Notification
Tidak ada notifikasi baru.

SHEREHE KUZIMU (32)

Mtunzi: Frank Silaa

SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI
ILIPOISHIA...
Hata hivyo huzuni yao haikudumu kwani walikumbuka kuwa yupo mtumishi wa Mungu, mwingine ambaye ni Nelson.

Neno la Mungu liliendelea kuhubiriwa ndani ya gereza na mtumishi wake, Nelson.

KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA NAYO...
Makumi kwa mamia walizidi kufunguliwa katika vifungo vya shetani.

Baada ya miezi minne baadae, Nelson naye aliachiliwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha dhidi ya kesi ya shambulio la mauwaji lililokuwa linamkabili. Kufikia muda huo tayari kulikuwa kumeshapatikana kwa watu wengine wa kuweza kuwaongoza wafungwa katika njia ya kuutafuta uzima wa milele.

Nelson alipotoka gerezani jambo la kwanza alimtafuta mke wake ili aweze kufahamu habari za nyumbani kwake. Alifurahi sana alipojulishwa kwamba mwane Benedict yupo nyumbani anaendelea vizuri. Kiukweli alifurahi sana na kumshukuru Mungu. Baada ya hapo siku iliyofuata asubuhi na mapema alifunga safari kutokea stendi ya mabasi ubungo, kuelekea mkoani Mbeya kuonana na Isaka. Alisafiri salama na kufika stendi ya mabasi ya mbeya usiku. Kwa vile walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu, Isaka alifika mapema ili kuweza kumlaki. Nelson aliposhuka garini alikutana na Isaka kisha wakakumbatiana kwa furaha sana. Baada ya salamu walikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Isaka.

Walipofika nyumbani, Nelson alikuta wageni wengi, ambao alitambulishwa kuwa wanatokea Uingereza kwenye taasisi moja binafsi lijulikanalo kwa jina la ‘Spiritual health.’ Katika maelezo aliyopewa Nelson ni kwamba taasisi hiyo inajishughulisha na kutoa misaada ya ujenzi wa makanisa katika nchi zinazoendelea. Pia wanatoa misaada ya kuwasomesha watoto ikiwa ni sambamba na kuwajenga kiroho katika shule zao za seminari zilizopo ulaya.

Watoto wawili wa Isaka ambao ni John na Peter wapo nje ya nchi wanasomeshwa na taasisi hiyo.

Walizungumza mengi sana usiku huo. Nelson alipata wasaa wa kutoa ushuhuda wake ambao uliwagusa kwa kiasi kikubwa wageni wale. Mkurugenzi wa taasisi hiyo Mr Lee alidondokwa na machozi tangu Nelson alipoanza kusimulia ushuhuda wake hadi mwisho. Tamati ya simulizi ya Nelson ilipelekea watu wote waliokuwa wakimsikiliza kupanguza machozi yaliyokuwa yakiwatoka mfululizo. Kwa kuwa muda ulikuwa umesonga sana, walikwenda kulala.

Ugeni mkubwa uliokuwa umekusanyika nyumbani kwa Isaka, ni kwasababu kesho yake ilikuwa ni siku ya uzinduzi wa kanisa ambalo limejengwa na ile taasisi. Kanisa hilo litakuwa chini ya mchungaji Isaka. Palipokucha mchungaji Harris Phillips, ambaye alikuwa mgeni rasmi kutoka Uingereza aliongoza shughuli nzima ya uzinduzi wa kanisa.

Ilikuwa ni siku ya furaha sana. Waumini wa kanisa la Isaka walijawa na furaha kubwa kwavile walipata mahala pema pa kufanyia ibada. Mwanzoni walikuwa wakiabudu katika jengo ambalo halikuwa hata na paa. Lakini sasa wamepata jengo jipya na la kisasa kabisa. Baada ya uzinduzi walikula na kunywa vilivyokuwa vimeandaliwa palepale kanisani.

Siku moja baadaye Mr Lee na wenzake walifunga safari ya kurudi nchini Uingereza kuendelea na majukumu mengine. Mkurugenzi huyo alimwahidi Nelson kuwa atamtafuta siku chache za mbeleni kusudi waweze kufahamiana zaidi. Ilikuwa ni furaha kubwa kwake kuweza kukutana na kufahamiana na raia wale wa nchini Uingereza.

Nelson alimshukuru Mungu kwa kumkutanisha na rafiki mwema maishani mwake, Isaka. Alifurahi zaidi na zaidi kushiriki katika uzinduzi wa jengo hilo la kanisa. Baada ya hapo na yeye alisafiri kuelekea nyumbani kwake mkoani Mwanza. Aliwasili salama nyumbani kwake na kupokelewa na mke wake na mwanae Benedict. Alifurahi sana alipomtazama mwanae na kumwona ni mzima na mwenye furaha.

Aliamini kupona kwake ni kwasababu ya uweza wa Mungu pekee na sio madaktari wala wauguzi. Alipiga magoti chini kisha akamshukuru Mungu wa mbinguni kwa kumponya mwanae, ambaye hali yake ilikuwa ni mbaya sana.

Vivian alishangaa kumuona mume wake anapiga maombi yasiyokuwa na mfano pale nyumbani. Licha ya kushangaa lakini pia alishikwa na hasira baada ya kusikia mume wake akitamka jina ambalo lilikuwa linamfanya apoteze nguvu na kuhisi kuungua.

Alipoona moto unazidi kumuwakia aliamua kuondoka mahali pale wakati Nelson alipokuwa anazidi kuchapa maombi kwa kwenda mbele. Robo saa ilipopita Nelson alifumbua macho yake baada ya kumaliza sala, na kukuta mke wake hayupo.

Nelson hakujali sana mke wake kutoweka wakati walipokuwa wakisali. Alijipa moyo labda pengine kwasababu utaratibu ulikuwa mpya na pia hakuwa amemweleza chochote kuhusu mabadiliko makubwa maishani mwake.

Usiku muda wa chakula Nelson aliamua kutumia nafasi ile kuzungumza na mke wake pamoja na mwanae.

“Jamani, nimechukua uamuzi wa kumpokea Mungu ndani ya maisha yangu kwa maana neno lake kupitia zaburi 25: 2 inasema hivi; ‘Ee Mungu wangu, nimekutumaini wewe nisiabike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.’ Maana yake ni kwamba adui wetu hapa duniani ni shetani ambaye katu hatuwezi kumshinda bila kuwa na Mungu ndani yetu.” Sauti ya Nelson ilisikika.

Mkewe na mwanae walikuwa kimya wakimtazama kwa makini bila kuzungumza chochote. Nelson aliendelea kuzungumza nao kwa upendo ingawa Vivian hakufurahishwa kabisa na mazungumzo ya mume wake. Uso wake ulionyesha hasira za waziwazi.

Kwasababu Mungu alikuwa hajamfunulia Nelson roho wa ibilisi aliyekuwa ndani ya nafsi ya mke wake, ndiyo maana hakuweza kuelewa sababu ya mke wake kununa pindi asikiapo habari za Mungu.

Tangu siku ile alipompokea Yesu maishani mwake alipokuwa ndani ya gereza, kuzimu walilijua hilo. Kitendo kile kililaaniwa vikali na ulimwengu wa kuzimu kwasababu ilikuwa ni njia ya kumkosa katika ulimwengu wao. Kwa kuwa walikuwa na malengo marefu naye, walijaribu kumuuwa mapema kabla hajakomaa kiimani lakini ilishindikana.

Nelson alikwenda kutembelea makaburi ya binamu zake, Frank na Christopha. Japokuwa lilikuwa ni pengo kubwa kwake lakini moyoni alijihisi kutopungukiwa na kitu kwavile alikuwa amempata mfariji wa kweli maishani.

Ile kampuni aliyokuwa anafanya kazi, waliamua kumsimamisha kazi kwa kuwa, muda mwingi anautumia katika mambo yake badala ya kufanya kazi. Kampuni ilipata hasara kubwa kutokana na kutokuwepo kwake kazini kwa muda mrefu. Kwavile alikuwa ameshapewa barua ya onyo kwa zaidi ya mara tatu, ulifuata uamuzi wa kumsimamisha kazi.

Ingawa ni kawaida habari za kufukuzwa kazi huwa zinakuwa ni mbaya kwa watu wengi, lakini kwa Nelson hali ilikuwa tofauti sana, kwasababu alipopewa barua ya kusimamishwa kazi alionekana kuwa na furaha na mwenye kumshukuru Mungu kila wakati. Baadhi ya marafiki zake walimuona kama vile hana akili nzuri tena, kwavile habari ya kufukuzwa kazi haikumsumbua akili hata kidogo. Mbaya zaidi ni kwamba, barua ya Nelson kufukuzwa kazi ilimtaka pia kukabidhi vitu vyote vya ofisi ikiwa ni pamoja na nyumba aliyokuwa anaishi. Alipewa wiki moja awe ameshakabidhi nyumba kwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo kwavile kuna mfanyakazi mwingine alipaswa kuhamia kwenye nyumba hiyo haraka iwezekanavyo.

Wakati hayo yote yanatokea Nelson alikuwa na shilingi elfu 20 kwenye akaunti yake. Fedha hizo zilikuwa ni kidogo sana, kwavile hazikuwa na uwezo wa kumuhamisha wala kumpatia nyumba nyingine kwa haraka. Ni wazi kabisa kwamba familia hiyo ilikuwa ikipitia katika wakati mgumu, lakini Nelson alizidi kulia na Mungu wake ili afungulie milango mingine ya baraka.

Lile duka la nguo lililokuwa linaendeshwa na Vivian kwa njia ya kichawi, liliwaka moto siku moja baada ya Nelson kupokea barua ya kufukuzwa kazi. Nelson aliendelea kumshukuru Mungu akiamini kwamba yeye ndiye mwenye kuruhusu hayo yote yatokee.

Kwa upande wa Vivian hali ilikuwa tofauti sana, baada ya duka la nguo kuteketea. Alihisi kuchanganyikiwa kwasababu ule mpango wa kuwapeleka watu kuzimu, usingefanikiwa tena kwa kiasi kikubwa. Jambo lile lilikuwa linakwenda kupunguza uhusiano mzuri aliokuwa nao na kule kuzimu. Malikia mkuu wa kuzimu alimpenda sana kwasababu yeye ndiye aliyekuwa anaongoza kwa kuwapeleka watu huko. Kwahiyo kutokuwepo tena kwa duka lile kungepunguza sana idadi ya watu wanaopelekwa katika ulimwengu huo wa ibilisi shetani.

Wiki moja ilikatika, Nelson akiwa bado hajapata pa kwenda ili aweze kukabidhi nyumba ya kampuni. Kilichofuata baada ya kuonekana kukahidi amri hiyo ya kuondoka ni kwamba, uongozi wa kampuni hiyo walitoa vitu vyake vyote, nje ya geti kwa nguvu. Bila kupoteza muda, siku hiyohiyo akaingia mfanyakazi mwingine katika nyumba hiyo, ambaye ndiye aliyekaimu nafasi yake kazini.

Baada ya Nelson kutolewa vitu vyake nje ya geti, uso wake ulitawaliwa na huzuni kubwa. Wapita njia pamoja na majirani walikusanyika kwa wingi katika eneo lile huku kila moja akizungumza lake, alilojisikia.

“Acha wafukuzwe, huwa wanaringa sana.” Nelson alisikitika sana baada ya kusikia maneno hayo yakitamkwa na mama mmoja jirani yake.

Kimya kimya Nelson alitamka maneno haya “Kama kweli wewe Mungu ndiye umeamua niabike, basi mapenzi yako yatimizwe, lakini kama ni hila la shetani, jitokeze Mwamba wangu unitetee.”

Kwa kadiri giza lilivyokuwa likipambana na nuru, umati wa watu waliokuwa wakimshangaa Nelson na familia yake, ulizidi kupungua. Giza lilipoishinda nuru, Nelson alibaki na familia yake pale nje wakipigwa na baridi huku mbu nao, wakiwashambulia sawasawa. Nelson alitumia hekima kumwendea jirani yake mmoja ambaye, walikuwa wanaivana sana, kisha akamuombea hifadhi mke wake na mwanae hadi siku inayofuata. Yeye alirudi kukesha kulinda vitu vyake ambavyo vilikuwa pembezoni mwa barabara.

Ng’ai ng’ai hadi pana kucha hakufumba macho yake, alikesha akiimba na kusali ndani ya gari lake ambalo nalo lilikuwa nje ya geti. Usiku kucha alihisi kuna nguvu fulani inamwambia aviuze vile vitu vyote alivyokuwa navyo, kisha fedha atakazozipata awasaidie wasiojiweza. Alipata mkanganyiko kidogo kutokana na nguvu ile iliyokuwa inamsukuma kufanya hivyo. Alijiuliza inawezekana vipi afanye hivyo ili hali hana pa kwenda? Alizidi kusali na kumuomba Mungu amwonyeshe mlango wa jaribu lile lakini alizidi kusikia sauti ya nguvu ile iliyokuwa inamsukuma kuuza vitu na kisha kusaidia masikini. Kwavile nguvu ile alikuwa anaisikia katikati ya maombi, moja kwa moja alijua ni nguvu ya roho mtakatifu iliyokuwa inamwongoza kufanya hivyo.

Kweli bila kupoteza muda palipokucha, ulifanyika mnada mkubwa wa kuuza vitu vyote palepale pembezoni mwa barabara. Kufikia saa tano asubuhi vitu vyote vilikuwa vimeshanunuliwa.

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Sherehe Kuzimu
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni