SHEREHE KUZIMU (33)
Zephiline F Ezekiel
---

Mtunzi: Frank Silaa
SEHEMU YA THELATHINI NA TATU
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Kwavile nguvu ile alikuwa anaisikia katikati ya maombi, moja kwa moja alijua ni nguvu ya roho mtakatifu iliyokuwa inamwongoza kufanya hivyo.
Kweli bila kupoteza muda palipokucha, ulifanyika mnada mkubwa wa kuuza vitu vyote palepale pembezoni mwa barabara. Kufikia saa tano asubuhi vitu vyote vilikuwa vimeshanunuliwa.
KAMA SIMULIZI HII UNASOMEA NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI KUPATA VIPANDE VYOTE KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA NAYO...
Sio gari, sio kikombe cha kunywea chai, vyote vilipata wateja ambao walilipa fedha taslimu.
Benedict na mama yake walihisi huenda baba huyo amerukwa na akili, kutokana na mambo aliyokuwa anayafanya.
“Eti mama, kweli ni sahihi baba kuuza hivi vitu vyote na kisha fedha zikasaidie masikini? Kwani sisi tuna tofauti gani na masikini wakati tumefukuzwa kwenye nyumba tuliyokuwa tunaishi?” Benedict alimtwanga mama yake maswali yaliyokuwa yanamtatiza.
“Sidhani kama akili ya baba yako iko sawasawa.”
“Kwani kakueleza baada ya mnada tunakwenda kuishi wapi?” Benedict alizidi kuuliza maswali.
“Ukitaka kujua kuwa amechanganyikiwa ni kwamba, hata yeye hatambui pa kwenda baada ya haya yote.”
“Ama kweli leo ni leo asemaye kesho ni mwongo.” Benedict na mama yake walikuwa njia panda.
Mnada ulipoisha Nelson alifanikiwa kupata jumla ya shilingi milioni 20. Bila kuchomoa hata senti tano, alizipeleka zote hadi kwenye kituo cha watoto yatima kilichokuwa jirani na pale kwake. Baada ya kuzikabidhi fedha zile alibakiwa na nguo alizovaa pamoja na simu yake ya mkononi. Hakuwa na kitu kingine chochote.
Mke wake ndiye alibakiwa na begi moja kubwa, ambalo ndani yake kulikuwa na nguo na vitu vyake vidogo vidogo pamoja na kibuyu cha kichawi.
Watoto yatima waliokuwa wakilelewa na kituo kile cha ‘Baraka village’ walifurahia msaada mkubwa walioupata siku ile kutoka kwa familia ya Nelson.
Lisaa limoja baada ya Nelson kumaliza kutoa msaada katika kituo cha watoto yatima, alipokea barua pepe kwenye simu yake kutoka kwa Mr Lee, mkurugenzi wa wa taasisi ya ‘Spitual health’ ya nchini Uingereza.
“Hellow! I would like to inform you that, our institution have decided to work with you immediately, to cover the chance of our engeneer who is suffering from stroke. We are willing to pay, all the cost of transfer to London, as well as to buy you, a new house. Also we are ready to assist your son in education up to university. We are waiting for your answer within 24 hours. Thank you. From Chief executive officer, Mr Lee.” (Habari yako, ninapenda kukujulisha kuwa, taasisi yetu imependekeza kufanya kazi na wewe kwa haraka sana kuziba pengo la mhandisi wetu mkuu ambae ameshikwa na kiharusi. Tupo tayari kugharamia gharama zote za kuihamishia familia yako huku London, sambamba na kuwanunulia nyumba mpya. Pia tupo tayari kumsomesha mwanao bure hadi chuo kikuu. Tunasubiri jibu lako ndani ya masaa 24. Ahsante. Imetoka kwa mkurugenzi mkuu. Mr Lee.)
Nelson hakuamini macho yake, alirudia kusoma ujumbe ule mara mbili mbili. Moyo wake ulilipuka kwa furaha isiyokuwa na kifani. Muda huohuo alijibu ule ujumbe kwamba yupo tayari kufanya kazi na taasisi ile. Alimsimulia mke wake ule muujiza ambao Mungu alimtendea, lakini simulizi hilo kwa Vivian ilipita sikio moja na kutokea lingine kwavile hakutaka kabisa kusikia habari za Mungu.
Baada ya muda mfupi Nelson alitumiwa barua pepe nyingine kutoka kwa Mr Lee iliyokuwa inamshukuru kwa kukubali kufanya kazi nao. Siku hiyo hiyo Nelson aliingiziwa fedha taslimu milioni 40 kwenye akaunti yake ya benki kwaajili ya maandalizi ya safari ya kuhamia Uingereza. Huo ni muujiza mkubwa ambao ulimtokea Nelson maishani mwake.
Nelson alichukua hifadhi ya muda mfupi katika hoteli ya M- tower jijini mwanza. Siku iliyofuata utaratibu wa kutafuta passport za kusafiria ulianza mara moja.
Kuzimu hali ilizidi kuwa mbaya, kila mara maombi ya Nelson ilikuwa ikiharibu vikao vyao. Walikosa kabisa muda mzuri wa kufanya vikao vyao, kwasababu ule muda waliokuwa wakiutumia, saa sita kamili hadi saa tisa usiku ndio muda ambao Nelson alikuwa akichapa maombi ya nguvu. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kule kuzimu, kwasababu hakuna chochote kilichokuwa kikifanyika kikafanikiwa. Hakuna kafara za damu zilizokuwa zikitolewa tena kwasababu majini na maajenti hawakuwa na nguvu ya kwenda duniani kuchukuwa watu.
Nelson aliendelea kupambana nao katika ulimwengu wa roho. Siku ya nne wakati Vivian yupo hotelini kibuyu kilihitaji damu kama kawaida. Hakuna kipindi ambacho kilikuwa kigumu kwake kama hiki, kutokana na kwamba kila aliyejaribu kumtoa kafara ilishindikana. Alizidi kuwa matatizoni kwasababu kibuyu kile kinaposhindwa kupata damu kwa muda muwafaka basi kitapambana na nafsi yake.
Mama yake Vivian alionekana kupaniki vilevile kwasababu kulikuwa na kila dalili ya damu yake na ya mwanae kumwagika. Kwa jinsi ilivyo ni kwamba, endapo Vivian atashindwa kabisa kumtoa mtu kafara katika msimu ule, basi mama yake ndiye atatumika katika kafara hiyo na mwisho wa siku yeye ndiyo atakuwa wa mwisho.
Ilifanyika kila namna kusudi damu ya kibuyu iweze kupatikana lakini kila njia ilionekana kubuma. Vivian na mama yake walikonda kwa mawazo. Vivian alikuwa akikutana na mama yake katika mikutano yao kwa njia za kichawi, kwavile mama alikuwa Arusha na Vivian alikuwa mwanza.
Siku chache baadaye mama yake Vivian alionekana kurukwa na akili, kwasababu alianza kuongea peke yake kwa kutoa siri za watu ambao aliwai kuwauwa. Majirani walisikitika sana, baada ya kusikia kwamba, mama huyo ndiye aliyeuwa watoto wake pamoja na mume wake. Haikuishia hapo walishikwa na butwaa zaidi baada ya kufahamu kuwa mama huyo ndiye aliyeuwa wajukuu zake pamoja watu wengine pale kijijini.
Baada ya kumaliza kutoa siri zake, jamii nzima ilifahamu maovu yaliyofanywa na mama huyo. Siku chache baadae alipoteza maisha kutokana na kufanyika kafara ya kibuyu cha mwanae. Mazishi yalifanyika huko nyumbani kwake Sakina, Arusha.
Ilibidi Nelson aahirishe safari ili aweze kumzika kwanza mama mkwe. Kwahivyo walifunga safari kutoka Mwanza kwenda Arusha kwenye msiba.
Vivian alikosa raha na alipoteza kabisa matumaini ya kuishi kwavile alijua kuwa, yeye ndiye atakayefuata kufa.
Zilipopita siku tatu baada ya Marwa kuzikwa, Adela aligundua kuwa amefanya kosa kubwa sana maishani mwake. Roho ilimuuma sana kwasababu usichana wake ulitolewa na mvulana ambaye hakuwa chaguo lake. Muda mwingi alikuwa ni wa kulia na kujilaumu sana kwa kufanya kitendo cha kumsaliti mwanaume wa ndoto zake. Hakujua nguvu iliyomsukuma hadi akajikuta anatumia shuka moja na marehemu, Marwa.
Alilia na kuteseka sana binti wa watu lakini ukweli ni kwamba kupenda kwake kulisababishwa na nguvu za giza. Ingawa hakujua kuwa Benedict ni mzima au ameshakufa lakini alijipa moyo ipo siku atakutana naye. Nafsi yake haikumtuma kabisa kuamini kwamba mvulana huyo ni marehemu. Alijipa matumaini kila kukichwa kwamba ipo siku ataonana na mwanaume huyo hatimaye watafunga pingu za maisha.
Suala la kujinga na shule kwa mwaka huo ilishindikana kwavile walitumia muda mwingi katika matibabu. Kwahiyo alijipanga mwakani ndiyo aendelee na masomo yake. Aliapa mwili wake kutoguswa na mwanaume mwingine tofauti na yule ambaye amechaguliwa na moyo wake. Kila alipolala kila alipoamka akili yake ilikuwa ikimuwaza mpenzi wake wa moyo. Ombi lake kuu kwa Mungu ni kukutana na laazizi wake.
Siku moja alipokuwa katika mawazo mazito ya kumuwaza mpenzi wake, alikumbuka kuwa, kumuomba Mungu pasipo kuwa na bidii ya kutafuta kile unachohitaji ni kazi bure. Aligundua kwamba, Mungu humbariki zaidi yule mwenye bidii ya utafutaji kuliko yule anayepiga magoti kila kukicha pasipo kujishughulisha. Kumbukumbu zilimjia siku moja walipokuwa wakisafiri kuelekea katika mashindano ya somo la mathematics shule ya jirani.
Siku hiyo, ndiyo siku ambayo aliweza kufahamu nyumbani kwa kina Benedict, japokuwa alionyeshwa wakati walipokuwa safarini. Nafsi ilimsukuma kufunga safari ya kuelekea Mwanza kwenda kumsaka mpenzi wake. Mapenzi yana nguvu sana jamani, kwani siku hiyohiyo baada ya kupata wazo hilo, alianza safari kutokea kijijini kwao kuelekea Mwanza.
Jua lilikuwa limeshatua tayari, wakati alipokuwa anaanza safari. Alipanga siku hiyo atakapowasili, afanye kila liwezekanalo aonane na mwanaume huyo, kusudi siku inayofuata asubuhi na mapema arudi shinyanga kwavile ilikuwa ni siku ya ubatizo wa mtoto wa dada yake.
Kwa bahati mbaya gari alilopanda liliharibika zaidi ya mara tatu wakati alipokuwa safarini. Lakini kwa kuwa Mungu ni mwema alifika salama, ingawa ilikuwa usiku sana. Kuharibika kwa gari mara nyingi pamoja na kuchelewa kuanza safari ndiyo ilipelekea kuwasili jijini mwanza majira ya saa tano usiku.
Tayari ilikuwa ni usiku sana. Kwahiyo ilimuwia vigumu kupata usafiri wa daladala ya kuweza kumfikisha mtaa aliokuwa anaishi huyo mpenzi wake. Ilimlazimu kuchukua usafiri wa bodaboda ambayo ndio usafiri pekee uliokuwepo kwa wakati ule. Alijaribu kuvuta kumbukumbu vizuri ya mazingira yale kusudi asiweze kupotea usiku ule. Zilipokatika dakika kumi na tano alimwambia dereva asimame. Tayari alikuwa ameshawasili katika mtaa husika.
Alifanikiwa kuiona nyumba yenyewe japokuwa macho yake yalikataa kuamini kilichokuwa kinaonekana. Watu wengi walionekana kuzingira nyumba ile ambayo ilikuwa inamalizikia kuteketea kwa moto. Alihisi kuchanganyikiwa kutokana na tukio lile la kutisha lililokuwa linatokea kwa wakati ule. Moyo wake ulikataa kukubaliana na kile ambacho macho yake yalikuwa yanashuhudia. Alijisogeza zaidi na zaidi ili aweze kushuhudia vizuri. Jeshi la zima moto pamoja na majirani walikuwa wanaendeleza juhudi za kupambana kuuzima moto ule.
Hata hivyo hakuna kilichokuwa kinaonekana kusalia ndani ya nyumba ile, kwani moto ulikuwa umeshachoma kila kitu. Moyo ulikuwa ikimwenda mbio sana. Shauku yake kubwa ilikuwa ni kutaka kujua kuwa, wenye nyumba wamesalimika ama wamefia ndani ya nyumba. Alimsogelea mmoja wa majirani ambaye alionekana kuwa na masikitiko makubwa sana. Dhumuni lake kubwa ni kutaka kufahamu kama moto ule umegharimu uhai wa mtu yeyote.
Adela aliihisi uchungu ambao hakuwahi kuhisi tangu alipotoka tumboni kwa mama yake. Alisikitika na kulia sana, aliposikia kwamba wenye nyumba wote wamefia ndani ya nyumba. Juhudi za kuwaokoa zilifanyika lakini ilishindikana kutokana na ukubwa wa moto. Ilikuwa ni kipindi kigumu sana kwake. Alijua kuwa mpenzi wake atakuwa ameteketea ndani ya moto ule. Hakuona sababu ya kuendelea kuishi bila kuwa na Benedict maishani.
Alichukua uwamuzi wa kukimbilia ndani ya nyumba ili na yeye aweze kuteketea na mpenzi wake.
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi Share App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni