Mwandishi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Madaktari wakawa wanapishana mlangoni, wengine waliingia na wengine kutoka. Mgonjwa aliyeletwa kwao alionekana kuwa wa maana sana, ilikuwa ni bora kuleta utani kwa mgonjwa mwingine lakini baba yake Latifa.
Baada ya msaa mawili, mlango ukafunguliwa na daktari kutoka, akawaita watu hao ofisini kwake kwa lengo la kuzungumza nao. Walipofika huko, akawaweka chini.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Kati ya watu waliokuwa na hamu ya kumsikiliza Latifa alikuwa Ibrahim, alijua kwamba angeumia hasa mara baada ya kumsikia msichana huyo akizungumzia kile kilichopita, hakutaka kujali sana, alichoamua kipindi hicho ni kumsikiliza tu.
“Hali ya mgonjwa si mbaya, alitoneshwa tu kidonda chake,” alisema Dk. Mimi, mwanamke mzuri mwenye umbo la kuvutia.
“Ila ninataka kuzungumza naye, naweza kufanya hivyo?”
“Hakuna tatizo, unaweza ila kama baada ya saa moja hivi, atahitaji muda wa kupumzika,” alisema Dk. Mimi.
“Sawa!”
Kusubiri halikuwa tatizo kabisa, alitaka kumsikia baba yake akizungumza kile alichokuwa akitaka kuzungumza. Alitaka kusikia kile ambacho hakuwa amekisikia kuhusu mama yake, kile alichosema Ibrahim kwamba mzee huyo alikuwa na la ziada.
“Nyamaza Latifa,” alisema Dominick huku akimvuta Latifa upande wake.
Walitulia kwa muda wa saa moja na ndipo walipoambiwa kwamba wangeweza kumuona mgonjwa wao. Wakainuka na kuingia ndani. Latifa alipomuona baba yake kitandani pale, uso wake ukajawa na tabasamu pana na kuanza kumsogelea.
Moyo wake ukaingiwa na hisia kali, ukapatwa na furaha kubwa kiasi kwamba alishindwa kuliuia tabasamu lake kutawala usoni mwake.
“Baba…”
“Naam mwanangu.”
“Nini kilitokea?”
“Maisha, maisha yalinipiga na ndiyo maana nipo hivi,” alijibu mzee Deo.
Latifa akanyamaza, akamsogelea baba yake kitandani pale na kumbusu katika shavu la uso huku machozi ya furaha yakimbubujika mashavuni mwake.
“Umefanana sana na mama yako,” alisema mzee Deo.
“Nani? Mimi?”
“Ndiyo! Mama yako alikuwa mrembo kama ulivyo,” alisema mzee Deo.
“Sasa kwa nini ulimfukuza wakati alipokuwa na mimba yako?”
“Nilimpenda sana mama yako, nilijitolea kwa kila kitu, nilitaka niishi naye japokuwa nyumbani kwao hawakuwa wakinipenda kisa tu nilikuwa mtu mweusi. Alipofukuzwa kwao, akakosa pa kwenda, alichoamua ni kuja nyumbani kwangu.
“Hata kabla hajafika, tayari wazazi wake waliwatuma watu wawili, walikuja huku wakiwa na bunduki, waliniambia kwamba endapo ningempokea mama yako na kuishi naye, hakika wangeniua, na waliniambia kabisa kwamba walitumwa na wazazi wake,” alisema mzee Deo na kuendelea:
“Niliogopa sana, niliona kweli ningeuawa, nilichokifanya ni kumfukuza Nahra huku nikiumia moyoni. Sikufanya vile kwa kuwa sikuwa nikimpenda, la hasha! Nilifanya vile kwa kuwa nyuma yangu niliwekewa bunduki. Alipoondoka, sikukaa nyumbani, niliondoka kwenda kumtafuta, usiku mzima nilimtafuta kila kona, ila sikufanikiwa kumpata, huo ukawa mwisho wa kuonana naye,” alisema mzee Deo, tayari naye machozi yalianza kumbubujika.
Watu wote waliokuwa mahali pale walikuwa kimya wakimsikiliza, mzee huyo alitia huruma kitandani pale, alionekana kukosa nguvu na alikuwa mtu aliyekosa tumaini kabisa.
“Nisamehe Latifa,” alisema mzee Deo.
“Nimekusamehe baba! Kila kitu kilichopita, kimepita, ni lazima tugange yajayo,” alisema Latifa, hapohapo akayapeleka macho yake usoni mwa Ibrahim aliyekuwa kimya.
“Ulimfahamu vipi Ibrahim?”
“Ni mtu ambaye amenisaidia sana, bila yeye nafikiri leo hii nisingekutana na wewe. Alinionyeshea upendo mkubwa sana, sikuamini kama kuna watu wenye roho nzuri kama alivyokuwa yeye. Nimekuwa naye kipindi chote, nilipopata tatizo, alinisaidia kwa fedha kidogo aliyokuwa nayo.
“Hakujua kama mimi ni baba yako, alinionyeshea upendo kwa kuwa aliona nastahili kufanyiwa hivyo japokuwa mke wake alikuwa ni tatizo kubwa. Binti yangu! Ibrahim alinihadithia kila kitu kuhusu wewe hata kabla hajajua kama mimi ni mzazi wako, naomba umsamehe, inawezekana mambo yote anayopitia, shida zote anazozipata ni kwa ajili ya laana yako, msamehe na sahau kila kitu,” alisema mzee Deo.
Latifa akayapeleka tena macho yake kwa Ibrahim, alipanga kutokusamehe katika maisha yake lakini kila alipokuwa akimwangalia, bado mwanaume huyo alionekana kuhitaji msamaha.
Alionekana kupigika katika maisha yake, alitia huruma lakini pamoja na hayo yote, alifanya kazi kubwa sana kumlea baba yake. Hakuwa na fedha za kutosha lakini nkiasi hichohicho kidogo alikitumia kwa ajili ya kumtibu baba yake, hakika alifganya jambo kubwa lililohitaji sifa kubwa kutoka kwake.
Hakuongea kitu, alichokifanya ni kumsogelea na kumkumbatia. Wote wawili walikuwa wakibubujikwa na machozi. Latifa hakuwa na jinsi, aliukana moyo wake na kumsamehe mwanaume huyo aliyeonekana kuhitaji sana msamaha.
“Nisamehe Latifa.”
“Nimekusamehe Ibrahim, Ahsante kwa yote uliyomfanyia baba yangu,” alisema Latifa huku akijifuta machozi.
“Naomba umsamehe Nusrat pia! Ni mwanamke mpumbavu asiyejua lile analolifanya. Naomba umsamehe.”
“Nimsamehe Nusrat?”
“Ndiyo!”
“Kwa hivi alivyomfanyia baba yangu?”
“Latifa! Hebu sahau kwanza. Wewe ni mtu mkubwa na mwenye heshima, tazama dunia nzima inakutazama wewe, usiposamehe, vipi wale vijana wanaotaka kuwa kama wewe? Nao watakapokosewa hawatakiwi kukosea kisa wewe haukusamehe? Vipi kuhusu wale watoto wanaotaka kuwa kama Latifa, kweli nao hawatakiwi kusamehe? Samahe saba mara sabini, au umesahau hilo?” aliuliza Ibrahim.
“Nakumbuka.”
“Basi naomba umsamehe!”
“Nimemsamehe!”
“Nashukuru!”
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha mapya, Latifa hakuwa na kinyongo, moyo wake ulilainika na hakutaka kuwa na kingo na mtu yeyote yule, alichokiamua ni kumsahmehe kila mtu aliyewahi kumfanyia ubaya kwa makusudi au bahati mbaya.
Alikuwa mtu mwenye mafanikio, bilionea, alichokifanya ni kumsafirisha baba yake nchini Marekani, alitaka akatibiwe huko na kuishi naye hukohuko. Kwa Ibrahim, japokuwa alimfanyia mambo mabaya nyuma hakutaka kumuacha hivihivi, aliamua kumsaidia kama alivyomsaidia baba yake.
Akamnunulia nyumba kubwa Mbezi Beach na kumgawia kiasi cha shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kufanya biashara zake kitu ambacho kwa Ibrahim kilikuwa kitu kikubwa, baada ya wiki moja, akaamua kumpa talaka Nusrat na kumuoa mwanamke mwingine na kuishi naye nyumbani kwake huku akifungua biashara kubwa.
Kwa Latifa, akaamua kufunga ndoa ya kishria Dominick na watu hao kuishi pamoja kwa amani ni na upendo ambapo baada ya miaka miwili, wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume waliyemuita kwa jina la Godlove.
Dawa yake ya kansa ya Morphimousis iliendelea kutikisa duniani, watu waliokuwa na magonjwa ya aina hiyo waliendelea kutibiwa na kupona. Aliendelea kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, utajiri wake ukazidi kuongezeka maradufu.
Baada ya miaka mitano kupita, wakapata mtoto wa pili wa kike waliyempa jina la Cecilia. Latifa alikuwa na furaha tele, moyo wake ulikuwa na amani, hakuwa na kinyongo na mtu yeyote, maisha yake yalikuwa ya furaha tele.
MWISHO
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi