KONSTEBO NGUZU (9)

Zephiline F Ezekiel

SEHEMU YA TISA
ILIPOISHIA...
"Uliponaje mwanangu, nyumba iliteketea yote ile. Tuliona kwenye Televisheni.." mama alimuuliza.

"Mama usimwambie mtu yeyote kama umeonana na mimi, mimi nipo hai na ninaamini nina kazi kubwa ya kufanya kabla sijasimama hadharani na kuutangazia uma kuwa ninaishi."

JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈

ENDELEA...
Alisihi Nguzu. Kisha akamkumbatia mama yake na kumbusu shavuni.

Upesi mama akaipapasa shingo ya nguzu katika giza lilelile.

Na hapo akatokwa na tabasamu pana lililosindikizwa na machozi ya furaha.

Aliyekuwa mbvele yake alikuwa yuleyule mtoto aliyetoka katika tumbo lake.

Martin Nguzu!

Ameponaje? hilo halikuwa swali lililomuhangaisha......

Bora uzima.

Walizungumza kwa dakika kadhaa kuhusu Majenga kisha wakaagana.

Akiwa anafanana na giza kwa jinsi alivyovaa alitembea kwa tahadhari kubwa huku akiamini wapo wengine wanaweza kuvaa kama yeye na kufanana na giza, akapiga hatua na kutoweka eneo lile.

Begani akiwa na mzoga wake...

_______

LILIANZA tumbo la kuhara, kila akiingia chooni linapoa anarejea chumbani. Linaanza tena anakimbilia chooni, linapoa.

Alikuwa amechanganyikiwa mno.

Hali hii ikamkumbusha kuwa angali akiwa mwanafunzi alikuwa anaugua haswa akisikia kuwa kuna bakora kwa ajiri ya wachelewaji ama ambao hawajafanya vyema kazi waliyoachiwa. Hivyo alikuwa mstari wa mbele kabisa kufanya kazi zote ipasavyo, kuheshimu sheria na kanuni za shule.

Na hata ilipotokea migomo hakutaka kushiriki, wenzake wakambeza na kumweka katika kundi la wanafunzi waitwao 'MBWA WAOGA' shuleni.

Alikuwa tayari kuitwa majina yale lakini alitambua kuwa anaitii sheria vyema.

Akaishi hivyo na akakua hivyo.

Akiwa katika utu uzima wake ana familia na yupo kazini, anajaribu kuisahau asili yake anaitaka pesa nyingi kwa njia zisizokuwa halali. Jaribio lake la kwanza linakuwa kuuza habari aliyoinasa mahali.

Kabla mchezo haujanoga anajikuta matatani.

Akatamani nyakati zirudi nyuma kidogo tu asijihusishe na hili jambo asilani. Lakini ni saa pekee inaweza kurudi nyuma na si wakati.

Juma Kihwele alikuwa amekamatika.

Akafikiria mtu wa karibu yake wa kuweza kumshirikisha hilo jambo, hasahasa ujumbe kutoka kwa Dokta. Kobo uliomfanya kupata tumbo la kuhara ghafla.

Mkewe, hapa asingethubutu kugusa hata kidogo kwa sababu tayari alikuwa amemwonya kuachana na masuala ya kufuatilia habari zisizomuhusu.

Akafikilia kukimbilia msikitini walau amweleze kiongozi wake wa dini. Huku napo akaona pagumu kuingilika, maana huku ni mambo kunyooshwa tu hakuna kona kona.

Kila sehemu aliyoiwaza akaona haiingiiliki.

Mwisho akajiwekea maamuzi ambayo aliyapa jina la 'NANI ATAMFUNGA PAKA KENGELE'

Katika maamuzi haya yeye alikuwa panya.

Akawavika vyeo vya U-paka Inspekta na mkewe.

Kisha akamchagua inspekta Kobo kwa kujipa imani kuwa yule ni mwanaume mwenzake hivyo watazungumza na yatamalizika tu.

Akaingia bafuni akausafisha mwili wake, akavalia nadhifu kisha akaamua kujihukumu. Akachukua simu yake na kuipekua nambari za Inspekta Kobo. Akajihisi kutetemeka wakati anapiga simu ile.

Kitetemeshi kikaisha alipogundua kuwa simu ile haipatikani. Akachukua maamuzi ya kumpigia Koplo Mtani yule aliyemsababisha akajiingiza katika mchezo huu asioujua. Lakini maamuzi yake yakayeyuka baada ya kujiona kuwa atakuwa anawaingiza watu wengi katika hili jambo aliloliita kuwa ni maongezi ya kiume dhidi ya Inspekta Kobo.

Kwa sababu alipajua ofisini kwake akaamua kwenda kimyakimya wakayamalize.

Akatoka na kuingia katika gari yake, akaitazama tasbihi iliyokuwa inaning'inia katika kioo cha ndani cha gari lake.

Kisha akawasha gari na kuondoka zake.

Baada ya dakika moja, gari jingine dogo likatoweka na kumfungia tela.

Hakujua kuwa wakati anawaza kumfunga paka kengele na wengine waliwaza hivyohivyo juu yake.

Kwa wakati mmoja Juma 'kimbelembele' alikuwa panya na hapohapo paka.

Kiumbe wa ajabu kupindukia!

Aliiendesha gari yake kwa utulivu huku kila mara akijilaumu nafsi yake kwa tamaa za ajabu ajabu.

"Tazama nimejenga nyumba nzuri kabisa, hata kama sijahamia bado lakini nina uhakika wa kuhamia siku yoyote, nina gari na nimekaribia kumnunulia mkewangu la kwake, nina amani ya nafsi, mtoto wangu anaishi vizuri kabisa, anasoma shule nzuri. Hiki nini kiliniingilia kichwani nikapatwa na tamaa mimi lakini, eeh! Ninaheshimika ofisini, bosi ananipandishia mshahara kila leo. Ni kipi nilitaka tena Juma mimi. Yaani shuleni waliponiita kimbelembele nilichukia na kuwaona hawanipendi, sasa najionea mwenyewe. Ona sasa naanza kuhangaika na kimbelembele changu, mtu mwenyewe Inspekta unakuta ana hasira zake huko anipige mabuti, mi kupigana sijui, jeshi lenyewe sijapitia..... Hivi Juma nilikuwaje mimi eeh!" alilalamika kwa sauti ya chini, malalamiko yaliyopelekea machozi kuanza kumbubujika.

Akashindwa kuona mbele vizuri, akaamua kuegesha gari lake kando.

Akajifuta machozi. Akaitazama simu yake na kugundua kuwa ilikuwa inaita pasi na kutoa mlio.

Akakumbuka aliiweka simu yake iwe katika hali ile. Akaishika kwa utulivu na kutazama. Ni mkewe alikuwa amempigia.

Akampigia kuuliza kulikoni.

"Mume wangu naomba urudi nyumbani muda huu, sasa hivi mume wangu... atawaua watoto huyu. Njoo mume wangu..." Alizungumza huku amepagawa mno mke wa Juma.

Simu ikakatwa bila kusubiri majibu kutoka upande wa pili.

Lile tumbo la kuhara lililosumbua kuanzia akiwa nyumbani likayasikia mazungumzo haya, kwa kirehere cha hali ya juu likatamani kusikia zaidi.

Likatoa wawakilishi palepale akiwa ameketi katika kiti chake cha gari....

Hali ya hewa ikachafuka...

"YAKIMBIZE maisha ama la acha maisha YAKUKIMBIZE. Uchaguzi ni wako siku zote..."

ALIBAKI katika mzubao kama mwanaume aliyemwona mwanadada mwenye mvuto akijongea kwenda upande wake akajilaghai katika kichwa chake kuwa amekutana na bahati ya mtende akajiandaa kumpokea, kisha mrembo yule anatokwa na neno la ghafla.

"Kaka umesahau kufunga zipu yako.."

Mzubao huo ulimkumba Juma Kihwele, alipotoka katika mzubao akahamia katika mlowano katika suruali yake.

Chozi likamtoka alipotambua kuwa haikuwa ndoto bali alikuwa kama anavyojiona.

Mbele na nyuma palikuwa pameshirikiana kumfedhehesha.

Ubahili akauweka kando, kabla harufu ile haijawafikia wasiohusika Juma Kihwele akapandisha vioo vya gari lake kisha akawasha kiyoyozi.

Alitambua wazi kuwa kiyoyozi hakitakuwa na msaada mkubwa lakini walau linatimia lile neno la 'Mchuma janga hula na wa kwao' kwanini yeye ale na wasiomuhusu?

Acha ale na kiyoyozi....

Akaigeuza gari kwa kasi akiwa ametaharuki.

Akawa amebadilisha uelekeo na kuelekea alipokuwa ametoka.

Jambo lile likawa na maana nyingine kwa waliomtazama...

______________________

KITENDO kile cha kubadilisha uelekeo kikawashtua wale waliokuwa katika gari iliyokuwa ikimfuatilia toka alivyoliacha geti la nyumbani kwake.

Dereva akabweka na kuwashtua wenzake, wote hawakuamini walipoiona gari ile ikiondoka kwa mwendo mkali. Kila mmoja akabaki kumlaumu mwenzake kwa kuukosa umakini.

Lawama zisingekuwa na msaada wowote dereva akapambana naye kutafuta njia ya kugeuza gari ili afukuzane na lindo lao walilolivizia kuanzia linatoka nyumbani

Sasa lindo limewatoroka ghafla. Wakabaki kujiuliza ni wapi ambapo waliteleza hadi yule bwana akawaona....

Swali hili likawafanya waanze kuamini kuwa bwana Juma ana watu wengi nyuma yake ambao wanamsaidia katika suala la ulinzi.

Hapa wakaongeza umakini na ile hali ya kumchukulia Juma kama mwandishi asiyekuwa na tahadhari katika maisha yake ikatoweka.

Hawakujua kuwa Juma Kihwele alikuwa amevurugwa vibaya mno, na hata ule mwendo kasi wa ghafla ulikuja ghafla kama ulivyoonekana na hakujua kama alikuwa anafuatiliwa.

JUMA aliwasili nyumbani, bila kujali kuwa alikuwa amechafua nguo yake alishuka upesi na kuingia ndani ya nyumba yake huku akiwa amenyoosha mikono yake juu kama namna ya kujisalimisha ili wavamizi wakijitokeza kwa nia ya kushambulia basi awe amejitetea tayari kuwa hana madhara yoyote kwao.

Huenda wataingiwa na huruma juu yake.

Hicho nd'o kitu pekee alichoweza kufanya kwa wakati ule.

Alilivuka geti lake huku akijilaumu kwa ubahili wake uliokithiri wa kushindwa kumlipa mlinzi ili awe analinda masaa ishirini na nne badala yake akaona usiku nd'o wakati pekee wenye hatari akaamua kulipia masaa kumi na mawili.

"Mlinzi mwenyewe analinda na rungu?" Alitoa kauli ya kupuuzia majuto yake.

Alitembea hatua kwa hatua hadi akaufikia mlango wa kuingilia ndani ya nyumba yake akabaini kuwa ulikuwa umefungwa kwa nje.

Bila shaka mvamizi yupo nje.

Huku akiwa anatetemeka akaufungua ule mlango, akaikuta familia yake yote ikiwa inatazama ukutani. Mama mwana pamoja na shemeji yake aliyekuwa pale kwa ajili ya likizo.

"Jamani.... kuna nini mke wangu?" Akamuuliza, mkewe akageuka huku akiwa anatetemeka na asiamini kuwa aliyesema naye alikuwa ni mumewe.

Akaanza kuangua kilio huku yote anayoyasema yasisikike vyema kiasi cha Juma kuanza kumkaripia kuwa anapaswa kuzungumza kwa utulivu ili wajue ni kitu gani kinaendelea.

"Ni nani alivamia hapa na kukueleza upige simu."

"Simjui, sijawahi kumwona hata siku moja."

"Anafananaje? na ni kitu gani anataka kwangu..."

Mkewe akamsogelea Juma na kumkumbatia, hakuwa na sababu nyingine ya kumkumbatia bali kumsihi waende chumbani.

"Hapana... tuzungumze hili jambo kwanza tuelewe muafaka!" alipinga vikali.

Mke akamsogelea tena na safari hii akamueleza ukweli kuwa alikuwa ananuka, anapaswa kwenda kusafisha mwili wake kwanza.

Akili ya Juma ikaingiwa na mchecheto, akatembea kinyonge kabisa kuelekea chumbani.

___________________

NJE ya nyumba ya Juma wale waliokuwa wakimfungia tela walikuwa wamewasili tayari na waliegesha gari lao mbali na nyumba yake. Walikuwa watatu na walitembea kama wasiofahamiana katika suala hili. Kila mmoja alijiweka katika shughuli zake, ilimradi iwe ngumu kujulikana kuwa kuna jambo wanafuatilia.

Umakini wa sasa ulikuwa umezidi wa awali ambapo walimchukulia Juma kirahisi sana. Sasa walikuwa makini kana kwamba wanapambana na adui mwenye hatari sana zaidi yao.

Silaha zao ziliwekwa tayari tayari.

Jicho moja pevu lilikuwa katika kona ngumu kufikika, lilikuwa limewapokea kuanzia walipowasili awali, wakamfungia tela Juma akiwashuhudia. Kisha akatengeneza vamizi la kumrejesha Juma nyumbani bila maafa yoyote, ili aendelee kuwasoma watu wanaomfuatilia Juma.

Akaivamia nyumba na kutoa kitisho kikali.

Zoezi likafanikiwa Juma amerejea na wao wamerejea.

Ni akina nani hawa? na wanataka nini kwa Juma?

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi

Chapisha Maoni