SIKUACHI BABY (11)

0
Mwandishi: Juma Hiza

SEHEMU YA KUMI NA MOJA
TULIPOISHIA...
“Nafurahi kusikia hivyo mpenzi ila kuna kitu nitafanya kwa ajili ya mapenzi yetu ili mume wangu asijue kinachoendelea.”

“Utafanya nini?”

KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
“Nitakuwa nikiwasiliana na wewe kwa siri na kila tutakapomaliza kuchat nitahakikisha nafuta meseji zote, hatojua kitu.”

“Una uhakika?”

“Ndiyo mpenzi tatizo lako wewe unaogopa sana.”

“Lazima niogope umeshaniambia mume wako ni mwanajeshi unafikiria nini kingine kama sio kuuliwa.”

“Hawezi kukuua mtu mimi nakupenda wewe halafu muda mwingi huo yupo kambini, akirudi tutaendelea kula raha zetu,” aliniambia Samira nilipokuwa nikizungumza naye kwenye simu.

Nilijikuta nikilainika taratibu na kurudia kuwa na mahusiano na Samira ya kisirisiri, naweza kusema nilichanganywa na uzuri wake na ndiyo uliyonifanya nikubali kirahisi kuendelea kuwa naye. Nilijitoa muhanga wa kimapenzi.

Moyo wangu bado uliendelea kuumia sana baada ya kumfikiria Bianka, alikuwa ni msichana wangu ambaye nilipanga kumtumia kingono kisha na kumuacha, sikupanga kuzaa naye lakini kwa wakati huo alikuwa tayari ana ujauzito wangu. Nilitamani kuona siku moja Bianka akikubali kuutoa ujauzito huo lakini hilo hakutaka kulikubali.

“Kwahiyo umekataa kuutoa huo ujauzito?”

“Ndiyo siwezi Metu kuua kiumbe kisichokuwa na hatia.”

“Bianka kwani ugumu uko wapi, tunatoa na kama tatizo ni mtoto tutazaa mwingine.”

“Metu wewe unaongea kwasababu hii hali haipo kwako, lakini jaribu kuwa na roho ya huruma hata kidogo mbona unakuwa katili kiasi hicho?”

“Nampenda sana huyo mtoto ndiyo maana nakwambia ufanye hivyo, sitaki kuja kumtesa.”

“Mimi siwezi Metu kwanza naogopa kufa.”

“Huwezi kufa mpenzi nikubalie,” nilimwambia kwa sauti ya kumbembeleza lakini hakuweza kukubali.

Niliendelea kumbembeleza akubali kuutoa ujauzito mpaka pale siku moja ambapo Mama yake aliamua kunisusia, hakutaka kuendelea kuishi na Bianka. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuishi na Bianka bila ndoa, yalikuwa ni maisha ambayo sikuyatarajia kwa wakati huo, sikuwa na jinsi ya kufanya kwa kile kilichokuwa kimetokea, nilikubaliana na kila kitu.

Nilishindwa kumueleza Mama yangu ukweli wa mambo yote yaliyokuwa yametokea, niliamini kama ningeweza kumueleza angenichukia sana kwa kitendo kile cha kususiwa mwanamke na kuanza kuishi naye.

                                             ****
Niliendelea kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Samira huku kila kitu kilichokuwa kikiendelea kati yetu kiliendelea kuwa kama siri. Nilizidi kushiriki kufanya naye mapenzi lakini pia sikuacha kuwa makini kujihami na mume wake ambaye alikuwa ni Mwanajeshi.

Penzi la Samira lilinichanganya mno, wazo la mume wake lilianza kuniondoka kichwani, nilianza kumdharau baada ya kuendelea kulifaidi penzi la mke wake bila ya madhara yoyote.

Alikuwa akinipa pesa nyingi sana na pesa hizo nilizitumia na Bianka, hakufamu lolote kuhusu maisha ya msichana huyo niliyekuwa naishi naye nyumba moja.

“Ni hakikishie usalama wangu,” nilimwambia Samira siku moja majira ya jioni tulipotoka kufanya mapenzi katika moja Lodge iliyokuwepo maeneo ya Tandika.

“Usalama upo ila kama nilivyokwambia naomba usiwatangazie watu kuhusu mahusiano yangu na wewe, mume wangu akijua kuwa bado naendelea na wewe itakuwa ni hatari kwetu,” aliniambia.

Dereva bodaboda mwenzangu Amani hakuacha kunishauri juu ya kuachana na Samira, kila siku alirudia kuniambia maneno hayohayo kuwa niachane na aina ya mapenzi ambayo mwisho wa siku yangeweza kuniletea matatizo makubwa katika maisha yangu.

“Kwanini usitulie na Bianka maana mpaka sasa ana ujauzito wako na unaishi naye,” aliniambia Amani tulipokuwa kijiweni.

“Bianka sio chaguo langu,” nilimjibu.

“Hutakiwi kusema hivyo kumbuka tayari ana damu yako,”aliniambia.

“Laiti ungejua natamani hata kesho huo ujauzito wake utoke maana nishamchoka” nilimwambia.

“Metusela badilika mshikaji wangu hayo maisha unayoishi siyo kabisa, rudi kwenye mstari.”

“Hayo mahubiri unayonihubiria hata sikuelewi kwani nikitembea naye kuna ubaya gani au kuna kitu unachopungukiwa?”

“Usicheze na mke wa mwanajeshi, utafanywa kitu kibaya.”

“Hawezi kunifanya lolote kwanza ni mchumba tu huo uwanajeshi wake mimi haunitishi lolote,” nilijibu huku nikijiamini.

     ****
Kama wasemavyo wahenga kuwa siku zote mbio za sakafuni huishia ukingoni hii ndiyo iliyonitokea. Katika kipindi ambacho nilikuwa nikitembea na Samira kwa siri siri, alikuja kupata ujauzito wangu.

Nilichanganyikiwa baada ya Samira kunieleza kuhusu ujauzito huo aliyokuwa nao, kwa upande wake hakutaka kuamini kama kweli alikuwa ni mjamzito, aliogopa mno na hakujua ni nini ambacho angeweza kumwambia mume wake ambaye tayari alishamfumania na kumkanya.

Hakukuwa na wazo lingine lililonijia kichwani na kumshauri zaidi ya kumwambia alitakiwa autoe ujauzito huo ambao ungeweza kuleta madhara makubwa hapo baadae, aliweza kukubaliana nalo.

Hatimaye mipango ya kisirisiri ya kuutoa ujauzito wa Samira ilianza kufanyika, nilipokuwa hospitalini nilikuwa nikimuomba Mungu muda wote tukio lile liweze kufanyika salama. Majibu ya daktari aliyokuja kunieleza baada ya kufanikiwa kuutoa ujauzito wa Samira yaliniweka katika hali ya sintofahamu.

“Imekuaje dokta?” nilimuuliza mara baada ya kumuona akitoka Theatre kwa wakati huo.

“Nimefanikiwa kuutoa lakini amepoteza damu nyingi sana,” alinijibu dokta.

“Kwahiyo tunafanyaje?”

“Hakuna cha kufanya tena?”

“Kivipi?”

“Nasikitika kukuambia kuwa Samira amefariki dunia,” aliniambia daktari.

“Unasemaje dokta?” nilimuuliza huku nikiwa kama sijamsikia vizuri, wakati huo nilikuwa nimeyakodoa macho yangu kwa mshangao mkubwa sana.

“Nasikitika kukuambia kuwa Samira amefariki dunia,” alirudia kuniambia tena maneno ambayo yalinichanganya sana, sikutaka kuyaamini hata kidogo.

Nilianza kuhisi joto kali likinitawala mwilini na haikuchukua sekunde jasho likaanza kunitoka, hofu ilikuwa imenitawala kwa wakati huo.

“Pole sana,” aliniambia dokta lakini sikuweza kumjibu, akili yangu haikuwa sawa baada ya kusikia kuwa Samira alikuwa amefariki dunia.

Hali ya usalama wa maisha yangu haikuwa shwari, kasi ya mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakinienda mbio, nilizidi kuwa katika hofu kubwa sana baada ya kumfikiria mume wa Samira endapo kama angeweza kuzipata taarifa hizi za kifo cha mke wake ambaye alifia mikononi mwangu ni nini ambacho angeweza kuamua kukifanya? hii ilikuwa ni moja kati ya kesi kubwa mno iliyokuwa ikinikabili.

Baada ya daktari yule kuniona nipo katika hali hiyo ya mawazo ilibidi aniite ofisi kwake ili aweze kuzungumza vizuri na mimi.

“Kwahiyo dokta hakuna njia yoyote ya kuyaokoa maisha yake?” nilijikuta nikimuuliza dokta swali ambalo lilimshangaza, akabaki akinitazama kwa mshangao, wakati huo tulikuwa ndani ya ofisi yake.

“Niambie dokta hakuna uwezekano wa kuurudisha uhai wake?”nilimuuliza tena kwa kujiamini.

“Mbona sikuelewi kijana,” aliniambia dokta.

“Hunielewi kivipi dokta?”

“Tangu lini umewahi kusikia mtu aliyefariki dunia akapona au akarudishiwa uhai?” aliniuliza yule daktari swali ambalo lilinirudisha katika fahamu zangu, nilizidi kuchanganyikiwa baada ya kusikia maneno hayo ya daktari.

“Mbona hii kesi ni kubwa sasa,” nilijisemea maneno haya ambayo nilihisi nayasikia peke yangu lakini kumbe haikuwa hivyo niliyatamka kwa sauti kubwa na yule daktari aliyasikia.

“Kesi! Kesi kivipi?” aliniuliza.

“Hapana, hapana dokta hakuna kitu,” nilimjibu.

“Hivi ulisema huyu ni mke wako wa ndoa?”

“Ndiyo.”

“Lakini kwanini mliamua kuchukua maamuzi haya au hamkupenda kuwa na mtoto?”

“Hapana ni mipango tu lakini kwa wakati huu hatukupanga kuzaa,” nilimjibu daktari kwa kumdanganya baada ya kuona anazidi kunidadisi undani wa maisha yangu.

“Pole sana kwa kumpoteza mkeo.”

“Asante,” nilijibu.

Nilipomfikiria mume wa Samira akili yangu ilizidi kutawaliwa na mawazo sana, nilifahamu hakukuwa na usalama tena wa maisha yangu na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufunzwa kwa tabia yangu ya kutembea na wanawake wengi niliyokuwa naona ufahari kuwa nao.

Nilikumbuka maneno ya Mama yangu aliyokuwa akinipigia kelele kila siku kuhusu kuoa, hakupendezwa na aina ya maisha niliyokuwa nikiishi japo mtaani nilisifika kuwa na tabia ya upole sanjari na heshima lakini siri na mwenendo mzima wa maisha yangu hakukuwa na mtu ambaye alifahamu.

Kama katika maisha yako hayajawahi kukusibu kama yaliyowahi kunisibu mimi katika maisha yangu basi muombe sana Mwenyezi Mungu yasije yakakusibu maana utatamani ufe kabla ya kukisubiri kifo chako ambacho ni halali yako kabisa.

Kifo cha Samira kilizidi kunipasua kichwa mno.

Siku hiyo nilirudi nyumbani mapema sana huku nikionekana kuwa mnyonge, haikuwa kawaida yangu kuwahi kurudi nyumbani. Bianka msichana niliyekuwa nikiishi naye kama mke wangu wa ndoa aliponiona aligundua tofauti yangu.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)