Vita vya Mapenzi (11)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“..Na kwambia labda sio mimi Kusekwa ila huyu mtoto atakoma na mimi, siku akitia mguu wake tu Tabora hii anakutana na Ndoa, huko Dar atarejea na mke asinichezee mimi,” Alibwata Mzee Kusekwa
“Vema aje akiwa salama. Hivi siku ile uliposema umempigia mlikubaliana kitu gani?”
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
“Enhee tena umenikumbusha, siku ile simu ilikatika kabla hatujamaliza mazungumzo, nae vile mshenzi hakunipigia tena bila shaka alijua tu kuwa hali ya hatari, sasa nikaweka vocha tena lakini nilipompigia hakupatikana tena, na mpaka kesho yake asubuhi nilimtafuta alikuwa bado hapatikani tu.”
“Mimi nadhani ungemtafuta tena ili hata kama utakutana na Mzee mwenzio huko ujue unamjibu nini mapema.” Maneno ya Mama Suhail yakajibiwa kwa vitendo na Mzee Kusekwa ambaye harakaharaka alitoa simu yake ili ampigie mwanae, lakini akiwa ameishikilia simu yake akajikuta yeye ndio anapigiwa na namba mpya asioifahamu. Akabofya kitufe cha kijani katika nokia yake ya tochi akaweka simu sikioni na kuongea
“Hallow”
“Mzee Shikamoo,” Sauti iliyotoka upande wa pili wa simu ilimuamkia Mzee Kusekwa
“Marahaba, nani mwenzangu?”
“Mimi naitwa Kilingo Mkude ni mfanyakazi katika kampuni ya Suhail, namuulizia Mzee Kusekwa”
“Mfanyakazi katika kampuni ya Suhail?”
“Ndio, Kwani wewe sio baba yake na Suhail?”
“Mimi ni baba yake ndio”
“Sasa Mzee mimi naulizia tu kama huyu bwana yupo huko?””
“Huko wapi, mbona haueleweki wewe?”
“Nina maana huko Tabora, huku Dar hayupo na hajaaga mtu tangu majuzi, simu zake hazipatikani, tumemtafuta kule kwenye nyumba yake ya mbezi hayupo, na hata kule Ilala mlinzi wake amesema hajamuona sasa tumepatwa hofu kidogo”
“Khaa, Suhail ana kampuni na nyumba Dar?”
“Mzee hivi wewe ni Baba yake Suhail kweli naona kama hatuelewani!”
“Hebu ngoja kwanza, emesema Suhail haonekani?Ameenda wapi?”
“Khaa sasa mzee mimi nakwambia kuwa hajaaga mtu halafu we unaniuliza ameenda wapi? !” Mkude akakata simu na kumuacha Mzee Kusekwa akiwa ameduwaa
“Vipi mbona hivyo?,” alihoji Mama Suhail kufuatia majibizano yalikuwa yakiendelea kati ya mumewe na mtu asiemjua. Mzee Kusekwa akamuelezea mkewe kila kitu hakika mama Yule nae alibutwaika
“Sasa haya majanga, Huyu mtoto ametoa wapi Kampuni jamani! Na ametowekaje ghafla! Isije ikawa huyo aliekupigia wewe ni muhalifu na ndie amemteka mwanagu jamani..” Mama Suhail alikuwa akihatahata kwa maneno
“Hilo nalo neno, hata mimi najiuliza huyu Kijana ametoa wapi namba zangu?”
“Au mume wangu ulisemezana nae maneno mabaya siku ile ulipoongea nae ndo maana akachukuwa uamuzi huo mbaya?”
“Hiyo wala haihusiani kabisa, Unajua kuna..” Kabla Mzee Kusekwa hajamalizia kauli yake akakatizwa na mtu aliyekuwa ‘Akibisha’ hodi, ilikuwa ni sauti ya Mzee Fungameza, Ilikuwa ni ghafla bin Vuu, Mzee Kusekwa alitamani ajifiche katika mfuko wa suruali yake, akiwa bado ameishiwa maarifa tayari Mzee Fungameza akaingia ndani na kuwanza kuwasabahi
“Wenyewe salama humu?”
“Salama kiasi, karibu bwana mkubwa,” Alijibu Mzee Kusekwa na kumfanya Mzee Fungameza kubaki roho juu
“Kunani tena jamani?”
“Mnhuu, si huyu mwanao Suhail..”
“Kafanya kipi tena?” Mzee Kusekwa akaanza kumsimulia Mzee mwenzie aliyekuwa ametulia juu ya kochi la kukereza huku akisikiliza kwa makini mpaka mwisho wa habari ile japo masuala ya Suhail kuwa anamiliki kampuni na ana nyumba Mbezi na Ilala hakuviweka wazi. ilikuwa ni habari inayoacha maswali mengi kuliko majibu. Baadhi yalikuwa yakiingia akilini na baadhi yakipita tu hewani
“Haya sasa mapya, Hebu mpigie huyo Mtu ili atujuze habari kamili maana hii si ya kupuuzia kabisa,” hatimaye Mzee Fungameza alivunja ukimya..
“Tatizo mimi sina namba yake.”
“Jamani Baba Suhail si umetoka kuongea nae sasa hivi, sasa hauna vipi namba yake?,” aliuliza Mke wa Mzee Kusekwa aliyekuwa ameketi kwenye kigoda
“Aaah mwenzangu nilishachanganyikiwa mie, hebu itafute humo umpigie,” Mzee Kusekwa alikuwa akiongea huku akimkabidhi simu Mzee Fungameza
*****
Katika Kasri la chini kwa chini la Mzee Sufiani bin Shamhurish ambalo kwa sasa linamilikiwa na mkwewe Suhail Kusekwa hali ilikuwa shwari kabisa, hapakuwa na ghasia wala rabsha za aina yoyote zaidi ya raha na burudani za fungate la maharusi wawili, tayari Mzee Sufiani alikwashaondoka na kuelekea zake Yemeni baada ya kuhakikisha amemfundisha Suhail namna ya matumizi ya ‘Khatam Budha’. Suhail alikuwa amejilaza juu ya kitanda cha kifalme, kitanda chenye nakshi za dhahabu na almasi huku akikandwakandwa na kusingwa mafuta na Mnyange Shekhia Bint Sufian, hofu ilikuwa imeanza kuyeyuka mithili ya theluji juani.
Akiwa kitandani alikuwa akiitazama ile Pete ya Budha kwa umakini hakika alishangazwa sana na uwezo mkubwa wa pete ile japo aliyaamini maneno ya Mzee Atrash kuwa Mzee Sufian hatomfundisha kila kitu lakini kwa hayo machache tu aliyofundishwa alishangazwa sana, aliamini kuwa atakuwa salama na tajiri mkubwa sana, mambo mawili yatokanayo na Pete ile yalimnyima raha mara kwa mara, la kwanza ni kila alipokumbuka kauli yam zee Sufiani kuwa atawajibika mara moja itakapohitajika kwenda kupambana na kuwaangamiza majini wa Budha endapo wataonesha kugundua alipo mzee Sufiani hata kama itakuwa huko Yemeni Pete ile itampa taarifa maalum na itamchukuwa kwa upepo mpaka huko na kufanya mashambulizi, pili kila alipomfikiria Mchumba wake halali Sharifa alihisi kuzimia.
Akiwa anaendelea kupata raha kutoka kwa mpenzi wake wa tangu chuoni na hatimaye sasa ni mkewe, Mke mwenye asili ya ujini, ndipo alipokumbuka kuwa hakuiwasha simu yake tangu mara ya mwisho alipoongea na Baba yake
“Hebu niletee simu yangu iko kwenye Suruali,” Suhail alimwambia Shekhia
“Simu ya nini tena jamani mume wangu,” alijibu binti Yule mtoto wa Jini kwa deko na maringo
“Unajua tangu nilipokuja huku simu ile haikuwa hewani, sasa najua tangu nimeshasababisha usumbufu mkubwa kwa vijana wangu wa kazi na hata kwa wazee nyumbani” Shekhia akainuka kitandani kwa kujivuta sana kama mtu aliechoka, akaeiendea suruali ya mumewe iliyokuwa imetundikwa katika ‘Enga’ maalum kisha akaingiza mkono mfukoni na kuitoa simu, akaanza kurejea nayo pale kitandani huku akiiwasha na kumkabidhi Suhail ambaye alipokelewa na meseji nyingi sana utadhani ameizima kwa mwaka mzima.
Zilikuwa ni meseji kutoka kwa baadhi ya matajiri anaofanya nao kazi kwa karibu sana, pia akakutana na meseji za Vodacom zikimtaarifu juu ya namba zilizokuwa zikimpigia muda wote alipokuwa amezima simu yake, aliitegemea hali hiyo lakini kilichomshtua zaidi ni simu kutoka kwa Kilingo Mkude na Frank Mkali wasimamizi wa kampuni zake, walionekana kumpigia zaidi ya mara kumi kwa kila mmoja.. ndipo haraka akabofya namba za Mr Mkude na kumpigia
“Yes Boss,” Alipokea Mkude na kusikilizia kidogo
“Niambie Mkude”
“Shwari kaka, are you Okey?”
“Ooo yeah, vipi nimeona mmenitafuta sana!”
“Ndio kaka, si kawaida yako umetoweka ghafla tukajua umepatwa na matatizo maana tumeanda Mbezi haupo, Ilala nako haupo aisee tukachanganyikiwa kabisa ikabidi sasa tukaripoti Polisi tu,” Majibu yale hayakumfurahisha sana Suhail lakini kidogo ilimfariji kuona yuko na vijana wanaomjali sana hivyo hakuonesha tofauti yoyote, akauliza tena
“Aisee nilipatwa na udhuru usiokwepeka kaka, haya niambie”
“Kilichoniacha hoi sasa wakati tunaendelea kukutafuta ndipo nikapata wazo la kuperuzi kwenye ‘Diary’ yako ofisini nikaona namba imeandikwa Baba ikabidi haraka nimpigie il nijue kama uko huko!”
“Umempigia baba?!,” Suhail alihoji kwa mshtuko kidogo
“Ndio lakini kila napojitambulisha tukawa hatuelewani maana namwambia mimi ni mfanyakazi katika kampuni ya Suhail akawa anashangaa kusikia unamiliki kampuni, nilipomuambia kuwa tumekutafuta katika nyumba yako ya Mbezi na Ilala ndo kabisa akawa hanielewi lakini…” Kabla hajamaliza kuongea Suhail akamkatiza
“KILINGOOOOOO.. Umeharibu kila kitu kaka, kwanini umempigia mzee aaakh”
“Lakini kaka mimi nilipoo..” Kabla Mkude hajamaliza kuongea Suhail akakata simu halafua akafuatishia na tusi kali la nguoni mpaka Shekhia akaonesha mshtuko
“Vipi mume wangu, kuna nini tena?,” Aliuliza Shekhia huku hiyo ‘Mume wangu’ akiitamkia kwa puani kama mwanamke wa Kitanga, hakika Pumu imepata Mkohozi
“Yaani hawa wafanyakazi wangu wapumbavu sana, wamenipigia simu wakaona sipatikani, wakaenda kunitafuta kwangu waliponikosa tu wakaenda kutoa taarifa kituo cha polisi kisha kama haitoshi wamempigia simu baba..”
“Lakini mume wangu ujue siku tatu mfululizo si haba lazima wapate hofu”
“Hata kama , mimi si mtoto mdogo bana, sasa wameshiniletea taabu kwa Baba maana ameshajua kuwa ninamilikia Kampuni na nyumba kadhaa”
“Aaah we nae vipi! Mali umiliki wewe halafu umuogope baba yako?Kwa utoto gani ulio nao?”
“Hapana, unajua habari kama hizo ilipaswa nimwambie mimi mwenyewe na si..” hata hakulifikisha neno lake mwisho Simu yake ikawa inaita, Alikuwa ni Mzee Kusekwa, Tumbo lakimunguruma kwa hofu, akajikaza na kupokea
“Hallow”
“Suahil?!,” Alianza kwa kuita jina Mzee Kusekwa, ilikuwa ni sauti iliyjawa na hofu kubwa sana, kwakuwa Suhail alikuwa ameshajua kuwa Mzee wake alazima angekuwa katika hali hiyo baada ya kuwambiwa kuwa kijana wake ametoweka ghafla
“Una matatizo gani?”
“Niko salama tu baba, nilikuwa safari ya dharura Nairobi ndio nimerejea sasa hivi”
“Nairobi kufanya nini we Mtoto?Hivi Suhail kwanini unataka kunitia jaka moyo we mototo?”
“Baba kwani kuna nini?”Suhail alijifanya hajui kinachoendelea
“Yaani pilipili yangu mwenyewe inanitoa kamasi sasa, umekuwa haueleweki kabisa, jangili si jangili, gaidi si gaidi, au umejiingiza katika makundi mabaya we mtoto? Sasa nasema hivi mimi kama baba yako, Kesho naomba uwe Tabora Laa sivyo mimi sio Baba yako utamtafuta aliekuzaa, umenielewa?..” Mzee Kusekwa alikuwa akiongea mpaka povu lilifurumia mdomoni, alipoona hajajibiwa akahoji tena “..Umenielewa wewe?!”
“Ndio Baba. Lakini,” Suhail alijibu, na alipotaka kuongeza neno simu ikawa imeshakatwa, Akaishia kushusha pumzi kwa nguvu, Kimya kikatawala ndani ya Kasri la Bagamoyo.
“Vipi imekuwa?” Shekhia alivunja ukimya
“Jiandae tuondoke sasa hivi, maji yameshazidi unga”
“Hee jamani Twende wapi sasa?”
“Twende Dar es Salaam, inabidi kesho asubuhi niende Tabora baba anasema nisipoenda basi nitafute baba mwingine, hii sasa hatari”
“Uende Tabora au twende Tabora”
“Ukafanye nini?”
“Ukanitambulishe kwa wakwe zangu”
“Tafadhali usinikoroge kichwa, nadhani tulikwishaliongea hilo kuwa haliwezekani kutokana na hali ya nyumbani” Suhail alijitutumua na kujibu kiukali kidogo japo alijua kuwa nguvu za Shekhia hawezi kupambana nazo ila kwakuwa alijua kuwa anapendwa sana na jina mtu Yule hivyo aliitumia fursa hiyo ipasavyo, Shekhia akanywea, wakakubaliana na kuwanza maandalizi ya kurejea Bagamoyo na walikubaliana kufikia Mbezi ili isiwe rahisi kwa jamii inayomfahamu kumtilia shaka.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni