Vita vya Mapenzi (1)

0

SEHEMU YA KWANZA
Kelele za Shangwe na mbinja vilisikika kutoka kwa makondakta na wapiga debe kadhaa waliokuwa nje ya lango la kituo cha mabasi cha Ubungo jijini Dar Es Salaam, wote wakimshangilia dereva wa basi la NBC Classic kwa umahiri wake na utundu alioutumia mpaka kuwa wa kwanza kutoa gari kabla ya madereva wengine wote kwa asubuhi ile.

Kutokana na wingi wa mabasi katika Stendi ile, yote yakiwania nafasi ya kuwahi kutoka ilihitaji dereva hodari na mweledi ili kuwapiku wenziwe, na hicho ndicho alichokifanya dereva yule mwenye ndevu nyingi mashavuni. Sasa kwa nini asipongezwe?

Abiria wake nao walikuwa wakimpa heko kimyakimya.

Safari hii ilikuwa inaelekea mikoa ya Morogoro, Dodoma, na hatimaye Tabora ambako ndipo hasa alipokuwa akielekea kijana mmoja mrefu wa wastani, maji ya kunde, na mwenye mwili wa wastani aliyekuwa ameketi mwanzoni kabisa ‘Seat No. 10’.

Sura ya kijana yule haihitaji ‘Degree’ hata moja ya saikolojia kutambua kuwa alikuwa na furaha kubwa moyoni. Japokuwa abiria wengi walionekana kuwa na nyuso zenye bashasha hasa baada ya dereva kuzikonga nyoyo zao kwa kuwahi kulitoa basi mapema na kuianza safari, lakini kwa kijana huyu palikuwa na vingi vilivyomfanya mara kwa mara aachie tabasamu bila kuhofia kutazamwa na abiria wenzie. Mbali ya kuwa alikuwa amefanya vizuri sana katika masomo yake aliyohitimu katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam lakini pia alikuwa na hamu ya kwenda kuonana na wazazi wake, nduguze na marafiki ambao kwa muda mrefu sana hakuwa ameonana nao. Lakini kubwa zaidi lilikuwa ni Sharifa. Mwanamke aliyempenda kwa dhati, aliyewekeana nae ahadi ya kufunga pingu za maisha na wazazi nao wakaridhia.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
Hakika safari ilikuwa na maana kubwa sana kwa kijana huyu.

Wakati mawazo yakiendelea kutalii kichwani mwa kijana huyu, mara kwa mara alikuwa akikatizwa na mzee mmoja mwenye asili ya ki-asia ambaye alikuwa akimuangalia sana mpaka kijana akawa anaingiwa hofu. Si kwamba mzee huyu alikuwa akimfananisha bali macho ya yule mzee yalionesha kitu cha ziada ambacho kiliifanya ile hofu ya yule kijana ifunikwe na hamu ya kutaka kukijua kitu hicho. Mara kadhaa kijana alijaribu kumkazia macho yule mzee aliyekuwa ameketi jirani yake kabisa katika ‘Seat No11’, lakini kila walipokutanisha macho, mzee yule alijibaraguza na kuangalia pembeni kana kwamba hakuwa akimuangalia tangu mwanzo.

Kijana alipoona kero ya kuangaliwa kama sanamu inamzidia akaingiza mkono katika kijibegi chake kidogo cha rangi nyeusi alichokuwa amekipakata miguuni kwake, akatoa miwani myeusi na kuibandika usoni ili asiendelee kupata bughudha ya kuangaliana na mzee yule. Hakuishia hapo. Akatoa ‘Ipad’ yake akaiunganisha na waya maalumu wa visikilizio na kuvipachika masikioni visikilizio vile na kuanza kupata muziki uliombembeleza na hatimaye kumsahaulisha habari za mzee yule.

Safari iliendelea kwa raha mustarehe, kila mmoja akifanya yake. Wapo waliokuwa wakiangalia TV maalum iliyofungwa ndani ya basi hilo, wapo waliokuwa wakisoma vitabu na magazeti, na wengine wakiwa wanauchapa usingizi tu. Hakika kila abiria alikuwa hana wasiwasi na safari yake. Dereva alionekana kuijua vyema kazi yake maana si tu mbwembwe za kutoa gari pale getini Ubungo bali hata barabarani aliyajua vizuri majukumu yake, ndani ya masaa kadhaa gari lilikuwa likiiacha morogoro, matairi yake yakizunguka kwa kasi huku yakiendelea kusuguana na lami.

Wakati safari ikiendelea namna ile, kijana wa kiti namba kumi alijisahau kabisa kuwa alikuwa safarini pamoja na jumuiya ya wasafiri wengine, akili yake ikiwa imechotwa kabisa na muziki aliokuwa akiusikiliza kutoka kwenye iPad yake, na akiwa katikati ya dunia yake ile ya pekee akitumbuizwa na muziki mororo huku akiwa amaefumba macho kwa raha zilizomzonga, alishtushwa na mkono laini uliomshika huku ukimtikisa bega lake la kulia. Alikurupuka kutoka kwenye ulimwengu ule wa raha na kutumbia macho, akikutana macho kwa macho na mwanadada mnyange akiwa amemchanulia tabasamu la kumcheka.

Baada ya kujipikicha macho na kujikumbusha kuwa pale alikuwa ndani ya basi, aliweza kumtambua kuwa yule dada alikuwa ni mhudumu wa ndani ya lile basi kutokana na sare maalum alizokuwa amevalia, lakini kilichomshangaza ni kitendo cha baadhi ya abiria waliokuwa jirani yake kuwa wakicheka huku wakimuangalia yeye. Alibaki akijiuliza ni lipi alilolifanya ambalo liliwafurahisha namna ile lakini hakupata jibu. Aligonganisha tena macho na yule mzee wa ki-asia, na kuona kuwa yule mzee alikuwa akiendelea kumuangalia tu. Hacheki wala hanuni, jambo ambalo lilizidi kumtisha. Alimgeukia tena yule mhudumu wa basi na kuonaakiinama na kusogeza kreti la soda, ndipo alipojua kuwa ulikuwa ni muda wa kupata vinywaji.

“Unatumia soda gani Pharell?” Msichana alimuuliza huku bado akiwa anatabasamu, na kijana alishtuka kusikia anatajwa kwa jina lisilo lake, lakini haraka akakumbuka kuwa kabla hajapitiwa na usingizi alikuwa akisikiliza wimbo wa Pharrell William, msanii kutoka marekani hivyo akatambua kuwa kwa kuwa ‘Earphone’ zake zilikuwa masikioni muda wote huku sauti ikiwa juu sana bila shaka alikuwa akiimba kwa sauti ya juu kwa kuufuatisha wimbo ule, ndio maana alionekana kituko kwa abiria wenzie.

Oh, shiit!

Haraka akachomoa vile visikilizio kutoka masikioni na kumjibu yule mhudumu kwa tahayari kidogo.

“Eeem, Nipatie Fanta,tafadhali.”

“Fanta gani?”

“Fanta ukwaju,”

Jibu hilo liliwafanya abiria wenzake waangue vicheko kwa mara nyingine tena huku wakimuangalia kwa uelewa mpya yule kijana , kwani pale kila mmoja akawa ameshaelewa kuwa kijana alikuwa mtundu sana.

“Mnh jamani kuna fanta ya ukwaju kweli duniani?”

“Basi kama hakuna nifungulie yoyote ile uipendayo wewe dada’angu” Mhudumu akamchagulia Fanta Orange na kumkabidhi huku akiunganisha na tabasamu pana. Wakati mhudumu anaifungua soda ile ndipo kijana aliposhtushwa na sauti ya yule mzee wa ki-asia, ambaye naye sasa alikuwa akitabasamu.“Suhail we’ ni mtundu sana, halafu leo unaonekana una furaha sana eeh?”

Heh!

Kijana alishangaa upeo wa kushangaa. Lile swali lilimuacha hoi, kwani kwa hakika alikuwa anaitwa Suhail.

Mnh, mzee! Um…umejuaje kama nina furaha…? Na jina langu…umelijuaje mzee?”

“Nimekusikia ukiimba muda mrefu tena kwa sauti ukisema ‘Because am happy’,” Mzee alimjibu huku akizidi kutabasamu na kumfanya Suhail sasa athibitishe mawazo yake kuwa ni kweli alikuwa akiuimba kwa sauti ule wimbo wa Pharrel William,‘Happy’. Lakini pia akaona kuwa yule mzee hakumjibu swali lake la pili.

“Duh, okay…na jina langu? Umelijuaje?” Akakumbushia. Mzee akazidisha upana wa tabasamu lake tulivu, kisha akampigapiga begani Suhail kwa namna ya kumpoza au kumuondoa hofu.

“Manta khouf’ ‘young man’,” Alimwambia kwa upole, akimaanisha kuwa “usiwe na hofu kijana”, kisha hapo hapo sura yake ikabadilika mithili ya mtu aliona au aliyekumbuka kitu kibaya sana. Mzee akakunja uso na kubaki akiangalia mbele kwa dereva, akimuacha Suhail akiwa amepigwa butwaa.

Safari iliaendelea kushika kasi, lakini hofu iliyokwisha ingia moyoni mwake, ilikuwa imeshika kasi zaidi. Soda haikunyweka tena, wakati mtungo wa maswali yasiyo na majibu ukijirefusha kichwani mwake.

Huyu mzee ni nani?

Amenijuaje mimi?

Mbona sina kumbukumbuku ya kupata kumuona popote pale duniani?

Na kwa nini tangu mwanzo wa safari ananiangalia sana? Na kikubwa zaidi, kwa nini baada ya kuongea name maneno machache tu akaebadilika ghafla kama aliyeona kitu kibaya?’

Maswali yalizidi kumtesa Suhail. Alitamani amhoji zaidi yule mzee lakini sura mpya ya mzee ilimhakikishia kuwa asingejibiwa hata swali moja. Mzee hakuwa na mpango naye tena, na badala yake alionekana kumakinika na kitu ambacho Suhail hakukiona wala kukijua..

Taratibu Suhail akaiweka vema usoni miwani yake na kujilaza kitini. Muda mfupi baadaye, akapitiwa na usingizi mzito.

Walipokuwa wanakaribia kuingia Dodoma, wakiwa katika mapori ya mwisho mwisho kabisa ambako hapakuwa hata na dalili ya makazi ya watu, kwenye kona ya mlima Kisera likatokea Lori kubwa likiwa na shehena ya magogo makubwa likija kwa kasi ya ajabu. Licha ya dereva wa Lori hilo kuliona lile basi aliendelea kuendesha kwa kasi ileile, na dereva wa basi akafanya jitihada ya kupeleka gari lake pembeni lakini Lori likamshinda nguvu derava na kupamiana uso kwa uso na basi lile.

Ilikuwa ni ajali mbaya kupata kutokea. Basi lilisambazwa vibaya na kupinduliwa hovyohovyo huku baadhi ya magogo yaliyochomoka kwenye lile Lori yakilifuata kwa juu na kuzidi kulipondaponda. Lile Lori lilianguka na kupindukia kwenye mashamba ya mahindi yaliyokuwa kando ya barabara, japo mashamba yale yalikuwa hayajalimwa kwa muda mrefu sana.

Suhail alishituka kutoka usingizini wakati ajali ikitokea na hakujua kilichotokea mara moja, ila baada ya muda mfupi akaelewa kuwa walikuwa wamepatwa na ajali. Tena ajali mbaya kabisa. Alijiona akiwa ametapakaa damu mwilini mwake, japo hakujua damu ile ilikuwa ikimtoka sehemu gani. Alijaribu kujikaza na kujiinua, lakini alihisi kuishiwa nguvu. Sauti za vilio vya maumivu na hamaniko za watoto, akina mama na hata za akina baba zilitawala ndani ya basi lile. Aliona miili ya baadhi ya abiria wenzake ikiwa tayari imeshaachana na roho zao, ikiwa imezagaa hovyo ndani ya basi lile. Wahka ukamshika. Woga ukamgubika.Alijikakamua na kujilazimisha kuinuka kiubavu-ubavu, akaketi.Na ndipo alipoweza kuona vizuri matokeo ya ajali ile. Hakika ilikuwa ni ajali kubwa na ya kutisha sana.

Baada ya muda mfupi wa taharuki ile abiria wachache walionusurika wakawa wameshainuka na kutoka nje ya basi huku wakisaidiana kuwatoa majeruhi wenzao na kupeanaa huduma ya kwanza kwa kadiri walivyoweza katika mazingira yake.

Kwa shida Suhaili akajilazimisha kuinuka ili atoke nje ya basi ajiangalie hali yake na ikibidi aungane na abiria wenzake kwenye kutoa msaada kwa wenzao, na katika kufanya hivyo ghafla macho yake yakaangukia kwayule mhudumu aliyekuwa akisambaza vinywaji ndani ya basi akiwa amelalachali, chuma kikiwa kimemtumbua vibaya tumboni, macho yakiwa yamemkodoka bila kuona. Alikuwa amepoteza maisha. Suhail akafuta machozi yaliyoanza kumtoka bila ya kutaka, akageuza uso wake upande mwingine kuikwepa taswira ile.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)