Vita vya Mapenzi (5)

0

SEHEMU YA TANO
TULIPOISHIA...
Ilipotimu saa saba mchana, Suahil alikwishawasili Dar. Alikwenda moja kwa moja hadi Ilala Bungoni akiwa na mabegi yake. Alichukuwa chumba katika hoteli moja kubwa na ya kisasa. Hakuwa na tatizo na pesa za kumuwezesha kukaa katika hoteli ya hadhi hiyo. Alipoingia hotelini kwake, alijitahidi kujisahaulisha kadhia ya Mzee Shamhurish.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Baadaye, Suhail aliamua kwenda kuzihifadhi pesa zile benki. Kwa kuwa alikuwa na akaunti katika benki mbili za NBC na NMB, aliamua kuzitawanya pesa hizo katika akaunti zake zote. Pia, alibakiwa na kiasi kingine kikubwa cha pesa. Alianza kupanga mikakati ya miradi. Aliamini kwa kuanzisha miradi haraka itamsaidia kuzidhibiti pesa hizo kutopotea. Suhail alikuwa na elimu nzuri tu tena katika masuala ya fedha na biashara.

Waswahili wanasema pesa hupasua mwamba. Wiki moja baade Suhail alifanya mambo makubwa kuliko wengi waliomfahamu wangeweza kuamini. Alinunua nyumba kubwa za kisasa katika maeneo ya Mbezi na Ilala. Ndani aliweka kila kitu cha kifahari. Pia alikuwa katika hatua za mwisho za kufungua kampuni yake kubwa ya masuala ya Bima na nyingine ya upakiaji na upakuaji mizigo bandarini. Pesa ipo Elimu ipo Mungu ampe nini Suhail!! Tayari alikwishapata Ofisi za kukodi maeneo ya Kariakoo na Posta, na alishaanza kutafuta wafanyakazi wa kuwaajiri katika kampuni zake baadhi wakiwa ni marafiki zake aliosoma nao chuoni lakini ili kuficha siri ya pesa hizo wengi aliwadanganya kua kuna mzee mmoja tajiri sana kutoka Yemeni ndio amemkabidhi mali zake amsimamie.

Maisha yalikuwa matamu japo kila siku alikuwa akipata taabu kutokana na usumbufu anaopata kutoka kwa wazazi wake pamoja na mchumba wake huko Tabora, alikua akihitajika aende haraka japo akafanyiwe hata tambiko na dua za wazazi kutokana na kusalimika katika ajali.

Wiki moja tena mbele akiwa tayari ameshafungua kampuni zake na shughuli za utendaji zikiendelea sasa akawa anapanga tu kwenda nyumbani kwao Tabora ili pamoja na mambo mengine akabadilishe hali ya maisha ya familia yake. Suala lake la kumuoa Sharifa lilikua likipita kichwani mwake lakini kila alipokumbuka kauli ya marehemu Mzee Shamhurish kuwa amuoe binti yake aliishiwa nguvu kabisa.

Kila akikumbuka historia yake na Sharifa tangu walipokuwa shuleni alijihisi dhalimu mkubwa endapo hatotekeleza ndoto yao ya kufunga ndoa. Lakini Kila alipokumbuka kuhusu Shekhia hakika Jasho lilimtoka.

*****

JUMAPILI moja tulivu Suhail akiwa nyumbani kwake Mbezi amejilaza kitandani huku akiperuziperuzi katika kompyuta mpakato yake ndipo ghafla aliposhtushwa na sauti ya mtu aliyekuwa akimwita kutoka nje ya chumba hicho. Sauti hiyo ilikuwa ikitokea sebuleni. Aliingiwa na hofu kuitikia kwani mule ndani hakuwa akiishi na mtu yoyote zaidi ya mlinzi tu ambae naye yupo getini huko na asingeweza kuingia ndani kwa kuwa mlango ulikua umefungwa. Akabaki anajiuliza huyu mtu kaingiaje ndani tena huku akimuita kwa jina lake kabisa!.

Wakati akiwa katika tafakuri iliyogubikwa na hofu mara ghafla hali ya hewa ikabadilika, Chumba chote kikawa kinanukia utuli mzuri kwa kiwango cha juu sana, yaani kama ni ‘Perfume’ basi huyo mtu aliejipulizia inaonekana alimaliza chupa ya lita kumi. Ilikuwa ni harufu kali mpaka sasa akaanza kuhisi maumivu ya kichwa. Akiwa bado hajaelewa kinachoendelea mara ghafla akaona mlango wa chumbani kwake ukifunguliwa taratibu. Moyo wake ukapiga chogo chemba! Akatamani akimbie akaufunge mlango lakini alikuwa ameshachelewa. Aliinuka haraka na kuketi papohapo kitandani. Macho yake yaliganda mlangoni ili kumtazama mtu aliyekuwa akiufungua mlango huo.

Jambo la ajabu, mlango huo ulifunguka hadi mwisho. Hakuonekana mtu aliyekuwa akiufungua. Akiwa bado hajui cha kufanya ndipo ghafla akashtushwa tena na sauti kali ya mtu akicheka kwa nguvu nyuma ya kitanda alichokuwa ameketi. Akageuka haraka huku akiwa ametaharuki. Hakuamini alichokiona. Mapigo ya moyo yakabadilika. Akawa anahema juujuu mithili ya mtu aliyekimbizwa kwa muda mrefu.

Macho yake yalikuwa yakitazamana na Mzee wa makamo aliyekuwa amesimama huku ameegamia dirisha kubwa la mbao lililofunikwa na pazia ya rangi ya samli, alihisi kumtambua Mzee yule lakini kumbukumbu zilikataa kumjia, akatuliza macho yake kwa sekunde kadhaa ndipo sasa fikra zake zikasalimu amri, akamkumbuka Mzee yule aliekutana nae kwenye basi siku aliyopata ajali, alikuwa ni Mzee Shamhurish. Suhail akakurupuka pale kitandani kwa kasi japo akiwa hajui hata anataka kufanyaje, ndipo mzee Shamhurishi akamtuliza kwa sauti yake ileile

“Tulia Suhail, unataka kufanya nini sasa? Ulidhani nitaingilia mlangoni? Huwa hatwendi hivyo..”

“We ni nani na unafanya nini humu ndani?” Suhail alijikuta akiuliza swali la kipuuzi huku akitetemeka, japo alimkumbuka vema mzee Shamhurish ambae kwake yeye aliamini kua mzee yule ni marehemu lakini alijichetua akili kujifanya hajamfahamu. Mzee Shamhurish akacheka tena kabla hajaendelea kuongea kwa ile sauti yake ya utulivu.

“We ni mtu mzima Suhail haupaswi kujifanya punguwani, ina maana umenisahau mimi? Mimi ni Mzee Shamhurish, haya umeshanikumbuka?,”

“Hapana sijakukumbuka, Mzee Shamhurish ninayemkumbuka mimi alikwisha fariki katika ajali ya basi, sasa wewe ni Shamhurish yupi?.”

“Kumbe una kumbukumbu, sasa nisikilize mwanangu, zingatia sana maelekezo niliyokupa kule kwenye basi kuwa unapaswa kumuoa Shekhia haraka iwezekanavyo sitarajii kukuona ukiendelea kula raha tu kabla haujatekeleza agizo hili, fanya hima uende Bagamoyo unasubiriwa huko kwa ajili ya ndoa. Pili tafadhali ile pete niliyokupa usiwe unaivua na kuiacha mbali kwani ile ndiyo siri ya mafanikio na ulinzi wako wewe na mkeo mtarajiwa najua kwua tangu ulipoivua wakati unaoga bafuni hukuivaa tena na ukaitelekeza hukohuko.”

“Mzee mimi sitaweza kumuoa huyo binti yako, kwani nami nina mchumba tayari,”

Jibu hilo la Suhail likamfanya mzee yule mwenye asili ya Kiasia kua kama mbogo aliyejeruhiwa kwa jinsi alivyopandwa na ghadhabu. Mzee akamsogelea Suhail mpaka pale kitandani alipokua ameketi, akachukua bilauri ya juisi iliyokuwa juu ya meza ya kioo na kummwagia yote usoni na maeneo ya kifuani kisha kitendo bila kuchelewa Mzee Shamhurish akamzaba Suhail kibao cha uso. Maumivu makali yakamfanya Suhail apige kelele kali na ya uchungu

“Yalaaaaaaaaaaaaaa!”

Kelele hiyo ndiyo iliyomtoa usingizini na kumfanya agundue kumbe alikua anaota tu, akainuka haraka pale kitandani akatazama huku na kule huku akitweta kama labda angemuona Mzee Shamhurish lakini hakuona kitu, akashusha pumzi kidogo, akainamia tendegu la kitanda ili apate kutuliza munkari lakini ghafla mapigo yake ya moyo yakabadilika na kupanda juu tena, hakuamini alichokiona.

Alikuwa ametapakaa juisi usoni na mwilini hasa maeneo yale yale ya kifuani alipomwagiwa na mzee Shamhurish ndotoni, sasa akabaki anajiuliza kama ilikua ni ndoto tu sasa imekuaje tena ajikute amelowana juisi wakati hakua na juisi yoyote pale kitandani. Taharuki ikaongezeka, akaanza kuvuta picha ya maongezi yake na Mzee Shamhurish alipokua ndotoni. Akakumbuka kuhusu maelekezo aliyopewa kuhusu pete na wakati huo shavu lake la kulia likichonyota kwa maumivu ya kibao alichopigwa usingizini.

‘Yaani kofi nimepigwa usingizini lakini maumivu mpaka uraiani! Hii sasa kali’, akajiangalia kidoleni wakati anafikiria kichapo alichopokea kutoka kwa Mzee Shamhurish na kugundua kuwa ni kweli hakuwa na pete ile na akakumbuka kuwa aliiacha kweli bafuni kama alivyoambiwa na Mzee Shamhurish, ‘Hii ndoto ni ya aina gani? Huyu mzee atakua amenitokea kiukweli, sasa nimekwisha Suhail mie. Mawazo ya hofu yalizidi kutalii ndani ya kichwa chake. Akaondoka haraka mpaka bafuni akaikuta pete yake palepale alipoiacha, akaichukua na kurudi mpaka sebuleni. Akaketi juu ya sofa akijaribu kujituliza kidogo

‘Sasa ni muda wa kumtafuta Shekhia bila ya kujali ndie yule nimjuae mimi au ni Shekhia mwingine vinginevyo nitauawa bure.” Mawazo yaliendelea kutembea kichwani na baada ya mawazo mengi kichwani aliamua kuwa kesho yake atakwenda Bagamoyo kumtafuta Shekhia. Akiwa anamalizia kupitisha wazo lake hilo simu yake ya kiganjani ikaita. Akaingiza mkono katika mfuko wake wa suruali akaitoa, alipoangalia jina la mpigaji akamtambua, Mzee Kusekwa.

“Hallow, Shikamoo Baba,” Aliamkia Suhail baada kupokea simu.

“Hakuna cha Shikamoo hapa, hivi we mtoto huna wazazi? Au ulijizaa mwenyewe?”

“Kwanini Baba?”

“Kwanini Baba,” Mzee kusekwa nae alijibu kama alivyoulizwa japo yeye aliibana sauti na kuitolea puani kuonesha keji kwa mwanae kasha akaendelea “..We ni Mpumbavu wa akili ama? Unauliza swali gani hilo? Kwanini hautaki kuja kwenu wakati unajua fika kwamba kila mtu alikuwa akuusubiria ujio wako kutokana na ajali uliyoipata, sasa unatutukanisha sisi kwa majirani kwa ujinga wako”

“Lakini Baba..”

“Hakuna cha lakini hapa, sasa nasema hivi kama mimi ni baba yako..” Kabla Mzee Kusekwa hajamalizia kusema alichokuwa amekikusudia simu yake ikakatika na kumuacha Suhail akiwa amekumbwa na fadhaa kubwa sana, akawa ameishika simu yake asijue cha kufanya, alitamani kumpigia mzee wake lakini alihofia majibu ambayo angekutana nayo, akiwa bado hajai afanye nini, Simu yake ikaita tena, Suhail akashtuka tena, akavuta pumzi akitafuta cha kujibu lakini alipoiangalia simu yake hakua Baba yake tena, Safari hii alikua ni Mchumba waker, Sharifa Fungameza. Alijua tu hapakuwa na jingine zaidi ya lawama mpya, Aliishia kuitazama simu mpaka ilipokatika, akaimalizia kuizima kabisa ili asipate bughdha ikamuharibia safari yake ya kesho!

*****

Upepo mwanana uvumao kutokea usawa wa bahari uliendelea kuvuma karibu kila pembe ya mji wa Bagamoyo, mji wenye karibu kila aina ya vivutio vya kitalii, Mji huu kihistoria ulikaliwa sana kwa kiasi kikubwa na wegeni wa kiarabu ambao walifika pwani ya Afrika mashariki kwa minajili ya kuendesha Biashara ya utumwa hivyo mila nyingi na tamaduni za hapo Bagamoyo zilirandana kwa karibu na maisha yao kila siku katika wilaya hiyo iliyo katika mkoa wa Pwani.

Watu wengi kutoka katika mataifa tofautitofauti wakimemo Waarabu na Wazungu hufika mahala hapo kwa ajili ya kufanya utalii, wenyeji nao kutoka ndani ya Tanzania aghalabu hufika mahala hapo kufanya kile kiitwacho utalii wa ndani. Lakini hali ilikuwa tofauti kwa Suhail Kusekwa ambaye nae aliwasili siku hiyo katika mji huo wa kihistoria kwa ajili ya kazi moja tu, kazi ya hiari iliyo ya lazima, nayo ni kumtafuta Shekhia mtoto wa mzee Shamhurish, japokuwa hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika Bagamoyo lakini hakuwa na hamu hata kidogo ya kutalii kwani akili yake ilikuwa imeshavurugwa na ndoto ya ajabu aliyoiota jana yake, Ndoto yenye dalili zote za kuashiria ujumbe wa kweli uliomfikia.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)