SHEREHE KUZIMU (20)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA ISHIRINI
ILIPOISHIA...
Kila mtu alikuwa aking’ata meno kutokana na baridi ilivyokuwa ikipenyeza katika ngozi ya miili yao. Kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inazidi kunyesha ilisababisha msafara uzidi kwenda kwa mwendo wa taratibu sana. Vivian alikuwa katika gari moja ambayo ilikuwa imebeba watu wa familia.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Mama yake pia alikuwepo katika gari hilo. Vivian alikuwa akiwasiliana na mama yake kwa ishara za kishetani ambazo hazikuweza kufahamika na mtu yeyote.

Watu waliokuwa katika misafara walikuwa wakiimba nyimbo za maombolezo.. Nyimbo zile zilisababisha wawe wanajisikia vibaya sana kwasababu roho wa ibilisi alikuwa ndani yao. Kwa mwedo wa taratibu saa saba mchana msafara ulifika katika eneo la makaburi kwaajili ya kufanya maziko. Maziko yalifanyika wakati mvua ikiendelea kunyesha. Kila mtu aliyekuwa msibani alionekana kulowa tepetepe kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Ilipotimu saa kumi na nusu jioni shughuli ya mazishi ilifikia tamati. Ndugu jamaa na marafiki waliokuwa wamemsindikiza Nelson msibani waliingia katika magari yao tayari kwa kuanza safari ya kurudi arusha.

Hadi kufikia muda ule mvua kubwa iliyoambatana na radi pamoja na upepo mkali ilikuwa ikiendelea kunyesha. Baridi iliendelea kupenyeza katika ngozi za waombolezaji na kusababisha wajikunyate kama vikinda vya ndege, vilivyotelekezwa na mama yao. Safari ya kurudi arusha iliendelea taratibu sana kutokana na mvua ambayo ilisababisha jioni ionekane kama usiku, vilevile ukungu mkubwa uliokuwa umetanda barabarani. Maji yalijaa barabarani kutokana na mifereji kujaa maji ya mvua. Mioyo ya wasafiri ilijaa hofu kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea. Vivian na mama yake walionekana kutokuwa na wasiwasi ingawa watu wengine wote walikuwa na mashaka makubwa kutokana na hali ya hewa ilivyokuwa mbaya. Kiukweli mvua ile haikuwa ya kawaida, kwasababu ilisababishwa na Vivian pamoja na mama yake ili waweze kumnasa mchungaji.

Gari la mchungaji lilikuwa ni miongoni mwa magari ambayo yalikuwa mbele ya msafara. Mchungaji alikuwa akiendesha gari lake taratibu na kwa umakini wa hali ya juu. Siti ya pembeni yake alikuwa ameketi mke wake, na siti za nyuma walikuwa wazee wawili wa kanisa. Mchungaji alikuwa akisali kimyakimya ili waweze kufika salama kwasababu hali ya hewa ilikuwa ni mbaya sana. Mama mchungaji pamoja na wazee wa kanisa nao pia walikuwa katika maombi ya kiroho kuiombea safari yao.

Ukimya ulitawala ndani ya magari yaliyokuwa katika msafara. Roho za watu zilikuwa juujuu. Vivian aliendelea kujipanga kutuma shambulizi lake katika gari la mchungaji ili aweze kuitoa roho yake ambayo alikuwa ametumwa kuzimu. Bila kuonekana na mtu yeyote aliendelea kufanya mambo yake ya kichawi ili aweze kufanikisha zoezi zito ambalo lilikuwa mbele yake. Hali ya hewa ilizidi kuwa mbaya, mingurumo ya radi ilichachamaa na kuzidisha hofu ndani uya mioyo ya wasafiri. Kutokana na mvua kuzidi kuwa kubwa ilisababisha msafara kusimama kwa muda kwasababu madereva walishindwa kuona mbele sawasawa. Muda ulizidi kusonga, kwa zaidi ya dakika sitini waliendelea kusubiri mvua ipungue kidogo.

Vivian na mama yake walikuwa wanafurahi kwasababu waliona kama mpaka gari la mchungaji limesimama kwa ajili ya mvua ambayo waliisababisha wao, basi ilikuwa ni dalili ya ushindi kwa Vivian. Baada ya muda mvua ilikatika kwahiyo magari yote yalirudi barabarani na kuendelea na safari. Madereva walionekana kukanyaga mafuta sawasawa kwasababu walikuwa wamechelewa sana. Hata watu waliokuwa ndani ya magari walijaribu kuwahimiza madereva wao kuendesha kwa spidi kubwa kusudi waweze kuwasili mapema. Wamama ndio walioonekana kutamani sana kuwahi nyumbani kwasababu wengi wao walidai kwamba wanahitaji kufika mapema wakaandae chakula cha watoto, kwasababu muda ulikuwa tayari umeshasonga sana.

Vivian aliona bora atumie nafasi ile ili kutimiza alichokuwa amekikusudia. Kwa namna ya kichawi Vivian alituma giza nene katika macho ya dereva wa kosta iliyokuwa ikitoka arusha kwenda Kilimanjaro. Dereva huyo ambae alikuwa anaendesha gari lake kwa mwendo mkali sana alishindwa kulimudu gari lake baada ya macho yake kupata giza la ghafla ambalo lilipelekea gari lake kugongana uso kwa uso na gari la mchungaji. Ilikuwa ni ajali mbaya sana ambayo ilihusisha magari mengine kadhaa ambayo yalikuwa nyuma ya gari la mchungaji. Gari la mchungaji lilipoteza mwonekano kabisa kutokana na ile ajali mbaya iliyokuwa imetokea punde.

Baadhi ya abiria waliokuwa katika daladala walisikika wakipiga kelele wakati ajali ilipokuwa ikitokea. Lakini mara baada ya ajali kutokea ukimya ulitawala. Kelele zilizosikika zilikuwa ni za mashuhuda wa ajali ambao walionekana kusikitika sana kutokana na walichokuwa wanakishuhudia kwa wakati ule. Mwili wa Nelson ulionekana kufa ganzi ghafla, kwasababu alishuhudia ajali ile ilivyokuwa ikitokea. Kwa mawazo yake ya haraka haraka alijua kwamba mchungaji pamoja na watu wote aliokuwa nao garini watakuwa wamepoteza maisha.

Kuzimu ilisimama kwa shangwe baada ya Vivian kufanikiwa kumsababishia mchungaji ajali. Mara baada ya ajali mbaya kutokea Vivian aliwasili ghafla kichawi, jirani na gari la mchungaji ili aweze kuitoa roho ya mchungaji na kuipeleka kuzimu. Katika hali isiyokuwa ya kawaida Vivian aliona kama vile gari la mchungaji limezungukwa na moto ambao ulikuwa unamuunguza. Alishindwa kuelewa ule moto ulikuwa umetoka wapi, alitafakari wakati alipokuwa amesimama umbali wa kama mita kumi na ushee. Alijaribu kutumia nguvu zake kuuzima moto ule lakini haikuwezekana. Alijaribu kila njia ili aweze kusogea karibu na gari la mchungaji lakini moto ulimzuia kabisa. Kilichomstahajabisha zaidi ni kwamba mchungaji na watu wote waliokuwa garini walionekana kutounguzwa na moto ule uliokuwa umezunguka gari lao. Alipoona kwamba ameshindwa kufanikisha zoezi alilokuwa amepewa, alisogelea gari la abiria ili aweze kuchukua roho za watu lakini napo alishindwa kwasababu aliona kuna moto uleule. Alikasirika sana kwasababu kuzimu walikuwa wameshapata uwakika wa damu na nyama kwa ile siku.

Nelson pamoja na watu aliokuwa nao kwenye gari walionekana kuchanganyikiwa. Kila mtu aliweka mikono kichwani kutokana na tukio lililokuwa linaonekana mbele ya macho yao. Ilikuwa ni ajali ambayo ilionekana kugusa mioyo ya watu wengi. Vilio vya wanawake vilitawala baada ya kuona ajali ile ambayo ilikuwa ni ya kuogopesha. Baadhi ya mashuhuda wa ajali ile walishindwa kustahimili kuendelea kuwepo katika eneo la tukio kwahiyo walisogea mbali kabisa na eneo la ajali. Wapo walioonekana kudondoka na kupoteza fahamu hususani wale waliokuwa wanamfahamu mchungaji aliyepata ajali.

Watu wote waliokuwa katika gari la mchungaji walionekana kuwa sawa kabisa japo kuwa gari lilionekana kupondeka mno. Halikadhalika abiria waliokuwa katika gari la abiria pia walionekana kuwa sawa ingawa walipata majeraha ya kawaida sana. Kiukweli ilikuwa ni ajali ambayo ilikuwa ni ya kushangaza sana kwasababu licha ya kwamba ilionekana kuwa ya kutisha lakini hakuna mtu ambae alionekana kupoteza maisha wala kupata majeraha makubwa. Mchungaji na watu waliokuwa wamenasa ndani ya gari lao ambalo lilikuwa limepondwa pondwa walitolewa na wasamaria wema. Watu walifurahi sana baada ya kuona wapo sawa kwasababu ndio walikuwa wanahofiwa kupoteza maisha kutokana na gari lao kuharibika kupita maelezo. Nelson alifurahi sana kumwona mchungaji Eugin Alvin na mke wake ni wazima kabisa. Kunusurika kifo kwa mchungaji na watu wake kulisababisha Nelson aamini kwamba kweli Mungu ni muweza wa mambo yote.

“Hakika uweza wa Mungu haufananishwi na kitu chochote.” Nelson alizungumza na mjomba wake ambae alikuwa akikodoa macho yake kumtazama mchungaji na wenzake ambao walinusurika kufa.

“Kweli kabisa, kwasababu hata mimi sikutegemea kwamba mchungaji na wenzake wangeweza kunusurika kifo katika ajali mbaya kama hii.” Mjomba alizungumza na Nelson huku na yeye akionekana kushtushwa sana na ajali ile.

Gari la polisi lilifika katika eneo la tukio na kukuta umati mkubwa wa watu waliofika eneo la tukio kushuhudia ajali mbaya iliyokuwa imetokea jioni ile. Ambulensi iliwachukuwa majeruhi wote wa ajali ile na kuwakimbiza hospitali kwaajili ya uchunguzi wa kitabibu zaidi. Nelson na wenzake walirudi kwenye gari na safari iliendelea. Kila mtu alisikika akimshukuru Mungu kwa kuweza kunusuru roho za watu waliohusika katika ajali mbaya ya gari. Saa mbili na nusu usiku Nelson pamoja na ndugu jamaa na marafiki waliokuwa wamemsindikiza kumpumzisha mama yake katika nyumba yake ya milele waliwasili jijini arusha. Nelson aliwashukuru sana watu wale ambao walionyesha moyo wa upendo na wa kipekee kushiriki nae katika kipindi kigumu alichokuwa akikipitia. Baada ya hapo kila mtu alikwenda nyumbani kwake akiwa anahisi kuchoka sana kutokana na misukosuko mikubwa waliyokuwa wamekumbana nayo katika safari yao ya kwenda na kurudi msibani.

**********

Vivian alikasirika sana baada ya kushindwa kuipata roho ya mchungaji. Ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kushindwa kutimiza malengo yake. Kilichokuwa kimetokea kilimuumiza sana, alishindwa kuelewa mchungaji Eugin Alivin alikuwa na nguvu gani ambayo haiingiliki. Alifikiri kwa muda mrefu bila kupata jibu kwasababu hakuwahi kukutana na maajabu kama yale ya siku zile. Alishauwa watu wengi sana waliojiita watumishi wa Mungu tena bila changamoto yeyote. Kushindwa kwake kupata roho ya binadamu hata mmoja kwa wakati ule ilisababisha hasira kubwa ndani ya moyo wake. Kuzimu walisikitika sana baada ya Vivian kushindwa kupata damu kwa wakati ule. Malikia mkuu wa kuzimu pia alihuzunika sana baada ya kupokea ripoti kwa Vivian kwamba shambulio la kutoa roho ya mchungaji limeshindikana.

Majeruhi walifikishwa hospitalini na wote waliruhusiwa kuondoka hospitali siku hiyohiyo kwasababu hawakuwa wameumia sana. Mchungaji aligundua ajali ile haikuwa ya kawaida kwahiyo alijua kuna vita vikubwa mbele yake kwahiyo aliendelea kujinyenyekeza mbele za Mungu ili aweze kumshinda adui shetani. Kwanzia siku hiyo mchungaji pamoja na mke wake walianzisha vita vikubwa vya kiroho dhidi ya mwovu shetani.

Kuzimu palikuwa hapakaliki kwasababu muda mwingi vikao vyao vilikuwa vinaharibiwa na maombi ya mchungaji. Japokuwa pamoja na misukosuko mikubwa iliyokuwa inaikumba kuzimu, lakini bado waliendelea na vikao vyao kwa shida ili waweze kumuangusha mchungaji na kanisa lake. Maisha ya Nelson yaliendelea kama kawaida ingawa yalitawaliwa na upweke sana.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi

Chapisha Maoni