Vita vya Mapenzi (3)

0

SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
Alikwishai chelewa habari ile, akajaribu kushika ‘remote’ na kubadili ‘channel’ kadhaa kama angeweza kuiona habari hiyo lakini haikuwa hivyo ikabidi tu sasa mama Yule ajikaze ili apate nguvu ya kumbembeleza binti yake

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
“Sikia mwanangu wewe ni msichana msomi na muelewa sana sasa kwanini unapenda kuongozwa na hisia? Wakati mwingine hisia hua si uhalisia wa jambo, huwezijua mwenzio yupo katika hali gani kwa sasa, cha msingi ni kuzidi kumuomba bawana Mungu wetu amuokoe”

“Lakini mama Maiti ni nyingi sana na majeruhi ni wachache lakini Suhail hayumo kabisa katika majeruhi hao waliokuwa wakihojiwa, itakua amefariki tu mama,” Sharifa alijibu huku akiendelea kulia kwa uchungu

“Hebu nyamaza kwanza ili tuelewanae, kutokuhojiwa kwake haimaanishi ndio amekufa na inawezekana waliohojiwa si wote na ndio maana hata katika maiti zilizooneshwa yeye hujamuona, lakini Je umeshampigia simu kujua kama atapokea au Laa?” Sharifa hakujibu swali la mama yake harakaharaka akaikimbilia simu yake iliyokua juu ya meza ndogo ya kunyooshea nguo, akaichukua na haraka akaipiga namba ya Suhail lakini simu iliita bila kupokelewa, alijaribu kupiga takribani mara tatu lakini simu iliita tu huku majibu yakiwa ni yaleyale, sasa hofu ndio ikazidi kupiga kambi moyoni mwake. Ikabidi sasa mama Sharifa nae achukue simu yake ili ampigie mumewe Mzee Fungameza ampashe habari hizo.

Simu ya Mzee Fungameza iliita kwa muda mrefu sana na hatimaye mwishoni ndipo akapokea

“Hallow.”

“Baba Sharifa uko wapi?,” aliuliza mama sharifa bila hata ya kusalimia

“Niko njiani naelekea kwa Bwana Kusekwa nina shida nae kidogo, vipi kwani?” Mzee Fungameza hakutaka kumueleza mkewe kua anaenda kwa Mzee Kusekwa kufuatilia habari za ajali hiyo ambazo tayari zimeshazagaa maeneo kadhaa ya mji, na imetapakaa habari kua Suhail amefariki katika ajali hiyo, alichelea kumueleza mkewe akihofia habari kumfikia Binti yake kwa wakati huo

“Una shida nae gani au ndo hiyo habari ya ajali?” Swali hilo likazidi kummaliza nguvu mzee Fungameza akajua sasa mambo yako wazi, akakaa kimya kama sekunde kadhaa kisha akajibu

“Ndio, lakini alaala jitahidi sana Sharifa asijue habari hizi kwa sasa, ni hatari”

“Ajue mara ngapi?”

“Khaa Kwanini umemuambia wewe??”

“Yeye ndo kaniambia mimi”

“Afanaaleki..hii sasa hatari..” Kikapita kimya cha muda mfupi kisha Mzee Fungameza akaendelea “..Nitakupigia baadae” kisha akakata simu

*****

Mtaa wa Rufita mkoani Tabora Nje ya nyumba ya Mzee Kusekwa ambaye ni baba yake mzazi na Suhail walikuwa wamejumuika majirani wawili watatu kwa ajili ya kumfariji jirani yao kutokana na habari hizo za ajali, ndipo punde Mzee Fungameza nae akawasili nyumbani hapo akiwa na Pikipiki yake ndogo, na baada ya kuipaki pembeni chini ya Mwembe ulio pembezoni mwa nyumba ya mzee kesekwa akaanza kujongea eneo walilokua wameketi akina Mzee Kusekwa na jirani zake

“Karibu bwana Fungameza..”

“Ahsante sana, habarini za hapa” Wakaitikia salamu wote kwa pamoja huku wakimkaribisha, baada ya kuketi hapakuwa na mazungumzo mengine zaidi ya Mzee Fungameza kuufungua mjadala

“Poleni na hekaheka jamani”

“Aah hatujapoa bwana mkubwa”

“Mimi nilikuwa huko maeneo ya Gongoni kwa bwana Kondela ndipo niliposikia habari hizi za ajali, na kwakua tayari nilikuwa nafahamu kua kijana nae alikuwa anakuja leo na basi ikabidi nifuatile ndipo nikaambiwa kua amepanda Basi hilohilo, aisee mwili wangu wote ukazizima kwa hofu”

“Ndio hivyo bwana, ajali ni mbaya sana na waliotoka ni wachache lakini cha ajabu kila tukifuatilia hatupati habari za uhakika maana hata simu yake haipokelewi”

“Mnh, kwahiyo mkipiga simu yake inaita tu?”

“Ndio inaita tu bila majibu yoyote” Baada ya majibizano hayo mafupi kila mmoja alionekana kuzama katika tafakuri ya kina kisha Mzee Fungameza akaibuka tena

“Hebu jaribu tena kumpigia inawezekana mazingira ya ajali yakawa yamembana sana hata ashindwe kujishughulisha na simu.” Kwa shingo upande Mzee Kusekwa akatoa simu yake na kuipiga tena namba ya Suhail, safari hii ikawa kama bahati hivi maana baada ya kuita kama mara tatu tu, kwani mara ya nne ikapokelewa, japo ni bora hata isingepokelewa tu maana hilo jibula mkato walilojibiwa liliwakata ‘maini’ kabisa

“Hallow, jamani tunaomba msubiri kwanza tunaendelea na uokoaji hatuwezi kuelewana kwa sasa” Maneno hayo yaliweza kusikika na kila mmoja aliyekuwa pale maana Mzee Kusekwa alikuwa ameweka ‘loud speaker’ katika simu yake. Majibu hayo yaliwamaliza nguvu wote, kila mmoja akaamini kua sasa inawezekana Suhail ameshapoteza maisha ndo maana hata simu yake inapokelewa na mtu mwingine, wote waliangaliana, hofu ikazidi. Majibu kutoka katika Simu hiyo sasa yakapelekea kufunguliwa mjadala mpya

“Mimi nashauri jamani tungeji pigapiga mifukoni ikiwezekana kesho Mzee Kusekwa na mtu mmoja waende huko Dodoma kuitambua miili..” alitoa rai Bwana Kituka, mmoja wa wale majirani waliokwenda kujumuika pamoja na Mzee Kusekwa, wazo lake likapita kwa asilimia zote na sasa ikabakia suala la pesa tu maana hali ya uchumi ya Mzee Kusekwa hakuna asieifahamu, ‘Dhooful-haal’

“Jamani mimi nakwenda kwangu mara moja nitarejea baade ila mimi ninajitolea kwenda na bwana Kusekwa mpaka huko Dodoma,” Alisema Mzee Fungameza huku akiinuka kwa ajili ya kuondoka, akamshika mkono Mzee Kusekwa na kutoka nae faragha kama vile anaehitaji kusindikizwa, walipofika pembeni Mzee Fungameza akatoa pesa takribani Tsh laki moja akamkabidhi mzee Kusekwa

“Hizi za nini Baba Sharifa?,” aliuliza Mzee Kusekwa

“Najua tayari tatizo lipo mbele yetu hivyo haipendezi sana kuchangiwachangiwa pesa na majirani labda mpaka itakapo bidi sana, sasa hizo ni pesa za nauli utakata Tiketi mbili za Basi ili kesho tuianze safari japo nao kama watakuchangia itakua ni ziada.”

“Nakushukuru sana Mzee mwenzangu, hakika umenifaa hasa, sina cha kukulipa ila Mungu anajua mbadala wa kukupatia”

“Usijali bwana Fungameza, hili letu sote, sasa tutawasiliana baadae” Wakaagana wazee wale marafiki, Mzee Fungameza akaondoka huku Mzee Kusekwa akirejea kwa wezee wenzie akiwa ‘mzito’ mfukoni

*****

Baada ya Suhail kuhangaika huku na kule ndani ya Basi akijaribu kupingana na ukweli kwamba Mzee Shamhurishi ameshakata roho, ghafla alipatwa na ujasiri akalifunga vizuri begi jekundu lenye pesa akalivaa mgongoni kisha akachukua begi lake dogo jeusi akalibeba mkononi na kuanza kutoka nje ya Basi.

Alipofika nje alikuta idadi ya watu ikizidi kuongezeka japo sio kubwa sana, wakati huo palikuwa na mitambo ya televisheni iliyofungwa huku wanahabari wachache waliowahi kufika eneo lile wakiendelea kuwahoji baadhi ya raia wema waliowahi kufika eneo la ajali. Wakati Suhail akiwa ameshasimama nje kuna akina mama kama wawili na vijana kama watatu hivi walionusurika kwenye ajali hiyo walikuwa wakimuangalia kwa mshangao tangu anashuka kwenye basi, wakamsogelea mpaka pale alipo

“Kaka vipi?,” alianza mama mmoja mnene hivi kuuliza swali

“Safi tu mama’angu,”

“Kumbe ulikuwemo ndani ya Basi muda wote?”

“Ndio, nyie wakati mnazitoa maiti nilikuwa nawaangalia tu lakini nilikuwa kama nilieishiwa nguvu sana, na hata sikujua nimeumia wapi mpaka sasa kwani wakati ajali inatokea mimi nilikuwa usingizini” wale abiria wakaangaliana kwa mshangao kisha mmoja akamtupia tena swali Suhail

“Mbona hatukukuona kabisa, na tulihakikisha hakuna aliebaki mule ndani?”

“Nadhani hamkuangalia kwa makini ila nilikuwepo humuhumo, mimi niliwaoneni”

“Mnh, yaani ndio wote tusikuone? Haya tuachane na hayo, mbona mizigo mkononi?,” Kijana mwingine alimuhoji suhail huku akimsontea kwenye lile begi lake dogo jeusi, Suhail alijua tu angekutana na maswali ya aina hiyo lakini akajikaza na kujitetea

“Jamani mimi inabidi tu niondoke maeneo haya haraka vinginevyo nitapatwa na matatizo makubwa” Abiria wale walizidi kumuangalia Suhail kwa tahadhari maana walimuona mtata sana kila nukta ilivyokua ikisonga mbele

“Hapana kaka, haupaswi kuondoka, tena ukiwa na begi hilo, kiusalama si kitu chema maana hatuwezi kuamini kama begi hilo na vilivyomo ni mali yako”

“Jamani iko hivi, mimi nilikuwa nawahi Dodoma kuripoti kazini ambako niliondoka tangu majuzi bila ya ruhusa maalum sasa kama nitagundulika nilikuwa safari na nimepata ajali hii nitafukuzwa kazi hivyo nawaombeni sana mnielewe ndugu zangu, sina nia mbaya” Suhail alijaribu kuwashawishi abiria wenzie wamuelewe, japo nao kiasi walikuwa wanashawishika lakini kiasi hawaamini ila baada majadiliano ya muda mrefu wakakubaliana kua wamkague Suhail katika hilo begi lake wajiridhishe kisha wamuache awahi kwenda kazini.

Suhail akawa anatetemeka akihofia pesa nyingi kama zile alizonazo katika Begi jekundu zitaonekana hakuna atakaeruhusu aondoke hivihivi lakini sasa cha ajabu kila abiria pale alikuwa akiliangalia Begi lile dogo jeusi tu, na hakuna hata mmoja aliejishughulisha kuangalia lile begi kubwa Jekundu lililokua mgongoni, Suhail nae aliligundua jambo hilo japo lilimpa faraja lakini lilizidi kumuacha na maswali mengi kichwani

‘Hawalioni hili begi au nini hasa?, kama wanaliona kwanini hawalitilii shaka! Na kama hawalioni je ni kwanini?’ Maswali mengi yalipita kichwani lakini hakupata majibu mpaka alipomaliza kukaguliwa katika begi lake jeusi na hatimaye akaruhusiwa na kuanza kuondoka eneo lile akiwa na mabegi yake yote mawili mpaka barabarani ambapo ilikuwa ni hatua ndefu kidogo tokea pale lilipokwama Basi lao.

Alipofika barabarani alikuta vijana wawili wakiwa wamepaki Bodaboda zao pembeni wakitaka nao kujongea kule lilipoangukia ajali lakini walipomuona Suhail akielekea usawa wao kila mmoja alianza kumuhoji kama angehitaji usafiri, Akamsogelea kijana mmoja akaongea nae na baada ya makubaliano alipanda kwenye Bodaboda yake na safari ya kuelekea Dodoma mjini ikaanza haraka.

Safari haikuwa ndefu sana kwa mwendo wa Pikipiki, takriban dakika 45 zilitosha kuwasili mjini na walipofika wakaenda mpaka katika moja maarufu lipo karibu na Stendi ya mabasi, Lilikuwa ni jingo la ghorofa na lenye nakshi ya na mapambo megine ua kuvutia, kwa juu ya Jengo hilo kuna bango kubwa liliosomeka ‘SEFLAVA LODGE’, baada ya kumalizana na dereva wake aliingia ndani kwa ajili ya kuchukua Chumba apumzike na kuweza kupanga sasa nini cha kufanya.

Naam akapokelewa na wahudumu mahiri waliokuwa tayari kupokea wageni. Baada ya kuandikishiana na wahudumu kwenye kitabu maalum cha kumbukumbu za wageni akapelekwa mpaka ghorofa ya pili, chumba No112 akakabidhiwa chumba na kuachwa hapo.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)