Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA TISA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Mbali ya umaarufu huo aliojizolea lakini pia Msigwa alikumbana na matatizo kadhaa ikiwemo kutishiwa na mara kadhaa kukoswakoswa kuuwawa na baadhi ya vigogo wa serikalini kwa tuhuma kadhaa alizowaandika, na wengine walidiriki kumfikisha mahakamani wakidai anawachafua lakini huko kwenye mikono ya Sheria aliwabwaga vibaya kutokana na ushahidi wa matukio ayaandikayo
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Hakika alikua na kipaji na mtandao mkubwa uliokua ukimpa habari nzitonzito za watu kibao, lakini hakujali kutishiwa aliendelea kutekeleza wajibu wake kwa umakini, umahiri, na Usiri mkubwa.
Umakini, Umahiri, na Usiri ndivyo hasa vigezo vya Suhail kwa mtu amtakae hivyo akalipigia mstari jibu lililopita kichwani mwake kua Msigwa ataumaliza mzozo, japo hawakua karibu sana kama zamani kutokana kila mmoja kubanwa na majukumu yake lakini walikua wakitembeleana mara moja moja na kutambulishana kwa wake zao na bahati nzuri au mbaya kila mmoja alikua ana mke tu na hawakua wamejaaliwa kupata watoto kila mmoja kwa sababu zake.
Akiwa katika gari yake aina ya ‘Land Cruiser’ akielekea kwa Msigwa maeneo ya magomeni alikua anaomba Mungu afike haraka ili afanye mazungumzo na rafiki yake huyo wa siku nyingi katika kulitafutia ufumbuzi tatizo lake na familia kwa ujumla. sasa alipofika maeneo ya Magomeni mapipa ikiwa si mbali sana na huko anapoelekea ndipo alipomuona mwanamke mmoja kupitia katika vioo ya pembeni vya gari yake akiwa amesimama sambamba na Abiria wengine waliokua kituoni hapo kusubiri daladala.
Alikua ni mwanamke ambae alihisi kumfahamu, lakini kumfahamu kwake tu haikua jambo kubwa bali hali aliyomuona nayo mwanamke Yule ilikua si ya kawaida sana kama alivyofikiri, akasogeza gari yake pembeni kabisa ya barabara kisha akashusha vioo vyeusi vya gari yake akachungulia nje ya gari ili amuhakiki mtu aliehisi kumfahamu, Hakika alikua ndie yeye lakini hakua sawa kabisa, alikua amevaa rafurafu tu huku akiwa na mabegi kama mawili hivi, pia alionekana kua kama anaelia hivi ikabidi haraka Suhail apaki gari Ashuke kwenye gari, akafunga vizuri milango pamoja na vioo kisha akaanza kurudi nyuma alipompita dada Yule
“Specyoza, mbona uko hivyo? Kuna usalama kweli?,” aliuliza Suhail kwa mshangao kutokana na hali aiyomuoa nayo mwanamke yule aliemfahamu vizuri kua ni mke wa rafiki yake kipenzi, Bwana Msigwa. Swali hilo la Suhail ni kama lililotumbua mfuko wa machozi ndani ya macho ya Specyoza maana sasa alishindwa kujizuia akawa analia waziwazi na kuruhusu mifereji ya machozi kutalii mashavuni mwake.
Hali hiyo ilimfanya Suhail ajisikie simanzi sana bila ya kujua tatizo la shemeji yake huyo japo kutokana na dalili zinazotafsiriwa na mabegi aliyoyabeba Specyoza ni dhahiri amegombana na Msigwa. sasa kutokana na mazingira yale ambayo hayakua mazuri kuongea jambo lolote kutokana na macho ya Abiria wengi kuwashambulia wao tu na kuwafanya kama vituko pale, ikabidi Suhail ambembeleze sana shemeji yake waondoke mahala pale wakaingie kwenye gari yake, Specyoza alikubali baada ya kubembelezwa kwa muda kidogo wakaondoka na kuifuta gari ilipokua imeegeshwa, Huku nyuma waliwaacha abiria wengi wakiwashangaa, wengine wakionekana kuguswa sana na hali ya mwanamke yule na wengine wakisikika kucheka na kurusha maneno ya kebehi.
Walipofika wakajitoma ndani ya gari kisha Suhail akaondoa gari taratibu bila ya kuongea chochote na Specyoza mpaka walipofika mbele kidogo ambapo wakaegesha gari pembeni mjadala ukaanza
“Haya kunani tena Shemeji yangu, imekuaje tena hivi?,” aliuliza Suhail huku akimgeukia Shemeji yake alieketi siti ya nyuma, lakini Specyoza alionekana kuzidiwa na hasira na uchungu maana kila alipojaribu kutaka kuongea ndivyo alivyozidi kulia kwa uchungu na sauti ya ‘kwikwi’, ikabidi Suhail ambembeleze sana ndipo akatulia kidogo na kuanza kuelezea mkasa uliomkumba
“..Rafiki yako kanifukuza, na kaniambia kuanzia leo mimi na yeye basi, hanitaki tena, wala hataki kuniona maishani mwake…” alishindwa kumalizia maneno yake akaanza kulia tena, akatoa kitambaa cha laini na kujifuta machozi kabla ya kuendelea kuongea “..Yaani Msigwa nimemsomesha chuo kwa pesa zangu mimi kipindi hicho nafanya kazi mgodini mpaka amemaliza chuo, akawa hana muelekeo wa kupata kazi na bahati mbaya kipindi hicho mimi nilikua nimeachishwa kazi huko Mgodini baada ya kuchukua pesa za ofisi ambazo nilimtumia yeye amalizie kulipa ada chuoni
Akaenda kwao Iringa na mimi nikaja Dar kwa Shangazi yangu ambapo baada ya muda nikapata kazi katika ofisi ya tiGo haikuchukua muda nikamchukua akaja hapa Dar nikawa naishi nae na kumuhudumia kwa kila kitu japo sikua tena na kipato kikubwa kama awali, Akaniambia kua tufunge Ndoa ilinikamkubalia bila kujali hakua na pesa wakati huo, tukafunga ndoa japo ndugu zangu walipinga kwakua hatukua tumejipanga kimaisha lakini mimi niliwapuuza.. Kaka yangu mimi akamtafutia hiyo kazi ambayo imempa pesa na umaarufu anaoutumia kuninyanyasa leo hii..” Kabla Specyoza hajaendelea kulalama ikabidi Suhail amkatize kwa kumtupia swali
“Pole sana Shemeji, Najua unaumia lakini tusifike huko mbali, Sasa kisa cha yote haya ni nini?”
“..Ni hadithi ndefu sana shemeji yangu, kama ujuavyo mimi na msigwa tangu tumefunga ndoa ni karibu mwaka wa pili sasa hatujabahatika kupata mtoto hivyo hilo limekua ni tatizo kubwa sana, Ndugu zake na Msigwa hasahasa dada zake wamekua hawataki hata kuniona na wanamshinikiza Msigwa aniache, mwanzo Msigwa alikua ana msimamo na alikua upande wangu katika kunitetea lakini sasa amebadilika na hali imekua mbaya zaidi maana nae sasa hanitaki waziwazi, kila kukicha ananizushia mambo ya ajabuajabu ili apate sababu ya kuniacha, nimezigundua njama zake muda sasa..” alisita kidogo, akatoa leso yake laini akajifuta machozi kisha akaendelea
“..Wiki iliyopita Msigwa alikua amepanga safari ya kuelekea Dodoma kikazi, ghafla name nikapokea taarifa kua kaka yetu mkubwa anaumwa huko kwake Morogoro hivyo ikanilazimu name kuondoka. Tukapanga kuondoka kwa pamoja siku ya jumamosi, na kweli ilipowadia siku hiyo tukapanda basi moja wote tukaondoka, Nilimbembeleza sana mume wangu tushuke wote hapo Morogoro ili nae akamuone Shejemeji yake lakini aligoma akidai kua anawahi jambo la muhimu sana huko Dodoma, sikua na pingamizi zaidi ya kumuacha aende tu nikamwambia kua kama hali haingelikua mbaya sana ningelirejea Dar kesho yake siku ya jumapili
Nilipofika Morogoro nikashuka na kumuacha yeye akiendelea na safari ya Dodoma, hapo Stand Morogoro nilipokelewa na watoto wa kaka yangu huyo ambae alikua mgonjwa, tukaondoka mpaka nyumbani ambapo nilikuta hali ya mgonjwa ikiwa si mbaya sana hivyo nikaendelea kukaa pale huku hali ya Mgonjwa ikiendelea kuimarika. Nilikaa pale Morogoro kwa siku kama tatu hivi ambazo ni hiyo Jumamosi niliyofika, Jumapili, na jumatatu, Kisha jumanne Nikarejea Dar lakini nilipofika nyumbani nikagundua kua simu yangu ambayo hua naweka line ya tiGo imepotea, nikaiangalia katika mifuko yangu yote bila mafanikio, ikabidi nimpigie simu kaka aniangalizie kule kama nimeiacha kwake, bahati nzuri akanijibu kua ameiona niliisahau juu ya Radio ya chumbani Nililaani kuisahau simu yangu lakini kumbe ilikua ni bora nilivyoisahau tu huo..”
Alishusha pumzi zake Specyoza au Specy kama ambavyo rafiki zake walivyopenda kumfupisha jina lake, kisha akaendelea “..Mpaka kufikia siku hiyo niliporejea Dar Msigwa hakua amerudi Dar hivyo nikawa peke yangu tu nyumbani, nilikua nikiwasiliana nae mara chache sana, haikunishangaza kwani hali ya maisha yetu sasa yalikua ni ya aina hiyo mpya ya kisirani muda wote, kutokana na ukimya wake huo sikuona haja ya kumfahamisha kuhusu simu niliyoisahau kule Morogoro kwa kua nilijua hua hanipigii mara kwa mara katika namba ile japo anaifahamu na anayo kwenye simu yake.
Hiyo namba ya tiGo nilipewa ofisini hivyo huitumia mara kwa mara kuwasiliana na wafanyakazi wenzangu wa kule kazini kwangu, hata hivyo nikajua endapo angepiga katika namba ile angekuta haipatikani kwani nilipowasiliana na kaka nilimwambia aizime tu ili asipatwe na bughudha ya kupokea simu. Sasa jana Ijumaa kaka alinitumia simu yangu kwenye Basi hivyo kwenye majira ya saa kumi alaasiri nikaenda ubungo kuichukua, nikaipata na kurejea nyumbani nilipofika nikakuta Msigwa nae ndo amerejea kutokea Dodoma, nikamsogelea pale katika kochi alipokua ameketi ili nimpokee ghafla nikashangaa napokelewa kwa kipigo cha mbwa mwizi. alinipiga makofi, ngumi, mateke, nk.
Nikamuuliza nimemkosea kitu gani mpaka ananipiga kiasi kile? Hakunijibu kitu akauchukua mkoba wangu akamwaga chini vitu vyote kisha akaichukua ile simu yangu ya tiGo niliyotoka kuichukua stendi. Simu ilikua imezimwa kwakua sikukumbuka kuiwasha tangu nilivyoipokea, akaiwasha yeye na kuiwekea ‘Security code’ punde ikawaka na zikaingia meseji kama nne hivi, alionesha kushtuka kidogo kama vile hakutegemea kuona zile meseji zikiingia muda ule, akazisoma kisha hapohapo akanirukia na kuanza kunipiga huku akinitukana kua mimi ni Malaya na hanitaki tena, akaniambia kwamba alipokua safari alipigwa simu na rafiki yake siku ya Jumatano
Saa sita mchana kua nimeonekana naingia Guest na kijana mmoja ambae ninafanya nae kazi pale tiGo anaitwa Msonjo, nilishangaa sana na sikutegemea kusikia habari hizo, huyo Msonjo ni kijana mmoja ambae hua ninaheshimiananae sana pale ofisini sasa leo naambiwa amkua bwana wangu tena Sikuamini, akanionesha hizo meseji zilizokua katika simu yangu ya tigo hapo sasa ndo nikachoka kabisa, zilikua ni meseji za kweli zikionesha Msonjo na mimi tunawasiliana mambo ya mapenzi
Ailishangaa zaidi nikamwambia Msigwa kua hicho kitu sikufanya na ninakishangaa hasa kwani hizo meseji zinaonesha nilikua nikiwasiliana na huyo Msonjo siku ya Jumanne ili kesho yake tukutane Guest sikuziandika mimi, na hata simu yangu haikua hewani tangu siku hiyo ya jumanne mpaka hiyo jana siku ya ijumaa, nikamuelezea jinsi nilivyoisahau hiyo simu kwa Kaka na mpaka alipoizima, Cha ajabu alionesha kushtuka aliposikia maneno yangu hayo mpaka mimi nikamshangaa lakini ghafla akaendelea kunipiga huku akinishutumu..
Mwisho akaniambia nifunge kila kitu changu niondoke Laa sivyo ataniua, Hakika nilichanganyikiwa sana nikampigia simu kaka huku nalia na kumueleza mkasa mzima ulivyokua, hata yeye alishangaa sana akaniambia kutakua kuna jambo tu hapo limejificha, hakuamini nilichomwambia kwakua simu inayonasibishwa na tukio hilo alikua nayo yeye.
akampigia simu Msigwa wakaongea kidogo tu lakini hawakuelewana ghafla wakaanza kujibizana vibaya na kutoleana maneno machafu
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi