MZIMU WA WAUFU (3)

0

SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
Siku moja baada ya kutoka kazini kwake aliamua kwenda pale dukani kusikiliza habari za mjini lakini pia alikua ameweka nia kua kama atapata fursa ajaribu kuwadokezea kuhusu ile Ndoto yake maana hakika pale dukani ilikua ni uwanja wa wajuvi wa mambo

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Lakini siku hiyo pale dukani hapakua na watu wengi, alikuapo muuzaji wa vitabu na Mzee mmoja kutoka kigoma ila nae kwa sasa anaishi pale Dar, anaitwa Mzee Kishindo, mzee huyu nae hua ni mtu wa maneno sana na hua ni rafiki pia wa Mzee Kikoko mara nyingi kikoko akija Dar hua karibu sana na Mzee huyu, ndipo Masumbuko akaona sasa acha achokoze kuhusu lile tatizo lake na ile Ndoto ya Ajabu

“Mzee Kishindo samahani”

“Bila samahani mwanangu”

“Mie nina swali,,”

“Kaswalie msikitini, hapa hakuna udhu” wakajikuta wamecheka wote “Hapana sio swala, nina jambo nataka kukuuliza”

“Anhaa kumbe una suala, haya uliza”

“Suala hilo linahusu Ndoto” baada tu ya Masu kusema hayo maneno mzee Kishindo akatabasamu kisha akanena

“Unanikumbusha taaluma yangu niliyosoma miaka karibu thelathini iliyopita, taaluma waliyopewa Mitume na manabii”

“Kumbe tatizo langu litakua limepata ufumbuzi”

“Ndoto sio tatizo mwanangu, ni ishara muhimu na dalili zilizojificha za jambo Fulani ambalo ujumbe wake unaupata kupitia Ndoto, na kama utazifanyia kazi hautopata tabu ila ukizipuuza utajuta, utajikuta unahangaika kila siku, utayalaumu Maji machungu kumbe mdomo wako ndo una homa” Masu alikua akicheka kwa vionjo vya maneno kutoka kwa Mzee huyu,

“lakini ziwe Ndoto kweli isiwe njozi zenu umelala haujaoga wala haujala sasa jinamizi linakukaba mpaka ufizi halafu unataka tukutafsirie ndoto yako tutawezea wapi!!!” Mzee alikua na maneno sana huyu mpaka sasa Masu akajikuta anaishiwa cha kuongea ikabidi tu ajitahidi kumrudisha kwenye mada

“Mie kuna ndoto hua inanijia, ndoto ya kutisha sana, cha ajabu hua inajirudia kwa kuendelea pale ilipoishia”

“Mmh,Hiyo kweli Ndot, enhee uliotaje?” Masu akaanza kumuhadithia mzee Kishindo kuanzia siku ya kwanza alivyoota kuhusu Dini ya WAUFI na jinsi anavyosumbuliwa na Hunudu, akaendelea kumsimulia mpaka ilipojirudia tena ndoto ile, ilikua ni hadithi ya kusisimua na kutisha, wakati Masu anaendelea kuongea wakaingia tena watu wawili nao wakawa wanasikiliza habari ile iliyoonekana kuwaingia sana lakini cha ajabu Masu akiwa anaendelea kuongea Mzee Kishindo alikua anacheka mpaka machozi ikabadi sasa Masu aache kwanza kusimulia, na alipoacha tu ndipo Mzee Kishindo akadakia

“Dini ya Waufi?”

“Ndio inaitwa dini ya Waufi, mbona unacheka sasa?”

“Hakuna dini ya Waufi mwanagu hapa duniani”

“Mzee usibishe, Mimi ndie nilieota, na wameniambia mambo yahusuyo dini yao hiyo karibu mara nne usingizini”

“Hata wangekuambia mara mia lakini ujue hakuna Dini inayoitwa waufi”

“Kwahiyo ni nini sasa?”

“Ulishamueleza baba yako juu ya kadhia hii?”

“Ndio nilienda mpaka Shinyanga kwa suala hili lakini kama unavyomjua Mzee Mwenzio, hakuna alichonishauri cha maana zaidi ya kuniambia kua naweweseka na majinamizi tu, akaniambia niwe nasali kabla ya kulala tu basi”

“Ha ha ha aha, baba yako anajaribuKuficha moto sasa moshi utamuumbua”

“Kivipi tena Mzee Kishindo?”

“Nina uhakika kua Kikoko anajua kila kitu juu ya tatizo lako, au pengine amesahau, na kama amesahau basi amesahau kitu muhimu sana, na asipokua makini tatizo hili litakutesa na hata kukuua kabisa”

“Mbona unanitisha Mzee, Kitu gani tena?”

“Unajua sababu ya wewe kuitwa Masumbuko baada ya kuzaliwa? Maana kwenu hakuna babu yako hata mmoja aliwahi kuitwa jina hilo”

“Hapana siijui” Mzee Kishindo akacheka tena kisha akaendelea

“Tatizo lako ni kubwa sana, na pia ni dogo sana kama litawahiwa, kama litawekwa wazi bila ya kuogopa athari zitakazotokea, najua baba yako anaogopa athari za kuliweka wazi tatizo hili, ila kama utakua na ‘kifua’ nitakueleza na kukusaidia nini cha kufanya japo itahitaji muda, pesa na subra”

“Nisaidie mzee, niko tayari kwa lolote”

“Una kifua??, sio hicho kidali kama bao la kuchezea kamari, Kifua cha kutunza kila aina ya maumivu?”

“Ndio, ninacho”

“Lakini sio leo, uje nyumbani kwangu siku ya ijumaa, kwanza nitakupa historia yaw ewe kuitwa Masumbuko kisha nitakupa maana ya Waufi, na kisha tutaanza safari ya kukupeleka Umamani kwenu milima ya Unyanyembe huko” Mzee Kishindo alikua anaongea huku akicheka sana, Masu alibaki njia panda, hakujua ni nini alichokielewa mzee huyu, ni nini ambacho mzee kikoko anakificha, Waufi ni nini kama sio Dini? nk lakini ikabidi tu sasa akubaliane na mzee Kishindo kua wataonana Siku ya ijumaa Baada ya mazungumzo yale, tayari Masu alikua ameshaingia hofu hivyo hata hakukaa sana na kwakua tayari duka lilikua limeshaanza kujaa wapiga porojo, ikabidi aage na kuondoka zake mpaka barabarani ili akapande daladala ya kumrudisha nyumbani kwake, akiwa amesimama kituoni anasubiri gari ghafla kuna gari ilikuja na kusimama kwa mbele, ilikua ni gari aina ya Verosa, kioo kikashushwa mpaka chini na kumfanya aonekane vema mrembo aliekua akiendesha gari hiyo, dada huyo alikua amevaa

Tshirt nyeusi na kofia ya kufuma ikiwa na rangi kama za wale Marasta, baada ya Masu kukutanisha macho na dada huyu akatoa mkono na kumuita kwa Ishara, lakini masu kila alipomuangalia dada Yule hakumtambua ila sura kama ilikua ikimuijia, ikabidi asogee tu kumsikiliza

“Mambo” alianza Dada Yule kwa kumsalimia Masu

“Poa, mzima?”

“Mzima tu hujanijua?”

“Hebu nikumbushe kidogo” Masu akajifanya kutabasamu kama kamjua kidogo

“We si ni Masu wa pale Mtaa wa Nyamwezi kwa wale ma Agrigator wa Mpesa”

“Naam ndio mimi, ofisi yetu inaitwa Birimuye”

“Sasa hunijui mimi kweli au unajifanyisha tu nawe!? “

“Sura inaniijia lakini sina kumbukumbuku za uhakika”

“Mie hua ni wakala wenu hua mnaniuzia Float”

“Aaah, nimekujua si unajua tena hua tunawahudumia watu wengi mpaka tunasahau, samahani wangu” Masu alijifanya kumjua lakini ukweli ni kwamba hakua akimkumbuka kabisa

“wala usijali, unasubiri gari za wapi?”

“Za buguruni”

“Haya ingia nikusogeze mpaka ilala, mie hua ndo nakaa pale”

“Ok ahsante nashukuru” Masu akaingia ndani ya gari kisha gari ikaondoka, ndani ya gari kulikua na kijana mwingine aliekua amekaa seat ya nyuma, ikabidi Masu ageuke ili amsalimie, Alipogeuka tu moyo wake ukalia ‘Paa!’ alishtuka mno, mara mapigo ya moyo yakabadilika, hofu ikazidi kutanda, alitamani ardhi ipasuke aingie, hapo hapo akatamani amwambie Yule dada amshushe haraka lakini akashindikana akahisi kama vile Mdomo ujeaa maji, jasho likawa linamfumka mwili mzima. Kijana huyo alikua ni kijana mweupe alievaa Tshirt nyeupe na kofia nyekundu, Masu alijitahidi kuvuta picha kua amemuona wapi kijana huyu, naam Kumbukumbu zake hazikimdanganya, ni kweli alimjua haraka kijana Yule.. Alikua ni Hunudu wa dini ya Waufi, na alimjua zaidi kutokana na ‘Chongo’ jicho buvu, Masu alichanganyikiwa sana kuona sasa yule kijana ambae hua anamsumbua usingizini kwenye ndoto kwa kujisifia kua nikiongozi wa dini ya Waufi leo amemuona ana kwa ana, Sasa alianza kuamini

kua ile si Ndoto ya kawaida, akaanza kukumbuka maneno ya Mzee Kishindo, akiwa bado anatafakari nini cha kufanya mara gari ikawa imefika maeneo ya Ilala bungoni ikakatiza upande wa kulia kwenye kile kibarabara kidogo kinachochepuka kule kilipo chuo cha habari kisha ikasimama pembeni halafu Hunudu akamshika mkono Masu na kumsalimia, Masu alikua akivuja jasho la woga na hofu

“Hali yako kaka Masu”

“HUNUDU!!!!?” Masu aliuliza swali kwa wahka wa hali ya juu sana

“Ndio mimi, kumbe una kumbukumbu sana!!,”

“Yaani umeamua kunifuata mpaka huku duniani?”

“Kwani hua tunaonanie mbinguni?” baada Hunudu kujibu vile wakacheka wote Hunudu na yule dada aliekua akiendesha Gari , ikabidi Masu amuangalie vizuri dada Yule maana aligundua kua nae ni lazima atakua ni mfuasi wa Waufu tu, wakati Masu anamuangali dada Yule huku Hunudu akaendelea kuongea

“Punguza hofu na woga”

“Shida yako nini hasa kwangu?”

“Mimi sina shida yoyote kutoka kwako zaidi ya kuja kukukumbusha mambo kadhaa”

“Mambo gani?!!” “Kwanza tambua popote uendapo na sie tupo, hauwezi kutukimbia, pili tulikukanya usitoe siri zetu hukusikia ukaenda kumuambia mkeo ukapewa adhabu ya kutoa kafara, ukakataa kumtoa mwanao, tukakuacha lakini sasa umeenda kutoa siri mpaka kwa watu baki tena huna hata woga, hivi haujipendi kijana?” Masumbuko alikua akitetemeka, mwili wake kama umeganda jinsi alivyokua katulia,

“Sasa sikiliza Masu leo usiku nitakuijia ukanywe Damu na pia uingizwe rasmi katika kitabu cha kumbukumbu ya wafuasi wa Waufi pia utamtoa Mwanao mmoja kama kafara yako, ukileta tena upuuzi sasa tutakua kinyama, naomba usiniangushe” Baada ya Hunudu kuongea maneno yake yaliyojaa vitisho vikali dhidi ya Masu, haraka Dereva ambae ni Yule dada akafungua mlango wa mbele na kumuambia Masu ateremke ili wao waondoke, Masu akateremka kwenye gari kama aliemwagiwa maji ya jinsi alivyoroana kwa jasho lake mwenyewe, aliposhuka tu mlango ukafungwa halafu Yule dada akamchombeza kwa kimombo

“Tutaonana usiku” halafu gari akatembea Masu alikua amechanganiyikiwa akaenda mpaka mbele huku kwenye Bara bara ya Uhuru akaiita bodaboda ikamchukua mpaka kwake

“Tsh ngapi unanidai”

“Elfu tatu tu kaka mkubwa” Masu akaingiza mkono mfukoni hata hakuhoji kwanini iwe pesa yote ile kutokea ilala tu hadi buguruni kisha huyo akaanza kuingia zake kwake

“Kaka mbona haujachukua chenchi?” Dereva wa boda boda alimkumbusha Masu lakini naona hata hakusikia yeye akawa anawahi tu kwake alipoingia ndani akamkuta mkewe yuko pale uwani akifuafua ngua za watoto, akapita bila hata ya salamu mpaka chumbani, ile hali ikamshangaza sana Judith nae ikabidi amfuate Chumbani

“Kuna nini mume wangu?”

“Ni bora nife tu sasa?”

“Ufe kwanini tena jamani?Hebu niambie kuna nini?”

“Ile ndoto kumbe sio ya kawaida kabisa”

“Imekuaje sasa?” Judith alijaribu kumshawishi sana Masu ili amuambie kilichotokea lakini Masu akawa anaogopa kumuambia akijua kua Waufi wanamuona, baada ya Judith kumsumbua sana ikabidi sasa amuambie tu ukweli wa mambo kuanzia yale maelezo ya kutatanisha aliyoambiwa na Mzee Kishindo halafu akamsimulia jinsi alivyomuona Hunudu uso kwa macho. Judith alipigwa na Butwaa na sasa badala amfariji mumewe yeye ndo akawa amechanganyikiwa mara mbili ya Masu mpaka Masu akawa sasa almanusura awe chizi,

“Mume wangu haiwezekani, hili jambo zito mie naenda kwa Mchungaji Jofrey kumueleza jambo hili”

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)