Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA AROBAINI NA TANO
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Nduguye huyo alipata kuniambia jina lake aliitwa Nadege Ndatabaye, kama ambavyo yeye aliitwa Amanda Ndatabaye.. tukiwa bado tuko katika jitihada za kumsaka huyo nduguye ndipo akapata ujauzito, ikamlazimu kusitisha kwanza biashara zake mpaka alipojifungua akiwa chini yangu kwa kila jambo, ndipo sasa alipoibuka huyu Suf..”
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Kabla Mzee Fungameza hajamaliza kuongea ikasikika sauti kali ya kilio, kilio cha uchungu na kutaabika.. alikuwa ni Mama Suhail akilia na kugaagaa sakafuni huku nguo zikimtoka maungoni, Mama Sharifa akajitahi kumzuia huku akimfunika nguo zake..
“Mama nini tena sasa?” Alihoji Ustadh Chaullah
“Inaniuma, inaniuma mie jamani! leo tumekumbwa na aibu ya mwaka.. sijui kwanini Mungu ameamua kutushushia mkasa huu..” aliongea huku akilia Mama Suhail, akaendelea “..Mimi ndiye Nadege Ndatabaye, na ni kweli nina pacha wangu aitwaye Amanda Ndatabaye niliyepotezana naye huko Rwanda tukiwa wadogo sana baada ya wazazi wetu kuuawa kikatili, na kupelekea mimi kuchukuliwa na mzee mmoja wa kitanzania na kuja kunilea huku wakati Amanda alibaki kule Rwanda akilelewa na Mwanakijiji mwenzetu wa kule..
Kadri tulivyokuwa tunakuwa kiUmri tukawa tunatumiana salamu kabla ya kupotezana kabisa kufuatia kifo cha huyu mzee aliyekuwa akinilea huku Tanzania, Mzee Yule ndiye alikuwa kiuanganishi chetu kama daraja kufuatia safari zake za mara kwa mara katika nchi hizi mbili..” Mama Suhail akaendelea kulia na kusaga meno huku akibwabwaja maneno “Kumbe masikini ndugu yangu alikuja kunitafuta, pengine angenipata ningemzuwia kujiingiza katika tama hizi” Ilikuwa ni habari mpya iliyozua mshikemshike mwingine, Kumbe Amanda ambaye ni Mama yao na Shekhia na Sharifa pia ni Pacha wa Mama Suhail, hivyo Suhail ni ndugu yao kabisa na akina Shekhia.. Mzee Kusekwa aliikumbuka historia hiyo kutoka kwa mkewe kwakuwa mara kadhaa wamekuwa wakijadiliana kuhusu utaratibu wa kumtafuta huyo Amanda
Hakika ilikuwa ni siku ya fadhaa!
Safari hii ilikuwa ngumu sana kunyamazisha kelele za vilio kutoka kwa akina mama hawa pamoja na watoto wao.. Shekhia naye akaanza kulia huku akimsogelea Sharifa na kumpigia magoti amsamehe kwa kila kilichotokea. Wakati hayo yakiendelea kuwachoma moyoni likazuka jingine jipya, Mzee Sufian aliyekuwa akipambana na roho yake, ilimshinda na kumponyoka, Akaaga dunia! kilio kikubwa kikaibuka kwa Shekhia, huku hofu ikiwavaa waliosalia.. ikawa sasa kila mmoja analia na lake! Ustadh akamwinua Suhail na kumuamuru afanye jambo, bila ajizi akainuka na kuliendea lile bakuli lenye yale maziwa yaliyowekewa Pete pale mwanzo, akalichukuwa na kuumwagia maziwa mwili wa hayati Sufian bin Shamhuri ambao ulikwisha tokwa roho, Mwili ule ukaanza kuyeyuka mithili ya ujiuji Fulani.. na baada ya muda ukakauka na kuwa jivu kama ilivyokuwa kwa Takadir Al-harab
“Hivyo ndivyo majini wanavyotoweka ama kufa, hatuwezi kuwazika kama tufanyianavyo sisi.. hivyo huo ndio mwisho wao.. hakuna maiti tutakayoendelea kuwa nayo humu ndani kisheria.. Poleni kwa yote yaliyowakuwa.. hivi ndivyo kadari ya Mungu ilivyotukia,” Aliongea na kuendelea “..Kila mmoja ameshajuwa kilichojiri kuanzia mwanzo mpaka sasa, huu ndio mwisho wa mkasa huu.. sasa ninyi kama wanafamilia ni jukumu lenu kukaa pamoja na kutafakari juu ya kadhia hii, hakika pana mafunzo makubwa sana kwa wenye kutafakari.. cha msingi machungu na dhoruba zilizotukumba kwenye mkasa huu zituimarishe na zisitubomoe, situfanye tuwe majasiri na wapambanaji wakubwa wa changamoto za namna hii katika jamii zetu…”
“Naomba niwaage wapendwa wangu,” Suhail alidakia wakati Ustadh Chaullah akiendelea na mazungumzo, familia nzima ikamsogelea kwa hofu na mashaka
“Majina ya mficho huwa ni mchezo mdogo sana na wa kipuuzi tu, na wa kisanii hivyo haihitaji akili nyingi sana kuufumbua japo umakini unahitajika.. kwa mfano, wapo ambao hutumia namba za idadi ya herufi za majina yao ili kuficha majina yao, wengine hutumia namba za kisanii ambazo husimama badala ya herufi na kuleta maana ya majina yao, na wapo ambao hutumia tarakimu za majina yao kinyumenyume nk.. sasa kwa hapo tutaziangalia hizi namba ambazo zitatusaidia kupata njia ya kutupelekea kuyajua majina husika kama si kuyafahamu moja kwa moja..”
Ukumbi mzima wa ofisi ulikuwa kimya kama kwamba hakuna watu, jasho ziliwafumka waheshimiwa licha ya kiyoyozi mwanana kilichokuwa kikiwapuliza, kijana akaendelea “..Nitaanza na huyu 5051-10s.. hiyo tano ya mwanzo ni namba ambayo kimuundo inaweza kufanana na herusi “S”, hiyo Sifuri nayo inafanana na herufi “O”, tano ya pili nayo ni kama ile “S” ya mwanzo, wakati hiyo moja inafanana na herufi “I”, hiyo kumi unaweza kuitamakwa kizungu ukaiita “TEN” Hivyo ukizijumlisha herufi hizo herufi zenye kufanana na hizo namba utapata kitu ‘SOSITEN’ na Ukiongeza na hiyo herufi ndogo ya “s” ambayo hutamkika “es” utapata kitu kama “SOSITENES” ambalo ni jina la mtu..” Ukumbi mzima ukamgeukia Mhe Sostenes Mitti(Waziri wa fedha) Hofu na mshawasha vikazizima, kisha kijana wa usalama akaendelea
“… nikija katika hilo jina mficho la pili ambalo ni 42&2c.. unaweza kucheza na namba na matamshi tu kisanii.. mfano hiyo “4” kwa kizungu inaitwa ‘four’ japo inatamkwa “FO”, hiyo mbili inaitwa ‘two’ japo inatamkika “TU” hiyo nane mkunjo ni alama inayomaanisha ‘And’ ambayo kwa Kiswahili hutamkwa “NA” Kisha inafuatiwa “2” ambayo hutamkwa “TU” halafu inakuja “c” ambayo kwa Kiswahili hutamkika “si” ukizijumlisha herufi hizo utapata kitu kama “FOTUNATUSI” Ukumbi mzima ukamgeukia Mhe Fortunatus Mwita ambaye moyo wake ulishindwa kuhimili mapigo yake na kujikuta akiishiwa nguvu na kuanguka chini akiwa amepoteza fahamu..
Wakiwa wamekumbwa na taharuki ile ndipo Mhe Sostenes Mitti aliona kuwa maji yameshazidi unga, liwalo na liwe! Akainama kama anaefunga kamba za viatu vyake na hapohapo akainuka akiwa na Bastola mkononi ikiwa tayari katika hali ya hatari ya kuruhusu risasi kuuingia mwili wa kaidi yeyote mle ofisini, akili ilikwishambadlika na kuwa kama ya mnyama, Ukumbi mzima ukazizima kwa hofu
“Mhe Mitti, unataka kufanya nini sasa? yaani pamoja na yote maovu mliyoyatenda kwenye taifa hili kupitia wadhfa mliopewa kwa kuaminiwa bado tena unataka kutuuwa?” Mhe Waziri mkuu aliongea kwa sauti isiyo na hofu wala woga
“Shut up, Niambie nani msafi humu kati yenu? kila mmoja ana yake aliyoyafanya kwa njia yake katika kujihakikishia anaulinda ugali wake.. Nani asiyetaka madaraka humu? na nani asiyetaka mali humu? Sasa nasema hivi atakayenisogelea hatua moja tu ataikuta roho yake ikimsubiri kuzimu mara baada ya kuufukia mzoga wake..”
Sauti ya Mhe Mitti ilikwishabadilika na kuwa kama ya mwuaji mkongwe. Wakiwa bado kila mmoja amesimama kivyake ndipo uliposikika mlio wa risasi iliyofyatuliwa, wote wakasambaa wakiruka huku na kule, Suti zikavurugika, vitambi vikawachomoza nje ya mashati yao yaliyochomoka.. Kimya kitandana! hapakuwa na sauti nyingine yeyote zaidi ya ile ya Mhe Mitti akilia kwa uchungu, kumbe ni yeye ndiye aiyepigwa ile risasi begani! na ghafla mpigaji wa risasi ile akaonekana akiteremka kutoa juu ya Paa la ofisi hiyo, Alikuwa ni Mwanadada Lillian Ufoo!
Haraka Mhe Sostenes Mitti na Fortunatus Mwita wakafungwa pingu, na katika hali ya kushangaza Mkurugenzi wa usalama wa taifa akaamuru na Kamanda Katinda Kuya naye afungwe Pingu, ndipo sasa zikachukuliwa Laptop zao na kuanza kufunguliwa, haikuwa rahisi kuzifungua kwa jinsi zilivyofungwa kwa namba za siri nyingi lakini hapakuwa na mchezo ambao ungemsumbua Ufoo, alitulia kama dakika mbili tu na kuweka wazi kila kitu, Taarifa zote za kiharamia zikitaja majina ya washiri, kazi na sehemu wanazofanyia mambo yao zilionekana..
Wakati huo IGP alipokea taarifa kutoka kwa Inspekta Kenjah kuwa tayari wamefanikiwa kuvamia lile jengo la Black Scopion kule Gongo la mboto ambapo wameupata mtambo wa Divier pamoja na watumishi kadhaa, Pia wameshawakamata maofisa wao akiwemo Chanzi na Rwehumbiza
****
“…Nimeumia sana na nimeteseka sana, siwezi tena kuendelea kuishi, inaniuma sana lakini sina budi kufa kwa amani… kabati kwangu kuna nyaraka za muhimu sana nilizoandika kuhusiana na mirathi.. mali zangu zote zikiwemo pesa na makampuni yangu mvigawanye kama nilivyoandika mwenyewe, wala msiviogope kwani kuanzia kesho hapatakuwa tena na himaya iitwayo budha kwani watateketea na kuangamia kwa kuiokosa Pete hii, Pete hii itayeyuka na kusambaa kabisa isibakie hata chembe muda utakapofika hiyo kesho wakati huo himaya ya budha nayo yote itakuwa ikiteketea na kupotea kabisa..
Naomba muishi na Shekhia kwa amani na upendo, msimtenge wa kumnyanyapaa.. huyo si jini kamili bali ana asili hiyo tu hivyo hana madhara yoyote…” Suhail alikuwa akiongea kwa unyonge kiasi cha kuwafanya sasa mpaka wanaume nao kutokwa machozi “..Mungu akijaalia Shekhia na Sharifa mkajifungua naomba kama watoto watakuwa wa kiume basi mmoja aitwe Noordin ikiwa na maana ya Mwanga wa ajabu na mwingine Aldin ikimaanisha Taa ya ajabu.. na kama watakuwa ni wa kike basi kila mmoja amchagulie jina lolote mtoto wake..” Kimya kikapita kila mmoja akimsikiliza Suhail ambaye alitulia kimya, alikuwa amemaliza kusema na amemaliza dakika yake ya mwisho kuwepo duniani,
Roho ikaachana na mwili, Suhail Kusekwa akafariki dunia
Kilipita kimya kama cha dakika tano, kila mmoja akiwa haamini anachokiona, ndipo sasa kilio kilipozizima mle ndani, hakuna aliyejizuia hata wanaume pia!, Sharifa alilia mpaka akapoteza fahamu, Mama Suhail naye alikuwa nusu mwehu kwa jinsi alivyo changanyikiwa. Majirani wakajaa ndani na kuanza pilikapilika za msiba mkubwa!
*****
Siku iliyofuata utaratibu wa kusafirisha maiti ya Suhail kuelekea Tabora ulifanyika na familia pamoja na jamaa wa karibu wakajumuika kwenda kumuhifadhi kipenzi chao, Suhail Kusekwa.
Ulikuwa ni msiba mkubwa uliokusanya mamia ya vijana na wazee, Msiba ambao mbali ya Simanzi na huzuni, pia uliacha funzo kubwa sana kwa jamii..
Hatimaye Suhail akazikwa katika makaburi ya Rufita, mkoani Tabora.
Upande wa mtandao wa Black Scopion nako mambo yaliwiva ambapo baada upelelezi kukamilika, Watuhumiwa wakafikishwa mahakani.. na hukumu kutolewa kila mmoja na yake.. Joram Ndege, Sostenes Mitti, Fortunatus Mwita na Ibrahim Basha bin Mende wakahukumiwa adhabu ya kifo kwani wao walishiriki katika mauaji kadhaa kikamilifu, waliosalia wote akiwemo Kamanda katinda Kuya, Chanzi, Rwehumbiza, na wale wafanyabiashara, pamoja na viongozi wote walioshiriki wakahukumiwa Vifungo vya maisha na kazi ngumu gerezani.
MWISHO
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi