MZIMU WA WAUFU (2)
Zephiline F Ezekiel
---
Jina: MZIMU WA WAUFU
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA PILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Baada ya kuwasili nyumbani hapo walitoka nje familia nzima kuja kumpokea Masumbuko.dada zake na wadogo zake walionekana kufurahi zaidi kumuona tena kaka yao, hawakujua kama ujio huu ni wa matatizo. Ilikua ni furaha kubwa kwao kuonana na ndugu yao aishie jijini Dar es Salaam, nyumba ilikua imefurika ndugu mpaka watoto wa mke mdogo wa mzee Kikoko aishie Shaikom nao walikuja kumpokea kaka yao
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Ki ukweli Mzee Kikoko alijitahidi sana kuwaweka pamoja na kiupendo wanae wote na wake zake japo changamoto za wake wawili hazikosi ndani ya nyumba Haraka haraka Jogoo akakamatwa kwa ajili ya mgeni japo na family nayo ‘Itasafiria nyota” kama ilivyo kawaida ya uswahilini, na baada ya salamu mazungumzo yakaanza kwa swalila Kikoko ambae alionekana kua hana raha tangu jana yake “Enhee mwanangu, hebu tutoe jaka la moyo maana hatujalala tangu jana tunawaza tu umepatwa na nini”swali hilo la Mzee Kikoko lilimtoa machozi Masumbuko ikabidi atoe kitambaa chake laini aanze kufuta machozi, kitu kilichozidi kuacha maswali kwa
wazazi wake
“Sasa ukishaanza kulia badala ya kusema tatizo nini ndo tutakuelewaje?” alidakia mama yake
“Baba ni matatizo ya ajabu sana, sielewi ni nini hasa”
“Matatizo gani hasa?” Ndipo sasa Masumbuko akaanza kuwasimulia wazazi wake kuhusiana na kadhia inayoendelea kutalii na kutanabahi katika falme za ubongo wake kupia Ndoto, Ndoto ya ajabu!
“Yaani Ndoto tu ndo ikufanye Ulie, Ushindwe kulala, ufunge safari kutoka huko kote mpaka Shinyanga kuja kushitaki, we ni mwanaume wa aina gani?” Baada ya maelezo marefu kutoka Masu sasa ikawa zamu ya Mzee Kikoko ambae hakuonesha dalili za kuguswa na jambo hilo, aliongea kwa ukali na katika hali ya kumshangaa mwanae, ikabidi sasa mama yake na Almas nae aingilie kumtetea mwanae
“Hii sio hali ya kawaida mume wangu, hakuna haja ya kumlaumu Masu, hata mimi nimeshangaa sana tu”
“Ulichoshangaa wewe ni kipi hasa”
“Haiwezekani mtu aote Ndoto halafu iwe na muendelezo kama Tamthiliya tena huku akipewa tahadhari ya kile alichokifanya, Haiwezekani”
“Nyote mmekutana, Mama na Mwana sawa na Pipa na mfuniko tu, Ndoto ni ndoto tu hata uiote mara kumi, kwa hiyo we ukiota umepata pesa halafu baada ya kuamka usizione hizo pesa utaanza kuzitafuta chini ya Mto?” aliuliza Mzee Kikoko huku akisamama na kuashiria kua anaondoka zake, ikabidi Masu ajaribu kujielezea vizuri lakini Mzee Kikoko hakumuelewa na hatimae akatoka zake nje na kuwaacha mtu na mama yake wakifarijiana.
Nje ya nyumba ya Mzee Kagomba, majira ya saa mbili za usiku walikua wamekusanyika watu wengi wakiwa wameketi huku wameizunguka meza ndogo ya mbao, wengi wa watu hawa walikua ni wazee mashuhuri kutoka maeneo tofauti tofauti ya mkoani Shinyanga, kama ilivyo Ada kila siku hukusanyika mahala hapo kwa ajili ya kupata kahawa ambayo ni sehemu ya Biashara zinazo msaidia Mzee Kagomba kujipatia Rizki, mbali ya kahawa Kikubwa zaidi kinachowafanya watu wengi kukusanyika pale na kuacha vijiwe vingine vingi vya kahawa si tu Ubora, usafi, na umahiri wa Mzee Kagomba katika kuiandaa kahawa hii Laa hasha Bali pia ni Mvuto wa Story za kila aina zipatikanazo maeno hayo, Kijiwe hiki cha kahawa kinafahamika zaidi kwa jina la BBC Kutokana na ukweli kwamba habari yoyote itakayotokea mjini hapo au hata nje ya mji huo iwe ya Kimichezo, kisiasa, kidini, nk basi lazima itaanza kufika hapo kabla hijazagaa kwingineko na wasimuliaji wa hapo ni mahiri kwa porojo sijapata kuona. Kila
mtu ni mjuaji kijiweni hapo na hakuna anaekubali kushindwa katika hoja yake, hata kama ukiwa hauna pesa ya kununu kahawa unaruhusiwa tu kwenda kupiga Soga na kama ukija na habari tamu na ya kusisimua basi utanunuliwa kahawa mpaka umalize kutoa habari hiyo.. Ilikua ni siku ya pili sasa Mzee Kikoko hajaonekana kijiweni hapo kitu ambacho si kawaida yake kupitisha japo siku moja bila ya kukanyaga ardhi ile ya Waswahili wa mjini, Wazee wenzie walikua wakiulizana kama mzee mwenzao amekutwa na jambo au imekuaje mpaka hajakanyaga pale!! Walikua wakimkubali sana kwa Story zake za Tambo na Porojo, Ikawa kama bahati wakati wanaendelea kumjadili nae huyo akawasili, kila mtu akafurahi, akapatiwa kiti na baada ya kuketi Mzee Kagomba akaanza kumtania
“We bwana haufi mapema hakyamungu..”
“Kwanini tena, au Izraeli kamchumbia mwanao?”
“Tulikua tukiulizana hapa hivi Mzee Kikoko amekufa na kuzikwa kimya kimya?”
“Utaanza kufa wewe, mimi utaniacha..”
“Haya hebu tujaalie hali ya Maungo yako..”
“Kwakweli mpaka tunaingia mitamboni hali yangu ni murua, naendelea tu kuvuta pumzi mwanana bila ya malipo” watu wote wakaangua kicheko kutokana na majibizano ya wazee hawa watundu wa maneno “Enhee mwenzetu ukapotelea wapi?”
“Ya kuacha tu, matatizo ya kila aina duniani hapa”
“Hebu tujuze, hii ndo BBC Lete maneno upate ushauri kutoka kwa mabingwa wa saikolojia waliosomea miembeni”
“Juzi alikua mwanangu Masu, lakini ujio wake haukua wa Kheri”..” “Enhee..”
“Kwanza kabla hajaja, alinipigia simu usiku mkubwa akiwa ametaharuki vibaya, nilijaribu kumtuliza anieleze tatizo lakini hakusema akaniambia kesho yake angepanda buss ili aje huku Shinyanga tuyaongee vizuri” Wazee wote pale kwenye Kahawa walikua kimya wakimsikiliza Mzee Kikoko
“Kesho yake sasa ambayo ni juzi ndo akaja na Buss nikaenda kumpokea stand kisha tukarudi mpaka nyumbani tulipofika nyumbani baada ya salamu na mazungumzo kidogo, nikamuuliza sasa anijuze tatizo lilikua ni nini hasa, cha ajabu mwenzangu akaanza kulia” Story ilionesha kuwatuliza masikio wadau wote pale, kisha baada ya kupiga funda moja la kahawa Mzee Kikoko akaendelea kutiririka na nyuzi
“Baada ya kumbembeleza aniambie tatizo, nikabaki mdomo wazi akaniambia kua Anasumbuliwa na Ndoto, anaota vitu vya ajabu vinamnyima usingizi na kumkosesha raha” Alipofikia hapo kijiwe kizima kilizizima kwa vicheko vya hali ya juu ikawa sasa ni kelele tu bila ya msikilizano…
“Amaa kweli ukiyastaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, yaani badala umrithishe mtoto mali we umemrithisha huo uoga wako na uzezeta..” maneno hayo yalikua ni ya Mzee Kagomba akimtani mzee mwenzie kisha wakacheka sanaa akadakia Mzee mwingine nae akasema
“Yaani mimi sijatulia ila Kikoko na mwane mmeshinda tuzo..“ Mzee Kagomba akadakia tena
“Waswahili wanasema Bata hata ale kokoto haachi kuharisha, mie nilijua una tatizo kubwa kumbe hujaacha tu maigizo yako“ wakati wakiendelea kucheka na kushangaa tukio hilo Mzee Kikoko hakumjibu mtu zaidi ya kuendelea kunywa kahawa yake, wengi walidhani ni mashara tu ya mzee huyu, na hapo ndipo ilisikika sauti ya Mzee Kapela aliekua muda wote kimya akivuta sigara yake taratibu, yeye akaja na Mpya
“Mie nadhani ni utoto unawasumbua tu, badala tumsikilize amalizie hiyo ndoto ninyi mnataka kutuharibia mjadala huu, Hebu Kikoko Endelea..” Bila ya ajizi Kikoko akaendelea kuwasimulia jinsi Ndoto ilivyomuanza mwanae ikiwa ni pamoja na vitisho alivyopewa, kilichowashtua wengi ni pale sasa Kikoko alipoanza kuwaelezea jinsi ile Ndoto ilivyoendelea pale ilipoishia siku ya kwanza ikiwa na wahusika wale wale, kila mmoja alistaajabu na sasa hali ya kijiwe ikatulia tena na kila mtu akaonekana sasa kuguswa na mkasa huu, na baada ya Kikoko kuhitimisha uwasilishaji wa hoja yake wadau wakaanza kutoa ushauri. Wengi waliendelea kusisitiza kua japo ni Ndoto ya Kushangaza lakini itakua ni Ndoto tu na haitakua na athari yoyote, Lakini Kagomba alikua tofauti na baadhi ya vijana pale, ye aliwaambia kua ile si Ndoto ya Kawaida na kawashauri waende wakamuone Mzee Maguno kwakua yeye ni mtaalamu wa kutafsiri Ndoto. Hali ile ya malumbano pale kijiweni iliendelea bila ya
kupata muafaka wa pamoja
Baada ya siku mbili za kuwa pale Shinyanga, Sasa Masu alikua tena ndani ya Buss la SABENA Akirejea jijini Dar, Kichwani alikua bado anazungukwa na hofu, hafu ya kutokewa tena na Hunudu wa Waufi, mbaya zaidi alitegea kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa baba yake lakini hali ikawa tofauti aliambulia maneno makali ya dhihaka tu akiambiwa kua ni majiamizi tu hayo yanamsumbua Hatimae jioni majira ya saa moja tayari Buss lilikua limeegesha ndani ya Stand ya mkoa Ubungo Buss Terminal, alipoteremka tu alienda moja kwa moja mpaa nje akavuka upande wa pili wa bara bara kule zinapopaki daladala za Ubungo to Gongo la Mboto akadandia hiyo ili ashuke Buguruni, alifanya hivyo na bahati nzuri hapakua na foleni ndefu hivyo hakuchelewa sana kwani ndani ya Dk kama 30 tu alikua ameshashuka katika kituo cha Buguruni Shelly na hapo akaanza kutembea tu kwa miguu kutokea hapo Shelly kwenda kwake maeneo ya kwa mnyamani anakoishi hivi sasa, haikua mbali kutokea hapo kituoni
Alipofika kwake alipokelewa na Mkewe Judith kwa shangwe na Furaha
“Karibu mume wangu..”
“Ahsante, habari za hapa?”
“Nzuri tu nyumbani hawajambo wote?”
“Hawajambo tu, vipi hawa(wanawe) hawajambo?”
“Nao wazima wako ndani wanaanda madaftari yao ya kesho shule” “Enhee nipe habari za huko, Baba uliongea nae? Na kasemaje?” Swali hili lilimuumiza sana Masu na alijisikia vibaya kumuambia mkewe kua baba yake hajampa ushirikiano wowote zaidi ya maneno ya karaha tu, lakini haina jinsi ilibidi amueleze ukweli tu!
JIRANI na msikiti mkongwe wa Idrisa uliopo Kariakoo mtaa wa Tandamti Jijini Dar es Salaam kuna duka kubwa la vitabu vya dini linalomilikiwa na Sheikh Jabu ambae mbali ya kuishi Dar es Salaam pia ana mke mwingine Tabora hivyo kufanya makazi yake kua sehemu mbili, Lakini pia Sheikh Jabu mzawa wa mkoani Kigoma, watu mbalimbali kutoka mikoa ya Kigoma na Tabora hufanya duka hilo kama vile sehemu ya kukutania na jamaa zao wa huko mikoani kirahisi kwa kua wengi wanapafahamu dukani hapo, pia Dukani hapo ni sehemu iliyozoeleka hata kwa wenyeji wa hapa jijini Dar es Salaam kama ni sehemu maarufu ambayo kila siku watu hukusanyika mida ya jioni kwa ajili ya kubadilishana mawazo, hua kuna mijadala mizito na malumbano ya hoja katika Nyanja tofauti toauti hasa Siasa, dini, michezo na uchumi Masumbuko nae hupendelea sana kwenda dukani hapo kupiga stori, Alipazoea dukani hapo kwakua mara kwa mara Baba yake Mzee Kikoko akija Dar hupendelea kwenda pale kupiga story na wazee wenzie hasa wa Kigoma pia Mzee Kikoko ni rafiki kipenzi wa mmiliki wa duka hilo Sheikh Jabu, Hivyo basi kutokana na umaarufu na usemaji wa Mzee Kikoko ikamfanya Masu nae akajikuta anafahamika sana Dukani hapo,
Siku moja baada ya kutoka kazini kwake aliamua kwenda pale dukani kusikiliza habari za mjini lakini pia alikua ameweka nia kua kama atapata fursa ajaribu kuwadokezea kuhusu ile Ndoto yake maana hakika pale dukani ilikua ni uwanja wa wajuvi wa mambo
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni