Mwandishi: Nyemo Chilongani
SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Afya ilikuwa yake lakini kwenda hospitali ilikuwa mbinde. Alichokifanya Issa ni kumbeba na kuanza kuondoka naye kinguvu. Muda wote Nahra alikuwa akilalamika kwamba hakutaka kwenda hospitalini lakini Issa hakujali, aliendelea kumbeba mpaka walipofika katika Hospitali ya Halmashauri, Tandale.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
“Apelekwe Muhimbili kwa vipimo zaidi,” alisema daktari mwenye sura ya upole na huruma, Dk. Mariamu.
Issa hakuchoka, kwa sababu alikuwa na kiasi fulani cha fedha, akachukua bajaji na safari ya kuelekea Muhimbili kuanza. Walipofika huko, vipimo vikachukuliwa na Nahra kuonekana kuwa na ugonjwa hatari wa UKIMWI.
Hiyo ilikuwa taarifa mbaya kwake, msichana aliyekuwa na mvuto kiasi cha kuwatetemesha wanaume wengi, leo hii alikwisha kabisa na kuambukizwa ugonjwa hatari wa UKIMWI.
Nahra alilia sana lakini kilio chake hakikubadilisha kitu, mtu pekee aliyekuwa akimfariji alikuwa Issa tu.
Siku zikaendelea kukatika, vipele vikaongezeka mwili huku ukiendelea kupungua mpaka kufikia hatua ya kuanza kupata mabakabaka fulani mwisho wa siku nywele zake kuanza kunyonyoka, zote hizo zilikuwa dalili za ugonjwa hatari wa UKIMWI.
Nahra aliendelea kuisha, aliharibika na kila siku alikuwa mgonjwa. Japokuwa kila siku alitamani sana kwenda klabuni kulewa lakini kwa hatua aliyofikia, hakuwa na nguvu za kuweza kusimama. Akawa mtu wa ndani tu.
“Ninakufa Issa, ninataka kumuona mtoto wangu,” alisema Nahra huku akitia huruma kitandani.
Issa hakuwa na cha kufanya, ni kweli kwa muonekano aliokuwa nao alionekana kutokuwa na muda mrefu kuendelea kuishi, alichokifanya ni kwenda kumchukua Latifa na kumletea.
Alikuwa amefanana naye kwa kila kitu kuanzia uzuri na hata ngozi ya mwili. Nahra alibaki akimwangalia mtoto wake tu, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni pale alipokumbuka kwamba alikuwa mfu aliye hai.
Huo ukawa muendelezo wa mateso aliyoyapata, mara kwa mara alikuwa akiletewa mtoto wake na kuanza kumwangalia, moyo wake ulimuuma, alikuwa akiyauma meno yake kwa hasira na kuwapa lawama zote wazazi wake na Deo ambao walimfanya kuwa hapo.
Kila kitu kikabadilika, mtu pekee aliyekuwa akiyaangalia maisha yake ya mateso kitandani pale alikuwa Issa tu. Siku zikakatika, mwili wake ulizidi kukonda na vipele kuongezeka, kwa kumwangalia tu, usingebaki kimya, machozi yangekulenga na kusema kwamba Nahra alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipitia mateso makali.
“Issa, kama nitakufa, naomba umsomeshe mtoto wangu mpaka chuo kikuu,” alisema Nahra huku akionekana kukata tamaa.
“Usijali, nitajitahidi, hata kama nitakosa fedha, nitakopa tu.”
“Issa, nilikwishawahi kukuelekeza nyumbani, si ndiyo?”
“Ndiyo.”
“Utaweza kupakumbuka?”
“Nafikiri nitaweza.”
“Basi hapo ndipo utakapotakiwa kwenda endapo utapata tatizo lolote kuhusu fedha,” alisema Nahra.
“Wataweza kunisaidia kweli?” aliuliza Issa.
“Watakusaidia tu, huyu ni mjukuu wao na si mtoto wao, hana kosa, watakusaidia tu, amini hilo.”
“Sawa, nitajaribu japokuwa sina uhakika, nikipata tatizo, nitakwenda huko, nisipopata, hawatoniona,” alisema Issa ambaye kila alipomwangalia Nahra, moyo wake ulimuuma mno.
Siku hiyo Nahra aliongea kwa shida sana, ilipofika saa saba mchana, mateso aliyokuwa akiyapata kitandani yakaisha na kukata roho. Huo ukawa msiba mkubwa kwa Issa, alibaki akilia sana lakini machozi yake hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile, Nahra alifariki kwa Ugonjwa wa UKIMWI.
Alichokifanya Issa ni kuelekea nyumbani kwa kina Nahra, japokuwa alielekezwa juu kwa juu lakini alifanikiwa kufika huko. Mtu wa kwanza kabisa kumpa taarifa za msiba alikuwa mlinzi wa getini, Chichi ambaye aliwapelekea taarifa wazazi wake Nahra.
“Acha afe, tulimwambia azae na mtu mweusi,” alisema mzee Patel, Mhindi aliyekuwa na roho mbaya.
Japokuwa Wahindi wengine walipewa taarifa kuhusu msiba wa Nahra lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejitokeza kwenda huko, walibaki majumbani mwao wakiendelea kuyafurahia maisha.
Kitendo alichokifanya Nahra cha kukubali kuzaa na mtu mwenye ngozi nyeusi, Deo kiliwachukiza mno, hawakutaka kumuona, hawakumpenda na hata hawakutaka kuufikiria uzao wake, kwao, uzao wa Nahra ukawa ni uzao wenye laana.
Baada ya kila kitu kumalizika na Nahra kuzikwa, Issa akawa na jukumu kubwa na zito la kumlea mtoto Latifa. Kila alipomwangalia, moyo wake ulimuuma mno kwani sura yake ilimkumbusha Nahra.
“Wazazi wa Nahra wana roho mbaya sana, wamemkataa Nahra na uzao wake wote,” Issa alimwambia dada yake, Semeni aliyekuwa na jukumu la kukaa na Latifa.
“Kisa?”
“Kazaa na mtu mwenye ngozi nyeusi, ni hatari sana.”
Latifa alikuwa mtoto mkimya, hakuwa mtoto wa kulialia kama ilivyokuwa kwa baadhi ya watoto. Hakukuwa na shida ya kumlea, kwa Semeni, alimchukulia kama mtoto wake wa kumzaa, huduma zote alizokuwa akiwapa watoto wake wa kuwazaa, alikuwa akimpa Latifa pia.
Mwaka wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia, Latifa aliendelea kukua huku uzuri aliokuwa nao ukiendelea kuonekana zaidi, ulipofika mwaka wa pili, watu wakaanza kupigishana kelele kwa kudai kwamba Latifa angeweza kuwa mwanamke mrembo kuliko wanawake wote duniani, uzuri wake ulimdatisha kila mtu.
“Aiseee! Kama malaika!” alisema jamaa mmoja.
“Kwani ushawahi kumuona malaika?” jamaa mwingine akauliza huku akicheka.
“Sijawahi, lakini huyu kama malaika, amini hilo.”
Uzuri wa Latifa ukawa gumzo Manzese nzima, kila aliyekuwa na hamu ya kutaka kumuona mtoto mzuri alikuwa akiambiwa kwenda nyumbani kwa Semeni kumuona Latifa.
Mwaka wa tatu ulipoingia, Latifa akaanzishwa shule ya chekechea. Miongoni mwa watoto waliokuwa wakimya, Latifa alikuwa mmojawapo, hakuwa mzungumzaji kabisa, hakuwa mtundu, alipokuwa akikaa muda huu, hadi muda wa kutoka alikuwa hapohapo.
Mbali na ukimya wake, walimu wakagundua kitu kimoja kwamba Latifa hakuwa mtoto wa kawaida, uwezo wake darasani ulikuwa ni wa juu mno. Yeye ndiye alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma na kuandika japo kwa mwandiko mbaya.
Uwezo wake huo ukawashangaza walimu wote, hawakuamini kama kungekuwa na mtoto ambaye angeweza kufanya vitu hivyo kwa haraka kama alivyokuwa Latifa.
Hata mitihani ya shuleni hapo ilipokuwa ikija, Latifa alikuwa akiongoza jambo lililowafanya walimu kumpeleka darasa jingine la juu kwani uwezo wake ulikuwa ni wa kitofauti kabisa. Kwa kifupi tungesema Latifa alikuwa genius.
Mpaka anaanza darasa la kwanza, Latifa alikuwa mtoto mwenye uwezo mkubwa darasani, katika kila mtihani, alikuwa akifanya vizuri kitu kilichowashangaza sana walimu kwani hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyewahi kusoma shuleni hapo huku akiwa na akili nyingi kama Latifa.
Mbali na uwezo wake darasani, Latifa alikuwa mtoto mrembo ambaye usingeweza kumwangalia mara moja na kuyaamisha macho yako. Mchanganyiko wake wa rangi ulivichanganya vichwa vya watu wengi kiasi kwamba wengine wakatabiri kuwa angekuwa miongoni mwa wasichana watakaoitikisa Tanzania.
Miaka ilikatika zaidi, mpaka Latifa anaingia kidato cha kwanza katika Shule ya Wasichana ya Jangwani, uzuri wake uliendelea kuwatikisa watu wengi wakiwepo wavulana waliokuwa wakisoma katika Shule ya Wavulana ya Azania.
“Kuna demu nimekutana naye, ni mkali balaa, anasoma hapo Jangwani, aisee huyo demu ni shida,” alisikika mwanafunzi mmoja akiwaambia wenzake.
“Yupo vipi?”
“Muhindi si Muhindi, Mswahilini si Mswahili, ni noma.”
“Hahaha! Utakuwa unamzungumzia Latifa.”
“Latifa! Latifa yupi?”
“Kuna msichana wa kidato cha kwanza, ni mzuri ile mbaya, halafu ana akili kinoma,” alisema mwanafunzi mwingine.
Stori juu ya uzuri wa Latifa ndizo zilizokuwa zikisikika, uzuri wake uliendelea kumdatisha kila aliyemwangalia. Watu wakazidi kuambiana kuhusu Latifa kiasi kwamba binti huyo akaanza kupata umaarufu katika shule hizo mbili.
Miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakimpenda Latifa alikuwa Ibrahim Musa, kijana mtanashati aliyekuwa akisoma katika Shule Wavulana ya Azania. Kila siku alipokuwa akisikia stori kuhusu Latifa, Ibrahim alihisi moyo wake ukitetemeka kwa mahaba mazito.
Hisia kali za mapenzi juu ya msichana huyo zikamtawala, kila alipokaa, alimfikiria Latifa na hata katika kipindi cha kuondoka shuleni hapo, hakuwa tayari kuondoka mpaka pale alipomuona msichana huyo.
Kwa mwaka mzima Ibrahim aliendelea kumfuatilia Latifa, hakuwahi kuzungumza naye, alimuogopa, ni mara nyingi alipanga kumfuata lakini kila alipotaka kumsogelea, mapigo yake ya moyo yalidunda mno na hofu kumjaa. Wavulana wengine walimfuata Latifa lakini mwisho hakukuwa na mvulana yeyote aliyekubaliwa.
Kila alipowaangalia wavulana waliomfuata Latifa na kujiangalia yeye, alijiona kutokuwafikia hata mara moja. Hakuwa mvulana tajiri, alitoka katika familia masikini ambayo haikuwa na mbele wala nyuma.
Ibrahim alikuwa kama Latifa, japokuwa alikuwa kijana masikini lakini alikuwa na uwezo mkubwa darasani, katika kila mtihani aliofanya, aliongoza kwa maksi nyingi kiasi kwamba alikuwa gumzo kwa walimu wote.
“Nataka kuwa daktari, ila daktari bila kuwa na mke mrembo haiwezekani, Latifa atanifaa,” alisema Ibrahim.
Moyo wake uliendelea kuumia kila siku, kumfuata Latifa na kumwambia ukweli aliogopa sana. Mwaka mwingine ukaingia na kupita, mwaka wa tatu ulipoingia, Ibrahim akashindwa kuvumilia, hakuwa tayari kujiona akiteseka na wakati kulikuwa na mtu ambaye angeweza kuyatuliza mateso yake ya moyo.
Siku hii alikuwa amejipanga vilivyo, alivalia nadhifu huku akiwa amevipiga kiwi viatu vyake. Aliipanga siku hiyo kuwa maalumu kuzungumza na msichana huyo, kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiusibu moyo wake.
Baada ya kufika shuleni, hakutaka kutoka darasani, alivumilia mpaka muda wa kutoka. Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele, mapigo yake ya moyo yakawa yanaongeza kasi ya udundaji, alipenda kuonana na Latifa lakini moyo wake ulijawa hofu kubwa.
Baada ya kengele kutoka, moja kwa moja akaelekea nje ya shule na kusimama barabarani. Macho yake yalikuwa katika geti la shule ile ya wasichana, alikuwa akimsubiria Latifa tu.
“Leo lazima kieleweke, siondoki mpaka nizungumze naye,” alijisemea Ibrahim.
Dakika ziliendelea kusonga mbele huku wanafunzi wakiendelea kutoka, alikuwa kama mtu anayewahesabu wanafunzi hao, mpaka mwanafunzi wa mwisho anatoka ndani ya ndani ya shule, Latifa hakuwepo.
“Mmmh! Hajafika au alipita ila sikumuona?” alijiuliza Ibrahim.
Hakutaka kuvumilia kusimama nje, alichokifanya ni kuelekea ndani ya shule ile na kukutana na walinzi, akaanza kuwauliza kuhusu Latifa, kwa sababu alikuwa maarufu, halikuwa tatizo.
“Hauna habari nini?” aliuliza mlinzi mmoja.
“Habari gani?”
Ibrahim aliyasikia mapigo ya moyo wake yakidunda kwa nguvu, hofu ikamuingia, akajikuta akianza kusali kimoyomoyo mlinzi yule asimpe taarifa mbaya kuhusu Latifa kwa kuamini kwamba moyo wake ungemuuma sana.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi