Mwandishi: Alex Kileo
SEHEMU YA THELATHINI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Walipokaribia katika maeneo ambapo Sajenti Minja alipata ajali, wakamshauri dereva taxi apunguze mwendo kwa maana kulikuwa na kona mbaya na pia bado walikuwa na kumbukumbu ya tukio baya lililomkuta Sajenti Minja katika eneo hilo.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Wakakata kona ya kwanza vzuri tu, ile wanakata kona ya pili tu, dereva taxi akafunga breki kali sana, ila alichelewa, maana tayari alishaikwangua kwa nyuma gari iliyopo mbele yake, ilikuwa ni gari ya Mchungaji Wingo ambayo ndani pia alikuwepo mama Kayoza.
Katika gari waliyokuwamo wakina kayoza, Happy binti Mchungaji alikuwa kachanganyikiwa kabisa baada ya kugundua gari iliyopo mbele ni ya baba yake, na omary pia alikuwa katika hali hiyo ya kutokujielewa, maana aliamini kabisa leo ndio arobaini yake.
Mchungaji Wingo na Mama Kayoza wakatelemka katika gari ya Mchungaji, na Mchungaji akionekana mwenye hasira ya kukwanguliwa gari yake, akawa anaifuata taxi waliyokuwamo wakina Kayoza, Omari na Happy binti wa mchungaji, hapo ndipo hali za vijana hao zikawa mbaya zaidi kwa hofu.
.Dereva taxi baada ya kuona yule dereva wa gari aliyoigonga anakuja, kwa haraka sana happy alimwambia taxi atelemke kwa maana yule anaekuja ni baba yake na yeye hataki ajue kama yupo ndani, Dereva taxi nae akaamua kutelemka, ili akabiliane na Mchungaji Wingo,
"kijana leseni yako umekatiwa na serikali au umeipata mitaani?", ndio swali la kwanza kuuliza Mchungaji baada ya Dereva taxi kushuka, Mchungaji Wingo alikuwa na hasira sana na hilo lilionekana wakati anaongea maana sauti yake ilikuwa inatoka na mitetemo ya hasira,
"nisamehe mzee wangu",Dereva taxi alikimbilia kujitetea badala ya kujibu swali, pia dereva taxi alishapata yoga kutokana na hasira alizokuwa nazo,
"inaonesha hata shule hukuenda, maana nimekuuliza swali jingine, we unaniambia vitu vingine",Mchungaji aliendelea kumshambulia Dereva taxi ambae aliamua akae kimya.
"Leseni nimepata veta, nilisomea pale" Dereva taxi alijibu huku akitetemeka,
"Angalia sasa ulivyo mjinga, jibu la swali la kwanza unaweka katika swali la pili" Mchungaji Wingo aliongea huku akitoa tabasamu lisilo la furaha, lilikuwa tabasamu la karaha.
Wakiwa bado wanaangaliana, Dereva taxi akiwa hana la kuongea kutokana na maneno ya Mchungaji Wingo, na Mchungaji Wingo akiwa anasubiri Dereva taxi aongee ili aendelee kumshambulia.
Mlango wa mbele wa taxi ukafunguliwa, akatetelemka Kayoza,
"shikamoo Mchungaji",Kayoza akasalimia kwa mashaka huku akimtazama mama yake aliyekuwa anamuangalia kwa jicho Kali mpaka Kayoza akawa anajiuliza ni kosa gani amefanya mpaka mama yake amuangalie kwa jicho Kali vile,
"marhaba, kumbe wewe ndio umemkodi huyu?",Mchungaji alimuuliza kayoza huku kidole chake cha shahada kikimuelekea Dereva taxi,
"ndio mchungaji",Kayoza akajibu kwa unyenyekevu,
"alichokifanya hapa unakubaliana nacho?",Mchungaji alimtumpia swali jingine Kayoza,
"hapana, ni bahati mbaya",Kayoza alimtetea Dereva taxi,
"angaliaga vitu vya kutetea kijana, uwaga nakuona una busara sana",Mchungaji alimwambia Kayoza,
Kayoza akaamua kukaa kimya,
"ee, nijibu kijana, kwa hiyo angetugonga tukafa bado ungeng'ang'ania bahati mbaya?",Mchungaji aliendelea kung'aka kwa sauti ya upole iliyojaa hasira,
"naomba unisamehe mzee wangu, nitakulipa pesa ya kupaka rangi katika eneo nililolichubua",Dereva taxi alidakia pasipo kuhusishwa, maana aliona ili kujiepusha na ile habari pale basi ni lazima akubali kulipa gharama za uharibifu wa gari ya Mchungaji,
"acha uhuni bwana mdogo, nani kakwambia anahitaji pesa yako?"Mchungaji aliongea kwa ukali,
"nakubali nimefanya kosa mzee, naomba unisamehe",Dereva taxi aliongea kwa huruma kiasi kwamba machozi yalikuwa yanataka kumtoka,
"Imeandikwa Samehe saba Mara sabini" Kayoza aliongea huku akitupa jicho lake pembeni lisikutane na jicho la mchungaji na kufanya mchungaji atoe tabasamu huku akimuangalia Kayoza,
"Imeandikwa na nani, sura ya ngapi na mstari wa ngapi?" Mchungaji alimuuliza Kayoza ambaye alikuwa hana jibu akabaki tu kuangalia chini,
"Ni neno la Mungu liko kwenye biblia" Kayoza alijibu na kumfanya Mchungaji acheke kabisa, kwa maana maneno anayoongea Kayoza yalikuwa yanamtoka tu bila kutarajia,
"Dereva we nenda bwana, mimi sina neno na wewe ila nilitaka nikufundishe ili usirudie kwa watu wengine",Mchungaji alimwambia Dereva taxi,
"asante sana mzee wangu",Dereva taxi alishukuru
"Usinishukuru Mimi, mshukuru huyu Mteja wako alietoa neno la Mungu" Mchungaji Wingo aliongea huku akiondoka eneo alilokuwepo Kayoza na Dereva taxi,
"Man turudi katika gari tuendelee na safari" Dereva taxi alimwambia Kayoza,
"Wapeleke hao, Mimi itabidi niondoke na hao wazee" Kayoza alijibu na kumfanya Dereva taxi ageuke na kwenda kupanda katika gari yake na kuliondoa kwa mwendo wa kistaharabu.
"we Kayoza mwenzako yuko wapi?",Mama Kayoza alimuuliza mwanae wakati anaingia katika gari ya Mchungaji Wingo,
"khe!, bi mkubwa hata sijakaa vizuri umeanza na maswali, ngoja nitulie kwanza",Kayoza alishangaa mama yake kuanza kumshambulia ndani ya gari,
"nijibu bwana",Mama alisisitiza tena kwa hasira,
"Alafu mbona unaonekana una hasira sana na Mimi, nimekukosea nini leo?" Kayoza aliuliza huku akimuangalia mama yake,
"Wewe usiniletee ujinga ujue, si nimekuuliza hapa? Badala unijibu na wewe unauliza, ndio ulivyofunzwa hivyo na shangazi zako" Mama Kayoza aliuliza huku macho yake yakiwa mekundu kwa ajili ya hasira aliyokuwa nayo,
"Umeuliza nini kwani?" Kayoza aliuliza tena na kumfanya Mama yake azidishe hasira,
"Mpumbavu mwenzako yupo wapi?" Mama Kayoza aliuliza kwa sauti ya juu mpaka Mchungaji akatabasamu kwa namna Mama Kayoza alivyopaniki,
"Atakuwa yuko nyumbani",Kayoza alijibu bila ya uhakika kwa maana hakujua kama Omary ataenda nyumbani au atakuwa bado anatanua na Happy binti Mchungaji,
"nyie hospitali si mlikuwa pamoja, sasa imekuaje mnarudi kwa mafungu?",Mama kayoza akaongeza swali lingine lililomshtua Kayoza, ila akajifanya yupo sawa tu,
"we umejuaje tulikuwa hospitali wakati hatukukuaga?",Kayoza nae akamtupia swali mama yake,
"sisi ndo tumetoka huko na tuliwaona",Mama Kayoza akamjibu mwanae
"mlikuwa upande gani, mbona hukuja eneo tulilokuwepo?",Kayoza akaendelea kuhoji,
"ningekuja vipi wakati mlikuwa na mkwe pale, si ndio kilichowaleta huku shinyanga, kutafuta wanawake tu wanaovaa hivyo hovyo",Mama kayoza alimjibu mwanae wakati anatelemka katika gari kuashiria wamefika, hill jibu lilimshtua Kayoza kwa maana aliamini kabisa Mchungaji atakuwa amewaona wakati Wapi na Happy.
Mama Kayoza na Mwanae baada ya kutelemka katika gari ya Mchungaji Wingo, wakamuaga mchungaji,
"Kijana kuweni makini sana na mabinti wa watu, huku shinyanga ni kubaya sana" Mchungaji Wingo alimwambia Kayoza kisha hakutaka kusubiri neno lolote kutoka kwa Kayoza, Mchungaji akaondoa gari yake kwa mwendo wa taratibu na kumuacha Kayoza akiwa anaitafakari ile kauli ya mchungaji Wingo ya kuwa makini na mabinti za watu,
"We Kayoza twende ndani, mbona umeganda kama kichuguu?" Mama Kayoza alimgutusha mwanae kutoka katika tafakari na kumfanya Kayoza atabasamu ili mama yake amuone yuko sawa.
Wkuingia ndani, ambapo walimkuta Omari anaangalia Runinga, Omari akamsalimia mama Kayoza.
"mkwe umemuacha wapi?",Mama Kayoza akamuuliza Omari huku akiwa bado na hasira zake,
"yupi tena huyo mama?",Omari akauliza huku anacheka kinafki, lakini nae tayari kengele ya hatari ilikuwa imeshagonga kichwani mwake, alidhani tayari picha yake na Happy Binti Mchungaji ilikuwa imeungua kumbe masikini ya Mungu hakuna kati ya Mama Kayoza wala Mchungaji Wingo aliyegundua kuwa yule binti waliyekuwa nae ni Happy binti Mchungaji.
"jifanye tu humjui, kumbukeni mna matatizo, msitake kujiongezea mengine",Mama Kayoza alimaliza huku akielekea chumbani kwake na kuwaacha vijana wake wakitazamana.
"vipi, kashtukia nini?",Omari alimuuliza Kayoza,
"anadai alituona hospital, ila sijajua kama wamegundua yule demu tuliekuwa nae ni happy, maana kauli zao sizielewi elewi zimekaa kimafumbo mafumbo ",Kayoza alimjibu Omari,
"He hii hatari, na mchungaji nae anasemaje?" Omary alimuuliza Kayoza huku wasiwasi ukianza kuchukua nafasi yake,
"Huyo hakuongea kitu kabisa, ila wakati ametushusha hapo nje, ameniacha na kauli tata sana, amesema tuwe makini na mabinti za watu" Kayoza alimwambia Omary,
"Itakuwa wamegundua nini?" Omary aliuliza kwa wasiwasi,
"Ila kama wangemgundua yule binti ni Happy wangetuambia tu, hakuna mzazi anaeweza kuvumilia mwanae kujiingiza katika mapenzi kabla ya ndoa, tena ukizingatia Baba mwenyewe ni mchungaji" Kayoza aliongea kwa kujipa moyo,
"Ila kweli man" Omary alimsapoti mwenzake,
"Nilivyoshuka katika taxi, mbona sikuwaona tena ndani ya
taxi? Maana kila nikijitahidi kuangalia sioni mtu", Kayoza aliuliza huku akicheka,
"tuliinama nyuma ya siti mwanangu", Omari alijibu kwa hali ya ushindi,
"mimi nilijua ndio tumekwisha",Kayoza nae akachomekea,
"we acha tu mwanangu, nilivyoona dereva kaingia ndani, nilimwambia awai, alivyonishusha tu, nikampatia mpunga wake kisha nikamwambia amuwaishe wife",Omari aliongea kwa kujiamini,
"ila mjomba, una zali",Kayoza alimfagilia Omari,
"mi bad number kaka, na nilipofika, nikamnyonya mate Happy hapo nje",Omari aliendelea kujinadi, lakini Kayoza hakuonekana kumsapoti tena na badala yake alikodolea macho nyuma ya Omari, ikambidi Omari ageuka aangalie anachoangalia Kayoza, hapo sasa ndio akakutanisha Macho yake na Macho ya Mama Kayoza ambaye alikua kasimama nyuma ya kiti alichokaa Omary huku akiwaangalia kwa jicho la hasira, hasira zaidi ya hasira alizokuwa nazo mwanzo……
…"nyie watoto mjue ni wapumbavu sana?",mama Kayoza aliongea kwa jazba, wakina Kayoza walitulia kimya, kisha akaendelea,
"mi nilifikiri kwa elimu ya chuo kikuu mliokuwa nayo mnaweza mkawa mnafikiri vitu vya maana, kumbe muda wote mnafikiria upumbavu tu, naishi na wajinga tu humu ndani tena mtanipa ugonjwa wa moyo bure, mi namfikiria kaka yangu, nyie mnafikiria mapenzi, hivi mnataka mimi nifanyaje?",Mama Kayoza aliuliza akitegemea kujibiwa, ila hakuna hata aliemjibu,
"eti Kayoza, si nawauliza nyie, ee?",Mama Kayoza aliongea huku akimuangalia mwanae,
"sasa mama unataka nikujibu nini",Kayoza aliongea katika sauti ya kupaniki",
"unamjibu nani hivyo?",Mama Kayoza alipamba moto, tena wa gesi, Kayoza akanyanyuka alipokaa na kuelekea chumbani kwao,
"endelea tu na kiburi chako, ila kina mwisho wake, na nina uhakika Kayoza utakuja kuniua na ugonjwa wa moyo", Mama Kayoza alimwambia mwanae wakati anaondoka, kisha akamgeukia Omari,
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi