KIJIJINI KWA BIBI (29)

0
Mwandishi: Alex Kileo

SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA
TULIPOISHIA...
mara yule kijana akabadilisha akaita Remmy, mh.., kuna kitu kinaendelea hapa, ngoja nichunguze mwenyewe", Mkuu wa Polisi alikata shauri na kuamua kuifatilia mwenyewe ile kesi.

"Ila kama yule babu alisema amemsahau jina huyo askari anaetuzunguka, inawezenaje amsahau Minja?, ila hapana, hii kesi ngoja niichukue Mimi mwenyewe kimya kimya, nitaujua tu ukweli.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Hata yule kijana atakuwa ndio Omary Mkwiji, sasa sitokurupuka kumkamata, nitaangalia kwanza namna ya kupata ushahidi, hii kesi imeshakuwa nyepesi tayari. Hapa ni kuendelea kujifanya sijui kitu, alafu nakuwa nawachunguza pole pole" Mkuu wa polisi aliendelea kuongea peke yake ndani ya gari.

Jumapili tulivu, Omari na Kayoza, huku wakiongozana na happy binti mchungaji, walikuwepo katika maeneo ya hospitali pembeni ya kitanda cha Sajenti Minja,

Hapo Happy hakuvaa kistara kama anavyovaaga na badala yake alivaa suruali ya jeans iliyombana na juu alivaa fulana nyeupe iliyomkaa vema, ukiwa nae mbali huwezi kumjua ni kama yeye, labda ungepata bahati ya kumsogelea ndio ungemjua.

Pembeni ya kitanda alichokuwa amelazwa Sajenti Minja, hakuna aliyeruhusiwa kuongea neno lolote kutokana na hali ya Sajenti Minja.

Walimuangalia kwa dakika tano na kisha wakaenda kwenye eneo la kupumzikia watu walioenda kuwaangalia wagonjwa wao. Lilikuwa eneo safi lenye bustani na miti kadhaa kwa ajili ya kivuli, ila wao walijitenga sana na watu kwa ajili ya kuwa na Happy binti mchungaji.

"Kumbe mjomba wenu ndio yule?" Happy alimuuliza Omary wakati wakikaa na kipindi hicho Kayoza yeye aliwaacha umbali kidogo, alikuwa bize na simu yake,

"Ndiyo yule, vipi unamjua?" Omary akamtupia swali Happy binti mchungaji,

"Yule ameshawahi kuzaba vibao yule, namkumbuka vizuri" Happy alijibu huku akicheka kutokana na tukio alilolikumbuka la kupigwa makofi na Sajenti Minja,

"Alikupigia nini sasa?" Omary aliuliza kanakwamba hajui, kumbe anajua kila kitu,

"Tuachane na hayo bwana, nunua ice cream tule" Happy aliamua kuipotezea hiyo mada,

"Hapa hospitali hawawezi kuuza Ice cream, labda tutoke nje ya hili eneo" Omary alijibu,

"Ngoja tupumzike kwanza, tutaenda baadae" Happy aliongea,

"Kayoza njoo utupige picha mshkaji wangu" Omary alipaza sauti kumuita Kayoza aliyekuwa amejitenga na wao.

Wakati wakina Kayoza wakiwa nje ya hospitali, ndicho kipindi ambacho mama Kayoza na Mchungaji Wingo walikuwa wanaenda kumuangalia Sajenti Minja pia,

walipofika, wakamtafuta Daktari, kisha wakaongea nae maneno machache kabla ya kuruhusiwa kwenda kumuangalia Sajenti Minja,

"ila nimeamua kuvunja kanuni tu, kwa ajili ya heshima yako na mchungaji, kwa sababu muda wa kuangalia wagonjwa umeshakwisha",Daktari aliwaambia huku akielekea sehemu ilipo wodi aliyolazwa Sajenti Minja,

"asante baba, maana nisingekuja leo, hakuna ambae angejua hali ya mgonjwa pale nyumbani",Mama Kayoza alimshukuru Daktari,

"kwani wale vijana ambao unakujaga nao hapa ukai nao?",Daktari akamtupia swali Mama Kayoza,

"kwanini baba?, wale ni wanangu, ninachokula ndicho wanachokula", Mama Kayoza alijibu baada ya kuuliza swali,

"Basi hao wanao wametoka hapa muda si mrefu", Daktari alijibu,

"alah!, basi mimi hawakuniaga",Mama kayoza alimaliza namna hiyo.

"Sasa hivi wameshaujua mji, kila kona wanaijua" Mchungaji Wingo aliongea,

"Tena wanazurura hao, alafu kibaya zaidi uwa hawaagi" Mama Kayoza aliongea,

"Sasa Mimi naona mtoke, muda umeisha wakubwa zangu" Daktari aliongea huku akiwaimiza watoke,

"Jamani baba angu ebu niongezee hata dakika mbili tu" Mama Kayoza alimuomba Daktari,

"Mama uje baadae, wakubwa zangu wakikuta nimewaruhusu kuingia muda huu, kibarua change kitakuwa mashakani" Daktari aliongea huku akiendelea kuwahimiza watoke,

"Mama tutoke tu, tuje baadae" Mchungaji Wingo aliongea huku akitangulia kutoka na Mama Kayoza akamfuata kwa nyuma.

Wakamuona mgonjwa wao, kisha wakatoka kuelekea sehemu ya kupumzikia, kwa mbali wakawaona wakina Kayoza wako na Binti ambae hawakumtambua, tena huyo binti alikua wanabusiana(kiss) mdomoni na Omari, kila baada ya dakika.

Mama kayoza na Mchungaji Wingo wakawa wameshika njia ya kwenda walipo wakina kayoza,

"Mungu wangu, awa watoto wapumbavu sana" Mama Kayoza alilalama baada ya kuona wanamdhalilisha mbele ya Mchungaji,

"Alafu hata yule binti waliekuwa nae ni mjinga, eneo la hospitali unavaaje vile kama huna wazazi?" Mchungaji Wingo aliuliza huku wakiwa bado wanaelekea sehemu walipo wakina Kayoza.

Wakiwa wanazidi kuwasogelea na wamebakiza hata zisizo nyingi sana, Mara pasipo kutegemea, Mchungaji Wingo akatoa sauti ya mguno,

"mh!"

"vipi mchungaji?",Mama Kayoza akauliza..

.."kuna fikra zimenijia",Mchungaji Wingo akajibu katika sauti iliyotulia,

"nishirikishe tu mchungaji",Mama kayoza, nae akaomba ubia,

"ujue katika mazingira kama yale waliopo vijana wako, sio vizuri sisi kufika pale, maana tunaweza kufanya wakose raha kabisa, hasa yule aliyekuwa na binti"

,Mchungaji Wingo alitoa busara zake,

"kwanini tusiende tu, wakituona ndio watapata funzo, hawatarudia tena kufanya uovu katika eneo la wazi kama hili",Mama Kayoza aliongea katika sura iliyojaa jazba,

"hapana mama, wewe waache tu, ila ukifika nyumbani uwaambie vyote ulivyoviona",Mchungaji alimwambia Mama Kayoza

"sawa mchungaji, ila hawa watoto wamenihaibisha jamani, loh!",Mama Kayoza aliongea kwa masikitiko.

"ni ujana tu mama, ila itafika kipindi watajua kuwa wanachofanya ni ujinga",Mchungaji aliongea kwa upole.

"Yaani wanafanya ujinga uliokithiri, badala wakae hata wafunge wamuombee mjomba wao, wao wanazidi kujiongezea dhambi" Mama Kayoza aliongea kwa masikitiko,

"Bado hawajawa na akili hizo, ila kama nilivyosema kuwa itafika muda watajitambua" Mchungaji Wingo alijibu,

"Alafu na yule binti sijui wa wapi?, ebu mchungaji niruhusu tu nikawaone nimtambue na yule binti" Mama Kayoza aliongea,

"Kwa jinsi alivyovaa vile, ukienda pale itakuwa kama anakudhalilisha tu mwanamke mwenzake. Sio uvaaji ule, mi mwanangu akivaa vile namchinjilia mbali" Mchungaji Wingo aliongea kwa hasira,

"Haya baba, tuondoke tu, nitaenda kupambana nao nyumbani" Mama Kayoza aliongea.

Wakabadili njia na kushika njia iendayo nje ya hospitali. Hakuna aliyekuwa anaongea tena, kila mtu alikuwa na wazo lake, ila Mama Kayoza alionekana ana hasira nyingi zilizochanganyikana na fedhea iliyotokana na kitendo kilichofanywa na watoto wake.

Hasira aliyokuwa nayo ilisababisha mpaka machozi yaanze kuchomozà katika ncha za macho yake,

"Mbona kama unalia mama?" Mchungaji Wingo alimuuliza mama Kayoza,

"Hapana, ni hasira tu. Yaani away watoto" Mama Kayoza alijibu Mchungaji Wingo,

"Hutakiwi kuwaza sana, utavuka mipaka na mwisho itakuwa dhambi, kuwa na moyo wa hekima mama" Mchungaji Wingo alimwambia Mama Kayoza,

"Sawa nimekusikia mchungaji" Mama Kayoza aliongea huku akijifuta machozi,

"mama unaelekea wapi sasa hivi?",Mchungaji alimuuliza mama Kayoza wakiwa nje ya geti la hospitali,

"nataka nipitie hapo sokoni nikachukue mahitaji ya nyumbani kidogo",Mama Kayoza alimjibu Mchungaji Wingo.

"ok, ni vizuri, maana hata mimi naelekea uko uko",Mchungaji Wingo aliongea huku akionekana kuvutiwa na jibu la mama Kayoza.

Kisha akawasha gari yake, na kuelekea maeneo ya sokoni.

Mkuu wa Polisi aliamua kuifatilia ile kesi kwa elimu yake yote aliyonayo, kwa mbinu zake zote alizokuwa nazo na kwa uzoefu wake wote aliokuwanao, ila hakutaka kumshirikisha askari yoyote, kwa maana alishakosa imani na askari wake.

Na kwa kuanza, aliamua kumfuatilia Omari kwanza. Aliamini kwa kiasi kikubwa, kuwa ile picha iliyotolewa katika magazeti, ni taswira ya Omari kabisa, ila alichokuwa anafuatilia ni ushaidi tu.

"Ukila na kipofu hutakiwi kumshika mkono" Mkuu wa polisi aliongea na kutabasamu mwenyewe.

"na nikipata ushaidi wa kutosha tu, nahakikisha Sajenti Minja nae anafunguliwa mashtaka, lakini kama atapona, kama akifa na yenyewe itakuwa sawa, kwa maana yeye ni msaliti. Anakaa na mtuhumiwa na hasemi, hata kama ni ndugu yake inatakiwa afuate sheria", Mkuu wa Polisi aliongea na nafsi yake, kisha akaendelea,.

"kesho nitamtafuta kijana mmoja wa mtaani, anisaidie kuchunguza taratibu hii kesi, siwezi kumpa askari hii kesi, bora nimtafute kijana achunguze taratibu nitamlipa pesa, tena itakuwa vzuri zaidi kama huyo kijana atakuwa anaishi mtaa ule ule wanaoishi wao".

Hayo ndiyo maamuzi aliyofikia mkuu wa polisi. Na uzuri wa huyu bwana ni kusimamia maneno yake, ni mtu aliyekuwa anasifika kutokana na utendaji kazi wake na pia kulikuwa na tetesi kuwa huyu ndiye atakuwa mkuu wa polisi wa nchi nzima mwaka unafuata.

Wakina Omary walikuwa bado wanaendelea kula starehe zao na walikuwa hawana habari kama tayari mama yao alikuwa amewaona.

Hiyo siku Omary aliamua kujikumbushia maisha yake ya chuo, kukaa katika garden na mtoto wa kike kama vile huku wakila ice cream ndio ilikuwa maisha yake.

Kipindi chote hicho Kayoza alikuwa amekaa kimya ingawa alikuwa anataka kuondoka ila hakutaka kumwambia Omary kwa maana alihisi kama atamuharibia au atamkatishia starehe mwenzake, na alipofikiria kumtoroka pia aliwaza akifika nyumbani akiulizwa mwenzake yupo wapi? atajibu nini na walitoka pamoja?

Ikabidi akae kinyonge tu huku akicheza game katika simu yake alipochoka alikichukua kitabu chake cha riwaya kilichoitwa FAZA WA KANISA kilichoandikwa na mwandishi ALEX KILEO, akawa anakisoma.

"jamani eee, mi naona tuondoke sasa",Kayoza aliwaambia wenzake baada ya kusoma kurasa kadhaa za kile kitabu cha riwaya,

"dah!, kweli mzazi, maana tumeuza kichizi", Omari alijibu kwa lugha ya vijana, akiwa na maana ya kwamba, wamekaa sana,

"tunaenda kwa miguu au?",Kayoza akauliza,

"leo kwa kuwa niko na malkia wangu hapa, nitakodi taxi", Omari aliongea huku akimshika mkono Happy binti wa Mchungaji.

"Tutembeeni tu, kwani tunawahi wapi?" Happy binti Mchungaji aliuliza huku akitabasamu,

"Hatutaki uchafuke, mrembo kama wewe ukichafuka kisa umetembea kwa miguu itakuwa aibu kwetu" Kayoza aliongea kwa utani na kufanya wenzie wacheke,

"Mbona mi nimeshazoea jamani" Happy binti mchungaji aliongea huku akideka kwa Omary,

"Umezoea kwenu ila sio kwangu. K ita gari mwanangu tusepe" Omary alimuagiza Kayoza kwa nyodo na kumfanya Kayoza aondoke huku akitabasamu kutokana na mbwembwe za jamaa yake huyo.

Wakatafuta taxi, wakakubaliana bei na dereva taxi, kisha safari ya kurudi nyumbani ikaanza.

Kayoza alikaa kiti cha mbele na Omary na Happy binti mchungaji walikaa siti za nyuma kwa ajili ya kuwa huru kufanya mambo yao kama wapenzi.

Walipokaribia katika maeneo ambapo Sajenti Minja alipata ajali, wakamshauri dereva taxi apunguze mwendo kwa maana kulikuwa na kona mbaya na pia bado walikuwa na kumbukumbu ya tukio baya lililomkuta Sajenti Minja katika eneo hilo.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)