Mtunzi: Sango Kipozi
SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Katika kisiwa hicho utakuta ngome moja imara, na ndani ya ngome hiyo, huishi hao mazimwi ambao hulinda upanga wa radi. Jitahidi uupate upanga huo ili ukusaidie katika mapambano ya kuzuia vitendo vitakavyozidi kueneza uwazi mkubwa katika dunia hii.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
ENDELEA...
Utakapofanikiwa kuupata upanga wa radi na kuondoka katika kisiwa cha mazimwi salama salimini, utaelekea katika nchi ya Azarbajan iliyoko kaskazini ya mbali ya dunia, baina ya milima miwili mirefu sana. Ili kuupata upanga wa radi kwenye kisiwa cha mazimwi, lazima uwe mwangalifu mno, uhakikishe kuwa unaingia kwenye ngome yao wakati ukiwa na hakika kuwa wote wamelala usingizi kwani….”
“Sasa, nitahakikisha vipi kwamba mazimwi hao wamelala ili niweze kuingia kwenye hiyo ngome?” Kibwe alimkatisha kwa mshangao.
“Utakapo sikia kelele nyingi na zogo kutoka ndani ya ngome kama vile unazomewa na kundi kubwa la watu, hapo ndio utaanza kuingia ndani polepole, na utakapofika ngomeni, utawakuta mazimwi hao wamelala sesa; fo-fo-fo! Humo ngomeni utaona mnara wa dhahabu, na juu ya mnara huo wa kipekee, utauona upanga wa radi uliowekwa nje ya ala yake na unang’ara kama jua.” Bunga alitoa maelekezo yale yaliyomshangaza mno Kibwe, aliyestaajabu sana kusikia kuwa eti zinaposikika kelele nyingi za mazimwi, ndio ishara kuwa wamelala! Alijiuliza sana moyoni mwake kama mambo yote yale aliyokuwa akisikia yalikuwa katika ndoto, au kweli yalikuwa alivyokuwa akiyasikia!
Wakati Kibwe anahoji uhakika wa mambo mengi yaliyomtokea katika kipindi kifupipale kwenye ule mji wa wala mawe, alimsikia tena Bunga akisema; “Ingawa utafaulu kuwakimbia mazimwi wa ngomeni, hutaweza kuvuka mpaka wa nchi hiyo ili kuendelea na safari yako, kwani njiani utazuwiliwa na kiongozi wa mazimwi hao, zimwi ‘Nyalile’ mwenye jicho moja. Kwa bahati nzuri icho hilo moja la zimwi ‘Nyalile’ halioni vizuri. Na kama atajaribu kukuzuia usipite, lazima umuimbie wimbo mzuri utakaomvutia na kumlaghai, ili asiweze kujua kama wewe ni mwanaadamu!” Lo! Hapo Kibwe akazidi kuhofu, na kuzidi kumaizi kuwa kazi iliyokuwa mbele yake, kamwe haikuwa rahisi! Aliogopa sana kusikia maelezo ya Bunga, na akakosa imani kabisa ya kuendelea na jukumu lile la kuiokoa dunia isikumbwe na janga la uwazi ulioikabili, pamoja na majanga mengine.
Bunga alifahamu wahaka na taharuki ya Kibwe baada ya kumpa maelezo ya jinsi safari yake itakavyokuwa, hivyo akazidi kumpa moyo akiongea naye kwa upole, na kumuhakikishia kuwa hatapata tatizo lolote katika safari hiyo, kama atatumia busara na kufuata maelekezo yake. “Nimekuambia tokea mwanzo kuwa wewe ndiwe mteule wa jukumu hilo, kwa hiyo kabla hujaondoka kuelekea kwenye safari hii ya aina yake, nitakupa silaha mbalimbali, ambazo utazitumia kadiri inavyostahili.” Baada ya kusema hivyo, Bunga alijisogeza ndani ya pango lake na kutoa mfuko mmoja mkubwa wa gunia na kumkabidhi Kibwe. “Humu ndani kuna silaha nyingi utakazozitumia utapozihitaji……” Bunga alizitoa zile silaha moja baada ya nyingine, akielezea kazi zake taratibu na kwa makini, Kibwe alisikiliza maelezo hayo kwa umakini mkubwa. Bunga akamuuliza iwapo ameelewa maelekezo yote. Kibwe akaafiki kuwa ameelewa.
“Haya kijana, hebu fumba macho kidogo….” Hatimaye Bunga alimuamuru, na Kibwe akafanya alivyoambiwa. Wakati macho yake yakiwa yamefumba, alihisi mtikisiko na akasikia mvumo ulioambatana na mtikisiko ule mithili ya mtu aliyekuwa kwenye gari moshi. Naam, hapo ndipo ilipoanza safari ndefu na ya ajabu ya Kibwe. Alipofumbua macho kuelewa ni jambo gani lililokuwa likiendelea, alijikuta ufukweni, na mbele yake ulikuwepo mtumbwi!!
***
Kibwe aliendelea na safari ile kama alivyoelekezwa na Bunga. Kwa muda mrefu mno aliendesha mtumbwi alioukuta ufukweni, hadi akachoka sana na kuanza kusinzia kwa uchovu. Alipokaribia kile kisiwa cha mazimwi, Kibwe alianza kusikia sauti nyororo na nzuri zikiimba wimbo ulioburudisha kupita kiasi! Alipotupia macho mbele kabisa ya kisiwa, akawaona mabinti saba wazuri, waliovalia mavazi ya hariri yaliyometameta juani, na waliovutia kupita kiasi. Lakini zaidi ya uzuri wao, sauti zao ndizo zilizomvutia Kibwe zaidi. Alitega sikio na kusikiliza kwa makini. Lo! Sauti zilikuwa si za kawaida! Kibwe akazidi kusinzia kwa burudani ilepamoja na uchovu aliokuwa nao. Mara akakumbuka maneno ya Bunga!
“Karibu na kisiwa cha mazimwi, kuna mabinti saba laghai wenye sauti nyororo za kimazingaombwe. Ukizisikiliza sauti zao nzuri kwa mfululizo, lazima utawafuata walipo, na ukifika kule watakuwekea ulozi kwenye kinywaji chako na kukufanya usahau kabisa kutekeleza malengo yako!
“Kwa hiyo nitafanyaje kujinusuru na ulaghai wao?” Kibwe aliuliza
“Utachukua hii ‘nta’ na kuziba masikio yako ili usiweze kuzisikia sauti zao.”
Haa! Sijui kwa nini Kibwe alitaka kusahau jambo lile muhimu kabisa. Haraka akatoa ile ‘nta aliyowekewa kwenye mfuko wa gunia na kuyaziba barabara masikio yake, kisha akaendelea na safari yake kwa amani hadi alipofika kisiwa cha mazimwi.
Kibwe alianza kuangalia huku na huko akitafuta sehemu ya kivuli aweze kupumzika kabla ya kuanza kutekeleza ile kazi iliyompeleka kule. Alipata sehemu yenye mti wenye matawi marefu sana yaliyokuwa yakiburuza hadi chini, na hapo akaketi na kutumia yale matawi kwa kujificha, ili asionekane. Baada ya kunywa maji aliyowekewa na Bunga kwenye ule mfuko mkubwa wa gunia, Kibwe alipata lepe zuri la usingizi, kutokana na upepo mwanana uliopuliza sehemu ile. Alilala kwa muda mrefu akapumzika vya kutosha, ili apate nguvu ya kuanza kuelekea kwenye ngome ya mazimwi, kuchukua upanga wa radi, kama alivyoelekezwa na Bunga.
Baada ya mapumziko yake, Kibwe alianza ufuatiliaji wa kazi iliyompeleka kule. Alikumbuka maneno ya Bunga. “Itakubidi kwanza uende kwenye mlima ambao chini yake kuna shamba kubwa la ufuta.” Alifahamishwa kuwa sehemu ile ilikuwa karibu na makazi ya wale mazimwi hatari wafuasi wa Zimwi mkubwa aliyeitwa ‘Nyalile’ na ambao kwa pamoja, wakati fulani waliwateketeza wakazi wa kisiwa hicho kwa kuwatafuna. “Lazima upande mlima huo hadi kileleni, na huko utakuta jumba wanamoishi mazimwi hao, lililozungushiwa ngome madhubuti.” Aliambiwa kuwa lazima akachukue upanga wa radi unaotoa cheche za moto kila unapotumiwa, na kumpa ushindi yule anaye utumia. Aliambiwa kuwa ile ndiyo silaha pekee ambayo ingemsaidia kupambana na mitihani mikubwa iliyokuwa mbele yake, akiendelea na safari yake kuelekea matokeo ya jua, baina ya mashariki na magharibi.
Kibwe alipita kwenye shamba kubwa la ufuta na kuanza safari yake ngumu ya kupanda mlima akielekea kileleni kwenye jumba la mazimwi. Katika jitihada zake hizo, mara kwa mara kijana yule aliteleza na kuporomoka, lakini alizidi kuupanda mlima bila kuchoka wala kukata tamaa.
Mchana kutwa Kibwe aliendelea na safari ile ya kupanda mlima, na ilimchukua takriban siku mbili njiani akila matunda ya porini kujinusuru na njaa. Kila alipokutana na wanyama wakali kama simba, chui , faru, mbogo na wengine, Kibwe aliwakwepa kwa kujificha vichakani. Hadi kufikia saa kumi jioni siku ya tatu jua lilipoanza kuchwa, kijana yule aliona ngome ndefu mno, iliyosimama kwenye upeo wa macho yake katikati ya msitu! Taratibu, huku akiangalia huku na kule, Kibwe alisogea karibu na ngome ile. Alipokaribia zaidi alistushwa na kelele na zogo kutoka ndani ya ngome ile madhubuti! “Huyooooo! Anakuja kuchukua upanga wetu! Haraka mkamateni! Mfuateni mumlete haraka kabla hajaingia ndani! Hayaaa! Kamataaa! Chinjaaaa! Uwaaaa! Nyongaa!” La haulaa! Kibwe alianza kukimbia kwa hofu ya kukamatwa na kutafunwa na mazimwi wale hatari, na kusahau kabisa usia aliopewa na Bunga!
“Utakapo sikia kelele nyingi na zogo kutoka ndani ya ngome kama vile unazomewa na kundi kubwa la watu, hapo ndipo utaanza kuingia ndani polepole, na utakapofika ngomeni utawakuta mazimwi hao wamelala sesa, fo-fo-fo ! Kutakapokuwa kimya basi tahadhari sana, kwani mazimwi hao watakuwa wako macho!”
Hilo lilikuwa ni onyo la Bunga kwa Kibwe.
Haa! Ilikuwaje akasahau jambo jingine muhimu kama lile? Hamadi! Palepale alipokumbuka onyo lile na taarifa ya Bunga kuhusu maajabu ya wale mazimwi, Kibwe aligeuka na kupiga mbio kuelekea kule ngomeni. Alipofika langoni huku akipumua kwa kasi, Kibwe alichunguli ndani kwa uangalifu na umakini mkubwa kuona kama wale mazimwi walikuwa wamelala. Hakuona dalili ya mtu au kitu chochote katika upeo wa macho yake. Taratibu aliingia ndani akinyata polepole na alipoangalia mbele zaidi, akaona eneo kubwa la wazi lenye bustani nzuri ya maua. Aliambaa na ukuta, huku polepole akinyanyua mguu mmoja mmoja, akishikilia pumzi yake kwa hofu ya kusikika na madude yale hatari aliyoambiwa na Bunga. Mwisho kabisa wa eneo lile la wazi, Kibwe aliona lango jingine kubwa lenye mbao za marembo marembo. Alinyata taratibu na alipogundua kuwa lango lile lilikuwa wazi, alilisukuma na kuchungulia uwani. Hamadi! Kibwe hakuamini macho yake kwa kile alichokiona!
Macho ya kijana yule yalikutana na kundi zima la madude makubwa kupita kiasi yaliyokuwa nusu ni watu, yaani kutoka tumboni kwenda kichwani na nusu, katika sehemu ya tumboni kwenda miguuni walikuwa kama sokwe! Kundi lile la madude yale ya ajabu na ya kutisha, lililala sesa kwenye nyasi za eneo lile, na huku kelele zao za kuzomea zikiendelea! Wakati sauti zao zikimbabaisha Kibwe, miili yao ilimtisha sana kwani ilikuwa na manyoya marefu kupita kiasi yakiburuza hadi chini kama ufagio! Viumbe wale walikuwa na midomo iliyojaa meno yenye ukubwa mithili ya pembe za ndovu! “Lo….. ndiyo maana ilikuwa rahisi sana kwa madude haya kuwatafuna na kuwateketeza mara moja watu wa kisiwa chote hiki, kutokana na urefu na wingi wa meno yao makali!” Kibwe aliwaza, akiwa na woga na wahaka mkubwa usio mfano.
Haraka Kibwe alifuata yale maelekezo ya Bunga, akianza kuwatambuka taratibu wale mazimwi waliolala huku wakipiga kelele na kuzomea kama kwamba walikuwa macho, hali iliyomfanya Kibwe azidi kuhofu, kwani muda wote alihisi kuwa huenda ghafla wakamrukia na kumshambulia. Hiyo Ilikuwa ni kazi ngumu mno kwa kijana yule na muda wote wa zoezi lile, jasho lilikuwa likimtiririka na mara nyingine alihofu kuwa huenda jasho lile likawadondokea na kuwaamsha wale mazimwi, na huo ukawa ndio mwisho wake!
MAJANGA YA SAYARI
Wakati Kibwe akiwa katika jitihada za kutekeleza malengo yake ya kuinusuru jamii kule machweo ya jua katika kisiwa cha mazimwi, katika sehemu nyingine iliyo baina ya mashariki na magharibi mbali kabisa kutoka kisiwa kile cha mazimwi, katika milki ya Sultani Bashar, majini yalitawala sehemu kuu iliyowapatia maji raia wa nchi ya Shamsi mjini Majabali.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi