Vita vya Mapenzi (8)

0

SEHEMU YA NANE
TULIPOISHIA...
Katika harakati zake za Kazi akakutana na Bwana mmoja Mtanzania wakapendana na kuamua kuishi pamoja kama mume na mke japokuwa walikuwa na tofauti kubwa mbili, tofauti ya utaifa na Dini zao, Bwana yule alijiona ana bahati sana ya kumpata mwanamke yule aliyekuwa akiwasumbua wanaume wengi kwa uzuri wake, Wakawa wanaishi kama mume na mke huku wakipanga mipango itakayowawezesha kufunga ndoa.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Siku ya Siku mwanamke yule akakutana na mwanaume mwingine aliemtaka kimapenzi, Mwanamke yule akakubali bila ya kujali tayari ana mtu wake na amekwisha panga nae kufunga ndoa, kilichomzuzua zaidi mwanamke yule mpaka akamkubali mwanaume yule mpya ni Pesa alizokuwa nazo mwanaume yule ambaye nae hakuwa mtanzania, alikuwa ni mwanaume mwenye asili ya ‘Weupe’. Hatimaye mwanamke yule akamkana na kumtenda vibaya mwanaume aliyekuwa tayari ameanza nae maisha kisha akakimbilia kwa tajiri huyu aliemuhadaa kwa kile alichokuwa nacho.

Vikaibuka vita vikubwa baina ya Wanaume wale wawil, ‘Vita vya Mapenzi’..

ilikuwa ni mpambano wa kumsaka nani mwamba zaidi, zilitumika hila na mbinu za kila aina lakini Kutokana na nguvu za ziada za mwanaume yule mweupe hatimaye aliishinda ile vita.. Mtanzania wa watu akasalimu amri, lakini kibaya zaidi Mwanamke yule alipomkimbia mwanaume wake wa mwanzo alimuacha na kitu kilichozidi kumpa simanzi na mawazo mwanaume yule..Japo kilikuwa ni kitu adhimu”

Mzee Atrash alisita kidogo kabla hajakitaja kitu hicho adhimu, mara akamtupia swali Suhail “..Umeshamjua huyo mwanamke na huyo Mwanaume?” Lilikuwa ni swali ambalo Mzee Atrash alijua vema kuwa Suhail asingekuwa na jibu ila alimuuliza ili kumzindua kutoka katika lindi la mawazo na hofu

“Hapana, sijawajua,” alijibu Suhail na kumfanya Mzee yule alievalia kanzu ya rangi ya Udhurungi aendelee kuongea

“Huyo mwanaume Mweupe ndie Mzee Sufiani, na huyo Mwanamke mfanya biashara kutoka Rwanda ni Mama Shekhia aliefariki kwa kusombwa na kimbunga.. Usaliti na Tamaa vikamponza mama yule..”

‘Usaliti na tamaa vilimponza vipi mama huyo? Kwani kifo chake kilisababishwa na Kimbunga au na Tamaa?’ Swali lilipita kichwani mwa Suhail, Kama vile Mzee Atrash aliyaona mawazo ya Suhail akaanza kutiririsha historia nyingine iliyoanza kuyaangunisha matukio yote na kumpa jibu Suhail, Jibu lililozidi kumnyima raha badala ya faraja

“Miaka ya nyuma kidogo palikuwa ni Himaya huko chini ya bahari zikiendesha utawala wao, Himaya moja kubwa sana ikiitwa Budha, himaya hiyo ilikuwa na utajiri na ulinzi mkali kuliko zote.. utawala wao ulikuwa ukiwaniwa kwa udi na uvumba kama iwavyo huku duniani kwetu ifikapo kipindi cha mchakato wa Uchaguzi, sasa ilipoanza kukaribia kipindi chao cha uchaguzi kila kikundi kikawa kinamuandaa Jini alieonekana kuwa na uwezo wa kuukwaa uongozi wa juu wa Himaya ya Budha, Sasa Kiongozi anaemaliza muda wake nae akawa anamuandaa jinni aliemtaka yeye ili aje amuachie madaraka hayo ili aje afiche maovu yote aliyokuwa akiyafanya kipindi cha utawala wake, wakati huo Wana Himaya wengine wa Budha Jini nao walikuwa wamemuandaa Jini mwingine aje ashike madaraka hayo, Jini huyo Aliitwa Sufian Ibn Shamhurish..”

Moyo wa Suhail ukapiga tikitaka ndani ya kifua chake, mapigo ya moyo yakaanza kukimbia mara dufu, licha ya hali ya upepo wa pwani uliotawala eneo la Mlingotini lakini Suhail alikuwa akifuka Jasho, hakutaka kuwamini anachokisikia kwamba Mzee Sufian ambaye ni Baba yake na Shekhia ndie Mzee Shamhurish aliyekutana nae kwenye basi na ukweli mgumu kuukubali ni kwamba ni Jini. Hamu ilimwisha, Hamaniko hilo ni dhahiri Mzee Atrash aliliona hivyo akakaa Kimya kidogo kabla ya kuendelea kuongea “..

Katika Himaya hiyo ya Budha Mzee Sufian Shamhurish alikuwa ni Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na Utajiri na alikishika kitengo hicho kwa umakini wa hali ya juu kiasi cha kufanya baadhi majini wenzie wamteue yeye ashike nafasi ya juu ya utawala huo.

Hapo sasa ikawa ni vita ya ushindani baina ya makundi mawili hasimu ikawa ni mshikemshike almanusura ya kuuwana, Katika hali hiyo ya kutafutana ndipo wanaompinga Bwana Sufian Wakaamua kumuundia kashfa kubwa itakayopelekea kumnyima sifa za kuwa mgombea wa nafasi hiyo ya juu kabisa katika Himaya yao, katika kumtafutia Kashfa wakawa wanafuatilia kama Bwana Sufian ameshawahi kupatwa na kashfa ya kujihusisha na Uzinzi, hawakubahatika kuipata kashfa hiyo kwa kuwa licha ya bwana Sufiani kuwa hajawahi kuoa lakini hajawahi kupatwa na tuhuma za uzinzi katika Himaya yao, Sasa katika kuendelea kumfuatilia ndipo wakagundua kuwa bwana Sufiani hua anakuja sana Duniani ndipo wakaanza kumfuatilia na kugundua kuwa alikuwa akijihusisha na Mwanamke mmoja ambaye amempora mwanaadamu kwa kutumia nguvu zake za kipesa.

Hapo sasa wakakusanya ushahidi wa kutosha, na kwa kuwa ni kinyume kabisa na Sheria zao kuwa na mahusiano ya kimapenzi na kiumbe kisicho cha jamii yao wakamtia hatiani, na wakajiridhisha kwamba hakuwa amemuoa mwanamke huyo hivyo akawa amepoteza sifa za kuwa Kiongozi wao. Bwana Sufiani hakukubali kushindwa kapambana kujisafisha kwa muda mrefu sana bila mafaniko, ndipo akaamua kutoroka na kundi la wafuasi wanaomuunga mkono, akatorokea Dunia na kuja kuishi Bagamoyo ambapo baada ya kununua nyumba yake akamleta mwanamke yule niliekutajia mwanzo na hatimaye Kumzaa Shekhia”

‘Kwahiyo Shekhia ni Jini Mtu?,’ alijiuliza Suhail, hakujibiwa chochote kwakuwa alijiuliza ndani ya fikra zake mwenyewe

“Majini katika himaya ya Budha wakaanza kufanya msako mkali wa kumtafuta Sufian, walimtafuta karibu kila kona bila ya mafanikio, lakini baadae wakagundu kuwa yuko Duniani ndipo wakamfuata, Kikubwa kilichowafanya wahangaike kumtafuta ni kwamba bwana Sufiani alitorokana kitu adhimu sana kwa mustakabali wa Himaya yao, kitu ambacho ni kama Roho ya himaya yao, kitu ambacho kinayabeba na kuyaongoza maisha ya Himaya yao kiulinzi na kiuchumi.

Kitu hicho kilikuwa ni Pete Kubwa isiyokuwa na Rangi, Iliitwa ‘Khatam Budha’ Pete hiyo alikuwa akiimiliki bwana Sufiani kwaku Kitengo cha Ulinzi na Fedha kilikuwa chini yake yeye hivyo akapata fursa ya kutokomea nayo duniani, sasa Wanahimaya wa Budha wakaingiwa na hofu kuwa hawana Ulinzi tena wala hawawezi kupata mali kubwakubwa za baharini na nchi kkwakuwa Zana yao hapo nayo tena ndipo msako ukabidi kupamba moto, lakini iliwapasa kuwa makini sana katika kumsaka kwakuwa walijua fika kuwa Pete ile ni Silaha, na kwa yeyote atakaingia vibaya kwa Sufian ataangamizwa.

Na kweli mara kwa mara walipokaribia kumtia nguvuni aliwagundua na kuwateketeza vibaya, akawapunguza kasi na idadi hivyo akawa anajiongeza tu makosa ya mauaji ya kwenda kujibu huko Budha kama atakamatwa..” Suhail alipigwa na mshtuko wa ajabu sana kusikia habari za Pete ile amabayo bila shaka nd’o hiyo aliyonayo mkononi, alipoiangalia akashangazwa kuona ina kito cha rangi nyeupe wakati alipokabidhiwa ilikuwa na kito cha Rangi ya Njano, akiwa bado anajiuliza maswali Mzee Atrash alianza tena kukohoa kwa nguvu baada ya kuwa muda mrefu ameongea bila tabu, akachukuwa maji kidogo ya kunywa, akapiga mafunda kadhaa, akapata nguvu mpya, akamuangalia Suhail alivyokuwa akijiangalia kidoleni alipoihifadhi Pete yake kabla ya kuendelea

“..Ndipo wale majini wakaona kwakuwa Bwana Sufian amempenda sana yule mwanamke wa kibanaadam hivyo wakaamua kumchanganya kwa kumuua mwanamke yule ili iwe rahisi kwao kumpata yeye, Na kweli wakatimiza lengo lao la kumuua mama yule Msaliti mwenye tamaa kisha wakaanza kumuwinda na Shekhia japo kwa Shekhia hawakuwa na lengo la kumuua kwakuwa Shekhia ni katika jamii yao, ni binti ya Jini mwenzao hivyo wakawa wanataka wamchukue ili wampeleke katika himaya yao ya Budha ili akikuwa aolewe hukohuko ili mwisho wa siku bwana Sufian atapatikana kiurahisi, haraka bwana Sufian akazigundua hila zao, akamuhamisha mwanae kutoka Bagamayo na kumpeleka Dar es Salaam ambako alikulia huko na kuendelea na masomo yake huko akiwa katika ulinzi wa hali ya juu.

Tatizo kubwa lililokuwa likimgharimu bwana Sufian Shamhurish mpaka akawa mara kwa mara anajulikana alipo hata kama atajificha wapi ni Nuru kali itokanayo na Pete ile, hakika ile Pete ilikuwa na Nuru kali sana kiasi kwamba popote atakapojificha ataonekana tu, Nuru ya majini ilikuwa ikizidiwa ukali na Nuru ya Pete hiyo hivyo miale ya Pete ile ilikuwa ikionekana japo kwa mbali na kusababisha awe ni kiumbe wa kuhamahama na kukimbiakimbia tu.

Ndipo sasa wazo likamjia kichwani kwamba Binaadam hua ana Nuru kali zaidi kuliko majini, na hata kuliko ile Pete hivyo ikawa ni lazima apate mwaadamu wa kumvisha pete ile kwakuwa akifanya hivyo itawafanya maadui zake wasiione tena Nuru ile na kumfanya yeye asijulikane alipo mpaka siku iatakapowadia yeye kurejea kule Budha kwenda kufanya mapinduzi makubwa nay a ghafla, lakini mwanadamu atakaekabidhiwa atakuwa akifanya kazi zote za kiulinzi na kiuchumi kwa maelekezo yake yeye...

Sifa za mwanaadamu huyo huyo atatakiwa kuwa mwanaume, mwenye Nidhamu, na awe na Nyota ya ‘Shamsi’, nyota yenye nuru ya jua. Kumpata mtu huyo ikawa ni kisanga kilichomhukuwa miaka kadhaa bila mafaniko.. Ndipo siku ya siku mwanae akampa taarifa kuwa amepata mchumba anependana nae kwa dhati ikabidi Mzee Sufiani ajiridhishe kwa kumfuatilia mchumba wa mwanae ndipo akamkuta kijana mmoja aliemvutia sana, alipomchunguza akagundua kuwa ana sifa za mwanadamu aliepaswa kuvishwa Pete ya ‘Khatam Budha’..na kwakuwa atakuwa ni mkwe hivyo atakuwa muadilifu na ataitumikia mamlaka yake kwa kila nukta”

“Mzee wangu NIMEKWISHA,” Sauti ya Suhail alimkatisha mzee Atrash aliekua akiendelea kuongea, ikabidi sasa Mzee Yule anyamaze kidogo kuacha maneno yake yamuingie Suhail, na alipoona sasa kijana ametulia kimya ndipo akaendelea

“..Pete hiyo inaweza kuleta utajiri mkubwa kama itaamrishwa kufanya hivyo, Pete hiyo inaweza kuleta maafa makubwa kwa maadui wa kijini na kibinaadamu kama itaamrishwa kufanya hivyo, na Pete hiyo ni ulinzi dhidi ya hila za kijini au kibinaadm kama itaamrishwa ikulinde.. Inahitajika elimu ndogo sana ya kuitawala na kuiamrisha Pete hiyo lakini taaluma ya matumiz sahihi ya Pete hiyo Mzee Sufian atamfundisha kijana aliemkabidhi ili aitumie vema kumlinda, japo najua kua hawezi kutoa taaluma zote za kiusalamia akihofia siku moja kugeukwa maana anawajua vema wanaadam..”

“Mzee yaani naona kama nachanganyikiwa kabisa, akili yangu kama haifanyi kazi sawasawa, naomba unisaidie Mzee.. lakini sasa mbona Mzee Shamhurish alifariki katika Basi?”

“Nikusaidie nini wakati ulisema unataka tu kufanya nao Biashara?, Shamhurish hakufariki kama unavyodhani wewe bali ilikua ni njia ya kuondokea huku Tanzania na kutokomea Yemen sasa Baada ya kumpata mtu wa kumpa pete yake tena mtu mwenye ni Mkwewe hivyo alipaswa aonekane hayupo tena katika Nchi hii kwa kufa au vinginevyo, hivyo hiyo ilikua ni kiini macho tu..”

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)