
Mtunzi: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Kisha akatengeneza vamizi la kumrejesha Juma nyumbani bila maafa yoyote, ili aendelee kuwasoma watu wanaomfuatilia Juma.
Akaivamia nyumba na kutoa kitisho kikali.
Zoezi likafanikiwa Juma amerejea na wao wamerejea.
Ni akina nani hawa? na wanataka nini kwa Juma?
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
haya yalikuwa maswali ambayo yalihitaji kupatiwa majibu upesi sana kabla naye hajajua ni kitu gani anaweza kufanya katika mchakato huu.
Aliitoa taarifa hii ya mashaka yake juu ya watu anaowaona eneo hilo, taarifa ikapokelewa huku akisisitizwa kuwa makini zaidi.
Masaa yalizidi kwenda bila kuona juhudi za watu wale kuingia ndani ya nyumba ya Juma, walibaki kurandaranda huku na kule bila kujua kuwa wanafuatiliwa.
Kwa kuwatazama jinsi walivyokuwa wanatembea na kufanya mawasiliano alihisi yawezekana ni askari waliopo kazini, ama waliopoteza kazi zao, na kama si maaskari basi yawezekana waliwahi kupata mafunzo ya kijeshi kwa sababu maalumu.
Akajinyoosha kidogo mwili wake na kujipima ikiwa anaweza kukabiliana na vijana wale.
Wakati anajinyoosha akabaki kujicheka kuwa anauhangaisha mwili wake wa nini wakati ana kijana wake wa kazi ambaye kamwe hazeeki.
bastola kiunoni!
Majira ya saa tatu usiku akapiga hatua na kujichanganya barabarani, na hapohapo akageuka muigizaji, akazuga kuwa amelewa na anayumbayumba.
Lengo lake likiwa kumfikia mmoja kati ya wale vijana.
Akafanikiwa kupita jirani na kijana mmoja, akajikuta akicheka ndani ya moyo wake alipotambua kuwa hata kijana yule naye alikuwa katika fani ya maigizo na alikuwa yu katika kitengo cha kuigiza kuwa ni kijana anayetumia madawa ya kulevya na sasa ametulia tuli baada ya kujidunga.
Safi! akajisemea kisha akamchokoza.
Akamsema maneno yanayoudhi huku akiendelea kujiweka katika hali ileile ya ulevi.
Yule bwana hakujibu kitu badala yake aliendelea kuwa mtulivu.
Wakati wote huu alipokuwa anamfanyia bughudha katika sikio lake alikuwa na kifaa kidogo kilichokuwa kinatumika kwa ajiri ya mawasiliano.
Yule bwana aliyekuwa amejiweka kama mtumiaji wa madawa ya kulevya hatimaye alinyanyua kichwa chake na kumtazama huyu mlevi kwa chati jinsi alivyokuwa anahangaika kumchokoza.
"Naomba uondoke hapa." alizungumza maneno machache kisha akainama.
Mlevi akaanza kucheka huku akidiriki kumzongazonga yule bwana, alifanya vile kwa sababu alijiamini kuwa yule bwana hana ubavu walau wa kuingiza hata ngumi moja katika mwili wake iwapo watakusudia kutupiana makonde na hata akifanikiwa kutupa konde halitamletea athari.
"Naomba uniache uondoke hapa wewe mlevi." alisisitiza. Lakini yule mlevi bado aliendelea kuwa pale. Mara atukane hivi mara aimbe vile.
Bwana aliyeketi akazidiwa na kero zile, akasimama wima na kumrushia ngumi kali yule mlevi, mlevi akaikwepa bila kujibu pigo.
Kukwepwa kule kukamfanya awe makini zaidi na yule mlevi. Macho yakamkagua haraharaka huku wakitazamana kama majogoo.
Akajaribu kurusha teke, mlevi akakwepa.
Wakati yule mlevi anakwepa teke lile, yule bwana aliyekuwa akikabiliana naye akaona kitu kilichomtisha.
Aliiona bastola.
Na hapohapo akazungumza maneno yaliyomchanganya yule bwana mlevi wa kuigiza.
"Angusha mbuyu kuna nyoka."
Maneno yale yakasafiri upesi katika akili ya yule mlevi wa kuigiza, akajaribu kuyafanyia kazi upesi lakini hakuweza kupata maamuzi sahihi.
Jicho likamtazama mlevi yule kutokea mbali kabisa katika kifaa maalumu, mlango wa chuma ukafunguliwa kisha mwanga ukatoka bila mlio wowote, mwanga ukasafiri kwa kasi kubwa na kisha ukaweka makazi ya muda katika kifua cha yule mlevi wa kuigiza.
Akatokwa na yowe kidogo kisha akaanza kujitupa huku na kule. Maneno aliyoongea hayakuwa nyoofu akaamua kunyamaza huku damu ikimtiririka.
Yule bwana aliyekuwa ameweka kambi chini ya mti ule akampekua na kutoa bunduki katika kiuno chake.
"Zahoro! huyu mjinga alikuwa na bunduki, huyu hakuwa mlevi aisee. Katumwa huyu hakutakiwa kuuwawa...... dah!" alizungumza kwa kutumia kifaa kilichokuwa sikioni.
Maneno yale aliyozungumza yakapita moja kwa moja kwenda mahali ambapo hawakutaka yafike. Na hawakujua kama yanavuka mipaka hiyo.
Yule bwana marehemu alikuwa akiwasiliana na mtu mwingine kabla hajauwawa. Hivyo alisikia yote hadi mwisho.
____
INSPEKTA KOBO akachanganyikiwa upya, hii ni baada ya kuyasikia maneno yaliyozungumzwa katika kifaa kilichokuwa sikioni mwa kijana wake aliyemtuma kufuatilia mienendo ya Juma Kihwele.
Alisikia sauti yake wakati akitapatapa na mwisho akaisikia ile sauti ya mtu aliyekuwanaye.
"Ni akina nani hawa?" alijiuliza huku aking'ata vidole vyake baada ya kukiri kuwa kuna watu hatari katika sakata hili ambalo kwa namna yoyote ile linaelekea kumwangukia na kumzika kabisa.
Kijana wake alikuwa ameuwawa!
"Angusha mbuyu kuna nyoka..." Hii sauti ikawa inajirudia katika kichwa chake. Ni kama aliwahi kusikia mahali...
"Yeees!" akarusha ngumi hewani, alikuwa amekumbuka kuwa sauti ile aliisikia usiku ule alipokwenda kwa Nguzu kwa ajili ya kumsihi aachane na Zubeda wake na alipoondoka nyumba ile ikachomwa moto na kuaminika kuwa imeondoka na uhai wa Nguzu.
"Huyu ni nani lakini? na kwanini wamchomee kijana wa watu ndani eeh!" akawaza na kuwazua kisha akaamua kutoka nje.
Akaingia katika gari yake na kunyoosha moja kwa moja hadi hospitali aliyokuwa amelazwa Zubeda. Akaingia moja kwa moja katika kile chumba kile ambacho alikuwa amekiwekea walinzi wa siri hasahasa baada ya mkewe kuingia mle ndani na kumuhoji Zubeda mambo mazito.
"Zubeda kila kitu kimeharibika na mambo yanazidi kuharibika, huu sio wakati wa kuzungumzia kilichotokea hapo katikati, huenda hicho kina unafuu. Naomba usikilize hii sauti kwa umakini na unieleze kama umewahi kuisikia... naomba usinifiche hata kama umeisikia katika mazingira ambayo haupendi mimi niyafahamu."
Akamwinamia na kumwekea kifaa sikioni kisha akakiwasha kile kifaa, Zubeda akaisikia sauti ya yule mwanaume ikizungumza yote iliyozungumza.
Koplo Zubeda akatikisa kichwa kuwa hakuna anachokielewa. Inspekta Kobo akashusha pumzi zake kwa juhudi zote, mambo yalikuwa yanazidi kuwa magumu.
"Vipi kuhusu Zahoro? unalifahamu hili jina?"
"Nawafahamu Zahoro kadhaa, ila sina ukaribu nao."
"Kuna mjinga anaitwa Zahooro nahisi amemuua kijana wangu." alizungumza kwa uchungu Inspekta huku akitazama juu.
Na alipoushusha uso wake alizungumza na Zubeda.
"Hautaendelea kulalia hiki kitanda, kuna watu wanaisaka roho yako wakati huu. Hakuna ninayemuamini kukulinda, nataka nikulinde mimi mwenyewe." Inspekta akanong'ona kwa hisia kali huku akiwa anamtazama Zubeda moja kwa moja machoni. Kabla Zubeda hajasema lolote Inspekta akaendelea, "Mke wangu ana hasira sana najua, lakini si sababu ya mimi kukuacha wewe katika hali isiyokuwa salama. Yameniumiza mengi katika hii dunia ya mapambano, nitajitonesha upya nikishuhudia maiti yako"
"Mlinde zaidi mkeo..." Zubeda akaingilia kati katika hilo.
"Yupo katika ulinzi wa hali ya juu." Alijibu Inspekta na hakutaka maongezi yaendelee, akatoweka kwa ajili ya kufanya hatua zote za kumwondoa Zubeda katika hospitali ile.
Zoezi likafanikiwa.
_________________
KUKUTWA ametupwa mtaroni?
Tena akiwa hana jeraha bali alama moja tu katika shingo lake...
Pigo la aina gani hii?
Nani alitoa pigo hilo barabara!
Haya yalikuwa maswali mfululizo yaliyopita katika kichwa cha kiongozi wa oparesheni isiyokuwa na jina rasmi. Hii ni baada ya kupokea taarifa kutoka jijini Mwanza kuwa kijana wake anayemuamini kupindukia alikuwa ameuwawa kwa kupigwa pigo moja kali kabisa shingoni.
Tabasamu hafifu lilimdondoka wakati anajaribu kufikiria upya juu ya jambo hili.
Akanyanyua mkonga wa simu yake, akataka kupiga mahali akaghairi na kubaki akielea katika mzani wa maamuzi.
Akaushusha ule mkonga na kunyanyua simu yake ya mkononi. Akabofya nambari zilizokuwa zimetoka kumpatia taarifa kutoka jijini Mwanza.
"Kwa hiyo umesema hakuna sehemu nyingine aliyojeruhiwa? Je ujumbe wowote kwa ajili yetu?" akatulia na kusikilizia upande wa pili ukijibu. Baada ya majibu akazungumza kwa ukali kidogo.
"Ongea na Cheyo, aamrishe askari wake wazunguke kila kona hapo Shamaliwa wakamate vibaka wote wanaorandaranda kijinga jinga mitaani. Wawabane watasema kama waliona hilo tukio. Mwambie asiache mtu hata mmoja."
Waliendelea kuzungumza kwa sekunde kadhaa kisha simu ikakatwa.
Jijini Mwanza baada ya masaa mawili eneo la Shamaliwa nje kidogo ya jiji hapakuwa mahali salama hata kidogo, ukizurura unakamatwa, ukikaa unakamatwa ukicheka unakamatwa ukilia unakamatwa.
Hadi waliokutwa wanakata majani ya ng'ombe nao walikamatwa.
Kamata kamata ile ikazua jambo juu ya jambo
_______________
KONSTEBO MARTIN NGUZU alikuwa anajaribu kuutafuta usingizi katika kitanda ambacho kilitawaliwa na kunguni waliokuwa na maksudi mabaya, taa ikiwashwa wanatoweka na ikizimwa wanaingia uwanjani kuinyonya damu ya Nguzu.
Mchezo huu wa kunguni wale ukawa kikwazo kikubwa kabisa kwake. Lakini hakuwa na yeyote wa kumlaumu kwa sababu alikusudia kujihifadhi katika nyumba ile ambayo lingetokea lolote lile angeweza kupiga ngumi moja pamoja na teke kisha dirisha likahama pahali pake na kuacha njia.
Bughudha hii ikamnyanyua mpaka nje, akazurura huku na kule pasi na uelekeo maalumu.
Katika kuzurura huku akaona haitakuwa jambo la heri kuzurura huku kichwa chake kingali wazi.
Akafanya tathmini ya muda mfupi huku akijishangaa namna ambavyo yu hai, lakini zaidi zilikuwa ni hisia mpya zinazokisumbua kichwa chake.
Majina mapya na mtazamo mpya katika fikra zake, jina Majenga lilikuwa la kwanza kabisa kujenga naye urafiki.
Sanjari na jina hili kuna ndoto ambazo zimekuwa zikimfuata bila kukoma, mara amuote mama yake mzazi na alipoifuata ndoto ile na kurejea jijini Mwanza anamkuta mama yake akiwa mikononi mwa mtu mbaya.
Anatokwa na pigo moja, pigo lililomwangusha yule bwana moja kwa moja.
Kuhusu lile pigo akajiuliza upya, ni lini amekuwa na uwezo wa kuangusha mtu kwa ngumi moja pekee?
Jibu lilikuwa rahisi sana kuwa hakuwahi kuwa na uwezo huo hapo kabla.
Utata mwingine uliomsumbua ni kuhusu magazeti yaliyoandika kuhusu kifo chake.
Kifo gani? Alijiuliza, lakini swali hili halikumshtua hata kidogo.
Kufa si jambo dogo ujue? alijisemea huku akiendelea kuzurura.
Hata tukio la kukuta pesa katika nguo aliyoianua katika kamba usiku ule baada ya kujinasua katika kifusi katika nyumba iliyokuwa imeanguka bado kilimtatanisha.
"Nani wa kusahau pesa katika nguo ndani ya jiji la Dar es salaam!!"
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi