Mwandishi: Nea Makala
SEHEMU YA KWANZA
TONY ni kijana mtanashati na mwenye muonekano maridhawa, tabasamu lake limekuwa likihadaa nyoyo za wasichana wengi. Sauti yake tulivu isiyo na mitetemo ilizidi kuwaburudisha wengi pindi ipenyapo masikioni mwao. Umaarufu wa Tony ulichagizwa na upekee wa falsafa na misimamo yake binafsi, kamwe hakuruhusu mtu afanye maamuzi kwa niaba yake. Juhudi na ubunifu katika kila alichokifanya ukampa Tony heshima ya kipekee na kuwa kifani kwa vijana wa rika lake.
Tony ni mtu anayependa kusoma na kufatilia vitabu na majarida mbalimbali ya wanafalsafa na wanasaikolojia, kwake yeye mwanamke ni kiumbe dhaifu kinachoendeshwa kwa hisia na mihemko lakini mwanaume siku zote ni bora anayeongozwa na nguvu ya kufikiri kwanza kisha hisia na mihemko huja baadaye. Misimamo yake ilimuaminisha kuwa Mapenzi ya kweli hupatikana zaidi kwenye riwaya na tamthilia, mwanamke yupo kwa ajili ya kumfurahisha na kumburudisha mwanaume, hivyo kwake kuwa na uhusiano na msichana zaidi ya mmoja halikuwa jambo la kushangaza. Tony ni kati ya vijana wachache waliojaliwa kuwa na maneno matamu na makali ambayo aliyatumia kama silaha ya kukata nyoyo za warembo wengi.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
Ni jioni moja tulivu iliyopambwa na mawingu mepesi huku mvua za rasharasha zikipunguza vumbi la mji mdogo na wa kitalii Bagamoyo, Sauti za ndege wanaorejea katika viota vyao zilichagiza kutoa melodi tamu masikioni mwa wapenzi wawili walioketi ndani ya sebule yao kubwa na yenye kupendeza wakiongea na kufurahi.
“Tony asante kwa mapenzi unayonionesha, nakili kuwa wewe ni mwanaume wa pekee sana,” alisema Theresa.
Theresa au Tedy amefahamiana na Tony kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, lakini kwa jinsi alivyompenda Tony ni kama amekuwa akifahamiana naye kwa kipindi cha miaka, ukweli alihisi amechelewa sana kuwa naye.
“Tedy wewe ni msichana mrembo na mwenye uzuri wa asili mimi ni wako nawewe ni wangu tuu,” Tony alijibu huku akiishika mikono ya mpenzi wake.
“Kuwa nami hivi siku zote, niahidi kuwa tutakuwa pamoja hata baada ya kifo, mi nawe ni moyo mmoja katika miili tofauti, kuwa nami usiniache Tedy,” aliendelea kuongea maneno ambayo moja kwa moja yalimfanya mwanadada yule kupata msisimko wa ajabu na kujihisi kuwa yeye ni msichana mwenye bahati kuliko wengine wote.
“Asubuhi kwangu haijakamilika bila uwepo wako, napenda kukuona mchana na jioni kadharika, wewe ni maumivu yasiochosha, nitakupenda daima.”
Tony alizidi kuzama na kuchukua nafasi kubwa moyoni mwa binti yule, wakati akiendelea kuongea na kumfanyia vituko vya hapa na pale ghafla simu yake ikaita, kuiangalia akakuta ni swahiba wake wa siku nyingi Darmian, akakaa sawa na kuipokea,
“Niaje wa obey!”
“Hakuna cha obey wala uswazi leo, kisanga kinakuja kwako”, alijibu Darmian.
“Nini?” Tony alishtuka kusikia kauli hiyo ya rafiki yake.
“Yaani hadi dakika hii, ninavyozungumza Vanessa anakaribia kufika kwenu sasa kama upo bado na Tedy jua kazi unayo,” alisema Darmian na kukata simu.
Taharifa ile ilimchanganya kidogo Tony japo alikuwa mtu wa kuchanganya sana wasichana lakini haikutokea hata siku moja akawakutanisha, anayafahamu vizuri sana maumivu ya mapenzi. Alijitahidi kila awezavyo asije gonganisha magari, mabadiliko yale ya muda mfupi yalimshtua kidogo Tedy na kuanza kuhoji,
“Vipi mpenzi mbona umebadirika ghafla kuna tatizo gani?”
“Hamna kitu nipo sawa”
“Mbona kama unahofu hivi?”
Tony akashindwa kutoa majibu mazuri kwa mpenzi wake, akajikuta njia panda asijue afanye nini ili kuepusha fumanizi ambalo ndani ya muda mfupi linaweza kutokea. Wakati akiendelea kufikiri, akapata wazo la kumpigia tena Darmian ili aone kama anaweza kumsaidia kumzuia Vanessa asifike nyumbani. Akapiga simu ikaita kwa muda mrefu bila majibu, wakati akiendelea kuyafanya hayo Tedy nae akaanza kupata wasiwasi asielewe nini kimemkuta mwanaume wa ndoto zake.
“Babe! Mboni hivyo sikuelewi ujue,” alisema Tedy huku akisogea zaidi alipo mpenzi wake.
Tony akasimama na kusogea mbali kidogo na alipokaa Tedy, akatembea umbali mfupi kisha akageuka na kumtazama mahabuba wake kwa tabasamu zito.
“Dunia yangu ipo mikononi mwako, wewe ni zaidi ya paradiso kwangu, uko kama mashairi nami ni muziki, wewe ni matamanio yangu, nami ni mpendwa wako”
Maneno yale yakaondoa hofu ambayo Tedy alikuwa ameshaanza kuipata akajikuta akifurahi mno, lakini wakati Tony anayaongea hayo tayari Vanessa akawa amefika mlangoni hivyo akaanza kupiga makofi ya pongezi kwa Tony. Vanessa akashtuka sana alipokutanisha macho yake na Tedy, vivyo hivyo Tedy nae akabaki katika sintofahamu kuona uwepo wa msichana mwingine pale japo hawakuwa wakifahamiana wala kuonana kabla. Tedy akajikuta akisimama kumtazama Vanessa ambaye alikuwa akipiga hatua fupi fupi kuelekea alipo Tony.
Tony hakuonesha kushtuka ila akajikuta akiangua kicheko kilichowashangaza Tedy na Vanessa, akachukua rimoti na kuwasha muziki kwa sauti ya juu kidogo. Akamfata Tedy na kuanza kucheza naye alipokaa sawa akamgeukia Vanessa ambaye alionekana kama anataka kuuliza kitu lakini maswali yote yaliisha baada ya Tony kumshika mkono ivyo naye akajikuta anatulia, wakacheza muziki kwa muda wa kama dakika 5, kisha Tony akazima na kukaa chini, nao pia wakafanya vile vile.
Tony akachukua maji na kumimina kwenye Bilauri ya shaba na kunywa hili kuburudisha Koo lake lililokauka. Kisha akawatazama Vanessa na Tedy kwa uchangamfu wa hali ya juu,
“Nimeamini msemo ule wa kuwa mwanamke ni pambo la nyumba, uzuri wenu umeifanya nyumba yangu kuwa kama paradiso ndogo, harufu ya manukato yenu…………..aaah so good” akashusha pumzi ndefu.
“Tedy huyu anaitwa Vanessa ni wifi yako,” Tedy akatoa tabasamu na kumpa mkono Vanessa.
Akamgeukia Vanessa na kusema maneno yale yale aliyosema kwa Tedy, Vanessa nae akatabasamu, alivyoona ametoa utambulisho ambao utakuja kuibua maswali ambayo hasingeweza kuyapatia majibu akatafuta namna ya kufanya hili wasigunduane kuwa ni wake wenza, Tony akafikiri kidogo kisha akamgeukia Vanessa na kumwambia,
“Wewe sio mgeni hapa, naomba ukajichukulie kinywaji ukipendacho na nikipendacho alafu tuje tusherekee”.
Van bila kusita akanyanyuka na kuelekea kule ambapo vinywaji vinaifadhiwa. Tony alivyoona Van ameenda akamsogelea Tedy na kumshika kiuno kisha kwa sauti ya taratibu akamwambia,
“Kuwa huru mpenzi wifi yako hana noma,” kisha akamsogeza karibu zaidi na kumbusu.
“Sawa honey nitakuwa huru”
Jibu lile lilimfurahisha Tony ambaye aliamua kutumia nguvu kubwa kucheza na akili za wasichana hao hili wasije kugundua kuwa wote wana nafasi sawa kwake, akaamua kucheza mchezo huo wa kumfanya mmoja dada na mwingine mpenzi kwa kuwatambulisha kila mmoja kuwa ni wifi wa mwenzie. Hama kweli mwanamke ni kiumbe kinachoongozwa na hisia bila kuwa na uwezo wa kufikiri kwa haraka, sijajua kwanini warembo wale hawakuhoji zaidi wakabaki kusadiki maneno yake na kila mmoja kujiona bora.
Tony akamwachia Tedy ambaye hakutamani kuachiwa hata kwa dakika moja,
“Honey naona wifi yako anachelewa kurudi ngoja nikamwangalie kwanza amekutwa na nini,” alisema Tony na kuanza kupiga hatua ndefu kuelekea kule alipo vanessa, lakini kabla hajafika akakutana naye njiani.
Tony akamshika mkono na kurudi naye kwenye stoo ya Vinywaji. Nyumba ya Tony ni kubwa mno na alitumia ubunifu wa hali ya juu kuhakikisha kila hitaji linakuwa na sehemu yake, alijitahidi kuweka maktaba ndogo ambapo huwa anajisomea vitabu na majarida mbalimbali, pia kukawa na sehemu ya kuhifadhia vinywaji tofauti na kwenye jokofu. Tony hakuacha kutenga sehemu maalumu kwa ajili ya kufanyia sala zake kwa Mungu japo changamoto za ujana zilimzidi nguvu.
Akaichukua ile chupa ya mvinyo aliyoishika Vanessa na kuiweka pembeni, hakupoteza muda akamvuta kwa karibu na kuanza kumbusu, Mapigo ya moyo ya Vanesaa yakaanza kwenda mbio kuliko kawaida,
“Kwanini umekuja bila kunitaarifu mapema, ona sasa nakosa uhuru wa kukubusu kutokana na heshima yangu kwa wifi yako”
“Samahani mpenzi sikuwa nafahamu kama una mgeni leo,” Vanessa alijibu.
Tony akaendelea kuvuluga akili ya mwanadada yule kwa kumshika na kumbusu kila mahali,
“I real missed you (nimekupeza sana),” alisema Tony
“I missed you too honey (nimekupeza pia mpenzi), Van akarudisha majibu.
Tony alivyoona amefanikiwa kwa kiwango kikubwa akamwachia Van na kuichukua ile chupa ya mvinyo,
“Twende wifi yako asije kujisikia mpweke”.
Wakaongozana hadi alipo Tedy kisha kwa pamoja wakafungua mvinyo ule na kuanza kuunywa taratibu huku wakisindikizwa na muziki laini.
Darmian baada ya kuona kuwa Tony alimpigia sana bila ya yeye kujibu akahisi hali ya hatari kichwani mwake. Ingawa alichoshwa na tabia ya rafiki yake ya kucheza na nyoyo za wasichana wengi kwa wakati mmoja lakini akaamua atafute namna ya kwenda kumsaidia hivyo akaamua ampigie rafiki yake mwingine,
“Oyah upo wapi wewe?” akauliza Darmy baada ya simu kupokelewa.
“Ndio nimetoka kazini naelekea nyumbani,” akajibu Yassir.
“Sasa tukutane basi hapo Mapinga twende kwa Tony naona ana tatizo kidogo”
“Tatizo!” akauliza Yassir kwa mshangao.
“Ndio! Jamaa naona leo kapata fumanizi”.
“Duuh! Kwa hiyo kawakutanisha Mirrium na Vanessa au?”.
“Aah! Mirrium mbona alishaachana naye kitambo sasa hivi ana mwingine anaitwa Tedy”.
“Duuh! Kweli ni shida, poa nipe dakika 10 nitakuwa hapo”
“Sawa usikawie asee”.
Darmian akakata simu na kuanza safari ya kuelekea walipopanga kukutana na Yassir.
Baada ya muda mfupi wakawa wamekaribia kabisa kufika nyumbani kwa swahiba wao, wakakuta geti limerudishwa tuu halikufungwa vizuri na kwa kuwa walishazoea kwenda mara kwa mara, wakaingia bila kusubili kukaribishwa. Wakapita katika bustani iliyo mbele ya nyumba na moja kwa moja hadi kwenye mlango mkubwa, lakini kabla hawajaingia ndani wakashangaa kusikia watu wakiongea na kufurahi. Maswali yakaanza kuzunguka vichwani mwao, shauku ya kutaka kujua nini kilichojili ikaongezeka.
Wakasikia watu wakiongea na kucheka mno, wakatazamana kwa mshangao kidogo sababu walijua wangekuta ugomvi mzito. Kwa pamoja wakaingia ndani na kukuta Tony akiwafanyia vituko vilivyowafurahisha mno, Tony alivyowaona akashusha pumzi ndefu na kunyoosha mikono juu kushukuru,
"Karibuni sana," akawakaribisha.
"Asante," Darmy akaitikia.
"Mambo zenu warembo," Yassir akawasalimu.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi