Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Watu wale wakawasogelea akina Suhail wakawasalimu huku wakiwapa mikono na kuwakumbatia kwa furaha, bado lilikuwa ni tukio lisilo na majibu kwa Suahil, baada ya Salamu ile wote wakafuatana mpaka katika lile zuria jekundu kisha wakaketi kwa pamoja kwa kuizunguruka duara ile sinia. Haikuchukuwa dakika tano ghafla ukafunguka mlango usawa wa lile kabati kubwa lililokuwa upande wa kushoto, kwa harakaharaka usingeweza kutambua kuwa pale palikuwa na mlango kwa jinsi palivyonakshiwa kitaalamu
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Baada ya mlango ule kufunguka wakasimama wote kuwashiria kuwa kuna mtu mzito anawasili eneo lile, ndipo sasa macho ya Suhail kwa mara ya tatu ukiachalia mbali mara ya kwanza kule kwenye ajali na mara ya pili kule usingizini, hapa akamuona Mzee Shamhurish akifika na kupokelewa kwa heshma na furaha na wale watu waliokuwa wamesimama, safari hii Mzee Shamhurish akiwa amevaa kanzu nyeupe huku amejifunika kichwani kwa kiremba chekundu kilichomfanya aonekane tofauti na vijana wengine wote mule ndani. Baada ya Salamu Mzee Shamhurish akaketi chini ndipo na wale wengine nao wakaketi
“Haya bwana Suhail karibu sana Bagamoyo,” alivunja ukimya Mzee Shamhurish huku akimtazama Suhail usoni
“Ahsante mzee,” alijibu Suhail kwa sauti iliyojaa kitetemeshi cha uoga
“Kwanza kabisa jisikie huru, jisikie kama upo nyumbani, ondoa hofu na mashaka moyoni mwako. Sisi sote hapa tunafuraha ya kuwa na wewe mahala hapa, sisi ni wenzio hivyo hakuna haja ya kuogopana ili tumalize zoezi lililo mbele yetu.. Hiki ndicho haswa kilichokuleta Bagamoyo na si huko kwa Mzee Atrash, siku nyingine kuwa makini kijana” akajiweka sawa katika zuria lile bwana Sufian Ibn Shamhurish kabla hajaendelea kuzungumza
“Na kama utakuwa makini sidhani kama yatatokea kama yale ya kule nyumbani kwako Mbezi..” kauli ile ikamfanya Suhail sasa athibitikiwe kichwani mwake kuwa lile tukio lililomkuta usingizini lilikuwa ni la kweli kama alivyoamini, hakuna na cha kuhoji zaidi ya kumsikiliza mzee yule “..Jamani hakuna muda wa kupoteza, huyu ndie bwana Suhail Kusekwa ambaye ni mchumba wa ndugu yenu Bi Shekhia, na leo ndio ile siku yao ya kufunga ndoa ili wakaishi maisha yao kama mume na mke, hovyo nadhani sasa tungeendelea na taratibu za kufunga ndoa hii maana leo nitahitajika kuondoka na kwenda yemen mara moja” Baada ya maneno ya Mzee Shamhurish yaliyouchoma moyo wa Suhail, akasimama mwarabu mmoja hivi mtu wa makamo akaanza kuzungumza
“..Taratibu zetu ni fupi sana, na kwakuwa Suhail amekubali kuoa na Shekhia amekubali kuolewa hivyo hakuna kingine zaidi ya kuwafungisha ndoa, pia kwa Suhail kutakuwa na mkataba wa matumizi ya ‘Khatam Budha’ ambao atausaini kwa kuzingatia mashart na vigezo..” Baada ya msemaji kufika mwisho akainuka kijana mmoja akakabidhi nakala mbili za mkataba kwa Mzee Shamhurish ambaye nae akakabidhi nakala hizo kwa Suhail ili azipitie na kujiridhisha ndipo aweke saini, Suhail akazipokea nakala hizo akiwa hana ujanja wa kukataa hata kidogo kutekeleza kilicho mbele yake, akaanza kuipitia mikataba ile lakini akili haikuwa pale kabisa, aliweza kuvielewa baadhi ya vipengelea vilivyo ndani ya mkataba ule lakini baadhi hata hakuviona kwa jinsi alivyohamanika, hakuwa katika hali ya kawaida kabisa, kichwa kilishavurugika
Baada ya kupitia kwa haraka na woga mara punde akawa amemaliza kupitia akazirejesha nakala zile kwa Mzee Shamhurish
“Umesoma kwa makini?,” alihoji mzee Shamhurish
“Ndio mzee.”
“Una uhakika?”
“Ndio” alipokiri tu akasogezewa kalamu ili aweke saini yake, akafanya hivyo katika mikataba yote miwili kisha akainua kichwa na kumuangalia Mzee Shamhurish alieonekana kuwa na furaha. Baada ya tukio lile akainuka tena Mzee yule alietoa maelekezo ya mkataba ule akaenda mpaka kwenye kabati akatoa bakuli kubwa, alipolitoa tu wote wakasimama, na Suhail nae akaamriwa asimamae kisha wakaongozana mpaka kwenye ile korido ndefu, wakaendelea kutembea kuelekea kule kwenye giza lakini hawakufika mbali wakasimama na kuufungua mlango uliokuwa upande wao wa kulia kisha wakaangia ndani.
Kilikuwa ni chumba kama vilivyo vyumba vingine vya mitaani, tofauti yake na uzuri wake na vilivyomo, kilikuwa ni chumba chenye hadhi ya Nyota tano kama ingekuwa ni Hotelini, hapakuwa na vitu vingi sana zaidi ya kitanda kikubwa cha sita kwa sita chenye mtindo wa sofa, Kabati kubwa moja, na ‘Dresing table’ moja iliyochongwa kwa mtindo ambao si wakawaida, na baadhi ya vitu vingine vichache sana mule chumbani. Juu ya kitanda walikuwa wameketi wanawake watatu, wote wamejitanda vizuri kwa Shungi zao. Walipofika pale karibu ya kitanda wote wakasimama kwa heshima ndipo Suhail akamuona vizuri binti aliyekuwa ameketi katikati, alikuwa Shekhia akiwa ametulia kiungwana sana huku macho ameyainamisha chini, japo hakuwa amevaa mavazi yale aliyomuona nayo kule nje
“Haya tuoneshe mkeo mtarajiwa hapo,” Sauti ya Mzee Shamhurish ilirindima chumbani huku akimuangalia Suhail, haraka Suhail akamsonta Shekhia kwa kidole chake, hapohapo Mzee Shamhurish akawaamuru wanawake wale akiwamo mwanae waketi, kisha yule Mzee alietoa maelekezo juu ya mkataba akarudi nyuma kama hatua tano hivi, kisha na wale wafuasi wengine wa Mzee Shamhurish nao wakarudi nyuma wote kwa pamoja kimyakimya, wale akina dada waliokuwa wameketi na Shekhia kitandani nao wakawafuata wenzao, Suahil alipoona vile nae akataka kurudi nyuma lakini akazuiliwa na Mzee Shamhurish, akabaki amesimama palepale hivyo pale karibu ya kitanda wakabaki wamesimama watu wawili, Suhail na Mzee Shamhurish wakati Shekhia akiwa ameketi kitandani,
“Ni kitu gani hicho ndani ya bakuli,?” Mzee Shamhurish alimuuliza Suhai
“Nadhani ni damu hii”
“Naam ni damu ya mbuzi, sasa vua Pete yako kisha uiweka humo ndani ya bakuli” Suhail akatii agizo lile, akaivua pete ile iitwayo “Khatam Budha’ kisha akaiweka ndani ya Bakuli kubwa lililo na damu. Alipoiweka tu akapigwa na butwaa, Damu ikaanza kupungua ndani ya bakuli, yaani bila shaka pete ilikuwa ikiinywa damu ile, macho ya Suhail yaliendelea kuliokodolea bakuli lile mpaka damu yote ikaisha na kubaki Pete tu ndani yake
“Hivyo ndivyo utakavyokuwa ukifanya kila baada baada ya mwezi mmoja utapewa maelekezo vizuri, sasa Ichukue na uivae tena,” Mzee Shamhurish alimuelekeza Suhail wakati huo wale watu wengine wakiwa nyuma kabisa huko, alipomaliza kuivaa tu Mzee Shamhurish akahitimisha
“Kuwanza sasa Shekhia ni Mkeo halali” kisha akampa mkono, hapo hapo wale watu wengine wakasogea wakiwa na furaha wakampa mikono Suhail, ilikuwa ni mikono ya pongezi kwa kufunga ndoa, Suhail hakuelewa hekma ya Kukabidhiwa mke baada ya Pete ile kunywa damu ya mbuzi lakini hakuwa na haja ya kuhoji chochote zaidi kupokea mikono ya pongezi, Kisha Mzee Shamhurish akaendelea kuongea
“Tutakuwa na tafrija fupi kwa ajili ya furaha hii ya ndoa Saa tatu kutoka hivi sasa, baada ya hapa nitahitaji faragha na Suhail kwa ajili ya kumpa maelekezo ya kuitumia ‘Khatamu budha’ kisha nitaondoka na kurejea Yemen Lakini Suhail na Shekhia mtabaki hapa Bagamoyo kwa siku saba mfululizo, Kuwanzia sasa Suhail utakuwa ndie mmiliki wa Ngome hii yote ya Bagamoyo japo utaamua muishi wapi wewe na mkeo”
Baada ya maneno hayo ya Mzee Shamhurish watu wote mule chumbani wakaanza kutoka nje kwa utaratibu maalum huku Mzee Shakhurish mwenyewe akiwa mbele yao na kuwaacha mume na mke wakiwa peke yao chumbani, wawili tu..
*****
Utendaji kazi katika kampuni ya Bright Future Distributor Ltd inayojijishughulisha na upakiaji na upakuwaji mizigo bandarani inayomilikiwa na Suhail ulikuwa ukilegalega kwa kiasi Fulani huku hofu na Sintofahamu vikatawala Bongo za wafanyakazi karibu wote, kwa jinsi walivyomuhusudu ‘Boss’ wao basi haikuwa suala rahisi wao kuendelea na majukumu yao wakati yapata siku ya tatu ‘Boss’ wao hajulikani alipo, kila alieulizwa hakujua ni wapi Boss wao alipokwenda, Simu zake hazipatikani kabisa.
Meneja wa kampuni hiyo Bwana Frank Mkali kwa kushirikiana na na Meneja mwenzie wa kampuni nyingine ya Suhail iitwayo Deseret Insuarence Brokers inayojishughulisha na masuala ya Bima Bwana Kilingo Mkude waliamua tu sasa kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi baada ya kujiridhisha kuwa hali haikuwa sawa maana majibu ya walinzi katika nyumba za Suhail yalikuwa hadhir kuwa Suhail hakuwepo ndani kwa siku tatu mfululizo na hawana taarifa yoyote juu yake huku gari zake zote zikiwepo nyumbani tu
Mr Mkali na Mkude mbali ya kuwa watendaji wakuu katika kampuni za Suhail lakini pia hawa ni jamaa zake wa karibu sana, walisoma wote katika Chuo kikuu cha mlimani japo hawakuwa karibu sana bali walifahamiana hivyo kwa Suhail ilikuwa ni faraja sana kuwapa ajira nzuri jamaa zake wale akiamini kwa kujuana kwao watakuwa waaminifu na wachapakazi wazuri sana
Kwa vijana hawa ilikuwa ni maswali tu ndani ya vichwa vyao kuwa imekuwaje jamaa yao waliotoka nae Chuo amekuwa tajiri ndani ya muda mfupi na hatimaye kuwa muajiri wao? Lakini majibu yasiyo mazito kutoka kwa Suhail yalikuwa yakiwaliwaza kiasi kidogo. Suhail aliwaambia kuwa zile mali zote ni za Mzee mmoja wa ki-Yemeni lakini hataki kujulikana hivyo yeye kwakuwa alikuwa akijuana nae kitambo Mzee Yule akamtaka afungue miradi ile na kuisimamia kama yak wake.
Baada ya kumaliza kutoa taarifa kituo cha Polisi kila mmoja akarejea katika kituo chake cha kazi kuendelea kuwajibika, Lakini Mr Mkude yeye hakuridhika kabisa akaendelea kuperuzi baadhi ya nyaraka za Suhail zilizomo ofisini mwake ili kama ataweza kupata namba za watu wake wa karibu, Na kweli alifanikiwa kuchukuwa namba kama tatu hivi..
“Leo asubuhi alikuja hapa Mzee Fungameza kukusabahi lakini ule ujie wako Mnh,” Aliongea Mama Suhail akimpa taarifa mumewe Mzee Kusekwa
“Najua tu anakuja kunitukana kikubwa, na sina hata cha kujitetea maana nitasema nini sasa,” alijibu Mzee Kusekwa kwa hasira, kikapita kimya cha muda kidogo kabla hajaendelea kuongea Mzee Kusekwa “..Mke wangu ukisikia aibu ndio hii, watu wanajiuliza iweje mtoto amepata ajali lakini hataki kurudi kwao?, mwishowe ataambiwa amewaibia abiria wenzie ndio kaamua kujificha kabisa”
“Kwakweli huyu mtoto anatuvua nguo sasa, Mzee Fungameza anajua kuwa tulikuwa tunataraji kuwanza mazungumzo ya mipango ya kuwaozesha vijana hawa sasa anaona kimya tu, hapati majibu yoyote sasa hii kama si aibu kitu gani?.” Mjadala ulikuwa mkubwa, hakika wazee hawa walikuwa wamekwazwa sana na kitendo cha Suhail kutokurejea nyumbani tangu alipopata ajali
“..Na kwambia labda sio mimi Kusekwa ila huyu mtoto atakoma na mimi, siku akitia mguu wake tu Tabora hii anakutana na Ndoa, huko Dar atarejea na mke asinichezee mimi,” Alibwata Mzee Kusekwa
“Vema aje akiwa salama. Hivi siku ile uliposema umempigia mlikubaliana kitu gani?”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi