
Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Sambamba na hilo, Vivian alipaswa kutoa kafara ya watu wasiopungua 300 kama kuonyesha heshima kwa malikia ambaye amekubali kumuachia kiti kwa hiyari. Bila wasiwasi wala kusita, Vivian anakubaliana na vigezo vyote alivyoelezwa na malikia ili ndoa yake iweze kufungwa na hatimaye akabidhiwe cheo.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Kwahiyo Vivian aliamua atumie njia ya tetemeko la ardhi katika kupata idadi ya roho alizotumwa kwa wakati muwafaka. Hiyo ndiyo ikawa chanzo cha kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi mkoani Kilimanjaro, ambalo lilimuhusisha Benedict ambaye nae amekusudiwa afe kutokana na tukio hilo. Idadi ya watu waliokuwa wamekusudiwa katika kafara hiyo inaonekana kutimia kabisa, kwani jumla ya watu 300 waliripotiwa kupoteza maisha katika tukio hilo la kiistoria.
Fikra za Nelson zilizidi kusumbuka kwa mawazo dhidi ya mtoto wake wa pekee, aliyebakiwa nae baada ya wengine kufa katika mazingira ya kutatanisha. Hakujua atakuwa katika hali gani endapo atapata taarifa kwamba mwanae wa pekee atakuwa kapoteza maisha. Misukosuko ya mawazo katika akili yake ilipelekea vidonda vya tumbo kuanza kumsumbua kwa mara nyingine. Upweke usioelezeka uliokuwa umemkumba, unasababisha anashindwa kuvumilia kuendelea kusikia habari zile kwenye vyombo vya habari, kwahiyo anaamua kufunga safari kwenda hospitali ya KCMC kumtafuta mwanae ili aweze kujua kama ni majeruhi au tayari ni maiti. Siku iliyofuata majira ya saa nne asubuhi, Nelson alichukua usafiri wa ndege kutoka mwanza hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA.
Baada ya hapo alichukua tax ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi hospitalini. Anafika hospitalini na kujaribu kupitia katika kitabu cha maiti ambao wametambulika lakini anakosa jina la mwanae. Anaamua kuchukua jukumu la kwenda kukagua miili ya wahanga wote wa tetemeko la ardhi, lakini napo pia anashindwa kufanikiwa kumuona mwanae. Kitendo cha kumkosa mwanae katika idadi ya watu waliopoteza maisha inasukuma hisia zake kuwaza kwamba huwenda mwanae ni majeruhi, hivyobasi anaanza kupita wodi moja baada ya nyingine ambapo napo anashindwa kufanikiwa kumpata mwanae. Moyo wake unazidi kuwa matatani kwa kuwaza ni wapi ambapo mwanae alipo.
“Au mwili wa mwanangu haujapatikana katika vifusi?” Nelson aliwaza kwa maumivu makubwa moyoni, ambayo yalipelekea macho yake kudondosha machozi.
Nelson alikuwa katika wakati mgumu kupitiliza, hata hivyo uvumilivu anaouonyesha ka sasa ni kwasababu ni mwanaume, ingekuwa ni mwanamke ingemuwia vigumu sana kuvumilia hali ambayo Nelson anaipitia. Anashindwa kuelewa afanye nini ili aweze kufahamu kama kweli mwanae ni mzima au ndio tayari marehemu. Anaonekana kuchoka mwili na akili vyote kwa pamoja.
*********
Baada ya Benedict kufanyiwa vipimo vya CT SCAN pamoja na MRI, ilibainika kwamba amevunjika sehemu mbalimbali za mwili wake. Kwahiyo waliamua kumpa uhamisho wa haraka kumpeleka katika Taasisi ya tiba ya mifupa Muhimbili (MOI). Hali yake bado ni mbaya sana na ndiyo sababu iliyopelekea kufanyiwa uhamisho wa haraka haraka, ili kuokoa maisha yake. Kiukweli kwa jinsi hali yake ilivyo tete ni Mungu wa Isaka na Yakobo asimame kumtetea kwasababu yupo katika hali ya kuvunja moyo mno.
Kidogo hali ya Adela inaendelea vizuri ingawa bado fahamu hazijamrejea. Bado yupo chini ya uangalizi wa madaktari kusudi hali yake iweze kuhimarika. Hakuna ndugu yake hata mmoja aliyeweza kufahamu kuwa amepatwa na matatizo. Kibaya zaidi, baba yake Benedict wala hamfahamu, kwasababu huwenda angeweza kuonyesha ushirikiano baada ya kumkuta wodini akiwa hoi bin taabani. Chakutia moyo katika hali yake ni kwamba vipimo ya daktari vimebaini kuwa licha ya kugongwa na kitu kizito kichwani lakini ubongo wake haujaathirika kwa kiasi cha kumletea madhara baadae.
Maandalizi ya harusi ya Vivian na Nelson kule kuzimu yalikaamilika, ingawa Nelson hakuwa akijua chochote kilichokuwa kikiendelea dhidi yake. Laiti kama angejua mipango ya mke wake, sio ajabu angeweza kupata ujasiri wa kumuuwa bila huruma. Harusi ya Vivian ilionekana kuandaliwa kwa mbwembwe zote kwasababu malikia alikuwa anampenda Vivian kupita maelezo. Kamati ya maandalizi ya harusi hiyo ilionyesha kujipanga sawasawa, kwani wako maajenti ambao walipangiwa majukumu ya kwenda duniani kuchukua mimba changa za kwenda kuliwa siku hiyo.
Lakini pia kwa wakati huohuo wako maajenti ambao walikuwa na majukumu ya kwenda duniani kuchukua damu za watu, kwaajili ya kunyweka katika siku hiyo ya harusi. Jumla ya mapipa 50 yalitakiwa kujazwa damu za watu ambayo itanyweka siku ya sherehe kuzimu. Maajenti wa kuzimu walitega mitego yao katika kona mbalimbali ili waweze kupata damu ya kwenda kunyweka siku ya tukio. Hayo yote yatatimia mara baada ya kifo cha Benedict ambaye ndiye amekusudiwa kuwa kafara ya ndoa ya wazazi wake. Roho za mauti zinamuandama ili ziweze kumshinda. Majini wanaiandama roho yake usiku na mchana ili waweze kuitoa lakini inaaonekana kushindikana.
Nguvu ya maombi inayofanywa na watu mbalimbali kuwaombea majeruhi wa tetemeko la ardhi, ndiyo inayopelekea majini yaliyotumwa roho ya Benedict kushindwa kufanya kama ambavyo wametumwa. Majeruhi wote wa ajali hii wamezungukwa na ukuta mkubwa wa maombi ya waumini, mapadri pamoja na mashehe ambao wamejitokeza kuwaombea heri mbele za Mungu. Kwahiyo Benedict yupo katika hali ya hatari mno kwani endapo maombi yatapungua basi roho yake itakuwa sadaka ya mashetani. Ingawa hali yake inaonekana kuwa mbaya sana ila nguvu ya maombi inasaidia kumnusuru asinyakuliwe na pepo la umauti.
*********
Baada ya Nelson kumsaka mwanae katika wodi mbalimbali bila mafanikio, akili yake ilizidi kukaribisha hali ya uchizi. Kwani alisikika akizungumza peke yake mithili ya mtu alirukwa na akili.
“Ee Mungu wa mbinguni, ninakuomba unionyeshe alipo mtoto wangu.” Nelson alizungumza kwa sauti kubwa, peke yake wakati alipokuwa kwenye moja ya wodi ya wagonjwa mahututi, jambo ambalo lilipelekea atolewe nje haraka ili kuepuka usumbufu kwa wagonjwa ambao walikuwa katika hali mbaya.
Ubongo wa Nelson ulikuwa kama vile umepata gazi, kwasababu baada yaa kutolewa nje ya wodi alibaki amesimama huku akishangaa shangaa kama vile mtu aliyepotewa na fahamu. Hali yake inasababisha dokta Millan Wanjau kulazimika kumsaidia zaidi, kwa kumchukua na kumkalisha katika benchi iliyokuwa nje ya wodi kisha akamuhoji maswali mawili matatu. Kutokana na maelezo dokta Millan aliyoyapata kutoka kwa Nelson, analazimika kwenda nae hadi kwenye ofisi ya mganga mkuu ili akaonyeshwe picha ya mgonjwa ambaye amehamishwa hospitalini hapo siku hiyo kwasababu ya kwenda kupatiwa matibabu zaidi katika hospitali ya taifa ya Muhimbili. Kwahiyo mgonjwa alipigwa picha ili iwe rahisi kwa ndugu zake kufahamu alipo endapo watafika hospitalini hapo kumtafuta.
Nelson huku akijihisi kutokuwa na nguvu aliongozana na daktari huyo hadi kwenye ofisi ya mganga mkuu ambapo pia hawakumkuta kwa muda huo. Daktari Millan alimtaka Nelson kukaa kwenye benchi iliyokuwa nje ya ofisi hiyo hadi mganga mkuu atakaporudi. Baada ya kama kakika 15 wakati Nelson akiwa amekaa kwenye benchi kichwa chake amekilaza juu ya magoti yake kwa mawazo, ghafla alisikia kelele la ufunguo unaolazimishwa kuingizwa ndani ya kitasa cha mlango ili mlango uweze kufunguliwa.
Nelson alizinduka kutoka katika dimbwi la mawazo lililokuwa linamzamisha. Macho yake yalikutana na Mama mmoja wa makamo, aliyevaa miwani, ambae alikuwa ni mrefu mweusi na mwembamba kiasi. Kabla Nelson hajamsalimia mlango ulifunguka na mama huyo aliingia ndani. Bila kupoteza muda Nelson aliingia ofisini humo ili aweze kusaidiwa shida yake. Baada ya salamu daktari huyo alimwonyesha Nelson picha ya mgonjwa ambaye alizidiwa na kusababisha kuhamishiwa hospitali ya taifa ya Muhimbili katika kitengo cha Mifupa (MOI).
Macho ya Nelson yaliganda katika picha iliyokuwa inaonyesha sura ya mwanae ambaye anaonekana kupumulia mashine kutokana na hali yake kuwa mbaya sana. Moyo wa Nelson unapata maumivu makubwa sana ambayo yanapelekea machozi kutengeneza njia katika mashavu yake. Mganga mkuu anajitahidi kumsihi Nelson ajikaze kiume kwani ndivyo maisha yalivyo. Nelson anaonekana kuumizwa sana na hali ya mwanae aliyemuona kwenye picha. Anafanya malipo ya awali hospitalini hapo kisha anapewa utaratibu wa kwenda kumpata mwanae hospitali ya Muhimbili. Kama wasemavyo waswahili ‘uchungu wa mwana aujuae ni mzazi’ Nelson anaamua kusafiri siku hiyohiyo kwa ndege ya abiria ya saa mbili usiku kutoka KIA kwenda dare s salaam.
Majira ya saa nne usiku, Nelson aliwasili dare s salaam kwa ndege aina ya Fastjet. Aliposhuka kwenye ndege alichukua tax ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi maeneo ya muhimbili. Kwavile muda ulikuwa umesonga sana, ilimbidi alale gesti hadi siku inayofuata, ndiyo aweze kwenda hospitali. Tumbo la Nelson lilikuwa linanguruma kwa sauti kubwa. Hiyo yote ni kwasababu kwa siku nzima hakuweza kula kitu chochote.
Tumbo lake lilikuwa linahitaji chakula lakini msongo wa mawazo aliyokuwa nayo, ilimpotezea kabisa hamu ya chakula. Bila kuoga wala kula, alijitupa kitandani na kisha kutekwa na mawazo mazito. Adhana ya alfajiri, ilisikika wakati Nelson akiwa bado hajapata lepe la usingizi. Anashuka kitandani na kuchukua viatu vyake vilivyokuwa uvunguni mwa kitanda kisha kuvivaa.
Huku akijinyoosha na kupiga miayo kila mara, Nelson anasikika akisonya kwa nguvu baada ya kuhisi maumivu ya kichwa ikiambatana na maumivu makali ya tumbo. Licha ya kuamka na uchovu mwingi lakini bado anaona suala la kwenda bafuni kuoga litampotezea muda wa kufika hospitali.
Kwahiyo anaamua kuondoka chumbani mule na kisha kuelekea katika hospitali ya Muhimbili ambayo ipo mita kadhaa kutoka katika gesti aliyolala. Maumivu ya tumbo yanazidi kupamba moto na kumsababishia maumivu makali mithili ya mtu aliyemeza vipande vidogovidogo vya chupa. Hata hivyo anajikaza kiume na kuzidi kusonga mbele kufuata barabara ya kumfikisha hospitali. Dakika kumi na tano baadae alifika hospitali huku akizidi kujihisi maumivu makali ya tumbo pamoja na kichwa.
Baada ya kujieleza kwa muudumu wa mapokezi, kwamba mwanae amefikishwa hospitalini hapo jana yake, kwa rufaa ya hospitali ya KCMC. Alipewa maelekezo ya kumfikisha katika wodi aliyolazwa mwanae. Baada ya kufika ghorofa ya tatu, Nelson alikuwa akihema kwa kasi sana kwasababu ngazi zilikuwa zimemchosha halafu maumivu bado yalikuwa yanamuandama.
Kwa jinsi alivyokuwa anajihisi vibaya, aliinama akiwa ameshika magoti kwa uchovu huku akisikilizia jinsi moyo ulivyokuwa ukimwenda mbio.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi