Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA SABA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
DAKIKA zipatazo ishirini na tano kwa mwendo wa teksi zilitosha kabisa kuwafikisha Mlingotini lakini kutokana na Miundombinu ya barabara kua si nzuri sana hivyo ikawalazimu washukie barabara kuu na kuanza kuanza kutembea kwa miguu kuelekea nyumbani kwa Mzee Atrash ambapo hapakua mbali sana kutokea barabarani hapo, Ndani ya dakika tano wakawa wanatazamana na Nyumba ya ‘Msumbiji type’ mali ya Mzee Atrash.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Nyumba hiyo hiyo iliyojengeka kizamani ilipigwa ‘Lipu’ kwa upande wa mbele na kushoto, lakini upande wa kulia matofari ya kuchoma yalionekana waziwazi. Miti mirefu ya Minazi, Mitende, mipapai, Migomba, nk iliyoonekana kupandwa kiustadi kuzunguuka nyumba hiyo iliupendezesha muonekano wa eneo hilo huku kijani kibichi cha miti midogomidogo kama vile Mikomamanga, mipera, michungwa nk kikitawala mazingira hayo na kuyafanya yajenge taswira kua ni nyumba ya Mswahili pwani haswa!
Waliingia ndani ya nyumba hiyo Suhail na Mwenyeji wake mwenye Kilemba cha njano kwa kupitia mlango wa Mbele huku wakifuatana mmoja mbele na mwingine nyuma kama watoto wa Bata, ilikuwa ni Korido Ndefu iliyotenganisha vyumba vinne vya upande wa kulia na vitatu vya kushoto. Waliendelea kutembea katika korido ile ndefu wakielekea mwisho kabisa ambapo kabla ya Mlango wa kutokea uani palikuwa na ‘Seating Room’ upande wa kushoto iliyokua imepambwa vizuri tu kwa mitindo ya kisasa licha ya kwamba kwa nje nyumba ilionekana ni ya kizamani sana.
Walipofika hapo ‘Seating Room’ walipokelewa na akina mama wawili waliokuwa eneo hilo, Mmoja akiwa amekalia kibao cha mbuzi huku akiendelea kukuna nazi na mwingine akiwa ameketi katika zulia lililotandikwa chini akiwa anajipaka hina katika vidole vyake vya miguuni, Baada ya salamu Suhail akakaribishwa aketi juu ya Kochi na baada ya kuketi ndipo Sasa Dada mwenye Kilemba cha njano akaanza kutoa utambulisho mfupi kwa mgeni na wenyeji
“Kaka Suhail karibu sana nyumbani, jisikie huru,” aliongea kwa utulivu dada yule
“Ahsante sana nimeshakaribia.”
“Nikutambulishe sasa kidogo, huyo anaekuna nazi ni mama yangu mzazi, na huyo mwingine hapo ni mama yangu mdogo, wote ni watoto wa Mzee Atrash..”
“Ooh, nashukuru sana kuwafahamu,” alijibu Suhail kabla ya dada mwenye kilemba cha njano kuendelea kutoa utambulisho kwa upande wa pili
“Jamani huyu anaitwa Suhail, ametokea Dar es Salaam, ni mgeni wa Babu”
“Haya karibu mwaya, jisikie uko nyumbani,” alijibu Bi mkubwa aliyekuwa akikuna nazi kisha sauti nyingine ya yule aliyekuwa akipaka hina nayo ikasikika ikimkaribisha Suhail, hakika nyumba hii ilitawaliwa na ustaarabu na ucheshi wa hali ya juu.
“Ahsanteni sana Mama”
“Ila sasa ufanye Subra Mzee anaswali ndani akimaliza utaingia kumuona, leo tangu asubuhi yuko ‘busy’ na wageni tu, akitoka huyu anaingia yule”
“Haina tatizo mama, Nashukuru” Baada ya maelekezo hayo sasa Ikabidi Dada mwenye Kilemba cha njano aondoke zake ili awahi kwa msusi wake kule Bagamoyo mjini, na kwakua tayari alikwishapewa ujira wake na Suhail alipokuwa ndani ya gari hivyo hakuwa na la ziada, akaaga na kuondoka..
Baada ya dakika kama Kumi na tano hivi Suhail akiendelea kuwaza na kuwazua juu ya mambo yanayoendelea kumkumba, akakatizwa mawazo na Sauti kavu ya kukwaruza iliyotokea chumbani
“Kama kuna mgeni aingie” Sauti ile iliwafanya wale akina mama waliokuwa wakiendelea na shughuli zao wamgeukie Suhail kwa pamoja kisha yule anaekuna Nazi akamfanyia kwa ishara Suhail kua aingie ndani akaonane na Mzee Atrash, akainuka na kujongea taratibu akielekea katika chumba cha kwanza kabisa upande wa kulia ilipotokea sauti ile, Badala ya kufurahia kuonana na mtu atakae mpa Ukweli wa mambo asiyoyajua badala yake Mwili wa Suhail ulizizima kwa hofu na woga, vinyweleo vikajitutumia katika ngozi yake, ubaridi ukabarizi karibu kila kona ya maungo yake
Akabisha hodi na kukaribishwa, akaingia.. Kilikuwa ni chumba kikubwa tu kilichosheni makabati makubwa ya vitabu, na Makochi mawili ya sofa ambayo hayakuonekana vizuri rangi yake kutokana na hali ya giza iliyomo ndani mule iliyosababishwa na madirisha kufunikwa na mapazia makubwa kila pembe
“Karibu tafadhali bwana,” Sauti ile kavu kutoka kwa Mzee yule ilitoka kwa kukwaruza ikimkaribisha Suhail. Mzee yule aliyekuwa ameketi katika Mkeka mdogo alionekana kua na umri mkubwa sana, licha ya Mvi zilizoonekana kujaa kichwani mbali ya kua Kibaraghashia alichokuwa amekimaa kilizima nusu ya sehemu kichwa chake lakini hata maungo yake yalikuwa yamechakaa kwa uzee wake
“Ahsante sana Mzee wangu,” alijibu Suhail huku akiketi chini jirani na Mzee Yule
“Haya nini hali zenu nyumbani huko utokeako?”
“Aaah huko tunamshukuru Mungu hatujambo, sijui ninyi hapa”
“Nasi hatujambo kadri ya hali, Karibu..” Salamu zilijichukulia dakika kadhaa kabla ya Suhail kuanza kujielezea
“Mzee mimi natokea Dar es Salaam, naitwa Suhail nimekuja hapa kwa ajili ya kuhitaji kujua jambo moja kubwa,..”
“Naam, lipi hilo?.”
“Kuhusu watu wawili, Shekhia na Mzee Sufiani.”
“Unataka kujua nini kuhusu wao na kwanini unahitaji kujua?”
“Nataka kujua kuhusu maisha yao kwa ujumla, Kuna Biashara tunahitaji kufanya nao hivyo nimeambiwa niwafuatile kwanza niwajue ndipo mambo mengine yatafuata,” Aliongea Suhail kwa kudanganya ili apate kujua habari nyeti bila ya kumfanya Mzee huyo ashituke
“Hua siongelei habari za mtu hovyohovyo tu, wala hua sitoi habari nyeti kwa mtu asiekua makini, kwa mtu muongo, kwa mtu msaliti na kwa mtu mwenye tamaa..” Akakohoa kidogo Mzee Atrash lakini kabla hajaendelea akawahiwa na Suhail
“Sijakuelewa Mzee”
“Utanielewa tu, Athari za Mtu Muongo, Msaliti, na Mwenye tamaa huzijui?”
“Nazijua,” alijibu Suhail huku akiwa anamuangalia usoni Mzee yule ambaye yeye hakuwa akimuangalia kabisa zaidi ya kuendelea kukiinamia kitabu chake kama vile yale ayasemayo anayatoa katika kitabu kile
“Vizuri, sasa mtu wa aina hiyo hua hana muamana, Ila pamoja na hayo, acha nikusaidie.. Nitakusimulia ila hua natoza pesa nyingi kwa huduma nazotoa hapa..”
”Nitalipa tu Mzee, haina tatizo”
”Hapana, kwako wewe sitakutoza hata Senti tano, nitakuhudumia bure tu.. nina sababu ya kufanya hivyo” Akakohoa tena Mzee yule ambaye bila shaka kifua kilikuwa kikimsumbua, Sasa Suhail akaingia rasmi katika uwanja wa tafakuri za hofu
“Miaka takribani Ishirini na tisa iliyopita katika eneo hili la Mlingotini alitujia mgeni, namwita Mgeni kwakua hakuwa katika jamii yetu, akanunua nyumba kubwa eneo la mbele kidogo hapo, akaikarabati vizuri sana nyumba ile na akawa anaishi hapo. Taratibu tukaanza kuzoeana nae na tukaishi nae kwa Amani na ujirani mwema, japokuwa alikuwa ni mtu wa kusafiri mara kwa mara lakini mara chache alizorejea alitutembelea majirani zake kutujulia hali, hiyo haikuwa ajabu kwani huo ndio haswa utamaduni wa Waungwana wa Bagamoyo, Bwana yule mwenye asili ya asia alietambulika kwa Jina la Sufian au Mzee Sufiani kama ambavyo vijana wengi walivyomwita kwa heshima.
Ilisemekana ni mfanya biashara mkubwa wa Mafuta na Madini na kwamba huzungukia mikoa na nchi kadhaa kwa ajili ya kutekeleza biashara zake hizo. Lakini katika kipindi chote alichokuwa akiishi ndani ya jengo lake hilo hatukuwahi kumjua mke wala mtoto wake zaidi ya vijana wawili wa kiarabu waliotambulika kama watumishi wake..” Mzee alisita kidogo kuendelea akakohoa kwa nguvu sana mpaka akawa kama anaeishiwa nguvu lakini baada ya sekunde kadhaa akatulia kidogo, akameza funda la mate, kisha akaendelea
“..Muda si muda ikafika siku moja bwana yule akaja na mwanamke mmoja hivi hakika alikuwa mzuri sana lakini hakuwa na asili ya asia kama yeye Sufiani, mwanamke yule alikuwa ni mweusi tu kama mimi na wewe kitu ambacho kiliwastaajabisha wengi pale Mzee Sufiani alipotutambulisha kua yule ni mkewe, si unajua tena hatukuzoea kuona wenzetu weupe wakioa kwetu sisi weusi, basi hatukua na jinsi zaidi ya kukubaliana nae tu.. hawakuja’aliwa na mtoto kwa wakati huo, waliishi wawili tu ndani ya jengo lao lilikuwa na uzio mkubwa sana na imara japo kwa sasa naona kama uzio wenyewe umeanza kupoteza mvuto wake, hawakua wakitembelewa na wageni mara kwa mara hivyo kuacha maswali kwa majirani wenzao kufuatia upweke wao huo..
Mwaka mmoja baadae wakajaaliwa kupata mtoto baada ya Bi mkubwa yule Kushika ujauzito ambao ulimsumbua sana kiasi cha kukaa nao tumbo kwa miezi kumi na tano badala ya tisa iliyozoeleka, ilikuwa ni gumzo mtaani hatimaye Mungu akaleta neema akajifungua mtoto wa kike waliemwita Shekhia Bint Sufian, Maisha yakaendelea..” Suhail alikuwa akiisikiliza kwa makini habari ile iliyoiteka akili yake na kuiacha na maswali ambayo alitegemea angeuliza mwishoni ili kukidhi adabu za mazungumzo, hakujua kua asingepata nafasi hiyo tena. Mzee Atrash akaendelea
“..Siku moja likatokea balaa la kile kimbunga kilichoibuka ghafla na kumsomba Bi mkubwa yule, kikampeleka juu na muda mfupi baadae kikamuachia na kumdondosha chini akiwa hana uhai, Japo majirani waliumizwa na kifo cha mwanamwama yule mzuri wa umbo na Sura lakini kwa wajuvi wa mambo tuliona ni sawa tu acha afe kidhalili kwakua alistahiki kifo hicho cha kinyama.. sina haja ya kuelezea hapo kwa kirefu kwakua Tayari Sauda kaishakueleza mlipokutana nae huko Bagamoyo mjini, kwa kifupi tu ni kwamba baada ya Sintofahamu ile kubwa tulizika bila ya Mzee Sufiani kuhudhuria, na kwakua Shekhia alikuwa mdogo sana na hapo nyumbani kwao hawakua na mtu mwingine hivyo iakabidi sasa achukuliwe na baadhi ya majirani mpaka baba yake aliporejea baadae sana..”
Maelezo ya Mzee Atrash yalizidi kumchanganya kichwa Suhail si tu kwa kusikia kua kifo kile kilimstahiki mama yake Shekhia bali pia alijiuliza Mzee huyu amejuaje kua amekwishaongea na yule dada mwenye Kilemba cha njano ambaye bila shaka ndie Sauda mwenyewe! wakati Sauda hakupata nafasi ya kuonana na Babu yake huyo tangu walipofika mpaka alipoondoka kurudi kule kwa Msusi!! Sasa alianza kupata picha ya kwanini Mzee yule alimpiga mafumbo kuhusu mambo ya ‘uongo’, aliamini kua mzee yule anajua vitu vingi sana.
Mzee Atrash alikiinamia tena kitabu chake na kuiperuzi mistari kadhaa kabla ya kuendelea kuongea kwa kuanza kutoa historia mpya iliyoonekana kama ni tofauti na mada iliyopo mezani
“Miaka kadhaa iliyopita Bi Mkubwa mmoja aliingia nchini Tanzania akitokea Rwanda, alikuwa akijihusisha na biashara za nguo hasa hasa vitenge hivyo uwepo wake wa mara kwa mara hapa Tanzania ukamfanya nae awe ni kama raia wa hapa, hakika alikuwa ni Mzuri wa Sura na Umbo, vitu vilivyowafanya wanaume wengi kumuhitajia. Katika harakati zake za Kazi akakutana na Bwana mmoja Mtanzania wakapendana na kuamua kuishi pamoja kama mume na mke japokuwa walikuwa na tofauti kubwa mbili, tofauti ya utaifa na Dini zao, Bwana yule alijiona ana bahati sana ya kumpata mwanamke yule aliyekuwa akiwasumbua wanaume wengi kwa uzuri wake, Wakawa wanaishi kama mume na mke huku wakipanga mipango itakayowawezesha kufunga ndoa.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi