Mtunzi: ___
SEHEMU YA KUMI NA NANE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Daima mabwana aliowapata, walikuwa hawa wa ‘kuokota’ Mabwana waliosukumwa na uchu tu wa kuwa na mwanamke. Hali hii ilimfanya msichana huyu ajikabidhi kwa kila mwanaume bila kujali lolote, akiwatimizia kila haja bila aibu wala kinyongo.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Lakini harakati zake za kuwaburudisha wanaume mara nyingi hazikumfikisha mbali. Mara kwa mara alikuwa akipewa ‘kwa heri ya kuonana’ na mabwana hao. Wengi waliwarudia wake zao. Wengine walikuwa wameishiwa. Na wengine walikusudia kuziponyesha pesa zao.
Ndiyo Sofia akayachukulia maombi ya ‘Mzee kijana’ huyu kama tunu aliyonunuliwa bila ya kutazamia. Aliyaona kama mwisho wa matatizo yake na mwanzo wa maisha mapya. Alimtazama tena Proper. Hakuona dalili yoyote ya mzaha katika sura yake. Kama kweli mtu huyu alikuwa na tatizo lolote, pesa hazikuwa mojawapo. Angekubali mara moja. Hata hivyo alikumbuka hali ya chumba chake, mazingira yaliyostahili jina la pango. Ndipo alipomweleza Proper kwa sauti iliyonasihi.
“Ningependa sana kukukaribisha kwangu. Lakini hali ya chumba kile… kwa kweli, hakifai kwa mtu kama wewe”.
Proper hakuwa mgeni kwa maisha ya wasichana wengi mjini. Alikwisha waona wengi ambao wawapo mitaani wanaonekana kama malaika kwa mavazi mazuri, lakini ukifika wanakoishi utadhani ni vijakazi. Alimsihi Sofia aondoe shaka. Alimweliezea kuhusu msingi wake wa kimaskani. Kwamba ameishi sana ‘gheto’ na maisha hayo anayapenda. “Nikiwa Dar hupendelea sana kutembelea sehemu za Manzese. Nikiwa Arusha makazi yangu ni Ngarenaro. Na nikiwa Moshi nastarehe zaidi nikiwa Majengo”, alimhakikishia. “Sababu hiyo ndiyo iliyonifanya niishi katika hoteli hii ndogo badala ya kubwa kama Mwanza Hoteli”.
Maneno hayo yalimaliza ubishi wa Sofia. Usiku uliofuata uliwakuta Kirumba katika chumba chake.
Chumba kilikuwa katika hali ambayo Proper aliitarajia. Raslimali za muhimu zilikuwa kitanda kikuukuu chenye godoro kukuukuu la sufi ambalo halikuwa na hadhi ya kuitwa godoro pia kulikuwa na sanduku, meza na sufuria mbili tatu zilizonuna kwa uchafu. Ambacho Proper hakutegemea ni ukarimu wa kunguni na mbu walikuwa huru katika chumba hicho. Walimlaki moja kwa moja bila kumpa fursa ya kujipumzisha.
Yote hayo Proper alilazimika kuyastahamili eti kwa sababu amependa, kumbe ni uhitaji tu. Alikusudia kujisetili akisubiri siku kuu ili atimize lengo lake. Hakuna askari wala mpelelezi yeyote ambaye angefikiria kumtafuta pale. Alitarajia kuwa wangeweza kumsaka katika mahoteli makubwa na kwenye vitongoji vikubwa vikubwa, siyo kwa malaya wa chini kama Sofia anayeishi maeneo yaliyosahaurika.
Siku mbili zikapita bila ya kitu chochote cha kawaida kutokea. Proper alishinda ndani akijisomea vitabu, nae Sofia alijishughulisha kutafuta vyakula na vinywaji. Sofia alikuwa akipewa pesa zilizozidi mahitaji yake ya kawaida. Proper alikuwa amemruhusu kununua mavazi mapya. Hali hii ngeni ilimuinua Sofia, akawa anapepea mfano wa kishata. Nafasi yoyote iliyojitokeza, ilitumiwa kufanya mapenzi. Sofia alijitia kila aina ya juhudu kumridhisha Proper. Lakini hakuweza kuutambua unafiki wa Proper. Akazidi kutekwa akili na vitendo vya mtu huyu. Hata hivyo sauti nyingine ilimnong’oneza atahadhari.
Jioni ya siku ya tatu, mambo yalianza kwenda mrama. Sofia alirejea kutoka mjini na gazeti mkononi. Alimfuata Proper aliyelala chali kitandani na kumfungulia ukurasa wa tatu ambao ulikuwa na picha sita chini ya kichwa cha habari kilichosema;
“TANGAZO LA POLISI.
JIHADHARI NA MTU HUYU- MARA UMWONAPO IARIFU POLISI. ANATAFUTWA KWA MAUAJI YA WATU WENGI NA ANAWEZA KUUA WAKATI WOWOTE, KUWAMAKINI”.
Proper alisoma haraka haraka. Kisha alizitazama picha hizo kwa makini. Moja ilikuwa yake halisi. Zilizosalia zilikuwa picha za kuchora. Zilikuwa zimechorwa kwa namna mbalimbali kuonyesha nywele zote; nyingine ilichorwa kuonyesha madevu mengi, nyingine kavaa miwani na kadhalika. Ni moja kati ya picha hizo ambayo ilikuwa imefanana kikamilifu na sura aliyokuwa akiitumia sasa. Alijitia utulivu na kumgeukia Sofia na kumwuliza kwa upole, “Ni hii tu uliyoiona habari ya maana katika gazeti lote”.
“Hapana. Nilitaka kukuonyesha huyo mtu. Naona mmefanana naye sana”.
“Tumefanana!” Proper alijitia kushangaa. “Mimi nafanana na huyo anayetafutwa kwa mauaji? Haiwezekani”.
“Mmefanana sana Beka. Nadhani ni wewe”.
“Usiwe mjinga Sofia, mimi siwezi kuwa muuaji”.
“Kweli kabisa. Hata yule rafiki yangu aliyekuja hapa jana amesema hivyo. Labda ungesoma hapa chini uone”.
Proper alianza kusoma kifungu hicho kilichoandikwa kwa herufi za mlazo.
Mtu huyu ni hatari sana, anatakiwa mapema mno. Zawadi nono ya shilingi laki nne itatolewa kwa mtu yeyote atakayewezesha kukamatwa kwake. Inasemekana kwa sasa yuko mjini Mwanza au mikoa ya jirani. Unaonywa tena kujihadhari naye…
“Ni wewe Beka?”, Sofia alisisitiza huku akimkazia macho.
“Siyo mimi”. Sauti ya Proper ilikuwa ya utulivu mkubwa.
“Kwani unanionaje mimi, naweza kuwa muuaji?”.
“Hapana, lakini hiyo picha inaonyesha ni wewe”.
“Achana na picha hii. Huoni kama huyu amechorwa tu? Usiwe msichana mjinga Sofia. Mimi ni mtu ninayejiheshimu sana huko kwangu. Wasichana kama wewe, wazuri zaidi yako, ninao kama ishirini hivi ambao wanalipwa mshahara mzuri kutoka katika mfuko wangu. Na wanaume wengi wasiopungua mia, wote wako chini yangu, wote wananiheshimu. Au kwa vile niko nawe katika chumba hiki hafifu ndipo umefikia hatua ya kuniita mwuaji?”.
“Sivyo mpenzi, ila…”
“Ila…”
“Nina mashaka yule rafiki yangu amekwenda kutoa taarifa polisi. Laki nne siyo pesa ndogo”.
“Polisi. Akiwaleta hapa, wakinikuta mimi watanitia ndani kufunza adabu. Ondoa hofu. Sofia njoo kitandani, tujipumzishe nikudokeze jambo. Lete ulimi tufurahi”.
Sofia alisogeza shingo. Hakutarajia radi iliyompiga ghafla. Lilikuwa pigo kali jepesi ambalo lilitua katika shingo na kulivunja kabisa. Sofia hakujua kapigwa na nini. Wala hakuona ugumu wa kufa. Alianguka chini na kupapatika kwa muda, kisha akakata roho.
Proper alifanya kazi haraka haraka. Aliuzoa mzoga wa aliyekuwa Sofia na kuulaza kitandani. Akaufunika vizuri kwa shuka. Kisha alikusanya vifaa vyake na kutoka nje. Giza lilikuwa limeanza kutanda. Hakuona haja ya kujificha kama alivyotegemea. Aliifuata polepole barabara iendayo mjini. Alipofika Mabatini, alisimamisha taksi na kuingia ndani.
Dereva taksi alikuwa kijana wa Kiarabu mwenye ndevu nyingi. Alimsalimu Proper kwa adabu, kisha akamuuliza wapi anataka kwend. Proper hakumjibu kwa maneno bali kwa kitendo fulani. Aliudidimiza mkono wake katika begi lake na kutoa bastola yake. Aliigandamiza ubavuni mwa kijana huyo.
“Ukifanya ujinga utapoteza maisha. Nataka wewe na gari hii mfuate matakwa yangu. Haya endesha mpaka nitakapokwambia wapi tuelekee”.
Huku akitetemeka, macho yakiwa yamemtoka, kijana huyo alilitia gari moto na kuliondoa taratibu huku mapigo ya moyo yakimwenda kasi kwa hofu.
“It’s him. It’s him. That’s his style” Inspekta Kombora alifoka. Kisha alijisahihisha haraka na kusema polepole; “Ndiye. Bila shaka ni yeye huyu muuaji”. Macho yake yalikuwa yakiwatazama wasaidizi wake wawili ambao waliketi mbele yake kimya wakimsikiliza.
Walikuwa wakijadili taarifa ambayo ilikuwa imewafikia muda mfupi kutoka Mwanza. Taarifa hiyo ililetwa na mtu mmoja ambaye alimgundua mtu huyo anayesakwa kwa udi na uvumba, Proper mahali alikojificha. Mtu aliyetoa siri alieleza kuwa anayetafutwa amejificha nyumbani kwa mwanamke fulani. Lakini makachero walipoivamia nyumba hiyo, waliambulia kukutana na maiti ya mwanamke aliyekutwa amelala chali kitandani. Tayari mhusika mkuu alikuwa ametoweka. Ushahidi uliopatikana ulieleza kuwa mtu huyo alimhukumu mwanamke huyo kifo baada ya kubaini kuwa amejulikana. Hakika mtu huyo ni hatari. Makachero walibaini baadhi ya vifaa vyake vya kazi na maandishi ya kijasusi. Mambo mengi yalikizonga kichwa cha Inspekta Kombora, lakini hakukata tamaa.
“Ni yeye. Msimpe nafasi tena akaponyoka”, Inspekta Kombora aliagiza huku akisisitiza. “Hakikisheni yeye au maiti yake inapatikana haraka kabla ya kesho”, aliongeza huku kila baada ya nusu saa akipiga simu kuulizia maendeleo ya operesheni hiyo.
Ilikuwa alfajiri ya siku ya pili Inspekta Kombora alipopata taarifa nyingine alipokuwa ofisini kwake ameketi na wasaidizi wake wakijadili. Taarifa mpya ilisema taksi moja aina ya Peugeo 504 ilikuwa imeokotwa katika pori la Ngara mpakani mwa nchi za Rwanda na Burundi kando ya barabara iendayo Burundi. Dereva wa gari hiyo aliokotwa akiwa hoi bin taaban mahututi. Hivyo hakuwa na chochote za kueleza alipoulizwa ilikuwaje gari hilo likaweza kuvuka vipingamizi vyote vya barabarani kutoka Sengerema, Geita, Biharamuro hadi kufika Ngara. Lakini baada ya kupatiwa matibabu, aliweza kueleza kuwa gari lake lilitekwa na mtu mmoja ambaye alikuwa akielekea Burundi. Kwamba mtu huyo alimpiga kwa dhamira ya kuua, huenda alimwacha hai kwa kukosea tu akidhani kuwa tayari ameua. Dereva huyo alipoonyeshwa picha ya Proper alimtambua mara moja.
“Ni yeye”, Inspekta Kombora alirudia tena. Lakini ni kitu gani kimempeleka huko mpakani?”.
“Ametoroka afande”, mmoja wa wasaidizi wake alimjibu.
“Amesoma alama za nyakati, ameona mambo yamezidi kimo. Akifika Bujumbura atapata usafiri ambao anaamini utamtoa nje ya Afrika mapema awezavyo”.
Inspekta Kombora alifikiri kwa muda kabla hajasema, “Labda. Hata hivyo, mimi sioni kama kwamba mtu huyu ametoroka. Sio mtu wa kukata tamaa mapema. Huyu mwendawazimu anakusudia kufanya unyama wake kwa vyovyote vile”.
“Mambo yamemzidi kimo afande, ndiyo maana anahaha kutoroka”.
“Hata hivyo, sidhani kama ana haki ya kuvuka mipaka ya nchi hii akiwa salama. Alikuwa mtu wa kufa. Na nitahakikisha kuwa Serikali ya Burundi inamtia mbaroni ili arejeshwe nchini kusubiri kitanzi chake”.
Inspekta Kombora alikuwa akiilaani bahati yake kimoyomoyo. Alijilaumu kwa kutangaza picha za mtu huyo gazetini. Ingawa hiyo ilikuwa njia yenye uhakika, lakini kwa polisi aliyehitimu, kitendo hicho huwa cha mwisho katika harakati za kumpata mtuhumiwa. Kitendo hicho mara nyingi humfanya mtuhumiwa kujianda kwa mbinu mpya. Ama, mtu kama huyo huweza kutenda uovu zaidi usiotazamika. Inspekta Kombora alifahamu kuwa kufa kwa mwanamke yule, na kuponea chupuchupu kwa dereva taksi, ni matokeo ya picha hizo zilizotokea gazetini. Inspekta Kombora alilaani baada ya kuona mpango wake umesababisha kifo cha mwanamke. Angejitakasa tu kwa kumnasa Proper au kwa kumfumua kichwa chake ‘kibovu’ kwa risasi.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)