KIBWE NA SAFARI YA AJABU (4)

0
Mtunzi: Sango Kipozi

SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
Wakati Kibwe akiwa katika jitihada za kutekeleza malengo yake ya kuinusuru jamii kule machweo ya jua katika kisiwa cha mazimwi, katika sehemu nyingine iliyo baina ya mashariki na magharibi mbali kabisa kutoka kisiwa kile cha mazimwi, katika milki ya Sultani Bashar, majini yalitawala sehemu kuu iliyowapatia maji raia wa nchi ya Shamsi mjini Majabali.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

ENDELEA...
Jambo hilo lilisababisha shida kubwa ya maji na ukame uliathiri maeneo mengi ya nchi ile, iliyokosa chakula cha kutosha kwa watu wake. Ili kuwanusuru raia wake na shida ile ya maji, kila mwaka Sultani Bashar wa nchi ya Shamsi, alimtoa kafara binti yake kwa joka moja kubwa ambalo lilimchukua binti yule na kuzama naye kwenye mto Sakara ulioko kati ya majabali mawili na kumpeleka kwa jini ‘Makattani,’ mfalme wa majini yote. Mpaka kufikia wakati ule Kibwe alipokwenda kisiwa cha mazimwi, tayari Sultani Bashar wa nchini Shamsi alikwisha watoa kafara watoto wake sita, binti mmoja kila mwaka na kila mara akiwapatia raia wake mwaka mmoja wa kuchota maji kutoka mto Sakara. Hatimae Sultani yule alibaki na binti mmoja tu, Bhaduri binti sultani ambaye kwa bahati mbaya kwake, alitakiwa kumtoa kafara wiki mbili zilizofuata kwenye mto uleule Sakara, ili kuwapatia raia wake mwaka mmoja zaidi wa kutumia maji yake!

“Ama kweli hali hii ni ya kusikitisha na kusononesha mno,” Malkia wa Shamsi amlalamikia mumewe Mfalme Bashar, huku akilia bila kizuizi! “Haya ni maonezi makubwa na ni unyanyasaji wa aina yake, wa kuwalazimisha mabinti zetu wajitowe mhanga, eti kwa ajili ya kunusuru raia wako! Hili si jambo la kibinaadamu hata kidogo.” Malkia yule alisema kwa masikitiko makubwa. “Sasa mke wangu unadhani tungefanya nini kulitatua tatizo hili sugu linalotukabili kila mwaka?” Sultani Bashar alimuuliza mkewe kwa upole.” Hata mimi nina majonzi makubwa kuhusu mabinti zetu, lakini hii ndiyo njia pekee ya suluhu kwa jambo hili.”

Katika mji ule mkuu wa Majabali nchini Shamsi, baada ya Suitani kufanya maandalizi ya kumpeleka kitindamimba wake Bhaduri kule mtoni Sakara kwa ajili ya kafara, aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kujiinamia kwa fikira na majonzi ya kumpoteza binti yake mwengine! Ama kweli Sultani yule alikuwa mtawala wa aina yake! Eti kudiriki kuwatoa kafara mabinti zake saba! Si jambo la kawaida asilani!

Kule Azarbajan nako kwa Sultani Kash Kash kaskazini ya mbali ya dunia, ingawa chini kabisa ya bahari, i jini ‘Makatta’na wenzake walikuwa wakiandaa vichafuzi vya hewa safi iliyowasaidia watu kuishi, na kuigeuza hewa ile kuwa hatarishi, lakini Mfalme wa nchi ile hakutambua hivyo. Hakujua kama hewa ile iliyogeuka kuwa moshi mnene ilipoanza kuzizima na kisha kuwazingira watu katika himaya yake, ndipo walipogeuka kuwa mawe ya theluji! Kwa kuwa hawakuelewa chanzo hasa cha janga lile, watu wote wa kule waliingia hofu kubwa na Mfalme wao alikuwa akimtafuta mkombozi atakaye wanusuru raia wake kutokana na janga lile!

“La mgambo! La mgamboooo! Likilia lina jamboo! Asiye mwana a eleke jiwee!” Kijumbe wa Mfalme Kash Kash alipita mitaani akiwatangazia raia wa Azarbajan kama kawaida wakati inapotokea dharura ama ya raha, au ya karaha, akianza kwa kupiga goma lake kubwa alilolibeba kifuani, na lililofungwa kwa kamba iliyopita mabegani na kuzungukia makwapani.

Kwa kupiga ile ngoma kijumbe yule aliwavutia watu na kuwasogeza karibu, ili waende kumsikiliza. “Jamani eeeh! Kuhusu janga linalotukabili la raia wengi kugeuka mawe ya theluji, mpaka hivi sasa bado haujapatikana ufumbuzi wa tatizo hilo, na wala bado hajapatikana mkombozi atakaye saidia kunusuru maisha ya raia wa nchi hii. Hivi sasa wazee wa baraza la Mfalme, wako mbioni kutafuta njia ya haraka ya ufumbuzi wa tatizo hilo. Kwa hiyo yeyote atakaye kuwa na mawazo tafadhali asisite kujitokeza na kuchangia, ili kulipiga vita janga hili la kihistoria nchini kwetu…..! La mgambooooo! La mgambooooo! Likilia lina jamboooooo!” Kijumbe yule alihitimisha tangazo lake na kisha kuendelea katika maeneo mengine ya mji wao mkuu. Tangazo lile lilitangazwa mara kwa mara katika miji mbalimbali ya Azarbajan, lakini hakujitokeza mtu yeyote aliyeweza kutoa ushauri kuhusu utatuzi wa tatizo lile.

Katika ngome ya jumba la mazimwi kwenye kisiwa chao, Kibwe alitumia muda ule ambao mazimwi wale walikuwa wakipiga kelele, kwa kuendelea kuwatambuka mmoja mmoja, hadi alipofika kwenye ule mnara wa dhahabu. Pale alipumua kidogo kabla ya kuanza kupanda mnara huo ambao juu yake ulikuwepo upanga wa radi alioutaka. Kelele za mazimwi zilizidi kuliko awali, kama kwamba walihisi kuwa kuna mtu karibu ya hazina yao.

“Naomba Mungu majitu haya yasiamke ama sivyo sitanusurika asilani!” Kibwe aliwaza. Alikumbuka kuwa mara tu, kelele zitakapokoma, ndio utakuwa wakati wa hatari kubwa kwake! “Na kutakapokuwa kimya basi tahadhari kwani watakuwa wako macho!” Bunga alimwambia.

Ingawa aliogopa sana na kuhofu, lakini kijana yule shujaa alipanda juu ya ule mnara mrefu akafika kileleni, na kwa uangalifu akauchukua ule upanga na kuutia kwenye ala yake, na kisha akaupachika kiunoni kwake na kuanza kuteremka chini kwa uangalifu! Alipofika chini, akarudia lile zoezi la wasiwasi la kuyatambuka yale mazimwi yaliyolala! Lo! Kwa bahati mbaya, alipokuwa akimalizia zoezi hilo, alilikanyaga zimwi la mwisho lililolala karibu na lango kuu la kutoka ngomeni, na hivyo, lilipokuwa kimya tu, kwa ishara ya kuamka, na menzake yote yakawa kimya! Masikini wee! Mazimwi yote yakawa macho!

 Kabla hayajataharuki na kugundua kuwa alikuwepo mtu ngomeni mwao na amechomoka na kupenyeza getini wakati mmoja wao akiamka, Kibwe alipiga mbio kama mshale! Alikimbia kuelekea mpakani mwa nchi ile kama alivyoambiwa na Bunga, akiazimia kupita katika njia kati ya mashariki na magharibi!

Walipoangalia mnarani na kukuta upanga wa radi umetoweka, mazimwi wote walitaharuki na kuwa na hasira nyingi “Bila shaka alikuwepo mtu humu ngomeni. Afuatwe haraka kabla hajaondoka na upanga wetu!” Baada ya kusema hivyo, wote walitimua mbio, huku vumbi likitanda kwa heka heka hiyo, na baadhi ya miti ikikatika kwa vikumbo vyao! Alipoangalia nyuma, kibwe aliona vumbi lililotanda hadi mawinguni! “Leo ndio hatima yangu mimi! Sijui kwa nini nilifika huku!” Kibwe alisema kwa majuto. Mazimwi yalipoanza kumkaribia alihisi miguu yake ikiwa inalegea mno na kukosa nguvu kwa hofu! Moyo wake ulienda kwa kasi mno! Alikumbuka maneno ya Bunga. “Wakikaribia kukufikia, watupie kichupa kimoja kati ya vichupa hivi vidogo vya mazingaombwe, ili uwacheleweshe.” Kibwe haraka alitoa kichupa kimoja na kukitupia nyuma yake kwa yale mazimwi. Lo! Mara ukatokea msitu mnene kupita kiasi. Mazimwi yalianza kuhangaika kukata miti ya msitu ule uliozuka! Kutokana na ukubwa wao, muda si mrefu yalifaulu kukanyaga kanyaga miti midogo na kuipiga vikumbo miti mikubwa, na kisha kuendelea kumkimbiza Kibwe, ambaye alipoona hivyo, alirusha kichupa cha pili, na mara zikazuka mbigili nyingi mno nyuma yake! Mazimwi yaliumiaumia miguu yao, na wengi wakaachwa nyuma. Kibwe aliyaona baadhi ya mazimwi yakizidi kumfuata, huku yeye akiwa amechoka mno kukimbia. Alipatwa na wasiwasi mkubwa, “Sasa nikishindwa kukimbia na madude hayo yanazidi kunifuata, itakuwaje?” alijiuliza huku akipapasa papasa kwenye fuko lake, kutoa kichupa kingine miongoni mwa vichupa alivyopewa na Bunga.

“Kwa kuwa mazimwi hupenda sana kula ufuta, utakapo watupia kichupa cha ufuta, wote wataketi chini na kuanza kula, na hivyo utapata nafasi ya kuwakimbia.” Kibwe alikumbuka maneno hayo ya Bunga! Mara moja akarusha kichupa cha ufuta, na hapohapo ukazuka mlima mkubwa wa ufuta, na kuwafanya mazimwi wote kuchanganyikiwa kwa uchu! ”Aaaaa! Ufutaaaa! Ufuta mtamuuuu! Nakula ufutaaa!” Wakawa wanajisemesha maneno hayo, kila mmoja akifurahia chakula kile akipendacho, na kumsahau kabisa Kibwe na upanga wa radi! Waliketi chini na kuanza kuushambulia ufuta! Kibwe naye aliongeza kasi ya mbio zake, akiruka mabonde na kuangukia kwenye makorongo na mito, misitu na nyika hadi kwenye mpaka kuelekea kaskazini ya mbali, kulikozizima baridi ya ajabu, iliyowagandisha watu na kuwageuza mawe! Pale mpakani alisimama ghafla akitahamaki na kuona moshi mwingi uliotanda mbele yake, na umbile la dude kubwa lililofichwa na giza la moshi huo, likiashiria kuwepo kwa jitu kubwa likishughulika chini ya mti mkubwa kupita kiasi! Muda wote aliokuwa akiwakimbia wale mazimwi, alimsahau kabisa kiongozi wao, aliyeitwa Nyalile!

Kibwe alitaka kufahamu ule moshi uliotanda vile ulitokana na nini. Huku akihofu, lakini kwa moyo wa kishujaa, taratibu alisogea kule kulikotoka moshi ule, akiangalia huku na kule kwa wasiwasi hadi akafika karibu kabisa na sehemu ile. Aliona kuwa ule moshi ulitokea bondeni, wakati yeye akiwa juu kidogo kwenye uwanda. Aliposogea na kukodoa macho yake vizuri ili aweze kuona kama kwenye ule utando wa moshi kulikuwa na nini, alihisi kama vile anaangalia umbile kubwa sana la jitu la miraba minne, likishugulika kufanya kazi fulani. Alipozidi kutazama kwa makini aliona kuwa lile halikuwa jitu la miraba minne tu, bali lilikuwa ni kitu kama mtu, na vilevile kama mnyama, likishugulika kuandaa chakula chake chini ya mti mkubwa sana! Lo! Kumbe alikuwa akiliangalia dude moja la kutisha mno, lililokuwa na manyoya mwili mzima, meno marefu kama pembe za tembo lakini yaliyojaa kinywa tele, na kuanzia tumboni kwenda miguuni, Kibwe alikuwa akiangalia mwili wa binaadamu mithili ya sokwe, isipokuwa ulikuwa mkubwa kupita kiasi! Uso wa dude hilo uliokuwa kwenye kichwa kilicho fanana na cha tembo, na katika paji la uso wake, kulikuwa na jicho moja tu!

Naam, kwenye bonde lililozungukwa na msitu wenye miti mirefu kupita kiasi, alikuwemo zimwi Nyalile, na juu ya bonde hilo, alikuwepo Kibwe akimwangalia! Utakisia mwenyewe hali ya Kibwe ilivyokuwa, mara alipotahamaki, akagundua jinsi alivyokuwa karibu kabisa na kubwa la mazimwi wote, ambalo sifa zake alizipata kutoka kwa Bunga! “Mama yangu weee! Sasa kweli niko hatarini!” Kibwe aliwaza. Alijibanza kwenye miti mirefu kabisa, huku jasho likimtoka, na hofu iliongezeka kila sekunde, wakati kijana yule alipoyaona yale aliyoyaona mle bondeni! Kwenye mafiga makubwa sana kupita kiasi, Nyalile alikua ameinjika jungu kubwa mno. Wakati likichemka, alimkamata ng’ombe mzima na kumnyonga na kisha kumtumbukiza ndani ya lile jungu. Pamoja na ng’ombe huyo Nyalile alichukua kama gunia mbili za mchele na kuutosa kwenye lile jungu lililokuwa likichemka kwa mchemko wa kelele kubwa za ngurumo pale msituni! Shughuli iliendelea na muda wote lile zimwi lilikuwa likichochea mapande ya miti mikubwa mafigani, kukoleza moto wake ili chakula kichemke vizuri.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)