
Mtunzi: George Iron Mosenya
SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
"Kwa hiyo unataka kuigeuza biashara hiyo habari? Na wewe ulipolala na yule dada wa mapokezi nani aligeuza biashara lile tukio lako ama wewe tu nd'o wayaona mabaya ya wenzako..... nilijua umeniitia mambo ya maana kweli mume wangu.
JE UNAISOMA SIMULIZI HII NJE YA APP YA CnZ Media?
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
IPAKUE ILI KUPATA MWENDELEZO KWA WAKATI
👉GUSA HAPA KU-INSTALL👈
ENDELEA...
Huo muda ningekuwa nimemfundisha Mariam kuhesabu moja hadi kumi na ameelewa kabisa. Yani we sijui upoje tu..." Akasimama na kutoka nje akiuacha mlango wazi.
Juma akabaki kimya kabisa, mkewe alikuwa amemgusa pabaya mno. Hakutaka kuikumbuka kabisa siku aliyofumaniwa na mkewe juu ya suala hilo la kujihusisha kimapenzi na msichana wa ofisini kwao. Ni kweli haikuandikwa popote, lakini hii haikuwa sababu nzito ya yeye kuachana na hili aliloligundua.
Ukimya huu haukumaanisha kuwa Juma aliamua kuachana na jambo hili. Akaona mtu sahihi wa kumshirikisha ni Koplo Mtani ambaye alimfahamu fika kuwa alikuwa ni mojawapo kati ya askari wasiokuwa waadilifu, rushwa ilikuwa rafiki yake wa karibu mno.
Kuisubiri asubuhi aliona ni kosa la jinai.
Akanyanyua simu na kumpigia kisha akamshirikisha hatua kwa hatua huku akiweka sharti la kutomtaja Inspekta anayejihusisha kimapenzi na Zubeda...
Licha ya kuwa mahiri sana katika kazi yake, lakini aliwapuuza wakongwe waliotangulia mbele ya haki waliponena kuwa hakuna siri ya watu wawili.
Juma Kimbelembele alikuwa ameisambaza na ipo kwa watu wawili naye akiwa wa tatu.
Kumshirikisha jambo lile Koplo Mtani kukampa ahueni, akajigeuza mara kadhaa akasinzia huku akiwaza kuigeuza habari hii mtaji. Aliamini fika kuwa hatakosa milioni kadhaa kibindoni ikiwa atazipanga karata zake vyema.
Wakati yeye anasinzia salama akiwa amejipunguzia uzito kiasi fulani katika mawazo yake. Upande mwingine nd'o kwanza palikuwa panakucha.
_____
MAPENZI RAHA, nilikuelezeni awali. Lakini huwa raha iso' kifani wakutanapo wawili wanaopendana kwa dhati. Halafu wasipishane sana umri na mitazamo katika uwanja huo wa mahusiano ya kimapenzi.
Muunganiko kati ya Konstebo Nguzu pamoja na Koplo Zuu ulikuwa wa aina yake, waswahili wanasema upele ulikuwa umepata wakunaji.
Siku hii hakuingia kazini mapema, aliwasiliana na mwenzake aliyekuwa na askari mwenzake aweze kumwakilisha katika majukumu yake hadi majira ya saa sita mchana.
Ikawa hivyo!
Nguzu akaamkia nyumbani kwa Zuu, wawili hawa walioshibana wakaanzia kupata kifungua kinywa kilichoandaliwa na Zuu mwenyewe.
Walikula kisha wakalishana huku wakisifiana mambo kadha wa kadha. Baada ya kula wakashushia maji ya matunda.
Kilichofuata ni Zuu kumshika mkono na kumkongoja chumbani Konstebo Nguzu, haikuwa mara yao ya kwanza kuingia katika chumba hiki. Awali Nguzu alikuwa akiogopa sana kufumaniwa lakini mazoea yakajenga kibanda cha kudumu katika mwili wake, kisha kwa sifa mazoea yakajibadili jina yakawa tabia.
Chumbani wakagida mvinyo wa bei ghali, kisha wakakubaliana waende kuogeshana bafuni.
Simu ya Nguzu ikaita ikawakatili uhondo wao.
"Jamali ananipigia, ngoja nimsikilize." Alimweleza Zuu kabla hajapokea ile simu.
Zuu akaelewa.
Baada ya kuongea kwa sekunde chache akakata simu, taharuki kiasi ikamvaa usoni.
"Nahitajika kituoni muda huu, mkuu wa kituo ananihitaji ni amri." alizungumza konstebo Nguzu huku akiwa amemkazia macho ya matamanio koplo Zubeda Msangi (Zuu).
Uzuri Zuu naye alikuwa ni askari alijua vyema maana ya amri. Kwa unyonge akakubali matokeo.
Akamuaga Nguzu kwa kumbusu katika papi za midomo yake. Machozi yakamtoka Zuu na asijue ni kwa nini yanamtoka wakati Nguzu akimuaga.
Wakakubaliana kuonana jioni ya siku hiyo wamalizie walichopanga kufanya asubuhi hiyo.
Wakabusiana tena kwa mara ya pili.
Nguzu akatoweka, uzuri alikuwa amebeba sare zake za kazi na alikuwa amezivaa tayari.
Akachukua usafiri wa pikipiki moja kwa moja kuelekea kituoni.
_____
UKIMWONA mtu mzima yu katika kilio pasi na sababu za msingi basi ana matatizo ya ziada katika akili zake, ama la ana tabia ya kulialia tangu utoto wake.
Lakini ukimwona mwanaume aliyekabiliana na majambazi kwa kutumia silaha, akawasambaratimba licha ya kupigwa risasi kadhaa zilizouvunja mguu wake. Ukimkuta huyu analia peke yake, kaa mbali kidogo kwanza uumize kichwa, si kilio cha kawaida asilani.
Inspekta Kobo alikuwa analia kama mtoto mdogo ofisini kwake.
Alikuwa na miaka arobaini na nane, heshima ya kuwa inspekta pekee haikutosha kuthamini mchango wake katika jeshi la polisi. Wakati wa ujana wake alitambulika kwa jina la Vandame kwa jinsi alivyokuwa akiyapenda mapambano, kwake tukio la ujambazi likitokea nd'o alikuwa anafurahi kwenda kukabiliana nao. Tena alipenda sana wakiwa na silaha.
Na hapo alikuwa na cheo cha chini bado, juhudi zake zikampandisha juu na hatimaye anazeeka akiwa Inspekta.
Haikutosha lakini walau.
Mlango wake uligongwa, akajifuta machozi upesi na kisha akamkaribisha aliyehitaji kuingia.
Mlango ukafunguliwa akausikia mshindo wa ukakamavu kisha ikafuata saluti.
Akaipokea kinyonge sana!
"Konstebo Martin, Martin Nguzu afande nimeitikia wito wako afande!" Kikakamavu mgeni akajitambulisha.
"Keti" akamsihi.
Nguzu akajitua katika kiti kilichokuwa jirani yake.
"Una umri gani konstebo?"
"Miaka ishirini na saba afande!"
"Ninaitwa Mathew Koboko, ama inspekta Kobo. Naamini hatujawahi kuonana, zaidi ya yote mimi sijawahi kukuona." akatulia akamtazama Nguzu. Nguzu akatikisa kichwa kukubali.
"Nina miaka arobaini na nane sasa, umri umenitupa mkono, siko imara sana nilivunjika mguu nikiwa nalitumikia jeshi, mkono wangu wa kuume pia unatetemeka mara kwa mara kwa sababu ya kutumia sana bunduki, mgongo wangu sio mzima sana nikiketisana naumia, nikitembea sana naumia. Akili yangu pekee nd'o ipo salama. Salama kwa asilimia zote" Akatulia na kumtazama Nguzu usoni. Kisha akamwomba radhi kabla hajapenga kamasi nyepesi zilizokuwa zikimwandama.
"Umeoa Nguzu?"
"Sijaona afande!"
"Mimi nimeoa mtoto wangu wa kwanza unamzidi miaka michache lakini ana mwili mkubwa zaidi yako." Akatulia na kulazimisha tabasamu kisha akaendelea tena.
"Nimekuita hapa ili nizungumze na wewe. Mimi kama Kobo na wewe kama Nguzu tena ni sawa na kijana wangu, lakini hapa tuzungumze kama wanaume wastaarabu walioketi baa kabla pombe hazijachanganya vichwa vyao. Najua wewe umekunywa pombe lakini sidhani kama umepitisha kiasi..."
"Nipo timamu afande!"
"Lakini umekunywa kidogo sivyo."
"Hapana afande!" Akakanusha Nguzu.
Inspekta Kobo akasimama taratibu, akayaendea maboksi kadhaa yaliyokuwa pale ofisini, akapekua boksi moja na kutoa chupa akaiweka mbele ya Nguzu.
"Nimekusamehe kwa kunidanganya kwa mara ya kwanza, usinidanganye tena kwa sababu hivi vyuma katika mguu wangu havinizuii kuurusha ukakufikia." akaiacha ile chupa na kurejea katika kiti chake.
"Haukuishia kunywa pombe pekee, Martin Nguzu umejipulizia marashi niliyoyanunua jijini Paris Ufaransa. Kwa kifupi umetoka nyumbani kwangu bwana mdogo. Nyumba inayonipa mimi faraja...." Akasita na kumwacha Nguzu apagawe kwanza.
Hakika alipagawa, hakuamini kuwa siku yaikeinaanza hivyo. Akatambua kuwa yupo ana kwa ana na mume mwenzake.
"Nilikwambia nimeoa Nguzu, lakini nipo salama zaidi nikiwa na Zubeda. Simtumii kwa sababu ya pote nilipomtoa, najua hajakwambia kiundani ni wapi nimemtoa... hawezi kukueleza kuwa nilimkutaanajiuza nikamnunua na hapo nikawa nimeyanunua maisha yake jumlajumla. Alikuwa amefyatuka akili zake na alikuwa amekata tamaa, nilitumia muda na uwekezaji mkubwa sana kumkomboa kutoka janga lile. Narudia tena ninaye mke ninayempenda hata kama yeye hanipendi, lakini kwa Zubeda ni sehemu ninayokuwa salama zaidi.
Siwezi kukulaumu eti umeniingilia katika anga zangu, kama ningekulaumu hata usingeiona sura yangu bali ni mimi ningeiona sura yako baada ya wewe kukatwa kichwa na vijana wangu. Nimeona niwe mstaarabu kidogo, maana na huu uzee nikiwa mkaidi haina maana ya kuwa mzee sasa.
Nguzu, imetosha kuingia nyumbani kwangu, niache basi nisije kufa na magonjwa ya moyo wakati risasi hazikuweza kuniua. Ujue nimelia sana leo hadi nimejishangaa, nimetambua wazi kuwa ninampenda sana Zubeda. Nawe ninakuomba uwe balozi wangu wa kweli, mtafute Zubeda mwambie mzee Kobo anampenda sana na sijawahi kumuwazia mabaya hata siku moja. Msihi haswa kuwa asinirudishe katikaujana wangu kwa namna yoyote ile. Unaweza kuondoka Konstebo Nguzu Martin Nguzu...." Alimaliza Inspekta Kobo kinyonge.
Nguzu akasimama akiwa anatetemeka sana, jasho likimtoka.
"Nenda nyumbani ukapumzike ukitoka humu ndani, nimekupatia mimi ruhusa hii Nguzu."
Nguzu akasimama huku akihema juu juu akapiga saluti na kutoweka pale ndani. Inspekta akamsindikiza kwa macho hadi alipotoweka.
______
Simu yake ilimgutusha kutoka katika dimbwi la mawazo. Ilikuwa ni namba ya Zubeda. Akatambua kuwa tayari mambo yamezidi kuharibika.
Akapokea huku akiwa anatetemeka sana, moyoni mwake akitamani hii iwe ndoto ya mchana.
"Laazizi! ukwapi?" Sauti tulivu kabisa ikahoji.
"Nyumbani vipi kwani?"
"Kuna tatizo Nguzu... tena linaweza kuwa tatizo kubwa sana tukilipuuzia."
"Ni kuhusu inspekta?" Nguzu akauliza.
"Si bora kingekuwa kile kibabu ninakiweza kile. Kuna mtu anaitwa Juma Kihwele sijui unamfahamu?"
"Hapana jina hilo ni geni kwangu Zuu. Kuna nini? na ni nani huyu?"
"Amenipigia simu anasema yeye ni muhariri na anahitaji tuonane kwa mazungumzo juu ya mimi kujihusisha kimapenzi na Inspekta halafu na sasa nipo na wewe. Sijui ameyatoa wapi haya maneno, Nguzu atatuharibia huyu wakati ambao sio muafaka hata kidogo. Nimekupigia maana hili linatuhusu mimi na wewe, nataka tumuwahi." Aakaweka kituo. Nguzu akapagawa, wakati anawaza kuwa ni jambo juu ya inspekta linakuja jingine khusu mwandishi.
"Nakusikiliza wewe, tunamuwahi vipi sasa?" akauliza kinyonge mno.
"Njoo nyumbani usiku tupange, kama saa tatu hivi."
"Hapana Zuu sitaweza kuja hapo usiku wa leo. Huoni kama tutazidi kulikuza tatizo... kwanini tusikutane sehemu ambayo sio hapo kwako?"
"Sawa panga wewe halafu utanifahamisha basi..." Akamaliza na kukata simu.
Nguzu akahisi kuugua, kama sio homa basi ni Malaria kali kupindukia.
Utamu utamu sasa ukageuka uchungu!
Hata kabla hajamweleza Zubeda yaliyojiri katika ofisi ya Inspekta Kobo yanatokea haya mengine ghafla!
Akapanga kukabiliana na hili jambo kabla halijakomaa, akasimama imara akapiga saluti na kujiapiza kuwa hatalala tena na kulialia kama mtoto badala yake atapambana kiume.
Hakujua kuwa wakati yeye akiamua kusimama, kuna ambao walikuwa wakikimbia mbio kali kwa nia ya kumzamisha katika shimo lenye kiza kinene.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Share CnZ Media App kwa Wapenzi wa Kusoma Simulizi Ili Tuwe Wasomaji Wengi