Notification
Tidak ada notifikasi baru.

SHEREHE KUZIMU (31)

Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA THELATHINI NA MOJA
ILIPOISHIA...
Mama Vivian ndiye aliyekabidhiwa jukumu la kuhakikisha kwamba mjukuu wake anafanyika kafara kuzimu. Jukumu hilo lilimuangukia mama huyo, baada ya kuomba aweze kumsaidia binti yake kutekeleza kafara hiyo kwavile imeonekana kumsumbua kichwa kwa muda mrefu.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Mama huyo amediriki kujitoa kutoa msaada kwavile ana majini wake ambao hawakuwahi kumuangusha katika kazi yeyote.

Malikia mkuu wa kuzimu anakubaliana na ombi la mama huyo kumtoa mjukuu wake kafara. Hapakuwa na jambo lolote lililokuwa likizuia harusi hiyo kufungwa isipokuwa Benedict ambaye amezungukwa na nguvu fulani ambayo walishindwa kuelewa ni nguvu ya namna gani.

Roho ya Benedict ilianza kuwindwa kwa mara nyingine na majini ya bibi yake. Siku tatu mfululizo kijana huyu alikuwa matatani kwavile alinasa katika mtego wa jeshi kubwa la majini. Hata hivyo majini hayo yanashindwa kufanikisha zoezi hilo bila kujua nguvu iliyokuwa ikimlinda mtu huyo.

Uongozi wa kuzimu unakasirika sana kwasababu zoezi hilo linaonekana kutofanikiwa kwa muda mrefu. Kikao kingine cha ghafla kinaitishwa kuzimu kisha kunajadiliwa mbinu nyingine ambayo waliamini ikishindikana watatafuta njia mbadala. Ilikubalika kwamba Benedict atumiwe jini la ukichaa ambalo litamfanya anyanyuke kitandani na kukimbilia barabarani kugongwa na gari.

Maafikiano hayo yalipofikia tamati, kweli lilitumwa jini hilo ambalo linaaminika kuwa na nguvu za ajabu.

Ghafla katika hali isiyokuwa ya kawaida, mgonjwa alipata fahamu iliyoambatana na nguvu kubwa ya mwili. Aliondoa mashine ya oxygen iliyokuwa inamwezesha kupumua barabara, kisha akachomoa na mrija wa dripu uliyokuwa mkononi. Baada ya hapo alianza kutoka mbio kuelekea nje ya wodi mithili ya mtu aliyechanganyikiwa.

Cha kushangaza ni kwamba hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona akinyanyuka kitandani japokuwa pale wodini kulikuwa kuna wauguzi na madaktari pamoja na mlinzi wa wodi yake. Kitandani alionekana Benedict akiwa hoi, lakini Benedict halisi alikuwa tayari ameshanyanyuka na kutoka nje mbio kutokana na jini lililokuwa limemvaa.

Kwa maana hiyo Benedict aliyetoka kimazingara, endapo angekumbwa na umauti huko alipo basi kile kivuli kilicholala pale kitandani kingeonekana kukata roho.

Kwa mwendo mkali kama wa umeme, Benedict alitoka mbio kuelekea barabarani. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaona kilichokuwa kikiendelea isipokuwa katika ulimwengu wa roho pekee. Baada ya dakika chache alifika barabarani ambapo magari yalikuwa yanakwenda kasi sana. Jini lililokuwa linamwendesha lilimsukuma kuingia barabarani wakati gari dogo lilipokuwa likipita kwa mwendo mkali sana.

Benedict alijitupa barabarani wakati gari dogo aina ya Toyota land cruiser, lilipokuwa likipita kwa mwendo mkali. Wakati alipokuwa tayari ameshajitupa barabani mita kama tano na ushee ndo dereva alishtukia kuna mtu amesimama barabarani. Hapakuwa na namna ya kuweza kuchuna breki za papo kwa hapo kwasababu gari lilikuwa likikimbia sana.

“Shindwa shetani!” Dereva alizungumza maneno hayo kwasababu aliona tukio lililokuwa mbele yake halikuwa la kawaida.

Dereva alipata ujasiri wa kuendelea kulihimili gari lake bila wasiwasi wowote. Hakufunga breki wala hakuwaza kufanya hivyo, zaidi sana aliendelea kuliendesha gari lake kama kawaida. Baada ya zile mita tano alizokuwa ameona mtu, gari lake halikugonga kitu chochote, jambo ambalo lilimshangaza sana. Alipohakikisha amevuka lile eneo salama alilisimamisha gari lake pembeni na kisha kurudi kwa miguu hadi kwenye lile eneo alilokuwa ameona mtu. Hapakuonekana kuwa na kitu chochote kilichogongwa.

Dereva yule alikuwa anawaendesha masista wa kanisa katoliki. Hata aliposimamisha gari pembeni ya barabara hakuwa amezungumza kitu chochote na masista waliokuwa ndani ya gari. Baada ya kuhakikisha kwamba hajangonga mtu yeyote alirudi kwa furaha ndani ya gari na kuwaeleza masista jambo ambalo alikuwa ameliona muda mfupi uliopita.

Masista walirudi katika eneo lile na kisha wakanyunyiza maji ya baraka na kisha wakarudi ndani ya gari na kuendelea na safari.

Dereva aliendelea kumshukuru Mungu kimya kimya wakati alipokuwa kwenye uskani wake. Alichokuwa amekiona siku hiyo amezoea kusimuliwa na madereva wenzake ambao mara kwa mara wamekuwa wakikutana na matukio kama hayo pindi wawapo safarini.

Benedict aliyekuwa na jini ndani yake, mara baada ya kusikia lile neno ‘Shindwa shetani’ alipotea ghafla katika lile eneo la hatari. Macho yake yalikuwa yakishuhudia gari lililokuwa limemfikia pale katikati ya barabara. Bila kujua namna ya kuweza kujitetea katika bonde lile la umauti, alitoweka ghafla bila kujua nguvu iliyoweza kumtoa pale barabarani.

Ile nguvu iliyomnyanyua katika lile eneo la hatari ilimtupa upande wa pili wa barabara. Alitua pembezoni mwa barabara mithili ya karatasi iliyokuwa inapeperushwa na upepo. Macho yalikuwa yanamtoka sana kwavile alikuwa haamini kilichokuwa kimetokea. Aliona lile eneo linajoto isiyokuwa ya kawaida kwahiyo alinyanyuka na kuanza kukimbia kukaa mbali na barabara.

Lile jini lililokuwa ndani ya Benedict lilihisi hali ya hatari pale barabarani. Yale maji ya baraka yaliyokuwa yamenyunyizwa yalikuwa yanamuunguza. Ndiyo maana akaunyanyua mwili wa Benedict pale kando kando ya barabara na kisha kukaa mbali na barabara. Hakuamini kilichokuwa kimetokea hata hivyo hakutamani kurudia tena kufanya jaribio la kumuuwa Benedict. Jini lile lilipata msukumo wa kumrudisha Benedict wodini. Lilifanya hivyo haraka sana bila kujua nguvu iliyokuwa inamsukuma kuondoka ndani ya nafsi ya Benedict.

Baada ya nafsi ya Benedict kurudishwa hospitalini pale, fahamu zilimrejea baada ya muda mfupi. Hali yake ilianza kuhimarika kwa kasi. Waugusi waliokuwa wodini, walishangazwa sana kwa namna ambavyo mgonjwa yule alikuwa akipata ahueni.

******

Nelson aliendela kusota maabusu, kwasababu kesi yake ilikuwa inapigwa kalenda kila siku. Mawazo yaliendelea kuusumbua ubongo wake kutokana na matatizo aliyokuwa anapitia. Kibaya zaidi ni kwamba hata taarifa ya vifo vya watoto wa mjomba wake hakuwa amepata.

Siku moja wakati alipokuwa gerezani, alikuwa akiwaza hatma ya maisha yake itakuwaje. Hakujua kesi inayomkabili itamfikisha wapi na pia hakufahamu mwanae yupo katika hali gani kutokana na kile kisu alichokuwa amechomwa. Moyo ulimuuma sana kwavile hakuwa na ndugu wala jamaa wa kuweza kumsaidia katika majaribu yaliyokuwa yanamuandama.

Alitamani mama yake mzazi angekuwa hai angalau angeweza kumsaidia hata mawazo. Mjomba ambaye naye alimsaidia tangu akiwa mdogo tayari alikuwa ameshakufa. Alihisi kama vile dunia imemtenga kwasababu hakua na ndugu yeyote wa karibu wa kuweza kumsaidia katika matatizo. Alijaribu kuwaza mustakabali wa maisha yake na kuishia kudondokwa na machozi.

Ndani ya gereza alipata rafiki mmoja ambaye alifahamika kwa jina la Isaka. Rafiki huyu alikuwa ni mcha Mungu. Wafungwa wengine walikuwa wanamuita Paster kutokana na tabia yake ya kuhubiri neno la Mungu kila wakati gerezani mule. Isaka alitokea kuwa rafiki na Nelson kwavile alikuwa akimfariji mara kwa mara pindi alipokuwa akimwaga machozi karibu kila siku.

Pamoja na kwamba Isaka alimsihi sana Nelson amrudie Mungu, lakini ilionekana kuwa ngumu sana kwake. Moyo wa Nelson ulijawa na lawama nyingi sana kwa Mungu kutokana na magumu mengi yaliyokuwa yanamkuta.

“Wewe unaniambia habari za Mungu gani ambaye hanisikii wala hanioni katika magumu ninayopitia. Pamoja na kumuomba kote huko lakini bado aliruhusu watoto wangu wakafa. Haikutosha mama yangu pamoja na mjomba wangu nao ni marehemu. Mtoto mmoja niliebakiwa naye sijui hata kama ni mzima hadi hivi sasa. Naishi duniani kama vile nimelaaniwa, halafu unanieleza habari za Mungu ambaye ni mbaguzi. Naomba uachane na mimi kabisa acha nife na shida zangu lakini sio kusikia hizo habari zako za kusadikika.” Nelson alizungumza na Isaka maneno mazito namna hiyo.

“Nelson neno la Mungu katika kitabu cha Yeremia 33:3 linasema hivi; ‘Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. Maana yake ni kwamba endapo tutamwamini yeye na kumwita katika matatizo yetu, basi atatuitikia na kutuvusha katika magumu tunayopitia.”

“Isaka, acha unafiki, sasa kwanini usimwite huyo Mungu aje kukutoa gerezani?” Ujumbe wa Mungu kupitia mtumishi wake Isaka haukumwingia vema Nelson. Kwahiyo Mungu aliendela kumtumia Isaka kunena na Nelson.

“Baadhi ya mambo mazito yanayotokea maishani mwetu yanatokea kwa kusudi fulani. Wakati mwingine Mungu uruhusu majaribu yatujie ili kupima imani zetu. Hata mimi kuletwa gerezani, ninaimani ni jaribu tu, ambalo nitalishinda kwa jina la Yesu kristo.” Isaka alisikika.

Nelson alikosa neno la kuzungumza kwahiyo alikaa kimya akiendelea kutafakari maaneno yale ya mtumishi wa Bwana. Maongezi yao yalizidi kushika atamu gerezani mule.

“Mungu ananena nasi kupitia Mathayo Mtakatifu ule mlango wa 11 mstari wa 28-29 ‘Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” Ndugu yangu, embu fikiri mara mbili mbili jinsi upendo wa Mungu ulivyo mkuu kwetu. Anakutaka umkabidhi mizigo mizito iliyokuelemea ili upate kupumzika. Kwanini ukubali kuendelea kuteswa na shetani? Kubali kuzaliwa kwa mara ya pili, ili uweze kupata furaha nafsini mwako.” Isaka aliendelea kupambana na roho ya kukata tamaa iliyokuwa imemvaa Nelson.

Nelson alihusianisha mapito yake na yale maneno ya mtumishi wa Bwana na kuishia kulia kama kichanga. Mtumishi aliendelea kumtia moyo, hatimaye alimuongoza sala ya toba, ikawa mwanzo wa Nelson kumpokea Bwana Yesu ndani ya maisha yake.

Nelson alianza maisha mapya ndani ya gereza.

Mapambio ya sifa yalitia fora. Ilikuwa ni mwendo wa kusifu na kuabudu kama Paulo na Sila walivyokuwa gerezani. Upako wa roho mtakatifu ulifunika gereza. Wafungwa wengi walikubali kuokoka kwa vile neno la Mungu lililokuwa linahubiriwa liliwabadilisha kwa kiasi kikubwa.

Wiki mbili baadaye Isaka aliachiliwa huru, baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha katika kesi ya ubakaji iliyokuwa inamkabili. Kuondoka kwake ndani ya gereza kulisababisha huzuni kubwa kwa wafungwa. Wengine walidiriki kulia machozi baada ya Isaka kuondoka. Hata hivyo huzuni yao haikudumu kwani walikumbuka kuwa yupo mtumishi wa Mungu, mwingine ambaye ni Nelson.

Neno la Mungu liliendelea kuhubiriwa ndani ya gereza na mtumishi wake, Nelson.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Sherehe Kuzimu
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni