SHEREHE KUZIMU (24)

Zephiline F Ezekiel
Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE
ILIPOISHIA...
Mwili wake uliishiwa kabisa nguvu na pia tumbo lilikuwa linanguruma kutokana na wasiwasi mwingi uliokuwa ndani ya mtima wake.

“Unaumwa?” Bi Diana alimuuliza mume wake ambae bado alikuwa anashangaashangaa kama vile abiria aliyeachwa na gari, stendi.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
“Hapana, nipo sawa.”

“Sasa kilichokuangusha na kupoteza fahamu ni kitu gani?” Bi Diana alihoji.

Bashingwa alimsimulia mke wake kila kitu, mpaka ndoto mbaya aliyoiota. Bi Diana alishtuka sana pindi alipokuwa akimsikiliza mume wake akimsimulia ndoto ile iliyokuwa ya kutisha. Mume wake alipomweleza kwamba alipozinduka katika ndoto mbaya aliyokuwa anaiota, hakumkuta kitandani, alipuuzia kwa kuona kwamba, huwenda ndoto ilimchanganya kwasababu yeye alikuwa kitandani amelala. Furaha ya kukamilika kwa mipango ya mauwaji ya wapinzani wao wa kibiashara ilitoweka ghafla ndani ya moyo wa Bashingwa. Mazingaumbwe yaliyomsibu usiku ule, yalisababisha akose raha. Hamu ya kuendelea kulala ilitoweka japokuwa siku hiyo alichelewa sana kulala, kwasababu alichelewa kurudi nyumbani.

Jogoo la la pili lilipowika alikwenda bafuni kuoga ili aweze kwenda kutafuta vijana wa kumsaidia kutekeleza jukumu la mauwaji kama ambavyo walikubaliana na wafanyabiashara wenzake. Ikiwa bado ni alfajiri sana, alimuaga mke wake kwamba anakwenda katika miangaiko yake. Alionekana kuwa na haraka kidogo kuliko siku zote, kwahiyo alitembea kwa mwendo wa fastafasta kutokea chumbani. Alipofika kwenye mlango wa sebuleni alifungua ili aweze kutoka nje kwasababu bado mlango ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Baada ya kufungua mlango Bashingwa alihisi kuchanganyikiwa baada ya kukutana na jeneza lililorembwa, barazani kwake.

Alilitazama jeneza lililokuwa mbele yake kisha akahusianisha na ndoto mbaya aliyoiota usiku na kubaini kwamba maisha yake yalikuwa mashakani. Alishindwa kufahamu jeneza lile limefika vipi pale nyumbani kwakwe wakati nyumba yake imezungukwa na uzio mkubwa halafu isitoshe getini kuna mlinzi. Kwa hasira alimwita mlinzi ili aweze kumuhoji kuhusiana na jeneza lile. Mlinzi alimshangaa sana bosi wake kutokana na suala alilomuitia. Alihisi pengine labda bosi wake amechanganyikiwa kwasababu hakuona jeneza alilokuwa anaonyeshwa na bosi wake. Bashingwa alikasirika na kumzaba kibao cha nguvu mlinzi yule baada ya kuhisi labda anacheza na akili yake.

Pamoja na hayo yote lakini bado haikusaidia, kwasababu mlinzi wa nyumba ile ya kifahari hakufanikiwa kuona jeneza alilokuwa anaonyeshwa na bosi wake. Bashingwa aliingia ndani kwenda kumwita mke wake ili aweze kumwonyesha lile jeneza alilolikuta barazani baada ya kufungua mlango lakini cha kushangaza ni kwamba aliporejea kwa mara nyingine pale barazani hata yeye mwenyewe hakuliona tena lile jeneza. Kwani tayari lilikuwa limeshatoweka.

“Lilikuwa hapa mke wangu.” Bashingwa alizungumza huku akimwonyesha mke wake kwa kidole sehemu ambapo jeneza lilikuwepo.

Bi Diana alishindwa kuelewa mume wake amekumbwa na maswahibu gani, kwasababu tangu usiku alimwona kutokuwa sawa. Kile kilichokuwa kimetokea alfajiri ile, ilikuwa ni jibu tosha kwamba kuna mtu anamfanyia mchezo mchafu. Aliamua kusitisha safari yake ili aweze kutafuta ufumbuzi wa tatizo lililokuwa linamtesa tangu usiku wa kuamkia siku hiyo. Aliamua kwenda kwa mganga wake wa siku zote ili akaweze kuaguliwa. Asubuhi hiyohiyo ikiwa bado hapajapambazuka vema, aliondoka nyumbani kwake na kuelekea kwa mganga wake ambae alikuwa anaishi maeneo ya Nyamagana, lakini kwa bahati mbaya wakati alipokuwa njiani, alipata ajali mbaya ya gari ambayo ilipelekea kifo chake.

********

Vivian aliamua kuwaonyesha yeye ni nani kwasababu walikuwa hawamfahamu vizuri. Walifanya kikao chao cha siri wakiamini kwamba Vivian na mume wake hawatafahamu lolote lililokuwa linaendelea. Lakini haikuwa kweli kwasababu Vivian alikuwa analindwa na majini ambayo ndiyo yaliyompasha habari za njama za yeye na mume wake kutaka kuuwawawa na umoja wa wafanyabiashara wa nguo jijini mwanza. Kwa hasira aliamua kuwatesa wote kwa mauzauza na kisha kuzitoa sadaka roho za kila mmoja halafu damu na nyama zao zikasheherekewa kuzimu. Aliamua kuanza na Bashingwa ambae ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya mauwaji.

Kifo cha Bashingwa kilikuwa kama vile ndiyo imefungulia vifo vya wafanyabiashara wengine, kwasababu kila siku alikuwa anakufa mmoja baada ya mwingine hadi wote walipomalizika. Vifo vya wafanyabiashara wakubwa katika mkoa wa Mwanza iliwahuzunisha watu wengi. Vivian aliwachukua wafanyaabiashara wote kimazingara na kuwapeleka kuzimu ambapo wote waliliwa nyama wakiwa wazima bila kuchinjwa kama vile adhabu. Kila mmoja ambaye alikuwa anafikishwa kuzimu, Vivian alikuwa anaamuru aliwe nyama akiwa mzima. Walikuwa wanakufa vifo vibaya sana kwasababu walinyofolewa minofu hadi umauti ulipokuwa unawafika. Nyama zao zililiwa kwa furaha sana kwasababu vile viumbe vya kule kuzimu walikuwa wanafurahia sana nyama inayoliwa kwa mtindo huo.

********

Nelson alikuwa anasikitika sana alipokuwa akipata taharifa za vifo vya wale wafanyabiashara wenzake. Moyo wake ulijawa na simanzi kuona wafanyabiashara wenzake wakifikwa na umauti kila kukicha tena katika mazingira ya kutatanisha mno. Hakujua kwamba watu waliokuwa wanapoteza maisha walikuwa maadui ambao walikuwa na njama yakuitoa roho yake ndani ya muda mfupi.

*******

Marwa ni kijana wa kikuria ambaye ametokea kumpenda sana Adela. Japokuwa Adela alishamtamkia zaidi ya mara mia kwamba hamtaki na wala hamuhitaji lakini kijana huyo hakuonyesha kukata tamaa. Alijitoa kufa kupona ilimradi Adela awe wake. Hakuwa tayari kumkosa mwanamke ambae mara kwa mara amekuwa akimfanya akose lepe la usingizi. Adela hakutokea kuvutiwa na Marwa hata kidogo licha ya kijana huyo kuonyesha juhudi kubwa za kutaka kuwa nae. Msichana mrembo, Adela alihisi moyo wake unampenda Benedict japokuwa bado hakuwa tayari kuingia katika mahusiano ya kimapenzi kwa muda ule. Kwa jinsi siku zilivyokuwa zinazidi kwenda, ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kunasa katika mitego ya kijana Benedict ambae, alijitahidi kwa uwezo wake wote kumwonyesha ni jinsi gani anavyompenda na kumthamini. Kama wasemavyo waswahili ‘penzi ni kikohozi kulificha huwezi’ Adela alishindwa kuendelea kumsumbua Benedict wakati moyo wake ulikuwa tayari umeshamkubali. Mwishowe alilikubali ombi la Benedict la kutaka wawe wapenzi.

Walifungua ukurasa mpya wa mapenzi uliotawaliwa na bashasha isiyomithilika, ingawa bado walikuwa mbali kijiografia kwani Adela alikuwa kijijini kwao Shinyanga wakati Benedict alikuwa nyumbani kwao Mwanza. Kupigiana simu pamoja na kutumiana jumbe fupi za maandishi kuliongezeka zaidi. Ilikuwa haipiti masaa mawili bila Adela kuzungumza na Benedict. Mwanzoni Benedict ndiye alikuwa na kiherehere cha kumpigia Adela simu pamoja na kumtumia meseji mara kwa mara. Ila mara baada ya Adela kumkubali Benedict awe mpenzi wake alionyesha mapenzi ya dhati yaliyokuwa yamejificha moyoni mwake.

Muda mfupi baada ya ukurasa wa mapenzi kufunguka, matokeo ya kujiunga na kidato cha tano yalitoka ambapo Adela alipata ufaulu mzuri mno na kupangiwa shule ya wasichana ya Machame iliyopo mkoa wa Kilimanjaro. Halikadhalika Benedict naye alipata ufaulu mzuri na kupangiwa shule ya wavulana ya Lyamungo iliyopo mkowa wa Kilimanjaro pia. Adela na Benedict walifurahi sana baada ya kupangiwa shule ambazo zilikuwa mkoa mmoja. Waliona ndio muda muwafaka wa wao kuweza kujinafasi na penzi lao ambalo lilikuwa na mashamsham ya hali ya juu. Tarehe 9 mwezi wa 7 ndio tarehe ambayo vijana wote waliochanguliwa kujiunga na kidato cha tano nchi nzima walihitajika kuripoti katika shule walizopangiwa.

Benedict alimshawishi Adela waondoke Mwanza siku nne kabla shule haijafunguliwa halafu wakifika mkoa wa Kilimanjaro wachukue nyumba ya wageni wajinafasi hadi siku ya kuripoti shuleni itakapofika. Benedict alikata tiketi yake pamoja na ya mpenzi wake katika basi la Fresh Coach linalofanya safari zake mwanza na Arusha kupitia Shinyanga. Basi lilipofika Shinyanga Adela pamoja na abiria wengine walipanda kwenye basi na safari iliendelea. Ilikuwa ni safari ya furaha sana kwa wawili hawa ambao walipendana mithili ya kumbikumbi. Walipofika mkoa wa Arusha walichuku usafiri mwingine ambao uliwapeleka moja kwa moja hadi mkoani Kilimanjaro. Mara baada ya kufika mkoa wa Kilimanjaro walipokelewa na mvua ya manyunyu iliyoambatana na baridi kali ambayo ilisababisha kila mmoja ahisi kutetemeka mwili. Walifikia katika nyumba mmoja ya wageni iliyopo mjini moshi maarufu kwa jina la Kibo guest house. Adela alikuwa amedhamiria usichana wake utolewe na Benedict kwasababu moyo wake ulitokea kumpenda kupita maelezo.

Marwa alibaki katika wakati mgumu sana kwasababu Adela aliondoka bila kumuaga. Kwa takribani siku nzima baada ya kupata taarifa ya safari ya Adela, alikosa kabisa raha kutokana na mawazo lukuki ndani ya ubongo wake. Safari ya Adela ya kimyakimya lilikuwa ni jibu tosha kwamba hapendwi na wala haitajiki. Muda mwingi amekuwa akitafakari mbinu mbalimbali za kumuwezesha kunasa mapenzini na Adela bila mafanikio. Ni dhahiri kwa kitambo kirefu amekuwa akijinyenyekeza kwa Adela lakini mwisho wa siku amekuwa akiambulia majibu ya mkato, ambayo yamekuwa yakiujeruhi moyo wake kila iitwapo leo. Marwa alijaribu kufanya upelelezi wa chini kwa chini kutoka kwa marafiki wa karibu wa Adela na kubaini kuwa sababu kubwa ya yeye kutoswa kila mara ni kwasababu ya kijana Benedict.

Marwa anakasirika sana baada ya kugundua kuwa, kuna mwanaume ambaye ndie anasababisha Adela asiweze kumsikiliza na kumwelewa. Hivyo basi moyo wake unajenga chuki na hasira dhidi ya kijana huyu ambae ndiye amekuwa kikwazo cha yeye kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na Adela. Ndani ya masaa 24 ubongo wake ulikuwa bize ukitafakari kwa kina huyu Benedict amempa nini Adela kiasi kwamba asisikie wala asione kwingine. Katika kuwaza kwake kwa muda mrefu alipata wazo la kumuangamiza Benedict. Aliapa kwenda kwa mganga kumloga Benedict afe ili aweze kuung’oa mchuma.

Kijana huyu wa kikurya anafunga safari ya kwenda kwa mganga mmoja ambaye amekuwa akiwapa ushindi wa mara kwa mara katika timu yao ya mpira wa miguu pale kijijini kwao. Mganga huyu ndiye anayesifika kwa kuwa fundi wa mafundi mkoani Shinyanga. Katika historia ya mganga huyu inasemekana aliwahi kuhamishia mlima Kilimanjaro mkoani kwake kwa muda wa masaa matatu. Ahmedi Juma, ndiyo jina la mganga huyu, japokuwa watu wengi wanamfahamu kwa jina la Kiboko, kutokana na sifa yake ya kutokushindwa na jambo.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi

Chapisha Maoni