NISAMEHE LATIFAH (5)

0
Mwandishi: Nyemo Chilongani

SEHEMU YA TANO
ILIPOISHIA...
“Habari gani?”

Ibrahim aliyasikia mapigo ya moyo wake yakidunda kwa nguvu, hofu ikamuingia, akajikuta akianza kusali kimoyomoyo mlinzi yule asimpe taarifa mbaya kuhusu Latifa kwa kuamini kwamba moyo wake ungemuuma sana.

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI

SASA ENDELEA...
“Latifa alipata ajali asubuhi, nimesikia hali yake mbaya sana, aligongwa na gari hapo Jangwani na amepelekwa hospitalini huku akiwa hajitambui. Tetesi zinasema kwamba anatakiwa kusafirishwa kupelekwa India kwa matibabu zaidi,” alisema mlinzi yule, Ibrahim akachanganyikiwa.

“Unasemaje?” aliuliza Ibrahim kwa mshtuko.

“Ndiyo hivyo, yaani leo watu wamemmisi sana, si unajua alivyokuwa mkali,” alisema mlinzi yule.

Ibrahim hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alihisi kuchanganyikiwa, alichokifanya ni kuanza kutimua mbio kuelekea Muhimbili kumwangalia, alionekana kama chizi, mapenzi yaliuendesha moyo wake vilivyo.

Ulisikika mlio mkubwa wa gari, watu wakapiga mayowe, wengine wakashika vichwa vyao, hawakuamini walichokiona, msichana mdogo aliyevalia sare za shule aligongwa na gari, alirushwa juu, akazungushwa, alipotua chini, hakutingisha, akatulia tuli.

Damu zilimtoka mfululizo, shati lake jeupe alilolivaa, ilikuwa vigumu kujua kama lilikuwa jeupe au jekundu, lilitapakaa damu hali iliyoonyesha kwamba msichana huyo alikuwa ameumia vibaya.

Watu waliokuwa pembezoni mwa barabara wakaanza kumfuata, dereva aliyekuwa amemgonga, hakukimbia, akateremka na kumfuata mahali pale alipoangukia. Kila mtu aliyemuona msichana huyo, alishika kinywa chake kwa mshtuko, kwa muonekano, msichana yule alionekana kufariki dunia palepale.

Kilichofanyika ni kumbeba na kumpeleka katika gari lile lililomgonga na safari ya kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuanza. Hakukuwa na mtu yeyote aliyegundua kwamba msichana aliyegongwa alikuwa Latifa, uso wake ulijaa damu huku akiwa ameumia vibaya kichwani.

“Mungu wangu! Huyu atakuwa amekufa,” alisema jamaa mmoja huku yeye na wenzake wakiwa garini kumpeleka Latifa hospitali.

Alipofikishwa hospitalini, akachukuliwa na kupelekwa katika chumba kilichoandikwa Theatre mlangoni, yaani chumba cha upasuaji. Kitu cha kwanza alichofanyiwa ni kuwekewa mashine ya hewa safi.

“Inatupasa tufanye kitu vinginevyo anaweza kufariki,” alisema daktari mmoja, bingwa wa upasuaji hospitalini hapo, Dk. Lyaruu.

“Kitu gani?”

“Mapigo yake ya moyo yapo chini, nipe CPR,” alisema Dk. Lyaruu.

Hapohapo mashine ya kushtulia mapigo ya moyo, Cardiopulmonary Resuscitation (CPR) ikaletwa na moja kwa moja kuanza kuyashtua mapigo ya moyo ya Latifa ambayo yalikuwa chini mno.

Kila kitu kilichofanyika mahali hapo, kilifanyika kwa harakaharaka, baada ya kuona kwamba mapigo yake ya moyo yanaanza kurudi katika hali yake, wakamtundika dripu na kuanza kuisikilizia hali yake.

Tayari wanafunzi walikwishaanza kukusanyika hospitalini hapo, kila mmoja alipatwa na mshtuko, taarifa waliyokuwa wameisikia kwamba mwanafunzi mwenzao aliyekuwa akisifika kwa urembo shuleni, Latifa alikuwa amepata ajali mbaya ya gari iliwashtua mno.

Hali iliyokuwa ikiendelea hospitalini hapo ilizidi kuwatia hofu wanafunzi kiasi kwamba kila mmoja akabaki akisali kimoyomoyo ili Mungu atende muujiza na hatimaye aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Ubongo wake umetikisika, hili ni tatizo kubwa, hebu subirini, muandaeni, nitarudi sasa hivi kuanza naye,” alisema Dk. Lyaruu.

Dk. Lyaruu akatoka ndani ya chumba hicho na baada ya dakika chache, alikuwa kwenye chumba kikubwa kilichokuwa kikitumika kwa kufanyia mikutano au vikao vya dharura.

Jopo la madaktari wanne likakutana, wote walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuizungumzia hali aliyokuwa nayo Latifa. Baada ya kufanyiwa uchunguzi, ripoti zikawekwa mezani na kuanza kujadiliwa.

“Ni ajali mbaya, ripoti zinaonyesha kwamba ubongo wake umetikisika na damu kuvilia kichwani, kuna vitu vinne vinaweza kutokea kama tusipofanya kitu fulani,” alisema Dk. Lyaruu na kuendelea:

“Kitu cha kwanza mgonjwa anaweza kupatwa na kichaa, hii ni hatari sana kwa afya yake,kitu cha pili mgonjwa anaweza kupoteza kumbukumbu zake jambo ambalo na jambo la tatu, mgonjwa anaweza kupata kifafa, lakini mbaya zaidi, anaweza kufariki,” alisema Dk. Lyaruu, madaktari wote walikuwa kimya wakimsikiliza.

Ilikuwa ni taarifa mbaya wasiyoitegemea, msichana mdogo ambaye alipata ajali na kuletwa hospitalini hapo alipatwa na tatizo kubwa lililoashiria kifo chake endapo tu asingeweza kutibiwa kwa ufasaha na kwa haraka.

Alikuwa msichana mdogo mno kupata mateso kama yale aliyoyapata. Msichana mrembo, mwenye akili nyingi, leo hii alipata ajali mbaya na kuufanya ubongo wake kutikisika.

“Kwa hiyo ili tuyaokoa maisha yake, ni lazima tulifungue fuvu lake, tuitoe damu hiyo, kama tutashindwa, haina budi kumsafirisha kuelekea nchini India,” alisema Dk Lyaruu, kila mmoja ndani ya chumba kile akashusha pumzi ndefu.

Kikao hicho cha dharura kikafungwa na kila mtu kuondoka katika chumba hicho. Vichwa vyao vilifikiria ni kitu gani kilitakiwa kufanyika ili Latifa aweze kupona na kurudi katika hali ya kawaida.

Hawakutaka kumuona akichanganyikiwa au kumbukumbu zake kufutika, hawakutaka kumuona akipatwa na ugonjwa wa kifafa, la zaidi, hawakutaka kumuona akifariki dunia, walitaka kumtibu na mwisho wa siku awe kama alivyokuwa kabla.

“Dokta, nini kinaendelea?” aliuliza mwanamke mmoja, alikuwa yule dereva aliyemgonga Latifa kwa gari.

“Subirini kwanza, kuna kitu kinatakiwa kufanyika,” alijibu Dk. Lyaruu huku akiwa na haraka.

“Nipo radhi kutoa kitu chochote kile, ninahitaji huyu mtoto apone, naomba mumsaidie,” alisema mwanamke yule huku akianza kububujikwa na machozi.

Alionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kumgonga Latifa kwa gari kilimchanganya. Kila alipokaa, hakutulia, alisimama na kuzunguka huku na kule, alionekana kama chizi.

Sehemu hiyo ya kusubiria kuwaona wagonjwa hakuwa peke yake, zaidi ya wanafunzi kumi walikuwepo mahali hapo huku kila mmoja akitaka kumuona Latifa, ambaye alikubalika, leo hii alikuwa hospitalini huku akiwa hajitambui.

Baada ya dakika ishirini, madaktari watatu na manesi wanne wakaingia ndani ya chumba cha upasuaji. Walipofika, kitu cha kwanza wakashikana mikono kwa kumzunguka Latifa na kuanza kumuomba Mungu kwa dini zao ili aweze kuwasaidia katika upasuaji uliokuwa unakwenda kufanyika ndani ya chumba hicho.

Kitu cha kwanza walichokifanya ni kumuingiza katika mashine kubwa iliyokuwa na kipimo kiitwacho Magnetic Resonance Imaging (MRI). Hicho kilikuwa kipimo maalumu ambacho hutumika katika kuangalia ni sehemu gani ya ubongo wa mwanadamu iliyokuwa imepata tatizo fulani.

Hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza kabisa ambayo walitakiwa kuichukua ndani ya mashine ile. Kikamera kidogo ambacho kiliunganishwa na kompyuta iliyokuwa chumbani mule ikaanza kuchukua kile kilichokuwa kikiendelea.

Kila daktari akashtuka, hawakuamini kama donge kubwa la damu ambalo lilivilia ndani ya ubongo wa Latifa lilikuwa kubwa kiasi kile. Japokuwa waliwahi kupokea wagonjwa wengi wa tatizo kama lile lakini hawakuwahi kumpata mgonjwa aliyekuwa na donge kubwa la damu kama ilivyokuwa kwa Latifa.

“Hapa kazi ipo, sidhani kama itawezekana,” alisema Dk. Pius, alikuwa mtaalamu mwingine wa upasuaji hospitalini hapo.

“Ooppss…! Sikujua kama damu inaweza kuwepo kwa wingi kiasi hiki. Hili ni tatizo kubwa, inatakiwa ahamishwe haraka kwenda kwa wataalamu zaidi, vinginevyo, anaweza kufariki,” alisema Dk. Lyaruu.

Hospitali ambayo ilikuwa vichwani mwao kwa haraka sana ni Ganga Medical Center iliyokuwa nchini India, huko ndipo alipotakiwa kupelekwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji ambao ungegharimu dola elfu kumi, zaidi ya shilingi milioni ishirini.

“Ni fedha nyingi, atazipata vipi?” aliuliza Dk. Lyaruu.

“Labda tukazungumze na yule mwanamke aliyemgonga, tukishindwa, tuwaruhusu waandishi wa habari wa Gazeti la Uwazi waitoe taarifa yake gazetini, naamini ataweza kupata kitu chochote kile,” alisema Dk. Pius.

Walichokifanya ni kumfuata mwanamke yule ambaye muda wote alikuwa mtu wa kulia tu. Walipomwambia kwamba Latifa alitakiwa kusafirishwa nchini India kwa ajili ya matibabu, akakubaliana nao kulipia kila kitu, si milioni ishirini tu, hata ingekuwa mia moja, alikuwa radhi kufanya hivyo.

Mawasiliano na Hospitali ya Ganga yakaanza kufanyika. Mtoto mwenye sura nzuri, aliyekuwa na akili darasani, aliyetoka katika familia ya kimasikini ambapo mama yake alifariki kwa ugonjwa wa UKIMWI, alihitaji kupelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu ya kuondoa donge kubwa la damu ubongoni mwake, kila kilichokuwa kikiendelea, Latifa alikuwa kwenye usingizi wa kifo, hakufahamu chochote kile.

Mawasiliano baina ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Ganga ya nchini India yakafanyika na siku mbili baadaye, Latifa, Issa, yule mwanamke aliyemgonga, bi Rachel walikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Indians Airlines wakielekea nchini India.

Kama kulia, bi Rachel alilia sana lakini haikusaidia kumuinua Latifa kitandani pale, bado alikuwa amepoteza fahamu, yaani toka alipomgonga kwa gari, hakuwa amerudiwa na fahamu mpaka siku hiyo.

Safari nzima ya kutoka nchini Tanzania kuelekea India, Latifa alikuwa akipumulia kwa msaada wa mashine ya hewa safi. Kama aliyokuwa amelazwa nchini Tanzania, alikuwa vilevile mpaka walivyokuwa wakiingia nchini India.

Gari la wagonjwa kutoka Ganga Medical Center lilikuwepo uwanjani hapo na baadhi ya madaktari waliokuja kumpokea Latifa aliyekuwa hajitambui. Mara baada ya ndege kusimama na abiria wote kuteremka, naye Latifa akateremshwa huku akiwa juu ya machela, wakamuingiza ndani ya gari na kuondoka naye.

Walichukua dakika ishirini njiani, wakafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja machela ikateremshwa na kuanza kusukumwa ndani ya hospitali hiyo kwa ajili ya kuanza kazi ya upasuaji ambayo ingewachukua kwa zaidi ya mwezi mzima mpaka kuhakikisha kwamba Latifa amekuwa katika hali nzuri.

Kabla ya kitu chochote kuanza, madaktari mabingwa wa upasuaji wakakutana katika chumba maalumu na kuanza kufanya mkutano wa dharura. Zaidi ya madaktari saba walikuwa ndani ya chumba hicho, ripoti kutoka nchini Tanzania katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikawekwa mezani na kuanza kuijadili.

Kikao hicho kilichukua saa moja, kikamalizika na kugundua kwamba Latifa alikuwa amepata tatizo ambalo kitaalamu huitwa Subdural Haematoma, tatizo ambalo husababishwa na mkusanyiko mkubwa wa damu katika ubongo.

Baada ya kila kitu kuwa sawa, mara moja oparesheni ikaanza kufanyika ndani ya chumba kile. Mlango ulikuwa umefungwa, ukimya ulitawala ndani ya chumba kile, upasuaji ule haukuwa mdogo, sehemu ndogo ya utosini ikachanwa na kisu kikali na kuanza kuangalia ndani.

USIKOSE SEHEMU IYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)