikiendelea.

Kila mmoja akafurahia, kumuona Latifa nchini Tanzania, ndani ya nchi aliyozaliwa kulimfurahisha kila mtu. Katika kipindi cha nyuma, aliondoka nchini Tanzania kama mtu wa kawaida, hakukuwa na mtu aliyemthamini, alionekana kuwa si kitu ila leo hii alikuwa amerudi tena, alipokelewa kishujaa zaidi ya walivyokuwa wakipokelewa viongozi wengine.

“Unajisikiaje kuwa Tanzania?” aliuliza mwandishi wa habari.

“Sina la kuongea, naomba mniache, moyo wangu una furaha mno,” alisema Latifa huku akionekana mwenye furaha mno, machozi yalikuwa yakimbubujika.

Hapohapo akachukuliwa na kuingizwa ndani ya gari la waziri huyo kisha safari ya kuelekea hotelini kuanza. Garini, Latifa alijisikia fahari mno, maisha yake yakaanza kurudi nyuma, kipindi alichokuwa akiishi Manzese kwa mama yake mlezi, bi Semeni aliyekuwa kaka yake mzee Issa ambaye kila siku alimchukulia kuwa baba yake.

Leo hii alikuwa ndani ya gari la heshima, miongoni mwa magari yaliyopandwa na viongozi wakubwa nchini. Moyo wake ulifurahi mno, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine alihisi yupo ndotoni.

“Latifa…” aliita waziri, bwana Kibonde.

“Ndiyo mheshimiwa.”

“Umeliletea sifa taifa hili, japokuwa Wamarekani wamekuwa wakikung’ang’ania lakini utaendelea kuwa Mtanzania,” alisema bwana Kibonde.

“Nashukuru sana! Ninajisikia kupendwa, ninapenda na kuvutiwa kwa kila kitu kinachotokea katika maisha yangu, kama nilivyowasaidia watu wengine, ningependa niwasaidie na Watanzania pia,” alisema Latifa huku akiachia tabasamu.

“Mama yupo hai?”

“Hapana! Alifariki miaka mingi iliyopita baada ya kuugua Ugonjwa wa UKIMWI, niliambiwa kwamba alikuwa mlevi mno,” alijibu Latifa na kubaki kimya, machozi yakaanza kumlenga.

“Pole sana! Na vipi baba?”

“Sijajua yupo wapi, nahisi amekwishakufa!”

“Kwa nini uhisi?”

“Sikuwahi kumuona, niliambiwa na baba yangu mlezi kwamba baba alimfukuza mama baada ya kugundua kwamba alikuwa mjauzito, tena hapo ni baada ya mama kufukuzwa nyumbani na wazazi wake kisha alikuwa na mimba ya mtu mweusi,” alisema Latifa.

“Pole sana! Kwa hiyo hujui kama baba yako yupo hai au la?”

“Sijui chochote kile.”

Waliendelea kuzungumza ndani ya gari, Dominick ambaye naye alipewa heshima kubwa alikuwa ndani ya gari hilo, hakuzungumza chochote kile, alibaki kimya huku masikio yake yakiwa makini kusikiliza na ubongo wake kuwa makini kukariri.

Safari ile iliendelea mpaka walipofika katika Hoteli ya Kilimanjaro, wakateremka na kisha kuingia ndani. Hakukuwa na wateja wengi, wale waliokuwepo, walitakiwa kubaki haohao na hata wale waliotaka kupanga hotelini, hawakuruhusiwa mpaka Latifa atakapoondoka.

Ratiba ilikuwa imekwishapangwa, Latifa alitakiwa kukaa hapo hotelini mpaka kesho yake ambapo angechukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huko, angefanya ziara ya kuzungukazunguka kwa wagonjwa kisha baadaye kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na mwisho kabisa kuitwa katika Kituo cha Televisheni cha Global.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)