Mwandishi: Shiwawa Binasalaan Al Jabry
SEHEMU YA NANE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Aliponiambia hivyo niliogopa sana na kubaki nikijiuliza kama wakienda kunichinja huko na kunichuna ngozi itakuwaje, kwa ujumla nilipa hofu kwani niliwahi kusikia baadhi ya matajiri walikuwa na tabia ya kuua watu.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Nikiwa nawaza hivyo, yule Mwarabu aliniomba niingie kwenye gari kwani muda ulikuwa unakwenda ndipo nilimweleza ngoja nikafunge mlango. Nilipoingia ndani
nilitumia kama dakika tatu kufikiria kama niondoke nao au nisiondoke lakini baadaye nikapiga moyo konde na kusema Mungu angenilinda. Baada ya kufunga milango
nilitoka nikaingia kwenye gari, akaliondoa na kuanza kuelekea barabara ya kwenda mjini, kidogo mapigo ya moyo yalipoa. Tulitumia kama dakika kumi tukawasili
kwenye hoteli moja nzuri ya ghorofa, akaegesha gari tukashuka akatuambia tumfuate.
Tulimfuata hadi sehemu iliyokuwa na lifti tukaingia, akabonyeza kitufe tukapanda hadi ghorofa ya mwisho tukaingia kwenye sehemu iliyokuwa na meza kubwa na
viti zaidi ya sita,Tv na vitu vingine. Tukiwa tumeketi, yule Mwarabu alimwita mhudumu ambaye alifika na kumsikiliza kila mmoja wetu alihitaji kula na kunywa
nini! Licha ya kunywa chai nyumbani, nilimwambia aniletee chai, chapati mbili na mayai mawili ya kukaangwa, wao wakaagiza soda.
Nikiwa nakunywa chai na wao wakiendelea kunywa vinywaji vyao, yule Mwarabu akaniambia kwamba jana nilimuuliza ili niwe tajiri natakiwa kufanya nini,
nikawambia sawa kabisa nilitaka kujua jambo hilo. Baada ya kumweleza hivyo, alicheka na kuniambia kama nilihitaji kuwa tajiri kwanza nipunguze matumizi
yasiyo ya lazima na niache starehe kama kunywa pombe nk. Wakati akinieleza hivyo simu yake ikaita, akapokea na kuanza kuzungumza na mtu aliyempigia ambapo nilimsikia akimwambia wapande ghorofa ya juu kabisa
Hazikupita dakika tatu walifika vijana wawili, tuliposalimiana nao mmoja wao akasema; “Bosi tumepata viwanja vitatu vizuri nadhani utavipenda kwani vipo
sehemu nzuri.” Baada ya yule Mwarabu kuambiwa hivyo, alifurahi sana na kuwaeleza kuwa waondoke waende wakavione ndipo walimalizia vinywaji na kuniambia
niendelee kunywa chai, wakashuka chini. Hata hivyo, dakika tano baadaye mmoja wa wale vijana alirudi na kuniambia kwamba bosi wao alisema haikuwa vizuri kuniacha peke yangu hivyo alinifuata.
Tulipofika chini tuliingia kwenye gari tukaondoka kuelekea sehemu iliyokuwa na viwanja hivyo, kwa kweli vilikuwa kwenye maeneo mazuri ya kujenga sheli. Wale
Waarabu walifurahi ndipo yule tajiri alisema turudi hotelini, tukaingia tena kwenye gari lake na kuanza safari. Tulipofika tulikwenda kukaa sehemu awali
ndipo alifungua pochi yake akatoa kitita cha noti ambapo alihesababu shilingi laki mbili akanikabidhi. Baada ya kunikabidhi aliniomba msamaha kwa usumbufu wote kisha akaniambia nirudi nyumbani nikaendelee na kazi zangu.
“Kijana utanisamehe kwa kukusumbua ila kwa kuwa kwako napajua nitakuja kukutembelea siku nyingine,”yule Mwarabu aliniambia.
Kwa kuwa biashara iliingia nuksi, niliwaaga nikateremka chini lakini nikajiwa na mawazo kwamba nisirudi nyumbani badala yake nitafute chumba cha kupanga
kisha nitafute kibarua chochote. Baada ya kufikiria hivyo nilikwenda mtaani ambako nilimuuliza kijana mmoja kama naweza kupata chumba cha kupanga akaniambia kuna mzee mmoja alikuwa na vyumba, akanipeleka.
Tulipofika tulimkuta mzee huyo aliyekuwa akiishi na familia yake na baada ya salamu yule kijana alimwambia shida yangu, akakubali kunipangisha chumba. Kwa
kuwa nilikuwa nina fedha siku hiyohiyo nilimlipa kodi ya miezi sita, nikanunua kitanda, godoro, blanketi, shuka moja, ndoo ya kuogea na ya kuwekea maji ya
kunywa na vikombe viwili. Siku iliyofuata ilipofika saa tatu asubuhi nilikwenda kwenye ile hoteli aliyonipeleka yule Mwarabu kwani niliamini nisingeweza
kukosa kazi ya kufanya. Nilipofika katika hoteli hiyo nilimfuata meneja na kumweleza shida yangu ambapo alinifahamisha kwamba hapakuwa na nafasi ya kazi.
Aliponipa jibu hilo nilifedheheka sana na kumsihi anipe kazi yoyote ningeifanya kwa bidii, meneja huyo alitulia kwa muda kisha aliniuliza kama naweza kufua
nguo, nikamwambia naweza. Baada ya kumpa jibu hilo aliniambia nitakuwa nasaidiana na kijana mmoja kufua mashuka, nilimshukuru sana kwa msaada wake. Meneja
huyo aliniambia kwa mwezi atakuwa ananilipa shilingi 65,000, kwa kuwa sikuwa na familia nikakubaliana naye.
Siku hiyohiyo nilianza kufanya kazi ya kufua mashuka huku nikishirikiana na yule kijana mwenyeji wangu, kwa ujumla nilifurahi mno kupata kazi hiyo. Siku ya
tatu nikiwa nimejipumzisha baada ya kumaliza kufua mashuka, nilimuona mzee mmoja aliyekuwa amebeba shati jeupe la mikono mirefu na suruali ya kaki akitokea
ndani ya ile hoteli. Aliponifikia alinisalimia kwa kusema; “Hujambo kijana?” Nikamwambia sijambo kisha nikamuamkia! Baada ya kuitikia salamu yangu alinipatia
zile nguo na kuomba nimfulie ambapo alitoa noti ya shilingi 2,000 akanikabidhi na kuniambia nikanywe soda, nikamshukuru. Yule mzee alisema nisijali ndipo
alikwenda sehemu aliyokuwa ameegesha gari akapanda na kuondoka, nilifua zile nguo na kuzihifadhi vizuri ofisini nikitumaini angerejea lakini hakurudi. Siku
iliyofuata nikiwa bize kufua mashuka, nilimuona yule mzee ambaye alionekana ni tajiri akitoka mle hotelini na kunifuata, baada ya salamu aliomba nimpatie
nguo zake. Kwa kuwa nilikuwa nimezihifadhi ofisini nilimwambia asubiri nikamchukulie, ambapo nilizichukua nikamkabidhi, akanishukuru. Yule mzee akiwa
anaelekea lilipokuwa gari lake ili aondoke, nilimuomba kama hatajali nizungumze naye jambo flani, akasema niwe huru kumwambia chochote.
“Unasemaje kijana wangu?” yule mzee aliniuliza. Kabla sijamweleza shida yangu nilirudia tena kumuomba msamaha kwa kumsumbua akasema hakuna shida ndipo
nilimwambia nilikuwa natamani sana kuishi maisha kama yake. Kufuatia kauli hiyo, yule mzee alicheka sana na kusema: “ Maliza kwanza kazi zako zote kisha
ukiniona nimerudi njoo chumba namba nane nitakuambia siri za utajiri wangu.” Baada ya kunieleza hivyo, nikawa nina hamu ya kujua alikuwa akifanya nini mpaka
aweze kumiliki gari zuri namna ile ndipo nilimuuliza alikuwa akifanya biashara gani! Yule mzee alicheka na kusisitiza atakaporejea nimfuate chumba namba nane ili anieleze kila kitu kisha aliniaga, akaingia kwenye gari lake na kuondoka.
Kufuatia yule mzee kukubali kunipa siri ya utajiri wake, nilifurahi sana nikawa namsubiri kwa hamu ili nijue alikuwa akifanya shughuli gani iliyomuwezesha
kupata fedha nyingi. Siku hiyo yule mzee hakuchelewa kurudi na alinikuta nikiwa napiga stori mapokezi ambapo nilimpokea mfuko nikaongozana naye kwenda
chumbani kwake. Tulipofika huko aliniambia nimuache alale kidogo akiamka ataniita, nikasema sawa lakini kabla sijaondoka aliniuliza kama nilikuwa nimekula, nikamwambia bado akanipatia shilingi 5,000.
Kufuatia kunipatia fedha hizo, nilikwenda kula ugali kwa sato kwenye kibanda cha mama lishe mmoja kisha nilirejea pale mapokezi kusubiria kuitwa na yule
tajiri. Tukiwa tunaangalia runinga, ndipo simu ya mapokezi iliita mhudumu akapokea akaanza kuongea na mpigaji. Alipomaliza aliniambia naitwa na yule mzee, nilikwenda fasta ambapo nilimkuta akinywa mvinyo huku kavaa bukta akiwa kifua wazi.
“Hivi kijana wangu unaitwa nani?” aliniuliza. “Kaloli,” nilimjibu. Baada ya kumtajia jina langu aliniuliza kabila langu nikamwambia Msukuma ndipo akaniambia
kwamba muda ule ulikuwa muafaka kuniambia siri ya utajiri wake. “Kijana, unaonekana unapenda sana uwe tajiri si ndiyo?” akaniuliza. “Ndiyo,” nikamjibu. Baada
ya kumjibu hivyo, alinifahamisha kwamba alikwisha wasaidia watu wengi sana kisha akaniuliza kama nitaweza masharti… yaani kumtumikia shetani!
Aliponiambia hivyo, nilimuuliza kumtumikiaje shetani ndipo mzee huyo alicheka na kuniambia kufanya mambo yake kama alivyokuwa akifanya yeye. “Kwani wewe
unafanya mambo gani?” Nilimuuliza. Kufuatia swali hilo aliniambia kwamba yeye alikuwa na uwezo wa kumwita jini yeyote mwenye nguvu akaja kumsikiliza.
Aliongeza kuwa, jini akifika alikuwa na uwezo wa kumuomba kitu chochote na kuletewa muda huohuo.
Baada ya yule mzee kuniambia hivyo nilimuuliza kama nami naweza kumuomba fedha akaniletea akasema siyo pesa tu kitu chochote nitakachokitaka. Aliponieleza
hivyo aliniuliza kama nipo tayari kumtumikia shetani nikakubali ndipo aliniambia tusubiri usiku uingie ili twende sehemu ambayo kazi hiyo itafanyika. Kabla
sijaondoka mle chumbani, alichukua karatasi na kuniandikia vitu vifuatavyo ambavyo alisema nikavinunue kwani vitatutumika katika zoezi hilo.
Kuku mweusi, udi ishirini, ubani maka na majani ya mtende, baada ya kunikabidhi ile karatasi aliniambia nikimaliza kazi zangu niende nikavinunue.
Kwa kuwa sikufahamu ningevinunua wapi, nilimuuliza akaniambia vinapatikana kwenye maduka ya dawa za asili. Siku hiyo nilifanya kazi yangu nikiwa mwenye
furaha kwani nilijua muda mfupi nami nitakuwa tajiri kama yule mzee ambaye alikuwa akiishi maisha mazuri sana. Nilipomaliza kazi, nilimuaga yule kijana
niliyekuwa nikifanyanaye kazi kwamba natoka kidogo, aliponiuliza nilikuwa nakwenda wapi nikamwambia nyumbani.
Licha ya yule kijana kuwa mtu wangu wa karibu, sikutaka kumshirikisha kabisa kwenye mpango wangu wa kumtumikia shetani. Sikutaka kufanya hivyo kuhofia siri
hiyo kuvuja na kusababisha watu kujua mambo aliyokuwa akiyafanya yule mzee tajiri aliyekuwa akiheshimiwa sana.
Baada ya kumuaga yule kijana nilikwenda kwenye duka moja la dawa asili, bahati nzuri vitu vyote nilivyovihitaji nilivipata kisha nilikwenda sokoni nikanunua
kuku mweusi na kumpeleka nyumbani. Ingawa nilipomaliza kazi nilipenda kushinda pale hotelini ambapo kuna wakati wateja walikuwa wakinituma na kujipatia fedha
za ziada, siku hiyo sikurudi hadi ilipofika saa mbili usiku muda tulioahidiana kukutana na yule mzee.
Nilipofika pale hotelini niligonga mlango wa chumba cha yule mzee, akanifungulia nikaingia ndani na kuketi kwenye kochi. Mzee huyo aliniuliza kama kila kitu
alichoniagiza nilikipata nikamwambia ndiyo, akasema safi sana na kunisifia kwamba nilikuwa kijana shapu! Baada ya kuniambia hivyo aliniuliza nikikutana na
jini sitatimua mbio, kwa kuwa nilihitaji kuwa tajiri kama yeye nilimweleza sitakimbia, akacheka. “Haya nisubiri kidogo nami nijiandae,” yule mzee aliniambia.
Baada ya kusema nimsubiri, aliingia bafuni akaoga kisha alitoka akachukua nguo na kuingia tena bafuni ambapo alibadilisha na kutoka.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi