KIBWE NA SAFARI YA AJABU (2)

0
Mtunzi: Sango Kipozi

SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
“Kwa hakika ingawa mwana mteule aliteketezwa na moto kwa njama za wale viumbe waovu kwa nia ya kutuondolea matumaini yetu, lakini hivi tunavyozungumza umejitokeza uwezekano mkubwa wa kupata ufumbuzi utakaorejesha matumaini kwa wanahewa wote nchini Sabaa, na jamii nyingine duniani.”

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

ENDELEA...
Alitabiri mmoja kati ya wanajimu waliohudhuria, ambaye kwa maelezo yake hayo hakuwatosheleza raia waliokuwa na shauku ya kupata majawabu ya maswali waliyokuwa wakijiuliza. Malkia Sultana alimwangalia mzee yule kwa makini na kisha akamuuliza. “Unaonaje ukitufichulia kuwa ni matumaini gani hasa yatakayopatikana, ili kila mmoja wetu aondokane na wasiwasi alionao hivi sasa?” Malkia yule alihisi kuwa mnajimu kwa makusudi kabisa, hakupenda kufichua ukweli wa sababu za ule utabiri, ambazo aliamini kuwa zilikuwa ni nzuri tu, lakini hata hivyo bado alitaka ufafanuzi wa namna fulani, ili kurejesha imani kwa raia wake, na kuwaweka katika hali ya utulivu. Raia wote nao waliafiki hoja za Malkia wao na wote wakamkodolea macho mnajimu yule, wakisubiri jibu lake la kuridhisha, lakini kabla yule mnajimu hajafungua mdomo kusema lolote, kishindo kikubwa, mithili ya kile kitolewacho na gari moshi likichemka, kilirindima eneo lote lile.

“Aaaa! Aaach-ch-chuuuuu! Aaaa---aaaaach-ch-chuuuuu!”

Pale uwanjani vumbi lilitimka kama kimbunga!

Jamii yote iliyohudhuria mkusanyiko ule iligutuka na kuruka kutoka vitini mwao. Vitu vidogo vidogo vilivyokuwepo katika eneo la mkusanyiko ule kama vile mazulia, viti ambavyo havikukaliwa, makaratasi na vinginevyo, vilirushwarushwa na kutawanywa huku na kule.

Hamadi!

Kumbe ilikuwa ni chafya moja ya nguvu iliyotoka miongoni mwa raia waliohudhuria mkusanyiko ule. Kila mmoja alitaharuki na kugeukia upande kilipotokea kishindo kile, kushuhudia ni nini hasa kilichotokea.

“Hayaaa! Hayaaaa! Jamani! hebu tulieni kidogo! Tulieni jamani! Bila shaka baadhi yenu mnafahamu jinsi Mzee wa Busara anavyokuwa kila anapokuwa na mawazo mazito, kutokana na matatizo ya aina hii.” Alisema mmoja kati ya wazee waheshimiwa.

“Mara nyingi anapofanya hivi huwa na wazo muhimu la kuchangia! Kwa hiyo ni bora tutulie na tumsikilize kwa makini ndugu zangu!” Mwingine aliafikiana na yule mzee muheshimiwa wa kwanza.

Naam. Mzee wa Busara alikuwa amejirundika kama kifusi pembeni kabisa ya ule uwanja! Kwa haraka haraka mtu angeweza kudhani kuwa ni kilima kidogo kilichotokana na takataka nyingi! Mzee yule wa ajabu alianza kujigeuzageuza na kunyoosha nyoosha shingo yake ambayo awali haikuonekana. Alikuwa kama mnyama mwenye miguu minne na mkia mnene kama wa mamba, na ngozi yake ilikuwa na magamba kama ya samaki, lakini zaidi yalionekana kama ya mamba kwani yalikuwa mapana mno!

“Aaaa—ch---chu---!” Alianza tena Mzee wa Busara akiwapa wahaka mkubwa wote waliokuwa wakimwangalia. Alichukua nafasi ile na kuanza kuelezea jambo lake, wakati ambapo wote waliohudhuria walikuwa makini kabisa, wakidhani kuwa litatoka chafya jingine babu kubwa liwatimulie vumbi kama awali!

“Sisi---eh! Mhh-khuu! Sisi t-tun-nafahamu kuw wa y-yapo mat-tumaini ma-kubwa m-mbele-yetu! Tusub-iri tu---aaach-ch-mhhh!” Mzee wa busara alijitahidi kuzuia chafya yake, ili asiwavuruge raia waliokuwa wakimsikiliza.

“Tuv-vute s-subira, maa n-na s-si muda mr-refu t-tutapata maj-jibu yatakayo turudishia imani na matumaini, pamoja na nusura tuliyoitegge—m-eaaaaaaa----c-h---u….....!” alisema mzee yule wa busara huku akizuia chafya zake kwa taabu sana, akiwa pembeni mwa uwanja na huku shingo yake ndefu ikizunguka zunguka kwa madaha kama shingo ya twiga mtoto. Alimgeukia mtu mmoja mdogo sana ambaye kimo chake kilikuwa mithili ya kimo cha ngedere. Mtu yule aligubikwa na ndevu nyeupe tupu zenye urefu wa kama mita thelathini hivi, zilizoburuza hadi aridhini.

“Na matumaini hayo yatadhihirika itakapokamilika miaka mia moja kamili tangu nchi hii ilipovamiwa na kuteketezwa na majini wa bahari.” Kijitu kile kidogo kiliongezea taarifa katika maneno ya Mzee wa Busara. Awali kabla ya uvamizi wa nchi ya Sabaa, kijitu kile ndicho kilichotarajiwa kuwa mwalimu wa yule Mwana Mteule aliyeteketezwa na moto wa majini, katika siku ambayo raia wa Sabaa waliazimia kumkabidhi kwake.

“Kwa hiyo hakuna yeyote kati yenu atakayekuwa na ufafanuzi wa ufuatiliaji wa jambo litakaloturudishia matumaini yetu?” Alidadisi Malkia Sultana, akiwaangalia wazee wake waheshimiwa na watabiri wake wa mambo waliohudhuria. Mmoja kati ya wanajimu aliyekuwa amejiinamia kwa muda wote wa mkusanyiko ule alisema; “Kwa hakika hatuwezi kufafanua zaidi kwani tutakapofanya hivyo tutavunja mwiko, na hivyo kuweka ugumu zaidi katika upatikanaji wa ufumbuzi wa mambo yanayohusika. Ila, tunachoweza kusema ni kwamba maelekezo ya dalili za madhara yanayoikabili sayari yetu na jinsi ya kukabiliana nayo, yameandikwa katika moja ya vidani vya fedha vyenye umbile la kucha za Simba, kwenye mkufu unaoning’inia shingoni mwa sanamu la shaba la kichwa cha Simba, katika nchi ya milima minne myeusi ya maangamizi, kwenye uwanda wa jabali la kisiwa cha Baharia!”

Raia wote waliohudhuria waliduwaa!

Kwenye milima myeusi ya maangamizi? Ndio wapi huko?!

Ukimya mkubwa ulitawala uwanja ule wa mikutano, kila mmoja akitafakari kuhusu taarifa ile mpya ambayo kwa hakika iliwakatisha tamaa zaidi, kwani walihisi kuwa lile ndilo lililokuwa jukumu la Mwana mteule, ambaye walikwisha mpoteza!

***

Naam, Kibwe alimsikiliza Bunga kwa makini sana, akijaribu kuhusisha taarifa ile ya kidudu Bungan a yale na maneno yake ya awali, kwamba ‘alimsubiri yeye kwa kipindi cha miaka mia moja’. Hapo akasikia mikoromo ya kutisha nje ya lile pango walilokuwemo. Akakumbuka yale majitu ya ajabu aliyoyaona kule nje muda mchache uliopita.

Alizidi kuogopa.

“Yale…ni majitu gani kule nje?” Kibwe alimuuliza yule mzee wa ajabu, huku akioneshea na akichungulia nje ya lile pango kujaribu kuyaangalia majitu yale aliyoyaona awali. Kama hapo awali aliogopa, basi safari hii, aliogopa maradufu, kwani baada ya lile giza la vumbi nene kutoweka, aliweza kuyaona vizuri sana yale majitu ya ajabu! Miili yao mikubwa kama milima ilikuwa na vichwa vyenye mapembe vilivyofanana na vichwa vya ng’ombe! Halafu lo! Mikono na miguu yao ilikuwa na makucha marefu ya shaba!

Wakati akishangaa kwa kuhofu namna ile, aliyaona yale majitu yakipasua majabali na kuchimbua milima. Huku yakikenua meno yao makubwa ya shaba yaliyong’ara mno kwa mwanga wa jua, Kibwe aliyashuhudia yale majitu yakitafuna mawe bila kizuizi kama kwamba yalikuwa peremende! Miguu ilimwisha nguvu, na kumfanya kijana yule anyong’onyee taratibu na kurudi chini, akiwa dhofu-l-hali kwa hofu.

“Ama hakika leo ndio kifo changu! Hakuna uwezekano wa kunusurika hata kidogo hapa! Na kama ninaota, mbona siamki mpaka sasa? Laaa! Sijui nitanusurika vipi mimi!” Aliwaza kijana yule kwa hofu na wahaka. Alimwangalia Bunga aliyeonekana kuwa hana hofu hata chembe, na kwa sauti ya kutetemeka, akamuuliza kwa mara nyingine, “Aaa...eeeh…hivi…eeeh…. wale ni kina nani babu….? Wametoka wapi…..na kwa nini….wanafanya vile wanavyofanya?”

“Wale kijana ndio wala mawe. Kila mwaka kwa muda wa miaka mia moja sasa, watu hao wa ajabu wamekuwa wakitokea, wakisindikizwa na upepo mkali, vumbi, dhoruba na matetemeko ya majabali. Wakifika tu, huanza kuchimbua milima na mawe na kupasua majabali, ili kujipatia chakula chao. Watu hao wala mawe wataendelea kufanya hivyo hadi kuimaliza dunia yetu yote, wakisababisha uwazi wenye kina kirefu kisichokuwa na mwisho!” Bunga alimwambia, na Kibwe akaduwaa akiwa kinywa wazi. Bunga alizidi kumkatisha tamaa ya nusra pale alipomweleza kuwa hata yeye anahofu kwamba hatimae, hata ile sehemu ya ardhi kwenye lile pango alikokuwa anaishi kumsubiri, pia itatoweka pamoja naye, na kuacha uwazi kama sehemu nyingine katika eneo lile, ambao uliwapoteza viumbe wengine wengi kabla yake.

“Oooh! Haponi mtu hapa!” Kibwe alijisemea kwa sauti huku akijishika kichwa kwa kukata tamaa.

“Wewe pekee ndiye utakayesaidia kuzuia hali hii isiendelee na labda kuirudisha vile ilivyokuwa awali Kibwe, kwani wewe bado ni damu changa, hujaanza kufikia umri wa kukata tamaa.” Bunga alimwambia, na Kibwe akamshangaa. Hakujiona yeye akimuokoa yeyote kutokana na maangamizi ya ile mijitu inayokula mawe, lakini pia alishangaa kwani hakuona uhusiano baina ya kuiokoa dunia na ule uwazi ulioikabili. Vyote kwa vyote, hakuelewa ni vipi yeye angeweza kuzuia ile hali ya hatari isitokee, hasusan akizingatia kuwa waliohatarisha hali ile ya dunia walikuwa ni majitu makubwa mno kwa yeye kuyadhibiti!

Kama vile aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, Bunga aliendelea kumwelezea hatua zipi achukue, ili kuinusuru dunia.

“Wewe ndiye mteule mwenye jukumu hilo Kibwe, pamoja na mengine ya kuitahadharisha jamii na kuiokoa dunia na ukame, na uwazi ulioikabili. Hiyo ni pamoja na matatizo ya kiafya na vifo vya binaadamu na viumbe wengine, na pia kuinusuru dunia na uovu na uadui miongoni mwao, pamoja na kuwajengea imani na matumaini...”

“Khah! Mimi?”

“Wewe, Kibwe! Kwa hiyo, ili ufanikishe kazi hiyo, lazima ufanye safari ndefu na yenye mitihani mikubwa. Safari hiyo ndiyo itakupatia ufumbuzi wa jambo hilo. Kwa vyovyote vile, usikubali kabisa kukata tamaa kwa jambo lolote litakalotokea, kwani utakapokata tamaa, azma yako haitatimia.” Bunga alisisitiza, mara kwa mara akikunja uso wake uliokomaa na uliopambwa na zile ndevu zake nyingi za mvi.

“Lakini bado sijaelewa jinsi nitakavyotimiza azma hiyo babu! Na hiyo safari nitakayoifanya ni kuelekea wapi baada ya kutoka hapa?” Kibwe alihoji, yote yale yakiwa ni mazito kwake. Maelekezo ya Bunga kuhusu safari yake yalizidi kumtia hofu, kwani yalimdhihirishia kuwa hakika safari ile ingekuwa ngumu mno na isiyo ya kawaida.

“Mara baada ya kuondoka wale wala mawe, takriban nusu saa kuanzia sasa, utaelekea magharibi ya dunia hadi ufike mahali kunakokuchwa jua, katika makutano ya mbingu na ardhi, ambapo jua huonekana kama kwamba linazamia hapo. Kwenye ufukwe wa bahari utaona mtumbwi. Tumia mtumbwi ule kwa safari yako ya kuelekea kisiwa cha mazimwi, viumbe ambao nusu;yaani kuanzia kuanzia tumboni kwenda miguuni ni wanyama, na kuanzia tumboni kwenda kichwani ni wanadamu. Katika kisiwa hicho utakuta ngome moja imara, na ndani ya ngome hiyo, huishi hao mazimwi ambao hulinda upanga wa radi. Jitahidi uupate upanga huo ili ukusaidie katika mapambano ya kuzuia vitendo vitakavyozidi kueneza uwazi mkubwa katika dunia hii.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)